KUBADILISHWA KWA HUKUMU NDANI YA QUR_ANI
  • Kichwa: KUBADILISHWA KWA HUKUMU NDANI YA QUR_ANI
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 18:6:58 1-9-1403

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

 NASKH NA MANSUKH NDANI YA QUR_ANI.1

KUBADILISHWA KWA HUKUMU NDANI YA QUR-ANI.

Mipango yoyote ile inayopangwa kwa ajili ya kuiongoza jamii fulani, hutekelezwa kwa kupitia hatua baada ya hatua, na kwa kutokana na hali ya watu wa zama hizo walivyo pamoja na zama zilivyo, basi inabidi lazima zizingatiwe hali za watu hao, na suala hili hupelekea kufuta baadhi ya sheria za mwanzo na kuweka sheria mpya, ili kuweza kuwakomaza watu hao  katika nyanja tofauti, kisheria na kiutamaduni, Na suala hili linaonekana wazi katika serikali za kidunia na Qur-ani pamoja na vitabu vyote vya mbinguni haiko nyuma katika suala kama hili, kwani kazi ya Qur-ani ni kuwapangia watu maisha yao, ktika mtindo ulio bora, na suala la kufutwa kwa baadhi ya hukumu na kuwekwa hukumu mpya katika upangaji wa sheria hutimizwa suala hilo hatua baada ya hatua hadi watu wa jamii wanaokusudiwa kuongozwa waweze kubobea, na sio kitu cha busara kwamba baada ya kutimizwa sheria hizo na kukamilishwa zije kufutwa na kuwekwa sheria nyengine, kwa hiyo basi ufutwaji na upangwaji wa sheria nyengine mpya hutimizwa katika zama ambazo watu hao watakuwa bado hawajakomaa kisheria, bali wako njiani kukomazwa hatua baada ya hatua.

Kwa hiyo Mtume anapokuja na ujumbe utokao mbinguni ujumbe huo hutimizwa hatua baada ya hatua, hadi ufikie upeo wake ujumbe huo, na inapofikia wakati anapofariki ujumbe huo ujumbe huo huwa tayari umeshafika upeo wake, na haiwezekani ujumbe huo kufutwa na kuongezwa tena kitu chochote kile ndani yake. Ufutwaji wa sheria na kuletwa sheria nyengine ni mfano wa Dokta anayeandika dawa fulani katika hatua ya mwanzo, katika njia ya kumtibu mgonjwa kisha kwa mara ya pili akaandika dawa nyengine mpya ili kuyatokomeza maradhi, kwani haina maana kuwa zile dawa za mwanzo zilikuwa hazina maana, bali ilikuwa ni moja kati ya hatua za kumtibu mgonjwa huyo, na Mwenyeezi Mungu katika Qur-ani akizungumzia suala la kufutwa sheria moja na kuletwa sheria nyengine, katika (Suratul-Baqara aya ya 106 )anasema hivi:-

مَا نَنسَخْ مِنْ آيَةٍ اَوْ نُنسِهَا نَاْتِ بِخَيْرٍ مِّنْهَا اَوْ مِثْلِهَا اَلَمْ تَعْلَمْ اَنَّ اللّهَ عَلـٰيَ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ[1]

Maana ya aya hiyo ni kama ifuatavyo:-

“Aya yoyote tunayoifuta au kuisahauliza tunaleta iliyo bora kuliko hiyo, au iliyo mfano wake. Hujui kwamba Mwenyeezi Mungu anao uweza juu ya kila kitu?” .

Maelezo kuhusiana na Aya ya 106 ya Suratul Baqara.

Baadhi ya mifano ya hukumu zinazonasikhiwa (zilizofutwa), kwa hukumu nyengine ni ulevi.

a) Ulevi ulikuwa halali kabla ya kuja uislamu. Kisha ukaharamishwa nyakati za sala, kisha ukaharamishwa kabisa.

b) Sala ilikuwa asubuhi na jioni tu, kisha ikawa mara tano.

c) Katika kufunga  ilikuwa pana khiyari, mtu akitaka atafunga, na akitaka atatoa sadaqa ya chakula awape masikini badala ya kufunga. Kisha ikawa lazima kufunga maadam hana udhuru wowote.

Kwenye Aya ya mia moja na sita, wamekanusha habari ya naskh, wakasema kuwa Aya za Qur-ani hazipingani, hapana shaka kuwa Aya za Qur-ani hazipingani, lakini amri zake – na hasa makatazo yake – hazikuwa zikiamrisha jambo na kulikataza kwa ghafla. Lakini mara nyingi huliamrisha kidogo kidogo na kulikataza kwa daraja – kidogo kidogo. Na hivi ndivyo kila mwenye hekima anavyofanya. Na Mwenyeezi Mungu kajisifu mara nyingi katika Qur-ani kuwa ni Mwenye hekima na Mambo Yake yote anayafanya kwa Hikima, Na kuamrisha kidogo kidogo na kukataza kidogo kidogo ndiyo Hikima, na mifano tulioitoa katika maelezo ya Aya hii inatosha kuonyesha uwongo wa kukataa kwao naskh, na Aya hii ya mia moja na sita inaonyesha dhahiri haya wanayoyasema Ulamaa wanaokubalisha Naskh.

Hayo yalikuwa ni maelezo kuhusiana na Aya hiyo ya 106.

Kwa hiyo basi aina yoyote ile ya ufutwaji huwa imeangalia namna ya watu na zama za wakati ule zilivyo, pamoja na kuzingatia maslahi yao, kwa kuzingatia maelezo tuliyoyatoa itakua imeshaeleweka kiasi fulani nini maana ya kufutwa hukumu na kuletwa hukumu nyengine, ijulikanayo katika lugha ya kiarabu kwa jina la (Naskh) na (Mansukh).

[1] (Suratul-Baqara aya ya 106 )

MWISHO