BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
FUNGAMANO LA FAMILIA NA MARAFIKI
2. FUNGAMANO LA FAMILIA NA MARAFIKI
Katika dunia, wanaadamu hutegemea familia zao, ukoo wao, au hata marafiki zao katika kuondoa mabalaa yanayowakuta, au kwa ajili ya kutatua matatizo waliyonayo, au kuomba msaada ili kupata mahitajio yao, ama siku ya Kiama wanaadamu wote wataghafilika na kuingiwa na hofu kiasi ya kwamba kila mmoja atakuwa akihangaika ili kujiokoa yeye na nafsi yake bila ya kufikiria wengine, hata kwa wale watu wake wa karibu aliokuwa na mapenzi nao na aliokuwa akiwathamini kuliko kitu chengine au watu wengine, watu hao wanaweza wakawa ni wazee au ndugu zake, katika qur-ani tunasema hivi:-
يَوْمَ يَفِرُّ الْمَرْءُ مِنْ اَخِيهِ . وَاُمِّهِ وَاَبِيهِ . وَصَاحِبَتِهِ وَبَنِيهِ[1]
Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye . Na mamaye na babaye . Na mkewe na wanawe .
Katika siku hiyo hakuna hata mmoja atakayeweza kumsaidia mwenziwe, hata baba hatoweza kumsaidia mwanawe, na mtoto pia hatoweza kumsaidia baba yake.
يَا اَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمْ وَاخْشَوْا يَوْماً لاَّ يَجْزِى وَالِدٌ عَن وَلَدِهِ وَلاَ مَوْلُودٌ هُوَ جَازٍ عَن وَالِدِهِ شَيْئاً إِنَّ وَعْدَ اللهِ حَقٌّ فَلاَ تَغُرَّنَّكُمُ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا وَلاَ يَغُرَّنَّكُم بِاللهِ الْغَرُورُ[2]
Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi, na iogopeni siku ambayo mzazi hatamfaa mwana, wala mwana hatamfaa mzazi kwa lolote. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Basi yasikudanganyeni maisha ya dunia, wala asikudanganyeni na Mwenyezi Mungu mdanganyifu.
Na siku hiyo hakutakuwa na rafiki wala familia yoyote itakayoweza kuleta faida kwa ukoo wake.
لَن تَنفَعَكُمْ اَرْحَامُكُمْ وَلاَ اَوْلاَدُكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ يَفْصِلُ بَيْنَكُمْ وَاللهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ[3]
Hawatakufaeni jamaa zenu, wala watoto wenu Siku ya Kiyama. Mwenyezi Mungu atapambanua baina yenu, na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
Katika siku hiyo (Kiama) hakutakuwa na mtu yeyote atakayekuwa na uwezo wa kumsaidia mwengine,.
يَوْمَ لاَ يُغْنِى مَوْلًى عَن مَّوْلًى شَيْئاً وَلاَ هُمْ يُنصَرُونَ[4]
Siku ambayo rafiki hatamfaa rafiki yake kwa chochote, wala hawatanusuriwa.
Uhusiano na mafungamano ya aina yoyote yale yatakatika, na zitabakia rehema za Mwenyeezi Mungu peke yake, rehema hizo hazitawafika wengine isipokuwa waja wake wema na watiifu. kama anavyosema Allah (s.w):-
إِلاَّ مَن رَّحِمَ اللهُ إِنَّهُ هُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ[5]
Isipo kuwa atakaye mrehemu Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
[1] Surat Abasa Aya ya 34-36.
[2] Surat Luqmaan Aya ya 33
[3] Surat Al-Mumtahinah Aya ya 3.
[4] Surat Ad-Dukhaan Aya ya 41.
[5] Surat Ad-Dukhaan Aya ya 4
MWISHO