BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
IMEANDIKWA NA NDUGU ZETU WA KIISLAMU
SHARTI ZA KUFIKIA MJA KATIKA UKAMILIFU
Katika makala iliyopita tulielezea sharti na vizuizi vinavyomfanya mwanaadamu asifikie katika ukamilifu, na hii ni kwa sababu hakuweza kumfahamu Mola wake, katika makala hii tutaendelea kuelezea masharti na vizuizi vinavyomfanya mwanaadamu asiweze kufikia katika ukamilifu.
2) Maisha salama na viongozi waaminifu.
Ijapokuwa kumfahamu Mwenyeezi Mungu ni mahitajio ya nafsi yaliyomo ndani ya nyoyo za wanaadamu, na fitra hiyo inawiana na akili na dalili, lakini kukua kwa fitra hiyo na kudhihirika matumaini ya akili na ya kimoyo mwanaadamu anahitajia mazingira yaliyo salama ili aishi katika mfumo wa maisha ambao utamuongoza yeye kufikia katika njia ya saada.
Kwa hiyo jamii ambayo inatawaliwa au iko mikononi mwa hukuma za kitaluti, na hukuma hizo zinawalazimisha raia wake kuwatii na kufuata wanayoyaamrisha, raia hao hawatonufaika na neema za Mwenyeezi Mungu,na hawatoweza kumfahamu Allah (s.w). jamii kama hiyo itakuwa haina suluhu yoyote na raia wake watabadilika na kuwa watu mafasiki, kama tunavyosoma ndani ya qur-ani kuhusiana na Firauna:-
فَاسْتَخَفَّ قَوْمَهُ فَاَطَاعُوهُ إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْماً فَاسِقِينَ[1]
Basi aliwachezea watu wake, na wakamt'ii. Kwa hakika hao walikuwa watu wapotovu.
Kwa hiyo ikiwa mwanaadamu anaishi katika jamii ambayo inatawaliwa na hukuma za kitaluti, na tawala hiyo inapinga maamrisho ya Mwenyeezi Mungu, basi ni lazima ahame katika jamii hiyo au nchi hiyo, na kuishi katika nchi ambayo anaweza kuishi kwa kufuata maamrisho ya Mola wake, jamii ambayo anaweza kufanya ibada zake, kama anavyosema Mwenyeezi mungu:-
يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ اَرْضِى وَاسِعَةٌ فَإِيَّايَ فَاعْبُدُونِ[2]
Enyi waja wangu mlio amini! Kwa hakika ardhi yangu ina wasaa. Basi niabuduni Mimi peke yangu.
Na kwa sababu hiyo basi Malaika wa Mwenyeezi Mungu hawakubali dalili za wale ambao walipotoka kwa sababu ya tawala za kitaluti.
Na anawajibu watu hao kwa kusema:-
إِنَّ الَّذِينَ تَوَفَّاهُمُ الْمَلآئِكَةُ ظَالِمِى اَنْفُسِهِمْ قَالُواْ فِيمَ كُنتُمْ قَالُواْ كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِى الاَرْضِ قَالْوَاْ اَلَمْ تَكُنْ اَرْضُ اللهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُواْ فِيهَا فَاُوْلَـئِكَ مَاْوَاهُمْ جَهَنَّمُ وَسَاءتْ مَصِيراً[3]
Hakika Malaika watawaambia wale ambao wamewafisha nao wamejidhulumu nafsi zao: Mlikuwa vipi? Watasema: Tulikuwa tunaonewa. Watawaambia: Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa na wasaa wa kuhamia humo? Basi hao makaazi yao ni Jahannamu, nayo ni marejeo mabaya kabisa.
*Hapo zamani alipohama Mtume pamoja na Sahaba zake kwenda Madina, alilazimishwa kila aliye Muislamu asisalie katika mji wa ukafiri, aache mali zake na watoto wake na kila chake aende huko Madina, kwani hapo katika mji wa kikafiri hataweza kufanya amali za dini yake. Uislamu wake utakuwa vipi – hauna amali, na Uislamu ni amali – sio itikadi tupu.
Basi ndio wanalaumiwa hapa, na kuambiwa kuwa watakufa vibaya, ila wale ambao walikuwa hawana njia yoyote ya kuweza kuhama kwenda huko Madina.
Na hao pia wamo hatarini, kwani labda wanaonekana kwa dhahiri tu kuwa hawawezi, na ikitazamwa kweli itaonekana kuwa wanaweza, basi na wao wamo hatarini pia.
Wengine hao waliosalia Makka, walitolewa na makafiri, kwenda katika vita vya badri kumpiga Mtume, wakenda na nia yao wasimpige Mwislamu, lakini haukukubaliwa kwao huo kuwa udhuru.
[1] Surat zukhruf Aya ya 54
[2] Surat ankabuut Aya ya 56
[3] Surat Nisaa aya ya 97
MWISHO