BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
TAWHIYD NA NIDHAMU YA DUNIA
Hakuna shaka ya kuwa Mwenyeenzi Mungu Mtukufu ameviumba vitu vyote duniani vikiwa katika nidhamu maalum, na Allah (s.w) anasema:-
الَّذِى خَلَقَ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ طِبَاقاً مَّا تَرَي فِى خَلْقِ الرَّحْمَنِ مِن تَفَاوُتٍ فَارْجِعِ الْبَصَرَ هَلْ تَرَي مِن فُطُورٍ[1]
Aliye umba mbingu saba kwa matabaka. Huoni tafauti yoyote katika uumbaji wa Mwingi wa Rehema. Hebu rudisha nadhari! Unaona kosa lolote?
Nidhamu hiyo ya uumbaji inathibitisha kuwepo kwa Mola mmoja, na Mola huyo ndiye aliyeviumba vitu vyote duniani, na kasha akaviweka katika nidhamu maalumu.
Kwani kama kuna mungu zaidi ya mmoja kusingelikuwa na nidhamu yoyote na kungelikuwa na hitilafu na tofauti baina ya muumba mmoja na mwengine, basi natuzingatie ayah ii inayothibitisha kauli hiyo.
لَوْ كَانَ فِيهِمَا آلِهَةٌ إِلاَّ اللهُ لَفَسَدَتَا فَسُبْحَانَ اللهِ رَبِّ الْعَرْشِ عَمَّا يَصِفُونَ[2]
Lau wangeli kuwamo humo miungu wengine isipo kuwa Mwenyezi Mungu basi bila ya shaka hizo mbingu na ardhi zingeli fisidika. Subahana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu,Bwana wa A'rshi (Kiti cha Enzi), na hayo wanayo yazua.
Maelezo kuhusiana na aya
Hii ni kawaida isiyoanguka kuwa “ Mafahali wawili hawakai zizi Moja” Basi wangekuwako waungu wawili wangepigana daima hata mmoja amshinde mwenziwe au wauwane; udhia wishe.
Na muda wote huo- wa kuzatiti vita mpaka kutiana mikononi- hawatashughulikia jengine ila hilo tu la kutafuta kushinda. Tena mambo atayaendesha nani?
Na wakiwa wengi zaidi kuliko wawili ndiyo vivyo hivyo- watapigana mpaka wamalizane. Au- tuseme wapatane. Na wakipatana basi watauparaganya tu mwenesho wa ufalme wao kwani kwa “Manahodha Wengi jahazi huzama.”
Basi Mwenyeenzi mungu ni mmoja tu. Wahadahu Laa Sharyka Lahuu.
Na watu mambo yao ndiyo vivi hivi. Yakiwa yanaendeshwa na chungu ya wakubwa – na kila mmoja hakubali kumsikiliza mwenziwe – basi yataharibika tu.
Ndiyo maana Mtume akihimiza kuwa sharti – katika kila mkusanyiko – apatikane mkubwa anayetiiwa na wote kwa anayoyasema yakaingia shariani;au akilini yakiwa hayahusu sheria. Akisema Mtume kuwa watu – wakishakuwa watatu – katika msafara wao – basi sharti wamfanye mmoja mkubwa wao kwani mambo hayatengenei yakiwa fujo, ovyo ovyo, hayana mkubwa. Inasemwa kwa kiarabu; Laa yasluhunaasu fawdhaa Laa saraatalahum. Yaani mambo hayatengenei yakiwa ovyo,hayana mkubwa au wakubwa wa kuyaendesha.
Na sharti ya hao wakubwa – ilivyoweka uislamu – ni wawe na elimu nzuri na utambuzi kamili. Ikiwa si hivyo, si wakubwa hao, wala mambo hayataendelea .
Inasemwa: Walaa saraata Idhaa Fuhhaaluhum saaduu.
TAWHIYD ( KUAMINI MOLA MMOJA) NDANI YA SHERIA ZA VITABU VYA MWENYEENZI MUNGU
Vitabu vyote alivyoviteremsha Mwenyeezi Mungu (s.w) vinathibitisha sheria moja , Nayo ni kuwa na imani ya Mola mmoja tu.
Ijapokuwa “ tawhiyd” na kuamini Mola mmoja ni dalili moja wapo inayoonesha nidhamu ya dunia, lakini vile vile sheria ya vitabu vyote vya Mwenyeenzi Mungu yaani (Qur-ani, Tawrati, na Injili) vimekuja na sheria moja tu, nayo ni kuamini Mola mmoja. Imamu Ali (a.s) katika wasia wake aliomuusia mwanawe Imam Hassan (a.s) anasema:-
[3]“واعلم یا بنی انه لو کان لربک شریک لاتتک رسله و لرایت اثار ملکه و سلطانه”
Ewe mwanangu elewa kuwa kama Mwenyeenzi Mungu angelikuwa na mshirika, Mitume yake ingelikuja kwako wewe, na ungeliona alama na uwezo wake Allah (s.w).
Ijapokuwa sheria za vitabu vyote vya Mwenyeenzi Mungu zinawiana kifikra na kijamii miongoni mwa wanaadamu, na zinahitilafiana katika baadhi ya hukumu,ama katika nguzo za dini, akida (itikadi), na tawhiyd hakuna tofauti yoyote . Kama vile anavyosema Allah katika Qur-ani.:-
وَمَا اَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلاَّ نُوحِى إِلَيْهِ اَنَّهُ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اَنَا فَاعْبُدُونِ[4]
Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipo kuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu.
[1] Surat Mulk aya ya 3
[2] Surat Anbiyaa aya ya 22
[3] Nahjulbalagha, barua ya 3
[4] Surat anbiyaa aya ya 25
MWISHO