BISMILAHI RAHMANI RAHIYMI
KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
TOFAUTI YA WANAADAMU
Katika makala iliyopita tulielezea kuhusu hekima za Mwenyeezi Mungu, na tukathibitisha hekima hizo kutokana na alama tunazozishuhudia katika ulimwengu huu mtukufu, katika makala hii tutaelezea alama nyengine zinazoonesha na kuthibitisha hekima za Mwenyeenzi Mungu ni uumbaji wa wanaadamu katika hali tofauti, kama inavyosema Qur-ani:-
هُوَ الَّذِى يُصَوِّرُكُمْ فِى الاَرْحَامِ كَيْفَ يَشَاءُ لاَ إِلَـهَ إِلاَّ هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ[1]
Yeye ndiye anaye kuundeni ndani ya matumbo ya wazazi kwa namna apendayo. Hapana mungu ila Yeye, Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Ushahidi mwengine unaoonesha rehema za Mwenyeenzi Mungu ni kuzaliwa kwa mamilioni ya wanaadamu katika maumbile tofauti, kabila, lugha,lahaja, n.k yote hayo yanaonesha tofauti iliyopo miongoni mwa wanaadamu, kama inavyosema Qur-ani:-
يَا اَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَاُنثَي وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوباً وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا إِنَّ اَكْرَمَكُمْ عِندَ اللهِ اَتْقَاكُمْ إِنَّ اللهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ[2]
Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane.
Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari.
Uumbaji wa mwanamke na mwanamme.
Alama nyengine inayoonesha na kuthibitisha hekima ya Mwenyeenzi Mungu, ni kuumbwa kwa mwanamke na mwanamme, kwa kuzingatia tofauti na maingiliano yanayoonekana baina ya mwanamke na mwanamme tutafahamu na kuelewa kwa undani kabisa hekima zake Allah (s.w).
Mwanamme na mwanamke katika baadhi ya mambo wako sawa na hawana tofauti yoyote, miongoni mwa hayo ni:-
Kutafuta elimu, fadhila za mwanaadamu, tabia njema, kuwa na imani thabiti, na kufanya ibada, yote hayo yanathibitisha kuwa mwanamme na mwanamke wako sawa katika kufanya matendo hayo.
Na kwa yule atakayefanya jitihada sana katika kuyafanya matendo hayo mema, atakuwa karibu na Mola wake, na Mwenyeenzi Mungu atampa ujira mkubwa kutokana na kufanya matendo hayo. Kama vile Qur-ani inavyosema:-
[3]مَنْ عَمِلَ سَيِّئَةً فَلاَ يُجْزَي إِلاَّ مِثْلَهَا وَمَنْ عَمِلَ صَالِحاً مِّن ذَكَرٍ اَوْ اُنثَي وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَاُوْلَئِكَ يَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ يُرْزَقُونَ فِيهَا بِغَيْرِ حِسَابٍ
Mwenye kutenda uovu hatalipwa ila sawa na huo uwovu wake, na anaye tenda wema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini,basi hao wataingia Peponi, waruzukiwe humo bila ya hisabu.
Kwa hiyo ili kufikia katika saada (njia iliyo bora) hakuna tofauti yoyote baina ya mwanamke na mwanmme, na wote hao wanaweza wakafikia kiwango kilicho bora kabisa kiimani na kiitikadi katika kumuabudu na kumtii Mola wao, na wakawa mfano (kigezo), kwa wengine.
Kama qur-ani inavyomuarifisha mke wa Firauna kuwa yeye ni mfano na kigezo kwa wengine.
وَضَرَبَ اللهُ مَثَلاً لِّلَّذِينَ آمَنُوا اِمْرَاَةَ فِرْعَوْنَ إِذْ قَالَتْ رَبِّ ابْنِ لِى عِندَكَ بَيْتاً فِى الْجَنَّةِ وَنَجِّنِى مِن فِرْعَوْنَ وَعَمَلِهِ وَنَجِّنِى مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ[4]
Maelezo kuhusiana na aya
Na hapa inabainishwa kuwa watu wema haitowafika balaa itakayowafika watu wao walio wabaya, kila mtu atalipwa kwa amali zake.
Cha kulipwa watu wema na wabaya “ni amali si ujamaa”.Na Mwenyezi Mungu amewapigia mfano walio amini - mkewe Firauni, alipo sema: Mola wangu Mlezi! Nijengee kwako nyumba Peponi,na uniokoe na Firauni na vitendo vyake, na uniokoe na watu madhaalimu.
Na kwa kutupia macho kauli ya Mwenyeenzi Mungu pale aliposema kuwa wanaadamu wote mwanamme na mwanamke wote wanatokana na nafsi moja. Tunathibitisha hayo kutokana na aya hii:-
يَا اَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُواْ رَبَّكُمُ الَّذِى خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالاً كَثِيراً وَنِسَاء وَاتَّقُواْ اللّهَ الَّذِى تَسَاءلُونَ بِهِ وَالاَرْحَامَ إِنَّ اللّهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيباً[5]
Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana,na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni.
Maelezo kuhusiana na Aya:-
Hapa inaonyeshwa kuwa Bibi Hawa kaumbwa katika udongo ule ule alioumbiwa Nabii adamu – siyo kaumbwa katika mbavu za Nabii Adamu,kwa hivi kila manamme ana ubavu mmoja wa kushoto kasoro kuliko mwanamke! Habari hii hakusema Mtume ingawa inatajwa katika baadhi ya vitabu vya tafsiri.
Hapa inahimizwa kumcha Mwenyeezi Mungu – kumhishimu ukafuata amri zake na ukajiepusha na makatazo yake; kwani Yeye ndiye aliyekuumba na akakuumbia vyote alivyokuumbia. Bali hata wewe mwenyewe ukitaka kumtia nguvu mwenzio asikuvunje,akufanyie unalomtaka akufanyie, unamwambia:-
“Nakuomba kwa jina la Mwenyeezi Mungu unifanyie…” kwa kuona kuwa hataweza kukuvunja maadam umemtaja Mwenyeezi Mungu. Unaona kuwa atalipa heshima ya jina la Mwenyeezi Mungu, hatalivunja, basi mbona wewe unalivunja jina la mwenyeezi Mungu?Unaacha alivyokuamrisha, au unafanya aliyokataza, unawataka watu wafanye usiyoyafanya wewe! Namna gani hivi!.Na inaambiwa hapa kuwa Mwenyeezi Mungu analiona kila jambo wanalolitenda waja wake, hata likiwa dogo vipi na likafichwa vipi.
Hayo yalikuwa na maelezo kuhusiana na aya hiyo tukufu, tukiendelea na mada yetu, Na kwa upande mwengine kwa kuzingatia mahitajio ya lazima katika maisha ya mwanaadamu,- kwa mfano nguvu, au mambo mengine yaliyopo baina ya mwanamke na mwanamme, kutokana na nguvu hizo au tofauti zilizopo baina ya mwanamke na mwanamme, - Mwenyeezi Mungu amewapa wadhifa watu hao (mwanamke na mwanamme) kutokana na sehemu waliyonayo. Kwa hiyo kwa sababu mwanamke ana hisia dhaifu na moyo mwenye upendo basi yeye ana wadhifa wa kuishughulikia familia na kuwalea watoto katika maadili mema ya kiislamu, na kwa sababu mwanamme hana moyo kama wa mwanamke,na kwa upande mwengine ana nguvu, na kiakili anadiriki zaidi Mwenyeezi Mungu amempa wadhifa mwengine.
Pale aliposema:-
الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلـٰي النِّسَاء بِمَا فَضَّلَ اللّهُ بَعْضَهُمْ عَلـٰي بَعْضٍ وَبِمَا اَنفَقُواْ مِنْ اَمْوَالِهِمْ فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللّهُ وَاللاَّتِى تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَاهْجُرُوهُنَّ فِى الْمَضَاجِعِ وَاضْرِبُوهُنَّ فَإِنْ اَطَعْنَكُمْ فَلاَ تَبْغُواْ عَلَيْهِنَّ سَبِيلاً إِنَّ اللّهَ كَانَ عَلِيّاً كَبِيراً[6]
Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, kwa kufadhiliwa na Mwenyezi Mungu baadhi yao juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayo yatoa.Basi wanawake wema ni wale wenye kut'ii na wanao jilinda hata katika siri kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameamrisha wajilinde.Na ambao mnachelea kutoka katika ut'iifu wanasihini, muwahame katika malazi na wapigeni. Wakikut'iini msiwatafutie njia ya kuwaudhi bure.Hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye juu na Mkuu.
Kwa hiyo Mwenyeezi Mungu amempa mwanamme wadhifa wa kuisimamia familia , na hii inaonyesha hekima ya Mwenyeezi Mungu katika nidhamu ya kimaumbile. Na kwa sababu hiyo basi pale Mwenyeezi Mungu alipoashiria kuwa mwanamme ni bora anasisitiza kwa kusema kuwa Yeye ni Hakiym (yaani mwenye hekima).
وَالْمُطَلَّقَاتُ يَتَرَبَّصْنَ بِاَنفُسِهِنَّ ثَلاَثَةَ قُرُوَءٍ وَلاَ يَحِلُّ لَهُنَّ اَن يَكْتُمْنَ مَا خَلَقَ اللّهُ فِى اَرْحَامِهِنَّ إِن كُنَّ يُؤْمِنَّ بِاللهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ وَبُعُولَتُهُنَّ اَحَقُّ بِرَدِّهِنَّ فِى ذٰلِكَ إِنْ اَرَادُواْ إِصْلاَحاً وَلَهُنَّ مِثْلُ الَّذِى عَلَيْهِنَّ بِالْمَعْرُوفِ وَلِلرِّجَالِ عَلَيْهِنَّ دَرَجَةٌ وَاللّهُ عَزِيزٌ حَكُيمٌ[7]
Na wanawake walio achwa wangoje peke yao mpaka t'ahara (au hedhi) tatu zipite. Wala haiwajuzii kuficha alicho umba Mwenyezi Mungu katika matumbo yao, ikiwa wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na waume wao wana haki ya kuwarejesha katika muda huo,kama wakitaka kufanya sulhu. Nao wanawake wanayo haki kwa Sharia kama ile haki iliyo juu yao. Na wanaume wana daraja zaidi kuliko wao.Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Maelezo kuhusiana na aya ya 34 ya suratun-Nisaa.
Hapa wanaambiwa wanaume wawe ndio wenye amri ya juu ya wake zao – wawaendeshe mwendo mzuri sio kujifanya washupavu hao wanawake –hawataki kutii amri za waume zao. Ikiwa hivyo hawatakuwa Waislamu wa kweli. Hata maelimu ya sasa – biology na nyenginezo yanaonyesha wazi wazi kuwa wanaume wamewashinda wanawake katika baadhi ya mambo takriban.
Tena zinatajwa baadhi ya sifa za wanawake wema na wazuri:-
Halafu ikatajwa adabu ya kutiwa wanawake wasiokuwa hivyo, kwanza waonywe kwa maneno tu na waume zao,yakiwa hayakufidi wawahujuru (wawatoe) katika malazi, - wasilale nao kitanda kimoja wala penginepo – wakitoacha jeuri zao hata kwa hayo pia,basi wanapewa ruhusa wanaume wawapige wanawake hao pigo la kuwatisha, sio la kuumiza.
Lakini hadithi za Mtume zimebainisha kuwa bora asifikilie katika daraja hii ya kupiga. Ajitahidi kumtengeneza katika taa kwa ile adabu ya kwanza tu, Ikiwa hapana budi na kwa ile ya pili basi, lakini asifikie ile ya tatu.
Akishindwa yeye kutengeneza awaite watu wawasuluhishe, kwani sulhu ndio kheri. Na hao watu inataka waingie wenyewe wasuluhishe hata kabla hawajatakiwa msaada wao, seuze wanapotakiwa.
Tena wanaonywa hapa hao wanaume wasiwafanyie jeuri wake zao bure kwa kujiona kuwa wao wakubwa.
Mwenyeezi Mungu Mkubwa kabisa zaidi juu yao. Na Maulamaa wengine wanafasiri “Haafidhatun Lilghayb” kwa tafsiri hii”-
Wawe wenye kuhifadhi siri zinazopita baina yao na waume zao, na siri zinazopita majumbani mwao, kwani mara nyingi wanawake wanakuwa waropokaji, wazee wa kizamani wakisema kwa kiswahili cha kizamani:-
“Mengi hayarongwa” yaani pana mengi kabisa ambayo haifai kabisa kuyasema, seuze kuyatangaza.
“Mambo ya nyumba kunga. Aibu kuyaeleza.”
Hayo yalikuwa na maelezo kuhusiana na aya ya 34 ya suratun Nisaa, na sasa tunaendelea na mada yetu. Lakini ni lazima tuzingatie kuwa ubora huo wa mwanamme ni katika kuisimamia na kuiongoza familia tu, ama katika fadhila za kibinaadamu na kijamii hakuna tofauti yoyote baina ya mwanamke na mwanamme.
[1] Surat Al-imrani aya ya 6
[2] Surat Hujurat aya ya 13
[3] Surat Ghaafir (Al-muumin) Aya ya 40
[4]Surat Tahriym Aya ya 11
[5] Suratun-Nisaa Aya ya 1.
[6] Suratun-Nisaa Aya ya 34
[7] Suratul-Baqara Aya ya 228
MWISHO