BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
QUDRA YA MOLA ISIYO NA MPAKA
* Uwezo na kudura ya Mwenyeezi Mungu katika nidhamu ya dunia inadhihirika vipi?
*Kuna uhusiano gani baina ya sifa ya elimu ya Mwenyeezi Mungu, na sifa ya uwezo wa Mwenyeezi Mungu?
* Hivi kweli hiyari ya mwanaadamu inaendana sambamba na Qudra (uwezo) ya Mwenyeenzi Mungu?.
Qudura ya Mwenyeezi Mungu isiyo na mpaka.
Baada ya elimu ya Mwenyeezi Mungu, miongoni mwa sifa nyengine muhimu kamilifu za Mwenyeezi Mungu ni Qudra na uwezo wake Yeye Allah (s.w), ambayo sifa hiyo ndiyo chanzo cha sifa nyingi nyengine za kitukufu za Allah (s.w). Viumbe vyote alivyoviumba Mwenyeenzi Mungu, vikubwa na vidogo, miti, mimea na wanyama, vinaonesha Qudra yake Allah (s.w), na alionesha Qudra yake hiyo pale alipomuumba mwanaadamu ambaye ni kiumbe bora takatifu, basi Mwenyeezi Mungu alipomuumba mwanaadamu huyo alijipongeza kwa kusema:-
ثُمَّ خَلَقْنَا النُّطْفَةَ عَلَقَةً فَخَلَقْنَا الْعَلَقَةَ مُضْغَةً فَخَلَقْنَا الْمُضْغَةَ عِظَاماً فَكَسَوْنَا الْعِظَامَ لَحْماً ثُمَّ اَنشَاْنَاهُ خَلْقاً آخَرَ فَتَبَارَكَ اللهُ اَحْسَنُ الْخَالِقِينَ[1]
Kisha tukaiumba tone kuwa damu iliyo ganda, na tukaiumba damu kuwa pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa, na mifupa tukaivika nyama. Kisha tukamfanya kiumbe mwengine. “Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mbora wa waumbaji”.
Basi hapana shaka ya kuwa uumbaji huo wa Mwenyeezi Mungu ni alama inayoonesha Qudra na uwezo wake Yeye Allah (s.w).
Kwa hiyo pindi mwanaadamu akizingatia kwa makini utukufu na uwezo wake Mwenyeezi Mungu, kutampelekea yeye kukuza na kuimarisha imani yake, katika kipengele hiki basi na tutupie macho maelezo ya Qur-ani kariym kuhusiana na maudhui hayo. – yaani – Qudra na uwezo wa Allah (s.w).
Ufafanuzi wa neno Qudra:
Katika Qur-ani kariym maana asili ya neno qudra ni kuwa na uwezo, na kinyume chake ni kutokuwa na uwezo, kama tunavyoshuhudia katika Aya hii tukufu.
ضَرَبَ اللّهُ مَثَلاً عَبْداً مَّمْلُوكاً لاَّ يَقْدِرُ عَلـٰي شَيْءٍ وَمَن رَّزَقْنَاهُ مِنَّا رِزْقاً حَسَناً فَهُوَ يُنفِقُ مِنْهُ سِرّاً وَجَهْراً هَلْ يَسْتَوُونَ الْحَمْدُ للهِ بَلْ اَكْثَرُهُمْ لاَ يَعْلَمُونَ[2]
Mwenyezi Mungu anapiga mfano wa mtumwa aliye milikiwa, asiye weza kitu, na mwingine tuliye mruzuku riziki njema inayo toka kwetu, naye akawa anatoa katika riziki hiyo kwa siri na dhaahiri. Je, hao watakuwa sawa? Alhamdu Lillahi! Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu.
Lakini wengi wao hawajui.
Kwa hiyo kwa kuzingatia aya hiyo tumefahamu kuwa mandhuri na maana ya neno qudura ya Mwenyeezi Mungu, yaani Mwenyeezi Mungu hufanya kila analolitaka, na humpa amtakaye.
اللهُ الَّذِى خَلَقَكُم مِّن ضَعْفٍ ثُمَّ جَعَلَ مِن بَعْدِ ضَعْفٍ قُوَّةً ثُمَّ جَعَلَ مِن بَعْدِ قُوَّةٍ ضَعْفاً وَشَيْبَةً يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ وَهُوَ الْعَلِيمُ الْقَدِيرُ[3]
Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni kutokana na udhaifu kisha akajaalia nguvu baada ya unyonge, kisha akajaalia baada ya nguvu unyonge tena na ukongwe. Anaumba atakavyo. Naye ndiye Mjuzi, Mwenye uweza.
UTUKUFU WA QUDRA YA MWENYEEZI MUNGU
1- Nidhamu ya kimaumbile:
Viumbe vyote duniani vikiwemo mabara, na viumbe vyote vinavyoishi duniani, vinavyoonekana na visivyoonekana, vyote ni katika utukufu wa uwezo wake Allah (s.w), na uhakika huo mtukufu umeelezewa katika Aya tofauti ndani ya Qur-ani, miongoni mwa aya hizo ni:-
وَاللهُ خَلَقَ كُلَّ دَابَّةٍ مِن مَّاء فَمِنْهُم مَّن يَمْشِى عَلـٰي بَطْنِهِ وَمِنْهُم مَّن يَمْشِى عَلـٰي رِجْلَيْنِ وَمِنْهُم مَّن يَمْشِى عَلـٰي اَرْبَعٍ يَخْلُقُ اللهُ مَا يَشَاءُ إِنَّ اللهَ عَلـٰي كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ[4]
Na Mwenyezi Mungu ameumba kila kinyama kutokana na maji. Wengine katika wao huenda kwa matumbo yao, na wengine huenda kwa miguu miwili, na wengine huenda kwa miguu mine. Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
2- Nidhamu isiyo ya kimaumbile.
Utukufu mwengine wa Mwenyeezi Mungu unaoonesha qudra ya Mwenyeezi Mungu ni nidhamu isiyo ya kimaumbile, katika nidhamu hii imeelezewa kwa uwazi kabisa kuwa Mwenyeezi Mungu kwa ajili ya kuwaongowa na kuwaongoza viumbe wake amewachagua Mitume na kuwatuma kwa viumbe wake ili kwa kupitia hao wanaadamu wapate kuongoka na kufuata njia ambayo itawaongoza katika saada.
Katika qur-ani tunasoma:-
يَا اَهْلَ الْكِتَابِ قَدْ جَاءكُمْ رَسُولُنَا يُبَيِّنُ لَكُمْ عَلـٰي فَتْرَةٍ مِّنَ الرُّسُلِ اَن تَقُولُواْ مَا جَاءنَا مِن بَشِيرٍ وَلاَ نَذِيرٍ فَقَدْ جَاءكُم بَشِيرٌ وَنَذِيرٌ وَاللّهُ عَلـٰي كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ[5]
Enyi Watu wa Kitabu! Bila ya shaka amekujilieni Mtume wetu akikubainishieni katika wakati usio kuwa na Mitume, msije mkasema: Hakufika kwetu mbashiri wala mwonyaji. Basi amekujieni mbashiri na mwonyaji. Na Mwenyezi Mungu anao uweza wa kila kitu.
3- Nidhamu ya siku ya kiama
Utukufu mwengine unaoonesha uwezo wa Mwenyeezi Mungu ni kumalizika kwa dunia, na kila mja kupewa hesabu na malipo ya amali zake.
لِّلَّهِ ما فِى السَّمَاواتِ وَمَا فِى الاَرْضِ وَإِن تُبْدُواْ مَا فِى اَنفُسِكُمْ اَوْ تُخْفُوهُ يُحَاسِبْكُم بِهِ اللّهُ فَيَغْفِرُ لِمَن يَشَاءُ وَيُعَذِّبُ مَن يَشَاءُ وَاللّهُ عَلـٰي كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ[6]
Viliomo mbinguni na viliomo duniani ni vya Mwenyezi Mungu. Na mkidhihirisha yaliyomo katika nafsi zenu au mkayaficha, Mwenyezi Mungu atakuhisabuni kwayo. Kisha amsamehe amtakaye na amuadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
[1] Suratul-Mu-uminuun Aya ya 14
[2] Suratun-Nahl Aya ya 75
[3] Surat Ruum Aya ya 54
[4] Surat Nuur aya ya 45
[5] Surat Maidah aya ya 19
[6] Suratul-Baqara Aya ya 284
MWISHO