BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
UHUSIANO WA DUNIA NA AKHERA
* Kuna uhusiano gani baina ya ulimwengu wa dunia na ulimwengu wa Kiama?.
*Kuna uhusiano gani baina ya matendo na amali anazozifanya mwanaadamu duniani na malipo atayolipwa siku ya Kiama?
UHUSIANO ULIOPO BAINA YA DUNIA NA AKHERA.
Kuna uhusiano baina ya dunia na Akhera, kiasi ya kwamba kutokana na matendo anayoyafanya mwanaadamu duniani, ndio malipo atayolipwa Akhera, ikiwa mwanaadamu
atafanya amali na matendo mema, basi atalipwa Pepo. Na ikiwa atafanya madhambi na kumuasi Mola wake, atalipwa moto.
Makadirio ya mwanaadamu ya siku ya Qiyamah yana uwiano na maisha yake ya duniani. Kwa hiyo, kwa wale ambao huishi duniani kwa kuvutiwa na anasa za dunia, na wakawa hawana shauku yoyote ya kufanya matendo mema, hapana shaka hawawezi kutapata malipo yoyote Siku ya Kiama. Kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani:-
فَإِذَا قَضَيْتُم مَّنَاسِكَكُمْ فَاذْكُرُواْ اللّهَ كَذِكْرِكُمْ آبَاءكُمْ اَوْ اَشَدَّ ذِكْراً فَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ رَبَّنَا آتِنَا فِى الدُّنْيَا وَمَا لَهُ فِى الآخِرَةِ مِنْ خَلاَقٍ[1]
Na mkisha timiza ibada zenu basi mtajeni Mwenyezi Mungu kama mlivyo kuwa mkiwataja baba zenu au mtajeni zaidi. Na wapo baadhi ya watu wanao sema:
Mola wetu Mlezi, tupe duniani! Naye katika Akhera hana sehemu yoyote.
*Mahujaji hapo zama za kijahili wanapokutana Minaa mwezi 11, 12, na 13 huwa wanashindana kutaja matukufu ya wazee wao kwa mashairi na kwa namna nyengine, ndiyo wanaambiwa hapa kuwa badili ya hivyo wawe wanamtaja Mwenyeezi Mungu. Na inaposemwa:- 'Na kuna baadhi..'ni kuonyesha kuwa tusishughulike kuomba dua za kufanikiwa na ulimwengu tu, tuombe dua za kufanikiwa na Akhera pia.
Na ikiwa mwanaadamu atakuwa kichwa ngumu katika kuikubali haki, na akawa tayari kuwapoteza wengine, basi mtu huyo atapata hizaya duniani, na siku ya Kiama atalipwa adhabu kali inayoumiza. Kama anavyosema Allah (s.w):-
ثَانِيَ عِطْفِهِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللهِ لَهُ فِى الدُّنْيَا خِزْيٌ وَنُذِيقُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عَذَابَ الْحَرِيقِ[2]
Anaye geuza shingo yake ili kupoteza watu waache Njia ya Mwenyezi Mungu. Duniani atapata hizaya, na Siku ya Kiyama tutamwonjesha adhabu ya kuungua.
Kundi jengine la watu, ni wale wanaofuata mafunzo na hekima walizopewa na Mitume, na imani asili waliyonayo katika nyoyo zao huwafanya wawe na shauku ya kutenda matendo mema, na humuomba Mola wao awape mema na mazuri duniani na Akhera. kama tunavyosoma katika Qur-ani:-
وِمِنْهُم مَّن يَقُولُ رَبَّنَا آتِنَا فِى الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِى الآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ[3]
Na katika wao wapo wanao sema: Mola wetu Mlezi, tupe duniani mema, na Akhera mema, na utulinde na adhabu ya Moto!
Na kwa sababu imani ya baadhi ya watu ni thabiti, basi Mwenyeezi Mungu huwasaidia na huwapa rehema zake ili wanufaike katika maisha yao ya duniani na Akhera. Kama anavyosema Allah (s.w):-
إِنَّا لَنَنصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِى الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الاَشْهَادُ[4]
Hakika bila ya shaka Sisi tunawanusuru Mitume wetu na walio amini katika uhai wa duniani na siku watapo simama Mashahidi.
* Wema wasikate tama. Watapata nusura tu japo itakawia vipi - na japo baada ya kufa kwao, ya haki anayoyalingania yatakuwa tu. Kwa hiyo, ikiwa wanaadamu hawata danganyika na weupe wa dunia, na wakapambanua kwa uwazi mema na mabaya; hapana shaka watauona uhakika kwa uwazi kabisa kuwa kuna uhusiano baina ya Dunia na Akhera.
Na yale waliyo bashiriwa duniani yanaendana sambamba na watakayo yakuta Akhera.
Na kwa upande mwengine, ikiwa wanaadamu hawatakuwa na hofu na nguvu za madhalimu, na wakaamini kuwa nguvu hizo hazitadumu, bali ni za muda mchache tu, na zinaweza kuzimika wakati wowote, basi ukweli na haki utathibitika kuwa, kuna uhusiano baina ya malipo ya Duniani na Akhera ya Waumini na Watu wabaya.
Katika kipengele hiki tutasadikisha uhusiano uliopo baina ya Dunia na Akhera.
Kuna uhusiano wa salama na amani Duniani na Akhera. Kwa hakika watu ambao waliishi duniani kwa kumcha Mwenyeezi Mungu na kufanya amali na matendo mema, na wakawafanyia watu wengine wema na ihsani, na wakajiepusha na kufanya madhambi au kumuasi Mwenyeezi Mungu, Basi watanufaika na amani ya Mwenyeezi Mungu duniani na Akhera. Kama inavyo ashiriwa ndani ya Qur-ani takatifu, mifano ya Nabii wawili waliobashiriwa amani. Mwenyeezi Mungu Mtukufu anasema kumwambia Nabii Yahya (amani ziwe juu yake):-
وَسَلاَمٌ عَلَيْهِ يَوْمَ وُلِدَ وَيَوْمَ يَمُوتُ وَيَوْمَ يُبْعَثُ حَيّاً[5]
Na amani iwe juu yake siku ya kuzaliwa, na siku ya kufa, na siku ya kufufuliwa.
Katika Qur-ani kumetajwa aina nyingi za utukufu wa amani za Mwenyeezi Mungu Lakini katika kipengele hiki tutaashiria mfano unauhusiana na amani alizojaaliwa Nabii Nuhu (amani ziwe juu yake). Katika Qur-ani tunasoma hivi:-
وَنَجَّيْنَاهُ وَاَهْلَهُ مِنَ الْكَرْبِ الْعَظِيمِ. وَجَعَلْنَا ذُرِّيَّتَهُ هُمْ الْبَاقِينَ. وَتَرَكْنَا عَلَيْهِ فِى الآخِرِينَ. سَلاَمٌ عَلـٰي نُوحٍ فِى الْعَالَمِينَ[6]
Na tulimwokoa yeye na ahali zake kutokana na msiba mkubwa. Na tuliwajaalia dhuriya zake ndio wenye kubakia. Na tukamwachia (sifa njema) kwa walio kuja baadaye. Iwe salama kwa Nuhu ulimwenguni kote!
Lakini ni lazima tuzingatie kuwa, sio Mitume ya Mwenyeezi Mungu tu inayopata amani na rehema za Mwenyeezi Mungu, bali hii ni rehema na sunna za
Mwenyeezi Mungu, na watapata wote ambao wamezitakasa nafsi zao
kwa kufanya amali na matendo mema, na watakaojiepusha na kufanya madhambi kwa kumuasi Mwenyeezi Mungu Muweza. Kama tunavyosoma katika Aya
tofauti za sura hiyo hiyo tuliyo ashiria hapo juu.
إِنَّا كَذٰلِكَ نَجْزِى الْمُحْسِنِينَ[7]
Kwa hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema.
[1] Suratul-Baqarah Aya ya 200
[2] Suratul-Hajj Aya ya 9.
[3] Suratul-Baqarah Aya ya 201.
[4] Surat Ghaafir Aya ya 51.
[5] Surat Maryam Aya ya 15.
[6] Saaffaat Aya ya 76-79.
[7] Surat Saaffaat Aya ya 80.
MWISHO