BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
3.MTUME MUHAMAD (S.A.W.W) NI MTUME WA MWISHO.
Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni mwisho wa Mitume yote, kama anavyosema Allah (s.w):-
مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ اَبَا اَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَكِن رَّسُولَ اللهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ وَكَانَ اللهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيماً[1]
Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
*Khaataman Nabiyyiin, maana yake mwisho wa Mitume.
Na inaonesha ukamilifu wa Mtume huyo, na Mtume wa mwisho ni yule ambaye anabakia kuwa mkamilifu hadi siku ya Kiama, na hakuna Mtume mwengine yoyote atakayekuja baada yake. Na hii ni kwa sababu akili inakubali kufuata kile kilicho bora na kikamilifu zaidi. Na vile vile Mtume wa mwisho ni yule ambaye ni m-bora zaidi kuliko wengine, kwa sababu Yeye ni mwenye kuchukua ujumbe wa dini iliyo kamilifu, na natija ya hayo ni kwamba dini ya kiislamu ni dini kamilifu zaidi, na Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni m-bora wa Mitume yote ya Mwenyeezi Mungu, kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani:-
هُوَ الَّذِى اَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَي وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلـٰي الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ[2]
Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini ya Haki ipate kushinda dini zote, ijapo kuwa washirikina watachukia.
4. MTUME (S.A.W.W) ANA CHEO CHA KUWA YUKO KARIBU ZAIDI NA MOLA WAKE.
Mtume Muhammad (s.a.w.w) amefikia cheo ambacho hakuna Mtume yoyote miongoni mwa Mitume ya Mwenyeezi Mungu aliyekifikia cheo hicho, wala hakuna Malaika yoyote miongoni mwa Malaika watukufu wa Mwenyeezi Mungu aliyeweza kukifikia cheo hicho, cheo hicho alichokifikia (s.a.w.w) ni kuwa Yeye yuko karibu sana na Mwenyeezi Mungu.
Mtume (s.a.w.w)amekifikia cheo hicho kwa sababu anastahiki kuwa nacho, kiasi ya kwamba anaweza kuona upeo wa mbingu iliyo juu kabisa,kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani:-
وَهُوَ بِالاُفُقِ الاَعْلَي[3]
Naye yuko juu kabisa upeo wa macho.
Utukufu wa moyo alionao Mtume Muhammad (s.a.w.w) umeleta athari kiasi ya kwamba amestahiki kupewa cheo hicho cha kuwa karibu zaidi na Mola wake, cheo ambacho - hata Malaika hawakunuafaika kuwa nacho – na kimemfanya Yeye (Mtume s.a.w.w) baadhi ya wakati anufaike kupokea Wahyi kutoka kwa Mola wake bila ya kupitia Malaika. Kama tunavyosoma ndani ya qur-ani:-
ثُمَّ دَنَا فَتَدَلَّي. فَكَانَ قَابَ قَوْسَيْنِ اَوْ اَدْنَي. فَاَوْحَي إِلَي عَبْدِهِ مَا اَوْحَي[4]
Kisha akakaribia na akateremka.
Akawa ni kama baina ya mipinde miwili, au karibu zaidi.
Akamfunulia mja wake (Mwenyezi Mungu) alicho mfunulia.
Aya hiyo inaonesha kuwa Mwenyeezi Mungu alimpa Mtume wake Wahyi kwa sababu yeye ndiye anayestahiki kupewa.
Vile vile ni lazima tuelewe kwamba Mwenyeezi Mungu ana uwezo wa kufanya kila analolitaka, na pale tuliposema kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ana upeo wa kuona mbingu ya juu kabisa, tusisahau kuwa utukufu wake huo pia unatokana na kudra na uwezo wake Allah (s.w). Kama alivyoonesha uwezo wake pale alipokihamisha kiti cha ufalme cha Malkia Saba kutoka Yemen hadi Palestina kwa muda wa kufumba macho na kufumbua, na kudra yake hiyo aliifanya kupitia katika mmoja wa viumbe vyake. Hebu zingatia Aya hii ya Qur-ani inavyosema:-
قَالَ الَّذِى عِندَهُ عِلْمٌ مِّنَ الْكِتَابِ اَنَا آتِيكَ بِهِ قَبْلَ اَن يَرْتَدَّ إِلَيْكَ طَرْفُكَ فَلَمَّا رَآهُ مُسْتَقِرّاً عِندَهُ قَالَ هَذَا مِن فَضْلِ رَبِّى لِيَبْلُوَنِى اَاَشْكُرُ اَمْ اَكْفُرُ وَمَن شَكَرَ فَإِنَّمَا يَشْكُرُ لِنَفْسِهِ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ رَبِّى غَنِيٌّ كَرِيمٌ[5]
Akasema mwenye ilimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea kabla ya kupepesa jicho lako. Basi alipo kiona kimewekwa mbele yake, akasema: Haya ni katika fadhila zake Mola wangu Mlezi, ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru. Na mwenye kushukuru, kwa hakika, anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake; na anaye kufuru, kwa hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi na Karimu.
Vile vile ni lazima tufahamu kuwa, tukisema kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w) ana upeo wa kuona mbingu sio kwamba Yeye ametoka katika ulimwengu wa kimada bali Yeye amefikia katika cheo hicho kwa sababu ya moyo wake uliotakasika na ndio akawa yuko karibu zaidi na Mwenyeezi Mungu, kama anavyosema Allah (s.w):-
مَا كَذَبَ الْفُؤَادُ مَا رَاَي[6]
Moyo haukusema uwongo uliyo yaona.
[1] Surat Ahzaab Aya ya 40
[2] Surat- Tawba Aya ya 33
[3] Surat Najm Aya ya 7
[4] Surat Najm Aya ya 8-10
[5] Surat Naml Aya ya 40
[6] Surat Najmi Aya ya 11
MWISHO