SHAHIDI MUTAHHARI NA SIFA ZA DINI
  • Kichwa: SHAHIDI MUTAHHARI NA SIFA ZA DINI
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 18:54:1 6-10-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

SHAHIDI MUTAHHARI NA SIFA ZA DINI

Kwa mnasaba wa kuwadia siku ya kuuawa shahidi Murtadha Mutahhari, msomi na mwanafalsafa mashuhuri wa Kiislamu nchini Iran, tumeona ni bora tuzungumzie, angalau kwa ufupi, nafasi ya msomi huyo maarufu wa Kiislamu katika kueneza Uislamu. Kila mwaka Shahid Murtadha Mutahhari, hukumbukwa, kuenziwa na kutukuzwa nchini Iran kupitia makumbusho ambayo hufanyika kote nchini kwa ajili ya kukumbuka nafasi yake ya kielimu na mchango mkubwa alioutoa kwa ajili ya mfumo wa Kiislamu wa Iran kabla na muda mfupi baada ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu nchini.

Makumbusho hayo hutukumbusha kwamba ulimwengu wa Kiislamu unahitajia wasomi na wanafikra wakubwa kama Shahid Mutahhari kwa ajili ya kuwaongoza Waislamu katika njia ya kufikia malengo yao matukufu. Shahid Murtadha Mutahhari anaweza kuchukuliwa kuwa nembo na mfano muhimu wa kuigwa na wanafikra pamoja na wasomi wengine wa Kiislamu katika kuungoza umma wa Kiislamu kwenye njia panda iliyojaa matatizo na njama za maadui wa Uislamu.
Alikuwa msomi, mwanafikra, mwanafalsafa, arif, mtu mwenye busara kubwa na mcha-Mungu ambaye alifanya kila aliloweza kwa ajili ya kulinda na kuutetea Uislamu duniani. Vitabu vingi vilivyoandikwa na msomi huyo katika nyanja mbalimbali vinabainisha wazi jambo hilo. Kuna sifa mbili muhimu ambazo zilidhihiri wazi katika maisha ya Shahidi Mutahhari. Ya kwanza ni utaalamu na ujuzi wake mkubwa katika masuala ya kielimu na pili ni juhudi zake za kuwabainishia watu mafundisho halisi ya kidini kwa mujibu wa mahitaji ya zama zao.
Alikuwa na hamu kubwa ya kuwafahamisha wanadamu saada yao kwa kuzingatia mafundisho sahihi ya kidini. Kupitia uandishi na hotuba zake katika sehemu mbalimbali, Ayatullah Mutahhari alifanya jitihada kubwa za kuuarifisha Uislamu kuwa dini pekee iliyo na uwezo wa kumdhaminia mwanadamu mahitaji yake ya humu duniani na huko Akhera. Katika sehemu nyingi za sura na aya zake, Qur'ani Tukufu inamthibitishia mwanadamu kuwa dini ndiyo inayomdhaminia mahitaji yake halisi. Inasema kama ifuatavyo katika aya ya 24 ya Surat al-Anfaal: "Enyi mlioamini! Mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume wake anapokuiteni kwenye yale yatakayokupeni uhai mzuri (wa dunia na Akhera. Fuateni amri zake Mwenyezi Mungu na makatazo yake).
Kwa msingi huo, kutekeleza maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu humdhaminia mwanadamu maisha bora humu duniani na huko Akhera. Kwa ibara nyingine ni kuwa Uislamu humletea mwanadamu maisha bora katika dunia zote mbili. Jambo lisilo na shaka ni kuwa Uislamu ni chanzo cha maisha, huishi milele na wala haufi na kutoweka kama inavyofanya mifumo mingine ya utawala na maisha ulimwenguni. Kwa ibara ya Ustadh Mutahhari ni kuwa, jua la dini kamwe halichwei. Kwa mtazamo wa msomi huyo mashuhuri, udharura wa kuhuishwa dini ni kutekelezwa kwake katika maisha ya kila siku ya mwanadamu, kukiwemo kutumiwa mafundisho yake kifikra na kivitendo.
Allama Mutahhari anasema kuwa ili masuala ya kijamii yaweze kudumu yanapasa kuandamana na matakwa ya mwanadamu. Anasema matakwa hayo kwa kawaida hugawanyika katika sehemu mbili ambazo ni matakwa ya kimaumbile kama vile kutafuta elimu na kupenda mambo mazuri yanayomkamilisha mwanadamu. Matakwa yasiyo ya kimaumbile ni tabia za kawaida na zinazotofautiana kati ya wanadamu. Tabia hizo ni kama vile za kupenda kunywa chai au wengine kuvuta sigara. Kwa sababu tabia hizi sio za kimaumbile, mwanadamu anaweza kuziacha wakati wowote anaotaka. Kwa mujibu wa wataalamu wa mambo, matakwa na mahitaji yasiyo ya kimaumbile sio ya kudumu na kwamba yale yanayodumu ni ya kimaumbile na ya dhati tu aliyoumbwa nayo mwanadamu. Kwa msingi huo, iwapo dini inataka kubaki na kudumu milele katika jamii ya mwanadamu inapasa kuoana na matakwa ya dhati ya mwanadamu au kuziba na kukidhi vyema mahitaji ya mwanadamu kwa kadiri kwamba kitu kingine kisije kikajaza nafasi hiyo.
Ustadh Mutahhari anasema kuwa katika mkondo wa maendeleo ya mwanadamu, mambo na vitu vingi hubadilika kwa mujibu wa mazingira mapya yanayojitokeza maishani mwake. Kwa mfano taa ya kwanza inayotumia umeme ulipogunduliwa na Thomas Edison, matumizi ya mishumaa na vibahaluli vya kawaida yalipungua kwa kiasi na kiwango kikubwa. Hii ni kwa sababu umeme uliweza kumuhudumia mwanadamu kwa njia bora zaidi na ya haraka. Licha ya hayo, kuna baadhi ya mambo ambayo hayabadiliki maishani mojawapo ikiwa ni dini. Kwa mtazamo wa Mutahhari dini ni jambo linaloandamana na matakwa ya kihisia na ya dhati ya mwanaamu kwa kadiri kwamba hakuna kitu kingine kinachoweza kuziba nafasi hiyo. Qur'ani Tukufu inasema kama ifuatavyo katika aya ya 30 ya Surat ar-Rum: "Basi uelekeze uso wako kwenye dini iliyo sawasawa - ndilo umbile Mwenyezi Mungu Alilowaumbia watu; (yaani dini hii ya Kiislamu inawafikiana barabara na umbo la binadamu).
Katika kipindi cha karne kadhaa zilizopita, nadharia mbalimbali zimekuwa zikitolewa kuhusiana na sababu za kudhihiri dini. Baadhi ya watu wamekuwa wakidai kwamba dini imetokana na woga, ujahili na upumbavu. Hii ni katika hali ambayo wengine wamekuwa wakisema kwamba mvuto wa mwanadamu kuelekea dini unatokana na hamu yake kubwa ya kutafuta uadilifu na mpangilio mzuri maishani. Wanaotetea nadharia hii wanadai kwamba, kadiri kiwango cha elimu ya mwanadamu kinavyozidi kuongezeka ndivyo hamu yake ya dini huzidi kudhoofika na kupungua. Nadharia hii ni kinyume kabisa na ukweli wa mambo ulivyo kwa sababu tunashuhudia wazi kwamba licha ya kuwepo maendeleo na ustawi mkubwa wa kielimu na kiviwanda duniani, lakini bado dini ingalipo miongoni mwa wanadamu, bali wamefikia natija hii kwamba, dini ni jambo ambalo kamwe haliwezi kutengana na jamii ya mwanadamu. Dakta Alexis Carrel, tabibu na mwandishi wa Ufaransa anaashiria pia athari kubwa ya dini katika dhati na nafsi ya mwanadamu na kusema kuwa dini ndiyo mara nyingine humuongoza mwanadamu na kumuepusha na masuala ya upotofu wa kifikra na kimatendo.
Katika sehemu nyingine, Ustadh Mutahhari anazungumzia jinsi dini inavyoweza kukidhi kikamilifu mahitaji ya mwanadamu. Anasema mwanadamu anahitajia dini katika masuala yake yote ya mtu binafsi na kijamii. Dini ni jambo la pekee linalodhibiti na kumuongoza mwanadamu katika maisha yake ya humu duniani. Victor Hugo, mwandishi na mshairi mwingine wa Ufaransa anasema hivi kuhusiana na umuhimu wa dini: "Kwa hakika iwapo mwanadamu anadhani kwamba mwisho wa maisha ni utupu na kuwa hakuna maisha mengine baada ya haya ya humu duniani, ni wazi kuwa maisha hayatakuwa na thamani yoyote kwake. Jambo linalofanya maisha ya mwanadamu kuwa mazuri, yenye furaha, kumpa uchangamfu na kupanua mtazamo wake ni dini."
Shahid Mutahhari anasema kwamba imethibiti leo kwamba maadili yasiyozingatia dini hayana msingi madhubuti, kwa sababu hayana nguzo ya imani. Maadili kama hayo yasiyozingatia mafundisho ya dini huwa hayadhamini thamani tukufu katika jamii kama vile uadilifu, usawa, utu na huruma. Hii ndio maana tunashuhudia kuwa licha ya kuwa jamii ya mwanadamu, hasa katika nchi za Magharibi, imepiga hatua kubwa katika nyanja za maendeleo ya kiteknolojia na kielimu lakini imeporomoka sana kimaadili. Hata hivyo Ustadh Mutahhari anapiga vita baadhi ya imani potofu na zisizo na msingi ambazo zimeingizwa na watu kwenye dini na kudai kuwa ni sehemu ya dini. Watu kama hao hutumia upotofu huo kuwakandamiza wenzao na kuwataka watekeleze masuala yasiyo ya kimantiki.
Anaamini kwamba iwapo dini itabainishiwa watu kwa uhalisia wake unaofaa, ni wazi kuwa mawimbi ya watu watapokea na kuingia kwenye dini hii tukufu makundi makundi. Tunakumbuka na kumpongeza msomi huyu mashuhuri wa Kiislamu kwa kujitolea katika kueneza dini na kuwafundisha wenzake mafundisho yake muhimu kwa juhudi zake zote. MWISHO