BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
NI WATU WA AINA GANI AMBAO HAWAPASWI KUTIIWA?
Mwenyeezi Mungu Mtukufu ili kuzuia dhulma na kuleta uadilifu katika jamii ametukataza kuwatii baadhi ya watu, na vile vile ametukataza tusiwachague watu madhalimu kutuongoza. Miongoni mwa watu hao ni kama hawa wafuatao:-
1- Watu wanaofanya israfu na kuleta ufisadi katika jamii.
Yaani ni wale watu ambao hufanya kila wawezalo kuleta ufidasi katika jamii, na hutumia mali za baytul-mali katika mahitajio yao binafsi au kwa wale walio karibu nao. Na hufanya israfu katika mali za baytul-mali kuwanyima watu haki zao, na kwa sababu hiyo basi Allah (s.w)anasema:-
وَلاَ تُطِيعُوا اَمْرَ الْمُسْرِفِين الَّذِينَ يُفْسِدُونَ فِى الاَرْضِ وَلاَ يُصْلِحُونَ[1]
Wala msit'ii amri za walio pindukia mipaka,Ambao wanafanya ufisadi katika nchi, wala hawatengenezi.
2- Wale wanaofanya maovu
Yaani ni wale ambao wanazipinga amri za Mwenyeezi Mungu, na hufanya maasi baada ya kumshukuru Mwenyeezi Mungu kwa neema alizowapa, na watu kama hao huidhalilisha na kuididimiza jamii, na kwa sababu hiyo basi katika Qur-ani tunasoma:-
فَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ وَلاَ تُطِعْ مِنْهُمْ آثِماً اَوْ كَفُوراً[2]
Basi ngojea hukumu ya Mola wako Mlezi wala usimt'ii miongoni mwao mwenye dhambi au mwenye kufuru.
3 - Walioghafilika kutokana na anasa za dunia.
Yaani ni wale ambao wamemsahau Mwenyeezi Mungu na akhera, na wameghafilika na mali za dunia, nuru ya akili na fitra imezima ndani ya nyoyo za watu hao, na wako mbali na rehema za Mwenyeezi mungu kwa sababu ya kufuata matamanio ya nafsi zao. Kama anavyosema Allah(s.w):-
وَاصْبِرْ نَفْسَكَ مَعَ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ وَلاَ تَعْدُ عَيْنَاكَ عَنْهُمْ تُرِيدُ زِينَةَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَلاَ تُطِعْ مَنْ اَغْفَلْنَا قَلْبَهُ عَن ذِكْرِنَا وَاتَّبَعَ هَوَاهُ وَكَانَ اَمْرُهُ فُرُطا[3]
Na isubirishe nafsi yako pamoja na wanao muomba Mola wao Mlezi asubuhi na jioni, hali ya kuwa wanataka radhi yake. Wala macho yako yasiwaruke kwa kutaka pambo la maisha ya dunia. Wala usimt'ii tuliye mghafilisha moyo wake asitukumbuke, na akafuata matamanio yake yakawa yamepita mpaka.
*Wakubwa wa Kikureishi waliokuwa makafiri walimwambia Mtume “ukitaka tukufuate basi wafukuze hao masikini waliokufuata”.
4- Wale waongo na wanaowalaghai watu.
Yaani ni wale ambao kwa ajili ya kuhifadhi manufaa yao ya kibinafsi huikadhibisha na kuipinga haki kwa wepesi kabisa, na wanapodai kuwa wanakubaliana na wale wenye dini hawana madhumuni mengine isipokuwa kuwalaghai kisiasa watu hao wenye dini. Na kwa sababu hiyo basi Allah (s.w) anasema:-
فَلاَ تُطِعِ الْمُكَذِّبِينَ وَدُّوا لَوْ تُدْهِنُ فَيُدْهِنُونَ[4]
Basi usiwat'ii wanao kadhibisha.
Wanatamani lau unge lainisha ili nao wakulainishie.
* Zinatajwa baadhi ya sifa za watu wabaya, ambazo inataka mtu ajiepushe nazo, na anaambiwa mtu asikubali kufanya unafiki katika dini,akabania haki, eleza haki tu kila mtu aisikiye.
[1] Surat Shuaraa Aya ya 151-152
[2] Surat-Dahr Aya ya 24
[3] Suratul-kahf Aya ya 28
[4] Surat Qalam aya ya 8-9
MWISHO