BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
FAIDA ZA KUIKUMBUKA SIKU YA KIAMA NO.3.
Kauli muhimu za Mitume ya Mwenyeezi Mungu ni kuwalingania watu kuamini Mola mmoja na kuwakumbusha maisha baada ya mauti. Jitihada kubwa walizozifanya Mitume baada ya kuwalingania watu kuabudu Mola mmoja ni kuihuisha Siku ya Kiama katika nyoyo za watu.
katika makala iliyopita tulielezea kuhusu baadhi ya faida za kuikumbuka siku ya Kiama, katika makala hii tutaendelea kuelezea faida nyengine.
6. Kufanya jitihada katika kufanya ibada na matendo ya kheri.
Waumini wanapofanya ibada na mambo ya kheri hawategemei malipo katika ulimwengu wa Kimada, bali hufanya ibada hizo kwa sababu wana imani ya kuwepo siku ya Qiyamah, na watu Waumini hufanya jitihada zao zote ili kubaki kuwa thabiti katika itikadi yao. Na hutegemea mafanikio yao kutoka kwa Mola wao. Mola ambaye amewaahidi kuwalipa malipo yenye kheri nyingi na baraka, na malipo hayo ni bora zaidi kwa ajili ya siku ya Qiyamah. Mwenyeezi Mungu Mtukufu anawaambia watu hao :-
اُوْلَئِكَ يُسَارِعُونَ فِى الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ[1]
Basi wote hao ndio wanao kimbilia katika mambo ya kheri, na ndio watakao tangulia kuyafikia.
Kwa maelezo zaidi, katika kipengele hiki tutaashiria baadhi ya matendo ya kheri ya watu hao.
A. Kuwapa msaada watu wanyonge.
Waumini kwa sababu wana imani ya kuwepo siku ya Qiyamah, husamehe hata chakula wanachokihitaji na kuwapa wanyonge, kama tunavyosoma kuhusiana na watu wa nyumba ya Mtume Muhammad (s.a.w.w).
وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلـٰي حُبِّهِ مِسْكِيناً وَيَتِيماً وَاَسِيراً. إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللهِ لاَ نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَاء وَلاَ شُكُوراً. إِنَّا نَخَافُ مِن رَّبِّنَا يَوْماً عَبُوساً قَمْطَرِيراً[2]
Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa.
Hakika sisi tunakulisheni kwa wajihi wa Mwenyezi Mungu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani.
Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu Mlezi hiyo siku yenye shida na taabu.
B. Kuwapa wanyonge wanavyo hitaji kwa siri.
Watu ambao wanapenda anasa za dunia, na wana sehemu fulani katika jamii huwasaidia wanyonge na kuwapa mali zao au vile wanavyovihitaji kwa ria, Na wakati wanapotoa mali zao, hutoa kwa kujifakharisha na kujionesha.
Ama wale watu ambao wana imani ya kuwepo siku ya Qiyama hutoa walivyonavyo na kuwapa wanyonge kwa siri au kwa dhahiri bila ya riya, kwa sababu wana imani kuwa kila walichonacho ni kutoka kwake Allah (s.w). kama tunavyosoma ndani ya qur-ani:-
إِنَّ الَّذِينَ يَتْلُونَ كِتَابَ اللهِ وَاَقَامُوا الصَّلاَةَ وَاَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرّاً وَعَلاَنِيَةً يَرْجُونَ تِجَارَةً لَّن تَبُورَ. لِيُوَفِّيَهُمْ اُجُورَهُمْ وَيَزِيدَهُم مِّن فَضْلِهِ إِنَّهُ غَفُورٌ شَكُورٌ[3]
Hakika wale wanao soma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakashika Sala, na wakatoa kwa siri na kwa dhaahiri katika tulivyo waruzuku, hao hutaraji biashara isiyo bwaga.
Ili Yeye awalipe ujira wao kwa ukamilifu, na awazidishie kutokana na fadhila zake. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye shukrani.
[1] Suratul-Muuminuun Aya ya 61.
[2] Surat-dahr Aya ya 8-10.
[3] Surat Faatir Aya ya 29-30
MWISHO