BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
MABASHIRIO YA THAWABU DUNIANI NA AKHERA.
6. Fungamano na uhusiano wa mabashirio ya thawabu duniani na Akhera.
Starehe na madhila ya Waumini duniani kwao wao ni sawa, kwa sababu hunufaika na starehe za duniani kwa neema za Mola wao, na hunufaika na mashaka ya
duniani kwa kukumbuka mabashirio ya Mola wao, kwa sababu nyoyo zao hutulia pale wanapokumbuka mabashirio ya Mwenyeezi Mungu ambayo huwaondolea
hofu, na nyoyo zao hufurahika wanapokumbuka ujira wa Mola wao. Kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani:-
لَهُمُ الْبُشْرَي فِى الْحَياةِ الدُّنْيَا وَفِى الآخِرَةِ لاَ تَبْدِيلَ لِكَلِمَاتِ اللهِ ذٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ[1]
Wao wana bishara njema katika maisha ya dunia na katika Akhera. Hapana mabadiliko katika maneno ya Mwenyezi Mungu. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
*Vile vile wale watu ambao wanapigana jihadi kwa ajili ya Mwenyeezi Mungu, na wakawa thabiti katika kukabiliana na Makafiri, basi Mwenyeezi Mungu
Muweza atawanufaisha watu hao kwa kuwapa neema za ushindi na uhuru duniani, na siku ya Kiama atawaandalia ujira mkubwa wa pepo.
Katika Qur-ani tunasoma:-
فَآتَاهُمُ اللّهُ ثَوَابَ الدُّنْيَا وَحُسْنَ ثَوَابِ الآخِرَةِ وَاللّهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ[2]
Basi Mwenyezi Mungu akawapa malipo ya duniani na bora ya malipo ya Akhera. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao mema.
Kwa hiyo, kutokana na maelezo hayo tumefahamu kuwa kuna uhusiano na fungamano baina ya utukufu, heshima, na uhakika wa bishara ya thawabu katika dunia
na Akhera, na inapatikana kwa kumuamini Mola Muwezi. Kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani Majiyd.
مَّن كَانَ يُرِيدُ ثَوَابَ الدُّنْيَا فَعِندَ اللهِ ثَوَابُ الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ وَكَانَ اللّهُ سَمِيعاً بَصِيرا[3]ً
*Anaye taka malipo ya dunia, basi kwa Mwenyezi Mungu yapo malipo ya dunia na Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona.
7. Fungamano la viongozi, duniani na Akhera.
Viongozi wa jamii ni dalili bora na muhimu inayoonyesha uongofu na upotofu wa wanaadamu, kama inavyoeleweka kuwa mema na mazuri yote yanaonekana na
kuthibitika kwa kuwafuata Maimamu wanaoitabua haki, na mabya na maovu yote yana uhusiano na Maimamu wanaofanya maovu na ukafiri. Kuna aina mbali
mbali za watu katika dunia, aina hizo za watu ni kutokana na mapendeleo yao ya kiitikadi, na vigezo vya amali zao vitashuhudiwa kutoka kwa viongozi wao wa
haki au wa kibatili, siku ya Kiama kutadhihirika fungamano la uwalii wa viongozi wema, na upotofu wa viongozi waovu, basi kila mmoja atavutwa ili amtafute
kiongozi wake. Kama anavyosema Allah (s.w).
يَوْمَ نَدْعُو كُلَّ اُنَاسٍ بِإِمَامِهِمْ فَمَنْ اُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَاُوْلَـئِكَ يَقْرَؤُونَ كِتَابَهُمْ وَلاَ يُظْلَمُونَ فَتِيلاً[4]
Siku tutapo waita kila kikundi cha watu kwa mujibu wa wakifuatacho - basi atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, basi hao watasoma kitabu
chao wala hawatadhulumiwa hata chembe.
Siku ya Kiama viongozi waovu walio batili wataelekea motoni pamoja na wafuasi wao, kama tunavyosoma kuhusiana na Firauna:-
يَقْدُمُ قَوْمَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَاَوْرَدَهُمُ النَّارَ وَبِئْسَ الْوِرْدُ الْمَوْرُود[5]ُ
Siku ya Kiyama atawatangulia watu wake na atawaingiza Motoni. Na muingio muovu ulioje huo!
Na Waumini pia wakiwa pamoja na Mitume na Maimamu wa haki wataelekea Peponi, na siku ya Kiama wataokoka na adhabu kali iumizayo, kama tunavyosoma
ndani ya Qur-ani:-
يَا اَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَي اللهِ تَوْبَةً نَّصُوحاً عَسَي رَبُّكُمْ اَن يُكَفِّرَ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيُدْخِلَكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا الاَنْهَارُ يَوْمَ لاَ يُخْزِى اللهُ النَّبِيَّ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ نُورُهُمْ يَسْعَي بَيْنَ اَيْدِيهِمْ وَبِاَيْمَانِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اَتْمِمْ لَنَا نُورَنَا وَاغْفِرْ لَنَا إِنَّكَ عَلـٰي كُلِّ شَيْءٍ قَدِير[6]ٌ
Enyi mlio amini! Tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba iliyo ya kweli! Asaa Mola wenu Mlezi akakufutieni maovu yenu na akakuingizeni katika Pepo zipitazo mito
kati yake, siku ambayo Mwenyezi Mungu hatamdhalilisha Nabii na walio amini pamoja naye. Nuru yao inakwenda mbele yao na pande zao za kulia, na huku
wanasema: Mola wetu Mlezi! Tutimilizie nuru yetu, na utughufirie! Hakika Wewe ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
[1] Surat Yunus Aya ya 64.
[2] Surat Al-Imrani Aya ya 148.
[3] Suratun Nisaa Aya ya 134.
[4] Surat Israa Aya ya 71
[5] Surat Hud Aya ya 98
[6] Surat Tahriym Aya ya 8.
MWISHO