UJUMBE WA MITUME
  • Kichwa: UJUMBE WA MITUME
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 21:48:20 1-9-1403

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

UJUMBE WA MITUME YA ALLAH (S.W) NO.1

NJIA WALIZOTUMIA MITUME KATIKA KUWAFIKISHIA WATU UJUMBE WA ALLAH (S.W.)

Mitume Mitukufu ya Mwenyeezi Mungu ilifanya jitihada zao zote ili kufikisha ujumbe waliopewa na Mola wao, na watukufu hao walitumia njia na miongozo mbali mbali iliyoweza kufikisha ujumbe huo, ujumbe ambao ni amana waliopewa na Mola wao kwa ajili ya kuwafikishia walimwengu, kwa hiyo ikiwa wanaadamu watafuata na kutii maamrisho ya watukufu hao hapana shaka watafikia katika malengo yale yaliyokusudiwa na Mola Mtakatifu.

Vipi Mitume iliwalingania watu katika dini ya Mwenyeezi Mungu?.

Ndani ya Qur-ani neno (tabligh) limekuja na maana ya (kufikisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu kwa watu), kama tunavyosoma kuhusiana na Mitume ya Mwenyeezi Mungu:-

الَّذِينَ يُبَلِّغُونَ رِسَالاَتِ اللهِ وَيَخْشَوْنَهُ وَلاَ يَخْشَوْنَ اَحَداً إِلاَّ اللهَ وَكَفَي بِاللهِ حَسِيباً[1]

(Hao wa zamani) walio kuwa wakifikisha (ujumbe) risala za Mwenyezi Mungu na wanamwogopa Yeye, na wala hawamwogopi yeyote isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ndiye atoshaye kuhisabu.

Hadafu na madhumuni makuu ya Mitume katika kuufikisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu ni kuwapa wanaadamu mafunzo na kuwataka wafanye amali na matendo mema, kama anavyosema Nabii Hud (a.s):-

اُبَلِّغُكُمْ رِسَالاتِ رَبِّى وَاَنَاْ لَكُمْ نَاصِحٌ اَمِينٌ[2]

Nakufikishieni ujumbe wa Mola wangu Mlezi. Na mimi kwenu ni mwenye kukunasihini, muaminifu.

Miongoni mwa hadafu na madhumuni mengine ya Mitume katika kuufikisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu ni kuwamalizia hoja wale ambao wanamkhalifu Mwenyeezi Mungu na Mitume yake,na vile vile wanakhalifu amri zake Allah (s.w), kama anavyosema:-

وَاَطِيعُواْ اللّهَ وَاَطِيعُواْ الرَّسُولَ وَاحْذَرُواْ فَإِن تَوَلَّيْتُمْ فَاعْلَمُواْ اَنَّمَا عَلـٰي رَسُولِنَا الْبَلاَغُ الْمُبِينُ[3]

Na mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume, na tahadharini. Na ikiwa mtageuka basi jueni ya kuwa juu ya Mtume wetu ni kufikisha ujumbe tu ulio wazi.

Mitume ya Mwenyeezi Mungu ilitumia njia tofauti katika kuufikisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu, baadhi ya wakati walibainisha hukumu, kuwapa wanaadamu mawaidha ya hekima, kutoa bishara zinazosababisha hofu nyoyoni mwa watu, na baadhi ya wakati wakatoa bishara njema zinazowapa watu matumaini.

Qur-ani tukufu ina sifa tofauti, miongoni mwa sifa hizo ni kuwa kitabu hicho kitukufu kinatambuliwa kuwa ndio kitabu kamilifu miongoni mwa vitabu vilivyoteremshwa, na mbali ya kuwa kimechukua ujumbe wa Mwenyeezi Mungu, vile vile kimewataka wanaadamu wawe na imani na kuikubali dini yao, na kufuata desturi za Mwenyeezi Mungu, na wabainishe njia zitakazosuluhisha jamii na kufikisha ujumbe wake Allah (s.w). kama anavyosema Allah (s.w):-

ادْعُ إِلِى سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ وَجَادِلْهُم بِالَّتِى هِيَ اَحْسَنُ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ اَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ وَهُوَ اَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ[4]

Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka.

[1] Surat Al-Ahzaab Aya ya 39

[2] Surat Al-Aaraf Aya ya 68

[3] Surat Al-Maidah Aya ya 92

[4] Suratun-Nahli Aya ya 125

MWISHO