AYA AMBAZO HUKUMU ZAKE ZIMEFUTWA
  • Kichwa: AYA AMBAZO HUKUMU ZAKE ZIMEFUTWA
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 20:35:52 1-9-1403

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

NASKH NA MANSUKH NDANI YA QUR_ANI.5

AYA AMBAZO HUKUMU ZAKE ZIMEFUTWA

Ufutwaji wa hukumu zilizokuja katika Qur-ani kwa mtizamo wa Wanachuoni waliopita, suala hili lilikuwa na upana zaidi, na kulikuwa kukipatikana mabadiliko kidogo tu baina ya Aya ya mwanzo iliyokuja na hukumu fulani, na Aya ya pili iliyokuja na hukumu yenye kufanana nayo, basi Wanazuoni wa zamani walikuwa wakiziingiza Aya hizi katika mtiriko wa Aya za Nasikh na Mansukh,   lakini maana ya Nasikh na Mansukh kwa mtizamo wa Wanazuoni wa kileo ni zile Aya tu zenye kufuta hukumu na zinazofutwa hukumu zao ndizo zinazoingia katika mtiririko wa Istilaha hii, yaani Wanazuoni wa kileo wanazihesabu zile Aya zilizochukua nafasi ya hukumu iliyopita ndizo Nasikh, na zile zilizofutwa hukumu zake ndio Mansukhu tu.

Basi kwa mtizamo wa Wanazuoni wa zamani, au mbele ya wale wenye kuukubali mtizamo huo kuna Aya nyingi za aina hii hadi kufikia mia mbili na ishirini na nane.

Suyutiy ambaye ni mmoja kati ya Wanazuoni wakubwa ni Aya ishirini na moja tu ndio alizozikubali, na Ayatu-llahi Khui yeye ameikubali Aya moja tu ni Mansukh, lakini kwa kutupia macho vipengele na shuruti tulizozizungumzia huko nyuma utakutia kwamba kuna Aya nane ndani ya Qur-ani ambazo zimefutwa hukumu zake kwa kupitia masharti maalumu.

Ni Aya nane ambazo ufutwaji wake ni katika kipengele cha nne tulichokitaja hapo mwanzo

Ufutwaji huu unapatikana kwenye Aya zisizopunguwa ishirini na kidogo.

MFANO WA AYA ZILIZOFUTWA HUKUMU ZAKE

Tukiendelea na mada inayohusiana na kufutwa baadhi ya Aya za Qur-ani katika sehemu hii tataziorodhesha baadhi ya aya hizo. Nazo ni:-

ايه نجوي))

NI AYA ILIYOWAWEKEA MIPAKA MASAHABA KATIKA KUZUNGUMZA NA MTUME (S.A.W.W).

Watu waliokuwa wakiishi katika zama za Mtume walikuwa huenda kwa Mtume katika nyakati tofauti, na walikuwa humuuliza masuala tofauti yenye faida na yasiyo na faida, na suala hili lilisababisha kumkosesha Mtume wakati wa mapumziko, ndipo ilipokuja Qur-ani na kuwaamrisha watu kuwa kila anayetaka kuuuliza suala basi kwanza anatakiwa kutoa sadaqa, kabla ya kuuliza suala lake. Na Aya hiyo iko katika (Surat Mujadila aya ya 12) inasema hivi:-

يَا اَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَاجَيْتُمُ الرَّسُولَ فَقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيْ نَجْوَاكُمْ صَدَقَةً ذٰلِكَ خَيْرٌ لَّكُمْ وَاَطْهَرُ فَإِن لَّمْ تَجِدُوا فَإِنَّ اللهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ[1]

Maana ya Aya hiyo ni kama hivi ifuatavyo:-

“Enyi mlioamini! Mnapomsemeza Mtume toeni Sadaqa kabla ya kumsemeza (ili wapewe sadaqa hizo masikini); hayo ni bora kwenu na ni ya kukusafisheni sana. Ikiwa hamkupata (cha kutoa), basi Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu”.

Kwa amri hiyo basi, wao wenyewe wakawa ni wenye kurudi nyuma, na ni mtu mmoja tu ndiye aliyekwenda kwa Mtume (s.a.w.w), na kumuuliza masuala baada ya kushuka Aya hii, naye alitoa dirham kumi, kisha akauliza masuala muhimu ya kidini mbele ya Mtume (s.a.w.w). Naye alikuwa ni Dinar ambaye ni Mtumishi wa Imam Ali bin Abi Talib (a.s).

Mpaka pale ilipokuja amri nyengine na kuifuta hukumu ya Aya hiyo, nayo ni (Aya ya 13 ya Surat Mujadilah) isemayo:-

اَاَشْفَقْتُمْ اَن تُقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيْ نَجْوَاكُمْ صَدَقَاتٍ فَإِذْ لَمْ تَفْعَلُوا وَتَابَ اللهُ عَلَيْكُمْ فَاَقِيمُوا الصَّلاَةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَاَطِيعُوا اللهَ وَرَسُولَهُ وَاللهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ[2]

Maana ya Aya hiyo ni kama hivi ifuatavyo:-

“ Oh! Mnaona tabu kutanguliza hiyo Sadaqa kabla ya kumsemeza kwenu? Ikiwa hamjafanya haya basi. (Yamekwisha hayo). Na Mwenyeezi Mungu amekusameheni. Basi simamisheni sala na toeni Zaka na Mtiini Mwenyeezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyeezi Mungu anayo habari ya mnayoyatenda yote”.

Na kwa kupitia Aya hii hukumu ya Aya ya mwanzo ikawa imefutwa.

Na mpaka hapa tumeona wazi kwamba, hukumu ya Aya ya mwanzo imefutwa hali ikiwa Aya yenyewe ingalipo katika Qur-ani, kwani hukumu ya mwanzo ilikuwa ni kutoa sadaqa kwa kila suala watakalouliza Masahaba, na Aya ya pili ikaja kuifuta hukumu ya Aya hiyo. ni

ايات صفح))

AYA YA KUSAMEHE NA KUVUMILIA MAOVU

Waislamu katika zama za mwanzo kabisa waliamrishwa kustahamili wanapotendewa maovu na Washirikina, kwani wao walikuwa ni madhaifu katika mji wa Makka, na iwapo watakabiliana na maovu hayo yawezekana jambo hilo kuwapelekea wao (Waislamu) kutoweshwa na Makafiri, na Mwenyeezi Mungu katika (Surat Jaathiya Aya ya 14) akamwambia mjumbe wake.

قُل لِّلَّذِينَ آمَنُوا يَغْفِرُوا لِلَّذِينَ لا يَرْجُون اَيَّامَ اللهِ لِيَجْزِيَ قَوْماً بِما كَانُوا يَكْسِبُونَ[3]

Maana ya Aya hiyo ni hii ifuatayo:-

“Waambie wale walioamini wawasamehe wale wasioziogopa siku za Mwenyeezi Mungu (za kuwatia adabu wabaya), ili awalipe watu kwa yale waliyokuwa wakiyachuma”

Ama baada ya jamii ya Kiislamu kupata nguvu ilitolewa idhini na Mwenyeezi Mungu ya watu kupigana vita vya jihadi. Kama vile Allah (s.w) katika (Suratul-Hajj aya ya 39) anasema:

اُذِنَ لِلَّذِينَ يُقَاتَلُونَ بِاَنَّهُمْ ظُلِمُوا وَإِنَّ اللهَ عَلـٰي نَصْرِهِمْ لَقَدِيرٌ[4]

Maana ya Aya hiyo ni kama hivi ifuatavyo:-

Wameruhusiwa (kupigana) wale wanaopigwa, kwa sababu wamedhulumiwa. Na kwa yakini mwenyeezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia;

Baadae ikatolewa dasturi nyengine inayokabiliana na desturi hiyo ya mwanzo, pale Allah (s.w) katika (Suratul Anfal Aya ya 65) aliposema:-

يَا اَيُّهَا النَّبِيُّ حَرِّضِ الْمُؤْمِنِينَ عَلـٰي الْقِتَالِ إِن يَكُن مِّنكُمْ عِشْرُونَ صَابِرُونَ يَغْلِبُواْ مِئَتَيْنِ وَإِن يَكُن مِّنكُم مِّئَةٌ يَغْلِبُواْ اَلْفاً مِّنَ الَّذِينَ كَفَرُواْ بِاَنَّهُمْ قَوْمٌ لاَّ يَفْقَهُونَ[5]

Maana ya Aya hiyo ni kama ifuatavyo:-

Ewe Mtume (wa Mwenyeezi Mungu! Wahimize walioamini wende vitani. Wakipatikana kwenu watu ishirini wanaosubiri watashinda mia mbili, (katika hao makafiri. Basi nyinyi mkiwa ishirini lazima msimame mpigane na watu miteni). Na kama wakiwa watu mia moja kwenu watashinda elfu moja ya wale waliokufuru, maana hao ni watu wasiofahamu (uhai wa Akhera, basi wanaogopa kupigana kwa ushujaa sana wasije wakafa. Basi watu mia katika nyinyi wasiwakimbie watu elfu moja katika wao).

Maelezo kuhusiana na Aya ya 39 ya Suratul-Hajj.

Waislamu waliishi Makka muda wa miaka kumi na tatu, wakiadhibiwa kwa adhabu zisizostahamilika. Na juu ya hayo hawakupewa ruhusa ya kujitetea. Na mwisho wakapewa amri ya kutupa watani wao, mali yao na watu wao, wahamie Madina. Huko ndiko ilikoshuka Aya hii kuwapa ruhusa ya kujitetea.

Na vile vile katika (Suratul-Baqara aya ya 194) Allah (s.w) anasema:-

الشَّهْرُ الْحَرَامُ بِالشَّهْرِ الْحَرَامِ وَالْحُرُمَاتُ قِصَاصٌ فَمَنِ اعْتَدَي عَلَيْكُمْ فَاعْتَدُواْ عَلَيْهِ بِمِثْلِ مَا اعْتَدَي عَلَيْكُمْ وَاتَّقُواْ اللّهَ وَاعْلَمُواْ اَنَّ اللّهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ[6]

Maana ya Aya hiyo ni kama ifuatavyo:-

Mwezi Mtakatifu kwa mwezi Mtakatifu. Na vitu vitakatifu vimeekewa kisasi (vikiondolewa hishima yake). Na wanaokushambulieni, nanyi pia washambulieni, na kadiri walivyokushambulieni. Na muogopeni Mwenyeezi Mungu (msiongeze kuliko walivyokufanyieni) na jueni kwamba Mwenyeezi Mungu yu pamoja na wanaomuogopa.

Maelezo kuhusiana na Aya ya 194 ya suratul-Baqara

Mwezi wa mfunguo pili, mfunguo tatu, mfunguo nne, na mfunguo kumi, (rajabu) ni miezi mitukufu. Na hata hao makafiri wa Kiarabu wa hapo zamani wakiiheshimu ila kwa nadra tu, ndio wakivunja heshima yake. Basi waliivunja heshima yake safari moja wakataka kumpiga Mtume na Masahaba wake. Basi Mtume akaambiwa kuwa wakivunja makafiri heshima ya miezi hii wakawapiga, na wao nawavunje wawapige – wasifunge mikono wakawa wanauwawa tu.

Na katika Suratul-Tawba Aya ya 5, Allah (s.w) anasema:-

فَإِذَا انسَلَخَ الاَشْهُرُ الْحُرُمُ فَاقْتُلُواْ الْمُشْرِكِينَ حَيْثُ وَجَدتُّمُوهُمْ وَخُذُوهُمْ وَاحْصُرُوهُمْ وَاقْعُدُواْ لَهُمْ كُلَّ مَرْصَدٍ فَإِن تَابُواْ وَاَقَامُواْ الصَّلاَةَ وَآتَوُاْ الزَّكَاةَ فَخَلُّواْ سَبِيلَهُمْ إِنَّ اللّهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ[7]

Maana ya Aya hiyo ni kama ifuatavyo:-

Na ile miezi mitukufu itakapokwisha (ile miezi minne waliyopewa), basi waueni (piganeni na) washirikina popote muwakutapo, na wakamateni mateka (kama wanavyokufanyieni) na wazungukeni na wakalieni katika kila njia. Lakini wakitubu na wakasimamisha Sala na wakatoa Zaka, basi iacheni njia yao (waacheni). Hakika Mwenyeezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu.

Maelezo kuhusiana na Aya ya 5 ya Surat-Tawba.

Makafiri wamekosea miezi inayoitwa (L-ashhurul Hurum, badala ya shawwal) inataka atie Mfunguo nne. Wala si kweli maneno yao haya:

“…makafiri walipewa muda wa miezi minne kuizunguka bara Arabu yote ili wajionee wenyewe mafanikio yaliyobashiriwa na Uislamu yametimia namna gani.” Kwani wakati huo ndio kwanza Bara Arabu inaanza kusilimu, waone mafanikio gani?.

Uislamu unavyowapa wasiokuwa Waislamu haki ya kufuata dini waitakayo na kuwakhami hasa, wasidhuriwe. Dini gani nyengine inayofanya hivi? Na juu ya hivi maadui wake wanatangaza kuwa Uislamu umesimama kwa upanga.

“Lakini akutukanaye hakuchagulii tusi”.

[1] (Surat Mujadila aya ya 12)

[2] Surat Mujadilah Aya ya 13

[3] Surat Jaathiya Aya ya 14

[4] Suratul-Hajj aya ya 39

[5] Suratul Anfal Aya ya 65

[6] Suratul-Baqara aya ya 194

[7] Suratul-Tawba Aya ya 5

MWISHO