MWANAMKE NDANI YA QUR_ANI
  • Kichwa: MWANAMKE NDANI YA QUR_ANI
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 3:21:16 2-9-1403

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

MWANAMKE NDANI YA QUR_ANI

MISINGI NA KANUNI ZA MAANDALIZI ZISIZOEPUKIKA

Kabla ya kuingia katika uchambuzi wa mambo yanayomuhusu mwanamke, na kujibu masuali na mishikeli hatuna budi kwanza tutaje misingi na kanunu ambazo ni muhimu katika kila utafiti unaomuhusu mwanamke kisheria.

Msingi wa kwanza: Ubinadamu kwa mwanamme na mwanamke, hakika ya wawili hao wameumbwa kwa asili, na nafsi moja kama isemavyo Qur’an:

هُوَ الَّذِى خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَجَعَلَ مِنْهَا زَوْجَهَا لِيَسْكُنَ إِلَيْهَا فَلَمَّا تَغَشَّاهَا حَمَلَتْ حَمْلاً خَفِيفاً فَمَرَّتْ بِهِ فَلَمَّا اَثْقَلَت دَّعَوَا اللّهَ رَبَّهُمَا لَئِنْ آتَيْتَنَا صَالِحاً لَّنَكُونَنَّ مِنَ الشَّاكِرِينَ

''Enyi watu! Mcheni mola wenu ambaye amekuumbeni kutokana na nafsi moja,na akaumba kutokana na (nafsi) hiyo wa pili wake, na akaeneza kwa wawili hao wanaume wengi na wanawake.''

Nafsi moja inamaanisha nafsi ya Adam (a.s) na pia kwa maana hii imeelezwa katika surat Al-a’araf (189).

Msingi wa pili: Ni haja ya kila mmoja anavyomuhitajia mwenzake na kuwa mkamilishaji wake, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

هُنَّ لِبَاسٌ لَّكُمْ وَاَنتُمْ لِبَاسٌ لَّهُنَّ  

  “Wao ni vazi lenu na nyinyi ni vazi lao ” (Al-baqarah :187).

Hivyo utafiti kuhusu mwanamke na haki zake hautofautiani na ule unaomuhusu mwanamme.

Msingi wa tatu: Ni msingi wa familia ambao ndio msingi wa mwanzo katika jamii.  Tukiangalia katika  mchakato wa maslahi binafsi, jamii au familia, hapana shaka kwamba hutangulizwa maslahi ya familia mfano. Itakapokinzana kazi ya mwanamke ya nje ya nyumba yake (kazi inayompatia  maslahi binafsi au hata ya jamii), na ulezi wa watoto wake pamoja na uendeshaji wa mambo ya nyumbani kwake, hapo anapaswa kutanguliza ulezi wa watoto pamoja na uendeshaji wa nyumba kwa sababu ndio jiwe la msingi katika jengo la jamii ya kiislam.

Msingi wa nne: Dunia  kuwa ni nyumba ya kupita na Akhera kuwa ni nyumba ya kudumu, ilihali Uislamu unamtakia mtu mafanikio katika zote nyumba mbili, mafanikio ambayo hayawezi kupatikana ispokua kwa kuyafuata kikamilifu mafunzo sahihi ya kiislam, kutoa haki zinazohusika na kusimamia majukumu ya kidini.

Na hivyo kutengenea kwa familia na  kustawi  kwake kunategemea utendaji na utekelezaji wa wajibu, sunna na tabia njema. 

Misingi na ustaarabu wa kiislam, kwa sababu hiyo utafiti kuhusu  haki za mwanamke katika familia na jamii unalazimika uwe unawiana na msingi huu, kwa lengo la kumuhakikishia mwanamke mafanikio yake ya kweli duniani na akhera.

Msingi wa tano: Ni uwadilifu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu ambao kimaumbile au kisheria ndio chanzo cha huu ulimwengu, kwa maana ulimwengu umesimama juu ya msingi wa uadilifu wa kiungu, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

إِنَّ اللّهَ يَاْمُرُ بِالْعَدْلِ وَالإِحْسَانِ وَإِيتَاء ذِى الْقُرْبَي وَيَنْهَي عَنِ الْفَحْشَاء وَالْمُنكَرِ وَالْبَغْيِ يَعِظُكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ

“Kwa hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha uadilifu na ihsani…” (Annahal:90).

Hivyo tafiti zote zinazowahusu mwanamme na mwanamke zinapaswa ziegemee msingi huu, kwa maana uadilifu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndio unaoyahukumu mambo yote ya mwanadamu na kuweka usawa baina yao kwa kuzingatia vyema maslahi ya kila upande.

Msingi wa sita: Ni tofauti za kimaumbile zisizoepukika baina ya wawili hawa, na hivyo ni kwa mujibu  wa hikma ya kiungu, mwanamme kuwa mwanamme na mwanamke kuwa mwanamke.

Na huo ndio mwanzo wa ukamilifu na kielelezo cha haja za kubadilishana, pia ndio sababu ya kubakia kwa uhai wa mwanadamu kijamii.

hivyo kila anae nadi wito wa usawa katika chombo chochote au hali yoyote bila kuzingatia tofauti hii ya kimaumbile, kwa hakika atakuwa amenadi wito uliovurugika usio wa kimantiki wala kiutekelezaji.

Msingi wa saba: Ni lengo la kumfikisha mwanamke katika kilele cha ukamilifu wake wa kibinadamu na  haki zake za kisheria ili aweze kusimamia nafasi yake aliyopewa.

Kinyume na lengo la Wamagharibi la kumshindanisha na mwanamme, na ili kulifikia lengo hili salama na endelevu ni muhimu kusisitiza yafuatayo katika utafiti wa masuala yanayowahusu wanawake:

- Kubainisha mtazamo wa Kiialamu kuhusu haki za mwanamme na mwanamke

-Kurekebisha kanuni zinazomuhusu mwanamke  kwa upande wa haki na tabia.

-Kumlea mwanamke na kumuelimisha, ili afahamu haki zake na nafasi yake katika jamii na familia.

-Kutilia maanani hijabu (utakatifu halisi wa kiroho kwa mwanamke) kwamba ni nguzo ya msingi katika utafiti huu.

Hivyo kwa kila utafiti na harakati za kumjenga  na kumboresha mwanamke ni lazima kuzingatiwa  ipasavyo misingi hii.

MWISHO