BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
FUNGAMANO LA VIONGOZI DUNIANI NA AKHERA.
7. Fungamano la viongozi, duniani na Akhera.
Viongozi wa jamii ni dalili bora na muhimu inayoonyesha uongofu na upotofu wa wanaadamu, kama inavyoeleweka kuwa mema na mazuri yote yanaonekana na kuthibitika kwa kuwafuata Maimamu wanaoitabua haki, na mabya na maovu yote yana uhusiano na Maimamu wanaofanya maovu na ukafiri. Kuna aina mbali mbali za watu katika dunia, aina hizo za watu ni kutokana na mapendeleo yao ya kiitikadi, na vigezo vya amali zao vitashuhudiwa kutoka kwa viongozi wao wa haki au wa kibatili, siku ya Kiama kutadhihirika fungamano la uwalii wa viongozi wema, na upotofu wa viongozi waovu, basi kila mmoja atavutwa ili amtafute kiongozi wake. Kama anavyosema Allah (s.w).
يَوْمَ نَدْعُو كُلَّ اُنَاسٍ بِإِمَامِهِمْ فَمَنْ اُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَاُوْلَـئِكَ يَقْرَؤُونَ كِتَابَهُمْ وَلاَ يُظْلَمُونَ فَتِيلاً[1]
Siku tutapo waita kila kikundi cha watu kwa mujibu wa wakifuatacho - basi atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, basi hao watasoma kitabu chao wala hawatadhulumiwa hata chembe.
Siku ya Kiama viongozi waovu walio batili wataelekea motoni pamoja na wafuasi wao, kama tunavyosoma kuhusiana na Firauna:-
يَقْدُمُ قَوْمَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَاَوْرَدَهُمُ النَّارَ وَبِئْسَ الْوِرْدُ الْمَوْرُود[2]ُ
Siku ya Kiyama atawatangulia watu wake na atawaingiza Motoni. Na muingio muovu ulioje huo!
Na Waumini pia wakiwa pamoja na Mitume na Maimamu wa haki wataelekea Peponi, na siku ya Kiama wataokoka na adhabu kali iumizayo, kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani:-
يَا اَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَي اللهِ تَوْبَةً نَّصُوحاً عَسَي رَبُّكُمْ اَن يُكَفِّرَ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيُدْخِلَكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا الاَنْهَارُ يَوْمَ لاَ يُخْزِى اللهُ النَّبِيَّ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ نُورُهُمْ يَسْعَي بَيْنَ اَيْدِيهِمْ وَبِاَيْمَانِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اَتْمِمْ لَنَا نُورَنَا وَاغْفِرْ لَنَا إِنَّكَ عَلـٰي كُلِّ شَيْءٍ قَدِير[3]ٌ
Enyi mlio amini! Tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba iliyo ya kweli! Asaa Mola wenu Mlezi akakufutieni maovu yenu na akakuingizeni katika Pepo zipitazo mito kati yake, siku ambayo Mwenyezi Mungu hatamdhalilisha Nabii na walio amini pamoja naye. Nuru yao inakwenda mbele yao na pande zao za kulia, na huku wanasema: Mola wetu Mlezi! Tutimilizie nuru yetu, na utughufirie! Hakika Wewe ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
Maelezo kwa ufupi ya makala zilizopita.
* Kila mwanaadamu hujijengea nafasi yake ya motoni au Peponi kulingana na matendo yake aliyoyafanya ulimwenguni, kwa hiyo, wanaadamu wote hujijengea Pepo au Moto hali wakiwa duniani, lakini kwa hakika siku ya Kiama watashuhudia Pepo na moto huo.
* Kuishi duniani kwa kuitakasa nafsi na maovu, ni alama inayoonesha amani na salama ya mwanaadamu siku ya Kiama, na kuishi duniani kwa kutenda maovu na kumuasi allah (s.w) ni alama inayoonesha tabu na adhabu ya mwanaadamu ya siku ya Kiama.
* Kutomkumbuka Mwenyeezi Mungu kwa utakaso duniani, husababisha tabu na mashaka katika maisha ya duniani na kutopata kheri yoyote siku ya Kiama.
* Kuwa mbali na njia njema (iliyonyooka) ya Mwenyeezi Mungu husababisha hasara na laana za duniani na Akhera, na kuwa katika harakati za kufuata njia njema katika maisha ya duniani husababisha kheri na baraka siku ya Kiama.
* Siku ya Kiama kila mtu atafufuliwa na kuwekwa pamoja na yule aliyekuwa akimfuata, ikiwa alikuwa akimfuata Mtume (s.a.w.w) kwa kufuata maamrisho yakena makatazo yake, basi siku ya Kiama atakuwa pamoja na Mtukufu huyo, na ikiwa alimfuata mtu aliyekuwa akidhulumu waja wa Mwenyeezi Mungu basi vile vile siku ya Kiama atafufuliwa naye huyo huyo muovu wake.
Masuala.
1. Kur-ani takatifu imewaarifisha watu wa namna gani ambao hawatanufaika na chochote siku ya Kiama?.
2. Madhumuni na malengo ya amani ya Mwenyeezi Mungu ni nini?
3. Mwenyeezi Mungu (s.w) ametanabahisha nini wale ambao wamejiepusha na
kujiweka mbali na kumkumbuka Yeye (s.w) kwa utakaso?.
4. Ni watu wa aina gani walioahidiwa adhabu kali duniani na Akhera?
5. Ni watu wa aina gani waliopewa bishara duniani na Akhera?.
6. Kuwafuata viongozi wema wa dini, kunaleta kheri gani siku ya Kiama?.
[1] Surat Israa Aya ya 71
[2] Surat Hud Aya ya 98
[3] Surat Tahriym Aya ya 8.
MWISHO