BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
MTAZAMO WA ALLAH (S.W) KWA WAJA WAKE
Mtume (s.a.w.w) anasema:-
“Mwenyeezi Mungu hatazami sura zenu wala mali yenu lakini anatazama amali zenu”, tazama aya ya 80 ya sura hii.
وَقَالُواْ لَن تَمَسَّنَا النَّارُ إِلاَّ اَيَّاماً مَّعْدُودَةً قُلْ اَتَّخَذْتُمْ عِندَ اللهِ عَهْداً فَلَن يُخْلِفَ اللّهُ عَهْدَهُ اَمْ تَقُولُونَ عَلـٰي اللهِ مَا لاَ تَعْلَمُونَ[1]
Na walisema: Hautatugusa Moto ila kwa siku chache tu. Sema: Mmechukua ahadi kwa Mwenyezi Mungu? Kweli Mwenyezi Mungu hatokwenda kinyume na ahadi yake. Au mnamsingizia Mwenyezi Mungu mambo msiyo yajua?
*Mayahudi kwa kujitapa kuwa ni watukufu, kwa kule kunasibikana kwao na Mitume, walikuwa wakidai kuwa hawataadhibiwa ila siku arobaini tu ambazo wazee wao waliabudu ndama, Mwenyeezi Mungu anawakadhibisha kwa Aya hizi kwamba, yoyote atakayefanya maovu ataadhibiwa kwa maovu yake, na hapana litakalomnusuru mtu ila imani na amali njema.
Basi wananasihiwa wale wanaojigamba kwa sababu na kuona kuwa nasabu zao zitawatosha mbele ya Mwenyeezi Mungu. Mungu ameyakataa haya katika mahala pengi katika Qur-ani, pamoja katika humo ni Aya ya 101 ya suratul-Muuminuun, na Mtume ameyakataa katika hadithi nyingi.
فَإِذَا نُفِخَ فِى الصُّورِ فَلاَ اَنسَابَ بَيْنَهُمْ يَوْمَئِذٍ وَلاَ يَتَسَاءلُونَ[2]
Basi litapo pulizwa baragumu hapo hautakuwapo ujamaa baina yao siku hiyo,
wala hawataulizana.
* Haya ndiyo yale yanayokaririwa ndani ya Qur-ani, na hadithi za Mtume kuwa nasabu haifai kitu huko Akhera, hakuna ya kweli zaidi kuliko ya Mwenyeezi Mungu, nayo ni haya, basi watu nawaseme uwongo wao, khiyari zao yatawafika wenyewe. “mtumaini cha ndugu hufa ali masikini”.
Hayo yalikuwa ni maelezo kufupi kuhusiana na Aya hizo tukufu, tukiendelea na mada yetu:-
Vile vile Nabii Mussa (a.s) alimuomba Mola wake na kumwambia:-
وَاجْعَل لِّى وَزِيراً مِّنْ اَهْلِي[3]
Na nipe waziri katika watu wangu.
Na Mwenyeezi Mungu akawakubalia maombi yao, na kuwaambia:-
قَالَ قَدْ اُوتِيتَ سُؤْلَكَ يَا مُوسَي[4]
Akasema: Hakika Umepewa maombi yako, ewe Musa!
Na vile vile tunasoma katika Qur-ani kuhusiana na Nabii Ibrahimu (a.s):-
الْحَمْدُ للهِ الَّذِى وَهَبَ لِى عَلـٰي الْكِبَرِ إِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ إِنَّ رَبِّى لَسَمِيعُ الدُّعَاء[5]
Alhamdulillahi! Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu aliye nipa juu ya uzee wangu Ismail na Is-haq. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kusikia maombi.
Mwenyeezi Mungu amewapa ukhalifa watu katika kizazi cha Mitume, au wale waliokuwa katika mikono ya Mitume, kwa sababu watu kama hao ndio wanaostahiki kuiendeleza njia hiyo tukufu walioiacha Mitume hiyo, na vile vile watu hao ndio wanaoweza kuihifadhi dini ya Mwenyeezi Mungu. kama anavyosema Nabii Zakariyya (a.s):-
وَإِنِّى خِفْتُ الْمَوَالِيَ مِن وَرَائِى وَكَانَتِ امْرَاَتِى عَاقِراً فَهَبْ لِى مِن لَّدُنكَ وَلِيّاً . يَرِثُنِى وَيَرِثُ مِنْ آلِ يَعْقُوبَ وَاجْعَلْهُ رَبِّ رَضِيّاً[6]
Na hakika mimi nawakhofia jamaa zangu baada yangu. Na mke wangu ni tasa. Basi nipe mrithi kutoka kwako.
Atakaye nirithi mimi na awarithi ukoo wa Yaaqub. Ewe Mola wangu Mlezi! Na umjaalie awe mwenye kuridhisha.
*Nabii Zakariyya (a.s) anamuomba Mola wake, amruzuku mtoto mwema na kuja kushika kazi yake atakapoondoka yeye,, na hapa pana mafundisho ya kuwa mtu akiomba mtoto anatakiwa aombe mtoto mwema, sio kuomba mtoto mwanamme, au mwanamke tu, kama wanavyofanya watu wengine, na vile vile tunapoomba tuombe kilicho chema.
[1] Suratul-Albaqarah Aya ya 80
[2] Suratul-Muuminuun Aya ya 101
[3] Surat Taha Aya ya 29
[4] Surat Taha Aya ya 36
[5] Surat Ibrahim Aya ya 39
[6] Surat Maryam Aya ya 5-6
MWISHO