UANDISHI WA QURANI
  • Kichwa: UANDISHI WA QURANI
  • mwandishi: Imeandikwa na Sheikh Taqee Zacharia
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 4:50:51 14-10-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

UANDISHI WA QURANI

KUANDIKWA KWA QUR'ANI TUKUFU (SEHEMU YA PILI).

{2}-KUPANGILIA AU KUUNDA AYA ZAKE KATIKA KILA SUURA.

Upangiliaji wa aya za Qur'an Tukufu kila suura katika utaratibu huu tunaouona katika Qur'an Tukufu, suala hili lilitimia -kwa wingi sana -kulingana na jinsi aya zilivyokuwa zikishuka:
Mfano: Suura ilikuwa ikianza na
(بسم الله الرحمان الرحيم)

kisha aya zote zinazoshuka baada Bislmillah Ar-rahmaan Ar-rahiim zinaandikwa au zinapangwa katika Suura hii, zikifuatana moja baada ya nyingine kwa hatua kulingana na kushuka kwa aya, mpaka inaposhuka Bismillah Ar-rahmaan Ar-rahiim nyingine,basi hapo inajulikana kuwa Suura hii imeisha na imeanza Suura nyingine.

Imam (wa sita) Jaafar Swaadiq (a.s) amesema:
کان يعرف انقضاء السورة بنزول((بسم الله الرحمان الرحيم)) ابتداءاً لأخرى.

"Kuisha kwa Suura kulikuwa kunajulikana kwa kushuka ((Bismillah Ar-rahmaan Ar-rahiim)), (na ulikuwa) mwanzo wa Suura nyingine " Na utaratibu huu tunauita {UTARATIBU WA ASILI.}. Nakuna jambo lingine ambalo limefanya kazi ya kupangilia baadhi ya Aya katika utaratibu unaokwenda kinyume na zilivyoshuka,na hii ni kwasababu ya Nassu kutoka kwa Mtume (s.a.w) na uainishaji wake khaasi (kwamba aya hii inatakiwa iwekwe katika Suura fulani na sehemu fulani). Mtume (s.a.w) -mara nyingine- alikuwa anaamrisha kuiweka aya katika sehemu makhsusi ya Suura iliyoshuka kabla na ambayo ilikuwa imeisha.

Imepokewa kwamba Aya ya Mwisho kabisa kushuka Katika Qur'an Tukufu ni kauli ya Mwenyeezi Mungu (s.w):
*والتقوا َيوماً تُرجعُونَ فيهِ إلى اللهِ ثمَّ توفّى کلُّ نفسٍ مَّا کسبت وهم لا يظلمونَ*

"Na ogopeni (au tahadharini) siku ambayo mtarejeshwa kwa Mwenyeezi Mungu,kasha kila mtu atapewa sawa sawa aliyoyachuma,nao hawatadhulumiwa" Jibriyl (a.s) akaashiria kwamba aya hii iwekwe baina ya Aya mbili ambazo zinaitwa Aayatur-ribaa na Aayatud-dayn katika Suuratul Baqarah,{ni Aya ya 281}.

Na huenda Suura ilikuwa ikianza kushuka,na kabla haijaisha, inaanza kushuka Suura nyingine na Suura hii ya Mwisho inaisha kabla ya kuisha Suura ile ya Mwanzo.Na hii ilikuwa ni kwa Amri ya Bwana Mtume (s.a.w) na kwa Ishara yake,kama ilivyo katika Suuratul Baqarah,Ni sura ya kwanza Iliyoanza kushuka katika mji wa Madina baada ya Hijra,lakini Suura hii iliendelea kushuka kwa miaka kadhaa mpaka hata baada ya mwaka wa sita,kwani kuna Aya nyingi sana (katika suura hii ya baqarah) zilizoshuka katika kipindi hiki cha mwishoni.Miongoni mwa Aya hizo ni Aya hii:

*إنَّ الصَّفى والمروةََ من شعائرالله فمن حجَّ البيتَ أو اعتمَرَ فلا جناحَ عليهِ أن يَطّوَّفَ بهما*

"Hakika Swafa na Mar-wa ni katika alama za (Dini) ya Mwenyeezi Mungu,basi mwenye kuikusudia Al-kaaba,au kuizuru,si vibaya kuizunguka" Hakika ya Suura hii imeshuka kipindi kile ambacho baadhi ya Waislaam walijiharamisha kufanya Saayi baina ya Swafa na Marwa wakiitikadia kuwa Saayi katika maeneo haya mawili ni katika vietendo vya zama za Kijahiliyya.Ndipo ikashuka aya hii tukufu ili kuondoa fikra hii iliyokuwa imesambaa katika bongo za baadhi ya Waislaam hao.

Jambo ambalo lilipelekea kushuka kwa aya hii baada ya Sulhu Hudaybiyya katika Umra (ya Qadhaa).Nao ni mwaka wa sita baada ya Hijra.Au huenda Nabii Muhammad (s.a.w) ameamrisha kuweka Aya hii katika sehemu hii ya Suura hii ya Baqarah.Na Mwenyeezi Mwenyeezi Ndiye mjuzi zaidi. Na hivyo ndivyo ndivyo zilivyoshuka aya za Suuratul-Hajji katika mwaka huo huo ambapo zinathibiti katika Suura hii kwa dhati kabisa.

3-UPANGILIAJI WA WA SUURA ZA QUR'AN TUKUFU
Zama za Mtume (s.a.w) zilikwisha Qur'an Tukufu ikiwa imehifadhiwa na kuandikwa sehemu mbali mbali kama vile kwenye maguo (ya ngozi),vipande vya mawe,na baadhi ya hariri pamoja na karatasi na katika vifua vya baadhi ya Maswahaba.

Suura zilikuwa zimetia kabisa katika zama zake (s.a.w) na zimepangiliwa Aya zake na majina yake,lakini kukusanywa na kuandikwa baina ya magamba mawili haikuwa hivyo katika zama zake,na hii ni kwasababu Mtume (s.a.w) alikuwa bado anasubiria kushuka kwa WAHYI,madam Wahyi bado haujakatika (yaani bado unashuka),basi haikujuzu kuandikwa Suura hizi na kuwa Msahafu ispokuwa baada ya kukamilika na wahyi kukatika,jambo ambalo halikuwa ni lenye "kuwa" au "kuwepo" au "kutimia" ispokuwa baada ya kuisha kipindi cha Mtume (s.a.w) na kukamilika kwa WAHYI.

Imam Swaadiq (a.s) amesema:Amesema Mtume (s.a.w) kumwambia Ali (a.s):
*يا عليُّ! القرآن خلف فراشي في الصحف والحريروالقراطيس، فخذوه واجمعوه ولا تُضيَّعُوهُ*

"Ewe Ali! Qur'an ipo nyuma ya godoro (au kitanda changu) langu katika Karatasi na Hariri na majarida,basi ichukueni na ikusanyeni na wala msiipoteze" Na Mtu wa kwanza kabisa aliyeikusanya Qur'an Tukufu na kuiandika baada ya Kufariki Mtume (s.a.w) moja kwa moja na kwa wasia kutoka kwake (s.a.w) ni Imam Ali Bin Abi Twaalib (a.s), kisha akafuatia Zaid bin Thaabit kuikusanya na kuiandika kwa amri ya Abi Bakri,kama walivyoikusanya wengine baada ya hao ambao ni Ibni Mas-uud na Ubayyi bin Kaabi na Abi Musa Al-ash-ariy na wengine kadhaa wasiokuwa hao, mpaka jambo hili likaishia kwa Uthman ambaye katika zama zake kulifanyika harakati za kuleta umoja katika misahafu ambapo ilikuwepo misahafu iliyokusanywa na maswahaba mbali mbali ikitofautiana katika kisomo,huyu anasoma hivi kulingana na msahafu aliokuwa nao na yule anasoma hivi kulingana na msahafu aliokuwa nao.Tofauti hizi za kisomo zilizokuwa zimekithiri zama hizo zilisababisha hali ya hatari sana kwa waislaam na maswahaba kwani walifikia hatua ya kuuana na kukafirishana na uadui wa kila aina.!

Hapo ndipo Uthman aliposimama (baada ya kupewa fikra na mmoja wa maswahaba kama tutakavyobainisha suala hilo sehemu ijayo) na kutuma kopi za Qur'an zenye aina moja ya kisomo katika kila sehemu ya mji,vijiji na nchi na kuwataka watu washikamane na aina moja ya kisomo kinachopatikana ndani ya kopi hizo za Qur'an na kuachana vile viaina vingine vya kisomo ambavyo ni kinyume na kisomo kinachopatikana katika kopi hizo alizozituma maeneo hayo.Tutakuja kuzungumzia kuhusiana na mada hii kwa kirefu inshaallah.

UFAFANUZI WA RAI YA MWENYE KUPINGA
Haya tuliyoyataja sehemu katika bahthi hii ndio maarufu sana kwa wapokezi wa athari na kwa wanabahthi na wachunguzi wa mambo yanayohusiana na Qur'an Tukufu,tangu zama za mwanzo mpaka siku yetu hii ya leo. Lakini tunakuta yupo mwenye kukataa uwazi huu na ufafanuzi huu kunako kukusanywa kwa Qur'an Tukufu na anaona kwamba Qur'an ukusanywaji wake huu na mpangilio wake kama ilivyo kwa sasa ulikuwa umetimia na kuwa hivi hivi kama ilivyo katika zama za Mtume (s.a.w).

Na Maulamaa wengi wa Kisalaf wamekwenda katika rai hii na akawaunga mkono Alam Al-hudaa As-sayyid Al-murtadha (Mwenyeezi Mungu s.w amrehemu) na akasimama katika dalili hii kwamba Qur'an Tukufu ilikuwa inasomwa na kuhifadhiwa yote kamili katika zama hizo hata baadhi ya Maswahaba walioihifadhi wakaainishwa,na kwamba Qur'an hii ilikuwa ikiletwa mbele ya Mtume (s.a.w) na kusomwa mbele yake.

Na kwamba baadhi ya Maswahaba kama vile Abdullah bin Mas-uud na Ubayyi bin Kaabi na wasiokuwa hao walikhitimisha Qur'an kwa Mtume (s.a.w) mahitimisho kadhaa.Na yote hayo yanajulisha (kwa mazingatio) kwamba Qur'an ilikuwa imekusanywa tiyari,na kupangiliwa {kama ilivyo kwa sasa}.

Lakini kuhifadhi Qur'an maana yake ni:Kuhifadhi Suura zote za Qur'an ambazo aya zake zimekamilika,sawa sawa uwepo utaratibu baina ya Suura au la.Na hivyo ndivyo hitimisho la Qur'an lilivyokuwa kwani maana yake ni:Kusoma Suura zote za Qur'an Tukufu pasina kuangalia wala kuchunga utaratibu maalum baina ya Suura hizo.

Au kuhifadhi kulikuwa na maana ya kuhifadhi (maintenance) Qur'an mzima iliyoshuka na kuidumisha pasina kuipoteza na kuigawanya (hatimaye kuleta mfarakano),jambo ambalo linajulisha kwamba kulikuwepo utaratibu maalum uliokuwa baina ya suura za Qur'an Tukufu kama ulivyo kwa sasa.

JINSI IMAM ALI BIN ABI TWALIB (A.S) ALIVYOIKUSANYA QUR'AN TUKUFU NA KUIANDIKA.
Tutarudi hivi punde Inshaallah ili kuendelea na sehemu hii kuhusiana na jinsi Imam Ali (a.s) alivyoikusanya Qur'an Tukufu na kuiandika. Jitahidi kufuatilia sehemu hii ijayo ili ujue tofauti zilizokuwepo za ukusanyaji wa Qur'an Tukufu kati ya Imam Ali na wakusanyaji wengine walioikusanya Qur'an, je wote waliikusanya na kuiandika kama alivyofanya Imam Ali (a.s) au la? Haya yote utayajua ukifuatilia sehemu ijayo ya bahthi hii inayoendelea.

Tazama:

Tafsirul-Iyaashiy:Juz ya 1,Ukurasa wa 19,Hadithi ya 5. Tazama:Al-itqaan:Juzu ya kwanza,Ukurasa wa 62. Suuratul-Baqarah Tazama Riwaya hii katika:Bihaarul-Anwaar:Juzu ya 92,Ukurasa wa 48,Hadithi ya 7 kutoka katika Tafrisi ya Ali bin Ibrahim. Tazama:Maj-maul-bayaan:Juz - ya 1, Uk -wa 15.