WAHYI WA MITUME
  • Kichwa: WAHYI WA MITUME
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 21:44:44 1-9-1403

BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI

WAHYI WA MITUME

Wahyi wa aina hii ndio unaotafautisha wahyi wanaopewa Mitume na wahyi au (ujumbe) unaowafikia watu wengine, wahyi wa aina hiyo katika Qur-ani umekuja zaidi ya mara sabiini. Kwa mfano Allah (s.w) katika (Surat-Shuraa aya ya 7) anasema:-

وَكَذٰلِكَ اَوْحَيْنَا إِلَيْكَ قُرْآناً عَرَبِيّاً لِّتُنذِرَ اُمَّ الْقُرَي وَمَنْ حَوْلَهَا وَتُنذِرَ يَوْمَ الْجَمْعِ لاَ رَيْبَ فِيهِ فَرِيقٌ فِى الْجَنَّةِ وَفَرِيقٌ فِى السَّعِيرِ[1]

Na namna hivi tumekufunulia Qur-ani kwa Kiarabu ili uwaonye watu wa Makka na walio (katika nchi zilizo) pembeni mwake. (Nao ni ulimwengu mzima kwani Makka iko katikati ya ulimwengu). Na uwaonye siku ya mkutano; Siku isiyo na shaka (kuwa itakuja). Kundi moja litakuwa Peponi na kundi jengine Motoni.

Mitume ya Mwenyeezi Mungu ni katika watu watukufu ambao wamefikia katika ukamilifu na walio tayari kupokea wahyi utokao kwa Mwenyeezi Mungu. Imam Hassan Askariy akielezea kuhusiana na jambo hilo anasema:-

“Mwenyeezi Mungu Mtukufu ameifanya mioyo ya Mitume kuwa ni mioyo bora miongoni mwa mioyo ya wanaadamu wote ulimwenguni, baadae akawachagua watu wenye mioyo hiyo kuwa ni Watume wake”[2].

Mtume Muhammad (s.a.w.w) anasema:-

“Mwenyeezi Mungu hakuwachagua Mitume ila baada ya kuziweka katika ukamilifu akili za Mitume hiyo, na alimfanya Mtume Muhammad (s.a.w.w) kuwa ni m-bora wa umati wake wote”.[3]

Kutokana na mazungumzo ya bwana Sadru Diyni Shirazi, yeye anasema:-

“Kabla ya kudhihirika Mtume kuwa amefikia katika cheo cha Utume, kwa hakika undani wake (batini) Mtume huyo anakuwa tayari ameshapewa cheo hicho (cha Utume)”[4].

Kuchomoza kwa wahyi ni mfano wa kuchomoza kwa ujumbe, ambao unatokea katika kipindi maalum, ama tofauti iliyopo baina ya uchomozaji wa wahyi na uchomozaji wa ujumbe ni kwamba, chanzo cha ujumbe kinapotokea yule mtu anayepewa muongozo kutokana na ujumbe huo anakuwa haelewi, bali hufikiria ni jambo lililomjia ghafla katika akili yake, hali ya kuwa Allah (s.w) humuongoza mtu huyo kwa njia hiyo ya maficho.

Na chanzo cha uchomozaji wa wahyi ni kwamba yule mtu ambaye anapewa wahyi huo (Mtume) anakuwa anaelewa kwa uwazi kabisa kwamba wahyi huo unatoka kwa Mola wake,  na kutokana na dalili hiyo basi Mitume inakuwa haikosei katika kuupokea ujumbe unaotoka kwa Mwenyeezi Mungu. Kwa sababu wanakuwa na elimu ya kutosha na iliyo kamili waliyopewa na Mola wao kuhusiana na uteremshwaji huo wa wahyi.

Zurara alimuuliza suala Imam Sadiq (a.s) kwa kusema:-

“Mitume inakuwa na uhakika gani (yakini gani) juu ya kile ambacho wanateremshiwa (kinachowafikia), kuwa ni wahyi kutoka kwa Mwenyeezi Mungu au ni wasi wasi waliotiwa na shetani?”

Imam alimjibu kwa kusema:-

“Mwenyeezi Mungu hawachagui waja wake hao kuwa Mitume ila baada ya kuiepusha na kila mabaya mioyo ya watu hao, na kile ambacho wanateremshiwa au kupewa na Mola wao huwa ni mfano wa kitu wanachokiona kwa macho yao”. (rejea Buharul-Anwar, juzuu ya 18, ukurasa wa 262, hadithi ya 16).

Mwenyeezi Mungu ili kuwaondolea maajabu miongoni mwa waja wake juu ya Mitume, (katika Suratul-Nisaa aya ya 163-167) anasema:-

إِنَّا اَوْحَيْنَا إِلَيْكَ كَمَا اَوْحَيْنَا إِلَي نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ مِن بَعْدِهِ وَاَوْحَيْنَا إِلَي إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَالاَسْبَاطِ وَعِيسَي وَاَيُّوبَ وَيُونُسَ وَهَارُونَ وَسُلَيْمَانَ وَآتَيْنَا دَاوُودَ زَبُورا رُسُلاً قَدْ قَصَصْنَاهُمْ عَلَيْكَ مِن قَبْلُ وَرُسُلاً لَّمْ نَقْصُصْهُمْ عَلَيْكَ وَكَلَّمَ اللّهُ مُوسَي تَكْلِيما رُّسُلاً مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلاَّ يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلـٰي اللهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ وَكَانَ اللّهُ عَزِيزاً حَكِيما لَّـكِنِ اللّهُ يَشْهَدُ بِمَا اَنزَلَ إِلَيْكَ اَنزَلَهُ بِعِلْمِهِ وَالْمَلآئِكَةُ يَشْهَدُونَ وَكَفَي بِاللهِ شَهِيداً إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُواْ وَصَدُّواْ عَن سَبِيلِ اللهِ قَدْ ضَلُّواْ ضَلاَلاً بَعِيدا[5]

Maana ya aya hizo ni kama ifuatavyo:-

Tumekuletea wahyi kama tulivyowapelekea Nuhu na Manabii (wengine) baada yake. Na (kama) tulivyowapelekea Ibrahimu na Ismaili na Is-haqa na Yaaqubu na Yunusi na Haruni na Suleimani; na Daud tukampa zaburi. Na (tuliwapelekea wahyi) Mitume tuliokuhadithia (habari zao) zamani na Mitume ambao hatukukuhadithia (habari zao). Na Mwenyeezi Mungu akamsemeza Mussa.(Hao ni) Mitume waliotoa habari nzuri (kwa watu wema), wakawaonya (wabaya), ili watu wasiwe na hoja juu ya Mwenyeezi Mungu baada ya (kuletwa hawa Mitume). Na Mwenyeezi Mungu ni mwenye nguvu na Mwenye hikima. Lakini Mwenyeezi Mungu anayashuhudia aliyokuteremshia (kuwa ni haki). Ameyateremsha kwa ilimu yake. Na Malaika (pia) wanashuhudia. Na Mwenyeezi Mungu anatosha kuwa shahidi. Hakika wale waliokufuru na kuzuilia (watu) njia ya Mwenyeezi Mungu bila shaka wamepotea upotofu (upotevu) ulio mbali (na haki). Kwa maelezo ya aya hizo itafahamika kuwa hakuna maajabu yoyote kutokea mmoja miongoni mwa waja wa Mwenyeezi Mungu kupewa wahyi,kwa sababu zama zilizopita katika kipindi chote cha Tarehe pia kulikuwa na watu ambao walikuwa na sifa hizo za kutemshiwa wahyi.

AINA ZA WAHYI WA MITUME

Kutokana na maelezo ya Qur-ani wahyi wa Mitume umegawika katika aina (njia) tatu. Ambazo tuzielezea njia hizo katika maelezo yanayofuata baadae.

Allah (s.w) katika (Surat-Shuura aya ya 51-52) anasema:-

وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ اَن يُكَلِّمَهُ اللهُ إِلاَّ وَحْياً اَوْ مِن وَرَاء حِجَابٍ اَوْ يُرْسِلَ رَسُولاً فَيُوحِيَ بِإِذْنِهِ مَا يَشَاءُ إِنَّهُ عَلِيٌّ حَكِيمٌ وَكَذٰلِكَ اَوْحَيْنَا إِلَيْكَ رُوحاً مِّنْ اَمْرِنَا مَا كُنتَ تَدْرِى مَا الْكِتَابُ وَلاَ الإِيمَانُ وَلَكِن جَعَلْنَاهُ نُوراً نَّهْدِى بِهِ مَنْ نَّشَاء مِنْ عِبَادِنَا وَإِنَّكَ لَتَهْدِى إِلَي صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ[6]

Maana ya aya hizo ni kama ifuatavyo:-

Na haikuwa kwa mtu kwamba Mwenyeezi Mungu anasema naye ila kwa ilhamu (anayotiwa moyoni mwake) au kwa nyuma ya pazia (la kumsikilizisha sauti inayotokana na Mwenyeezi Mungu pasi na kumuona Mwenyeezi Mungu) au humtuma Mjumbe, (Jibrili); naye humfunulia (humletea Wahiyi) kiasi anachotaka kwa idhini Yake; bila shaka yeye ndiye aliye juu, Mwenye hikima.

Na namna hivi Tumekufunulia Wahyi kwa amri yetu. Ulikuwa hujui kitabu ni nini wala imani; lakini tumefanya kitabu hiki (Qur-ani) ni nuru ambayo kwa (nuru) hiyo Tunamuongoza Tumtakaye katika waja wetu. Na kwa yakini wewe unaongoza katika njia iliyonyooka:

Katika maelezo ya hapo juu tuliashiria kuwa wahyi wa Mitume umegawika katika aina tatu, hapa tutzitaja na kuziorodhesha aina hizo:-

1. WAHYI WA MOJA KWA MOJA.

Ni Wahyi ambao huteremshwa moja kwa moja ndani ya moyo wa Mtume. (bila ya kuwepo kitu au jambo linalopelekea kumfikia Mtume Wahyi huo). Mtume Muhammad (s.a.w.w) kuhusiana na jambo hilo anasema:-

ان روح القدس ينفث في روعي

yaani kwa hakika roho takatifu imo ndani ya nafsi yangu. Kwa maelezo hayo ni jambo linaloonesha kwa uwazi kabisa kuwa roho takatifu haimaanishi Jibrili (a.s).

2. KUUSIKIA WAHYI KWA NJIA YA SAUTI

Aina hii ya wahyi humfikia Mtume kwa kusikia kwa masikio yake, na hakuna mtu yoyote mwengine anayesikia sauti hiyo ya wahyi isipokuwa yeye (Mtume). Mtume huisikia sauti ya Mwenyeezi Mungu pasi na kumuona. mfano wa mtu ambaye anazungumza kwa nyuma ya pazia, na ni kutokana na dalili hiyo basi ikatabiriwa kwa kusemwa hivi:-

 “او من وراء حجاب”

Yaani au kwa nyuma ya pazia. Wahyi alioteremshiwa Nabii Mussa (a.s) katika mlima wa Turi ulikuwa kwa mtindo huo, na vile vile wahyi alioteremshiwa Mtume Muhammad (s.a.w.W) ndani ya usiku wa Miraji ulikuwa kwa mtindo kama huo.

3. KUTEREMSHIWA WAHYI KWA KUPITIA MALAIKA

Jibrili (a.s) alikuwa akiufikisha ujumbe wa Mwenyeezi Mungu kwa Mtume Muhammad (s.a.w), kama vile Qur-ani inavyothibitisha hayo katika (Surat-Shuaraa aya ya 193-194). Allah (s.w) anasema:-

نَزَلَ بِهِ الرُّوحُ الاَمِينُ عَلـٰي قَلْبِكَ لِتَكُونَ مِنَ الْمُنذِرِينَ[7]

 Maana ya aya hizo ni kama hivi ifuatavyo:-

Ameteremsha haya Mhuyisha Sharia mwaminifu, (jibrili). Juu ya moyo wako, ili uwe miongoni mwa Waonyaji.

NAMNA YA UTEREMSHWAJI WAHYI

Wakati Mtume Muhammad (s.a.w.w) alipokuwa akiteremshiwa wahyi wa moja kwa moja unaotoka kwa Mola wake alikuwa akijihisi mzito , kiasi ya kwamba kutokana na uzito huo mwili wake ulifika hadi ukawa moto na wenye kuunguza kupita kiasi, hadi kuchuruzikwa na kijacho kwa wingi katika paji lake la uso, na pindi ambapo ulipokuwa ukiteremshwa wahyi huo kama alikuwa amepanda ngamia au farasi basi kiuno cha mnyama hayo hupinda hadi kufikia karibu na ardhi kutokana na uzito wa wahyi huo. Imam Ali (a.s) anasema:

“Katika kipindi alichoteremshiwa Mtume Suratul-Maidah, alikuwa yuko juu ya ngamia katika sehemu inayojulikana kwa jina la (Shuhabaa). Wahyi ulikuwa mzito kiasi ya kwamba mnyama huyo alisimama na tumbo lake lilishuka chini karibu kufika katika ardhi. “Nilikiona kitovu cha mnyama huyo kinakaribia kugusa ardhi”, wakati huo Mtume Muhammad (s.a.w) alijizuilia kwa kuuweka mkono wake juu ya kichwa cha mmoja wa Masahaba zake”[8].

Ibadat bin Samit anasema:-

“Wakati Mtume alipokuwa akiteremshiwa Wahyi alibadilika rangi, wakati huo alikuwa akiinamisha kichwa chake chini, na Masahaba wake pia walifanya hivyo[9]”,

Baadhi ya wakati Mtume Muhammad (s.a.w.w) alipokuwa akiteremshiwa wahyi alijishikisha magoti yake na magoti ya mtu mwengine, mtu huyo hakuweza kustahamili uzito wa magoti ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.).

Sisi hatujui, na nafikiri hakuna mtu anayejua kwa nini Mtume alipokuwa akiteremshiwa wahyi alikuwa katika hali kama hiyo, kwa sababu hatuelewi uhakika au siri ya wahyi huo, ili kufahamu zaidi kuhusiana na maelezo hayo ya namna ya uteremshwaji wahyi, unaweza kurejea ndani ya vitabu vilivyozungumzia kuhusu namna ya uteremshwaji wahyi[10]

[1] Surat-Shuraa aya ya 7

[2] (rejea Buharul-An-war, juzuu ya 18, ukurasa wa 205, hadithi ya 36).

[3] (rejea Usuli Kafi, juzuu ya 1, ukurasa wa 13).

[4] (rejea Sharhi Usuli Kafi, juzuu ya 3, ukurasa wa 454).

[5] Suratul-Nisaa aya ya 163-167

[6] Surat-Shuura aya ya 51-52

[7] Surat-Shuaraa aya ya 193-194

[8] (rejea Tafsiri Ayashi, juzuu ya 1, ukurasa wa 388).

[9] (rejea Tabaqaat ibn saad, juzuu ya 1, ukurasa wa 131).

[10](rejea Tamhiyd fi Ulumil-Qur-ani, juzuu ya 1, ukurasa wa 66 na kuendelea).

MWISHO