UFUTWAJI WA HUKUMU NDANI YA QUR_ANI
  • Kichwa: UFUTWAJI WA HUKUMU NDANI YA QUR_ANI
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 17:39:27 1-9-1403

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI 

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

NASKH NA MANSUKH NDANI YA QUR_ANI.2

UFUTWAJI WA HUKUMU NDANI YA QUR_ANI.

Katika makala iliyopita (makala kuhusiana na Naasikh na Mansukh no 1), tulielezea mada hiyo ambayo inahusiana na kufutwa kwa baadhi ya hukumu ndani ya Qur-ani. Na tukatoa mfano wa kufutwa kwa baadhi ya hukumu hizo kwa mfano – Katika surat Baqarah Aya ya 126, tumeelezea kwa ufupi kuhusiana na kufutwa kwa baadhi ya hukumu.

Lakini aya Naasikh ndani ya Qur-ani zimekuja aina tatu tu.

Aina ya kwanza:

 Naskhu L-hukmu watilaawa jamiy`an (yaani iliyofuta aya za Qur-ani pamoja na hukumu).

Na aina ya pili:

Naskhu L-hukmu duna tilaawa (yaani iliyofuta hukumu bila ya kufuta aya za Qur-ani).

Na aina ya tatu:

 Naskhu tilaawa duwna L-hukmu (yaani iliyofuta aya za Qur-ani bila ya kufuta hukumu).

Hapana shaka kuwa kuna hekima kubwa za Mola kubadilisha aya zilizo bora yaani Naasikh ni kwa ajili ya kuwapunguzia umma huu mambo mazito kwa mambo mepesi au mambo ya madhara kwa mambo ya faida au manufaa kwao. Ingawa hukumu za aya hizo zimefutwa lakini aya za Qur-ani Tukufu bado zipo ndani ya Qur-ani na mpaka hivi sasa zinasomwa na watu. Na hekima ya Mwenyezi Mungu kuziacha, kwani ingelikuwa zimefutwa sisi tusingezijua aya hizo wala sababu za kufutwa kwake, nazo ni nyingi sana zimetolewa ndani ya Qur-ani Tukufu.

Hayo yalikuwa ni maelezo kwa ufupi kuhusiana na Aya Mansukh, kwa kuendelea na mada hii ni vizuri tukafafanua istilaha hizo:-

UFAFANUZI WA NENO NASKH NA MANSUKH.

Naskh katika Istilaha ya lugha ya Kiarabu ina maana ya kuondoa hukumu iliyokuweko mwanzo ambayo ilionekana kuwa ni hukumu ya daima, na kuletwa hukumu nyengine mpya badala yake, kiasi ya kwamba hukumu mpya huwa imechukuwa nafasi ya hukumu iliyopita, bila ya kuwepo uwezekano wa kuzikusanya hukumu mbili hizo.

Hapa inawezekana mtu akatia shaka na kusema:-

Basi ile aya iliyopita ina maana gani katika Qur-ani kwani haina faida yoyote ile, bali ni maneno yaliyobakia yenye kusomwa, jawabu ya watu wenye shaka kama hiyo ni kwamba.

Jambo la kwanza kabisa kuwepo kwa aya zilizofutwa na zile zenye kufuta hukumu ya mwanzo kunapelekea kuifahamu tarehe ya uteremshwaji wa sheria na mpangilio wake, na kulifahamu suala hili ni moja kati ya faida zinazomfanya mtu azitambue sheria za dini.

 Na jambo la pili linalotakiwa kufahamika ni kwamba ni lazima watu wawe na mazingatio ya kwamba moja kati ya nyanja muhimu za Qur-ani ni kuwa Qur-ani ina miujiza ya ubainishaji, na miujiza hiyo ni lazima ibakie milele.

 Jambo la tatu ni kwamba aya nyingi zilizofutwa zimefutwa kwa kuangaliwa sharti fulani na namna ya zama zilivyo, kwa hiyo basi kama shuruti hizo zitajirudia tena katika zama fulani basi aya hizo zitarudi tena kufanya kazi zake kama zilivyokuwa zikifanya hapo mwanzo, kwa mfano, inawezekana kitu fulani kikawa kimeharamishwa katika zama za Mtume fulani na kikahalalishwa tena katika zama za Mtume fulani, kwa kuzingatia namna ya zama zilivyokuwa.

Katika sehemu hii na tuangalie mifano ya Aya za Mansukh:-

Mfano wa kwanza wa aya Mansuwkh.

 Hapo zamani ilikuwa kabla ya mtu kumsemeza Mtume (S.A.W.W) kwa siri ni wajibu kwa mtu yule kwanza atoe sadaka. Kama alivyosema Allah (S.W.) katika Suratil Mujaadala aya ya 12.

يَاأَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَاجَيْتُمْ الرَّسُولَ فَقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيْ نَجْوَاكُمْ صَدَقَةً[1]

Maana yake, “Enyi mlioamini! Mnapomsemeza Mtume toeni sadaka kabla ya kumsemeza (ili wapewe sadaka hizo maskini)...”

Lakini ikaja aya Naasikh ambayo ilifuta kutoa sadaka kabla ya mtu kumsemeza Mtume (S.A.W.W) kwa siri. Kama ilivyokuja katika Suratil Mujaadala katika aya ya 13.

أَأَشْفَقْتُمْ أَنْ تُقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيْ نَجْوَاكُمْ صَدَقَاتٍ فَإِذْ لَمْ تَفْعَلُوا وَتَابَ اللَّهُ عَلَيْكُمْ فَأَقِيمُوا الصَّلاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ[2]…

Tarjuma:

“Mbona mnaona taabu kutanguliza hiyo sadaka kabla ya kumsemeza kwenu? Ikiwa hamjafanya haya basi. (Yamekwisha hayo). Na Mwenyezi Mungu amekusameheni. Basi simamisheni Sala na toeni Zaka...”

2. Mfano wa pili wa aya Mansuwkh.

 Hapo zamani ilikuwa mwanamke ambaye hajaolewa akizini basi huzuiwa katika nyumba. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu (S.W.) katika Suratin Nisaa aya ya 15,

وَاللاَّتِي يَأْتِينَ الْفَاحِشَةَ مِنْ نِسَائِكُمْ فَاسْتَشْهِدُوا عَلَيْهِنَّ أَرْبَعَةً مِنْكُمْ فَإِنْ شَهِدُوا فَأَمْسِكُوهُنَّ فِي الْبُيُوتِ[3]…

Tarjuma:

“Na ambao wanafanya uchafu (wa kuzini) miongoni mwa wanawake wenu, washuhudizieni watu wanne katika nyinyi. Watakaposhuhudia, basi wazuieni majumbani...”

Maelezo kuhusiana na Aya ya 15 ya surat Nisaa.

Hizi ni Aya zinazotaja adabu ya kutiwa:-

A)Wanawake wanaofanya machafu.

B) Wanaume wanaofanya machafu.

c) Wanawake wanaofanya machafu na wanaume.

Yote haya mabaya kabisa, na zaidi ni yale ya wanaume kwa wanaume, kisha ya wanaume na wanawake, na baadaye wanawake kwa wanawake.

Lakini ikaja aya Naasikh ambayo ilifuta kuwazuia majumbani wanawake waliozini na bado hawajaolewa. Kama ilivyokuja katika Suratin Nuur katika aya ya 2.

الزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِنْهُمَا مِائَةَ جَلْدَةٍ[4]…

Tarjuma:

 “Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanaume, mpigeni kila mmoja katika wao mijeledi (bakora) mia...”
Hiyo ilikuwa ni mifano ya Aya Mansukh, mbali ya mifano hiyo kuna mifano mengine mingi ambayo tutaielezea katika makala ijayo.

[1] Suratil Mujaadala aya ya 12.

[2] Suratil Mujaadala aya ya 13.

[3] Suratin Nisaa aya ya 15

[4] Surat Nuur Aya ya 20

MWISHO