BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
SIFA WANAZOTAKIWA MAKHALIFA KUWA NAZO
2- UADILIFU
katika maelezo yaliyopita tulielezea kuhusu sifa wanazotakiwa Mitume kuwa nazo, na tukaelewa kuwa moja katika sifa hizo ni elimu, tukiendelea kuelezea sifa nyengine, sifa ya pili wanayotakiwa Mitume kuwa nayo ni uadilifu, Mitume wanatakiwa pindi wanapotoa hukumu za kiislamu, au wanapomhukumu mtu wasihukumu kutokana na yale wanayoyapenda katika nafsi zao, yaani wasihukumu kutokana na matamanio yao ya kibinafsi, bali wahukumu kutokana na yale ambayo Mola wao amewaamrisha, na wala wasihukumu kwa kutegemea vyeo vyao binafsi au kutokana na sehemu waliyonayo katika jamii, bali wahukumu kwa kutegemea ridhaa ya Mola wao. na ikiwa hawatafanya hivyo basi watakuwa hawastahiki kuwa viongozi katika jamii. kama anavyosema Allah (s.w):-
وَإِذِ ابْتَلَي إِبْرَاهِيمَ رَبُّهُ بِكَلِمَاتٍ فَاَتَمَّهُنَّ قَالَ إِنِّى جَاعِلُكَ لِلنَّاسِ إِمَاماً قَالَ وَمِن ذُرِّيَّتِى قَالَ لاَ يَنَالُ عَهْدِى الظَّالِمِينَ[1]
Na kumbukeni khabari hii: Mola wake alipomfanyia mtihani (Nabii ) Ibrahimu kwa amri nyingi; naye akazitimiza, akamwambia " hakika mimi nitakufanya kiongozi cha watu (wote)." Ibrahimu akasema:-
" je, na katika kizazi changu pia?" Akasema " (Ndio lakini) ahadi yangu haitawafikia (waovu) madhalimu wa nafsi zao". (itawafika walio wazuri).
*Nabii Ibrahimu alipofanyiwa mitihani yote ya amri za Mwenyeezi Mungu na makatazo yake na ya mambo mengine, na akafuzu, Mwenyeezi Mungu alimwambia kuwa kampa daraja ya Uimamu juu ya viumbe. Nabii ibrahimu alifurahi akashukuru na akamuomba kuwa na katika kizazi chake wapewe Uimamu pia, Mwenyeezi Mungu akamwambia kuwa nasaba tupu ya kunasibika naye (Nabii ibrahimu) haitakuwa sababu ya kuwapatia Uimamu - sharti wafanye amali nzuri - . Na yote haya ni kufundishwa na sisi pia kuwa tusitegemee nasabu zetu, siyo nguzo ya kuegemea, nguzo ya kuegemea ni amali njema zinazofanywa kwa nia njema. Mtume akasema: " Mwenyeezi Mungu hatazami sura zenu wala mali yenu lakini anatazama nyoyo zenu na amali zenu." tazama Aya ya 80 ya sura hii hii.
وَقَالُواْ لَن تَمَسَّنَا النَّارُ إِلاَّ اَيَّاماً مَّعْدُودَةً قُلْ اَتَّخَذْتُمْ عِندَ اللهِ عَهْداً فَلَن يُخْلِفَ اللّهُ عَهْدَهُ اَمْ تَقُولُونَ عَلـٰي اللهِ مَا لاَ تَعْلَمُونَ[2]
Na walisema: Hautatugusa Moto ila kwa siku chache tu. Sema: Mmechukua ahadi kwa Mwenyezi Mungu? Kweli Mwenyezi Mungu hatokwenda kinyume na ahadi yake. Au mnamsingizia Mwenyezi Mungu mambo msiyo yajua?
* *Mayahudi kwa kujitapa kuwa ni watukufu, kwa kule kunasibika kwao na Mitume, walikuwa wakidai kuwa hawataadhibiwa ila siku arobaini tu, ambazo wazee wao waliabudu ndama,Mwenyeezi Mungu Anawakadhibisha kwa aya hizi kwamba: yoyote atakayefanya maovu, ataadhibiwa kwa maovu yake, na hapana litakalomnusuru mtu ila imani na amali njema. Basi tunawanasihi wale wanaojigamba kwa nasabu na kuona kuwa nasabu zao zitawatosha mbele ya Mwenyeezi Mungu, Mungu ameyakataa haya katika sehemu nyingi ndani ya Qur-ani, mfano aya ya 101 ya Suratul Muuminun,
فَإِذَا نُفِخَ فِى الصُّورِ فَلاَ اَنسَابَ بَيْنَهُمْ يَوْمَئِذٍ وَلاَ يَتَسَاءلُونَ[3]
Basi litapo pulizwa baragumu hapo hautakuwapo ujamaa baina yao siku hiyo, wala hawataulizana. Vile vile na Mtume ameyakataa kwa hadithi nyingi.
*Haya ndiyo yale yale yanayokaririwa katika Qur-ani, na hadithi za Mtume kuwa nasabu haifai kitu huko Akhera, hakuna ya kweli zaidi kuliko ya Mwenyeezi Mungu, nayo ni haya, basi watu nawaseme uwongo wao, khiari zao yatawafika wenyewe, “Mtumaini cha ndugu hufa masikini” Janatu Naimu Filjinani Jini na Insi Waitamani.
Jumla ya watu Hawaioni Ila kwa amali kutaqadama
Thamani ya pepo Ukiitaka Dhiki moyo wako kutozunguka
Thubutisha taa Yake Rabbuka Ili akujazi Majazi mema.
Hayo yalikuwa ni maelezo kwa ufupi kuhusiana na Aya hiyo ya 124, tukiendelea na mada yetu; waislamu wote wanaelewa kuwa baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) mtu M-bora aliyekuwa muadilifu katika kuwagaia watu mali za Baytul mali, au kuhukumu kwa kuzingatia hukumu za kiislamu katika yale ambayo Mola ameamrisha, au hata katika ubora wa kuiongoza jamii ya Kiislamu katika zama zile, sio mwengine isipokuwa ni Imamu Ali (a.s), kama tunavyosoma katika kitabu chake cha Nahjulbalagha:-
و الله لو اعطیت الاقالیم السبعة بما تحت أفلاکها علی أن أعصی الله فی نملة أسلبها جلب شعیرة ما فعلته[4]
Naapa kwa jina la Mola wangu, ikiwa mtanipa mali zote zilizomo katika mbingu na ardhi au zaidi ili nimnyime sisimizi hata kwa chembe aliyoibeba, ili nipinge amri za Mola wangu, nawahakikishia kuwa sitofanya hivyo.
[1] Suratul-Baqarah Aya ya 124
[2] Suratul-Baqarah Aya ya 80
[3] Suratul-Muuminun Aya ya 101
[4] Nahjulbalagha , subh Saalih,خ 224. na Nahjulbalagha feydh خ 215
MWISHO