WANAFIQ NDANI YA QUR_ANI
  • Kichwa: WANAFIQ NDANI YA QUR_ANI
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 22:22:4 1-9-1403

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
WANAFIQ NDANI YA QUR-ANI

WANAMHADAA MWENYEZI MUNGU NA ATAWALIPA KWA KUHADAA KWAO
Mwenyeezi Mungu Mtukufu anasema:-

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللّهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُواْ إِلَي الصَّلاَةِ قَامُواْ كُسَالَي يُرَآؤُونَ النَّاسَ وَلاَ يَذْكُرُونَ اللّهَ إِلاَّ قَلِيلا مُّذَبْذَبِينَ بَيْنَ ذٰلِكَ لاَ إِلَي هَـؤُلاء وَلاَ إِلَي هَـؤُلاء وَمَن يُضْلِلِ اللّهُ فَلَن تَجِدَ لَهُ سَبِيلاً[1]
Hakika wanaafiki wanamkhadaa Mwenyezi Mungu, na hali ni Yeye ndiye mwenye kuwakhadaa wao. Na wanapo inuka kusali huinuka kwa unyong'onyo, wanajionyesha kwa watu tu, wala hawamdhukuru Mwenyezi Mungu ila kidogo tu. Wanayumba yumba baina ya huku na huko. Huku hawako na huko hawako. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea kabisa hutompatia njia.
Ufafanuzi wa aya.
Wanafiki walikuwa wakijitia pamoja na Waislamu katika mambo yao yote, ili wasipate kutambulikana kuwa wao wanafiki. Lakini walikuwa hawayaonei raha, wanafanya kwa kuwa hawana budi tu. Wao wanachunga manufaa yao ya kidunia tu – yakiwa kwa makafiri au Waislamu,hawako huku wala hawako huko.
Hakika wanafiki wanamhadaa Mwenyezi Mungu, na hali yeye ndiye mwenye kuwahadaa.
Makusudio ya kuhadaa kwao ni kule kuonyesha imani kwa Mtume na kuficha ukafiri. Kwa sababu mwenye kumhini Mtume ndio amemhini Mwenyezi Mungu. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu:
إِنَّ الَّذِينَ يُبَايِعُونَكَ إِنَّمَا يُبَايِعُونَ اللهَ يَدُ اللهِ فَوْقَ اَيْدِيهِمْ فَمَن نَّكَثَ فَإِنَّمَا يَنكُثُ عَلـٰي نَفْسِهِ وَمَنْ اَوْفَي بِمَا عَاهَدَ عَلَيْهُ اللهَ فَسَيُؤْتِيهِ اَجْراً عَظِيماً[2]
Bila ya shaka wanao fungamana nawe, kwa hakika wanafungamana na Mwenyezi Mungu. Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao. Basi avunjaye ahadi hizi anavunja kwa kuidhuru nafsi yake; na anaye tekeleza aliyo muahadi Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atamlipa ujira mkubwa.
Makusudio ya kuwa Mwenyezi Mungu anawahadaa ni kwamba yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu atawaadhibu kwa hadaa yao na unafiki wao. Na wanapoinuka kwenda kuswali, huinuka kivivu.
Wataichangamkiaje na wao wanaikanusha? Hawatarajii thawabu kwa kuitenda wala adhabu kwa kuiacha; isipokuwa wanaitekeleza kwa kuwinda dunia tu na kuifanya ni nyenzo ya uchumi. Mwenyezi Mungu anasema:

وَاسْتَعِينُواْ بِالصَّبْرِ وَالصَّلاَةِ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلاَّ عَلـٰي الْخَاشِعِينَ[3]
Na tafuteni msaada kwa kusubiri na kwa kusali; na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu.
Ufafanuzi.
"Kwa hakika hiyo Swala ni ngumu isipokuwa kwa wanyenyekevu.”
Ingawa maneno haya wanaambiwa mayahudi, lakini yanawahusu watu wote, kama ilivyo ada  ya Qur-ani. Subira imesifiwa mara nyingi katika Qur-ani, mtu akisubiri katika kuendelea na mema aliyoamrishwa na katika kuacha mabaya anayoyapenda, na akasubiri juu ya mashaka na tabu za ulimwenguni bila shaka atafaulu duniani na Akhera.
Unaweza kuuliza: Mtu akiswali kwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na pamoja na hayo anapenda watu wamuone, ili wamhisabu katika watu wema au asituhumiwe kuwa aniipuuza dini. Je hii itakuwa ni ria?

Jibu: Hapana! Maadamu msukumo wa kwanza ni wa amri ya Mwenyezi Mungu na radhi zake; mengine yanafuatia tu, Imam as-Sadiq (a.s.) aliulizwa kuhusu mtu ambaye anafanya jambo la kheri, kisha akafurahi kwa kuonwa na mtu mwingine akilifanya jambo hili (nini hukumu ya mtu huyo)? Imam akajibu: "Hapana ubaya kwa hilo, ikiwa hakuifanya kwa hilo, kwani hakuna mtu asiyependa Mwenyezi Mungu amdhihirishie kheri mbele ya watu,."
Wanajionyesha kwa watu.
Kwa sababu wao huswali kwa ajili ya kuwinda na kupata faida.
Wala hawamtaji Mwenyezi Mungu ila kidogo tu. Yaani wakati wa kujionyesha kwa watu. Ama wakiwa peke yao, hawamtaji kabisa. Imam Jafar as-Sadiq (a.s.) anasema: "Mwenye kujionyesha (ria) ana alama tatu: Anakuwa mvivu  akiwa peke yake, anachangamka akiwa na watu na hupenda kusifiwa kwa asilolifanya."
 JE WATU WOTE HUJIONYESHA
Unaweza kuuliza: Hakuna yeyote anayedhihirisha ukweli wake kwa watu na kuwaambia kila analoitakidi. Ni nani anayeweza kumwambia kila mtu anayoyajua. Na akifanya hivyo, basi atahisabiwa katika wenda wazimu, bali ni nani ambaye - mara nyingine - hafanyi asiyoyapenda na kuyataka? Kisha utaziepuka vipi desturi na maadili ya jamii? Je, unaweza kumwambia mtu uliyekutana naye, ambaye humpendi, akakwambia 'natamani kukuona,' na wewe umwambie: nachukia kukuona? Na kama utamwambia hivyo je unavyoona wewe au waonavyo watu utakuwa uko sawa? Mwisho je watu wote wanafanya ria (kujionyesha), kwa sababu hawaitakidi yote wayasemayo; wala hawaamini yote wayafanyao?

Jibu: Kuna tofauti baina ya Ria na Mudarat. Ria ni kudhihirisha unafiki na uzushi ili uwe pamoja na wema na wewe si katika wao. Na Mudarat ni kuwa mpole na kutowachukilia na kuamiliana na watu bila ya kulenga chochote zaidi ya kutaka kuishi nao katika uelewano na maafikiano.

Ni kweli kuwa mara nyingine unafanya mambo kufuata desturi ya jamii; ukapongeza, kutoa rambi rambi au kutabasamu na kumheshimu mtu kwa jamala tu si kwa kuamini, lakini jambo hili ni salama halina tashwishi yoyote.
Wala halihisabiwi kuwa ni ria maadam kulifanya kwako kunaafikiana na jamii. Vilevile si wajibu juu yako kama utatokewa na kosa - hakuna maasum – kulitangaza kwa watu. Ndio ni wajibu kuwadhihirishia usafi sio makosa. Vilevile ni kweli kuwa unasema uongo unapomwambia unayemchukia 'mimi nakupenda,' lakini ni uongo ulio katika masilahi na hulka njema. Mwenyezi Mungu anasema:
وَإِذْ اَخَذْنَا مِيثَاقَ بَنِى إِسْرَائِيلَ لاَ تَعْبُدُونَ إِلاَّ اللّهَ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَاناً وَذِى الْقُرْبَي وَالْيَتَامَي وَالْمَسَاكِينِ وَقُولُواْ لِلنَّاسِ حُسْناً وَاَقِيمُواْ الصَّلاَةَ وَآتُواْ الزَّكَاةَ ثُمَّ تَوَلَّيْتُمْ إِلاَّ قَلِيلاً مِّنكُمْ وَاَنتُم مِّعْرِضُونَ[4]
Na tulipo funga agano na Wana wa Israili: Hamtamuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu; na muwafanyie wema wazazi na jamaa na mayatima na masikini, na semeni na watu kwa wema, na shikeni Sala, na toeni Zaka. Kisha mkageuka isipo kuwa wachache tu katika nyinyi; na nyinyi mnapuuza.

"Na semeni na watu kwa uzuri" .

اَلَمْ تَرَ كَيْفَ ضَرَبَ اللّهُ مَثَلاً كَلِمَةً طَيِّبَةً كَشَجَرةٍ طَيِّبَةٍ اَصْلُهَا ثَابِتٌ وَفَرْعُهَا فِى السَّمَاء[5]

Je hukuona vipi Mwenyezi Mungu alivyopiga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri mizizi yake ni imara na matawi yake yako mbinguni."
Ufafanuzi

Inapigiwa mfano kheri namna inavyotanda vizuri ikaleta ikaleta nafuu kila upande.

فَقُولاَ لَهُ قَوْلاً لَّيِّناً لَّعَلَّهُ يَتَذَكَّرُ اَوْ يَخْشَي قَالاَ رَبَّنَا إِنَّنَا نَخَافُ اَن يَفْرُطَ عَلَيْنَا اَوْ اَن يَطْغَي[6]
Nendeni kwa firaun hakika yeye amepetuka mpaka. Kamwambieni maneno laini huenda akaonyeka au akaogopa.

Mwambieni maneno laini, huenda akazingatia au akaogopa.Wakasema: Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tunaogopa asije akapindukia mipaka juu yetu au kufanya jeuri.

Kuna Hadith isemayo: "Tamko jema ni sadaka, hupewa thawabu alisemaye, thawabu za wenye fadhila na ihsan." Hadith nyigine inasema: "Ameniamrisha Mola wangu kuwachukulia watu upole (Mudarat), kama alivyoniamrisha faradhi (wajib)." Wamekongamana mafakihi kwamba uongo ni wajibu ikiwa utakuwa ni kutetea nafsi isiyo na hatia na kuiepusha na maangamivu. Na kwamba ukweli ni haram katika ufitini na usengenyaji. Kwa hiyo mfitini ni mkweli na msengenyaji ni mkweli, lakini wanashutumiwa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele za watu.

Baada ya yote hayo ni kwamba ria ya haramu ni ile ya kudhihirisha mambo asiyokuwa nayo mbele za watu; anajionyesha kuwa ana kheri ili apate hadhi ya watu wema na huku mwenyewe ni katika waovu wafisadi.
Maandiko ya Qur'an na Hadith yako kwenye misingi ya kufanya lenye masilahi na kuacha lenye uharibifu. Penye masilahi ni amri na penye uharibifu ni katazo. Kwa hiyo ndio ikajuzu kusema uongo pamoja na masilahi na ikawa haramu kusema ukweli pamoja na uharibifu wenye masengenyo na upeke peke.

Na heri yoyote muitendayo - kuwatendea mayatima na wananwake – basi Mwenyezi Mungu anaijua. Kwa ufupi maana ya Aya ni kuwa waislamu walimtaka Mtume kuwabainishia hukumu ya wanawake. Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamwambia Mtume wake:
waambie Mwenyezi Mungu amewabainishia sehemu ya hukumu hii na sasa anawabainishia sehemu nyingine, la muhimu kwenu ni kufanya uadilifu na kuitumia hukumu hiyo. Kisha akawabainishia Mwenyezi Mungu (s.w.t.), katika Aya inayofuatia hukumu ya mwanamke, anayehofia unashiza wa mumewe na kuachana na mumewe.
 وَإِنِ امْرَأَةٌ خَافَتْ مِن بَعْلِهَا نُشُوزًا أَوْ إِعْرَاضًا فَلاَ جُنَاْحَ عَلَيْهِمَا أَن يُصْلِحَا بَيْنَهُمَا صُلْحًا وَالصُّلْحُ خَيْرٌ وَأُحْضِرَتِ الأَنفُسُ الشُّحَّ وَإِن تُحْسِنُواْ وَتَتَّقُواْ فَإِنَّ اللّهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا [7]
Ikiwa mke atahofia mumewe kuwa nashiza au kumtelekeza, basi hapana vibaya juu yao kusikilizana kwa suluhu; Na suluhu ni bora. Na nafsi zimewekewa mbele uchoyo. Na mkifanya wema na mkajihifadhi, basi Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa myatendayo.
 وَلَن تَسْتَطِيعُواْ أَن تَعْدِلُواْ بَيْنَ النِّسَاء وَلَوْ حَرَصْتُمْ فَلاَ تَمِيلُواْ كُلَّ الْمَيْلِ فَتَذَرُوهَا كَالْمُعَلَّقَةِ وَإِن تُصْلِحُواْ وَتَتَّقُواْ فَإِنَّ اللّهَ كَانَ غَفُورًا رَّحِيمًا[8]
Wala hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wanawake hata mkikamia. Basi msipondokee kabisa kabisa, mkamwacha (mwingine) kama aliyetundikwa. Na mkisikilizana na mkamcha Mungu, basi Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.
 وَإِن يَتَفَرَّقَا يُغْنِ اللّهُ كُلاًّ مِّن سَعَتِهِ وَكَانَ اللّهُ وَاسِعًا حَكِيمًا
Na watakapotengana, Mwenyezi Mungu atamtosheleza kila mmoja kwa wasaa wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye hekima.

[1] Suratun-Nisaa aya ya 142-143
[2] Suratul-Fat-h aya ya 10
[3] Suratul-Baqara aya ya 45
[4] Surat- Ib-rahim Aya ya 24
[5] Surat-Taha aya ya 44-45
[6] Suratun Nisaa Aya ya 128
[7] Suratun Nisaa aya ya 129

MWISHO