WATU WA SABT
  • Kichwa: WATU WA SABT
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 13:38:56 6-10-1403

WATU WA SABT

Qurani Tukufu inatuambia: Sura Al-Aaraf, 7, Ayah ya 163 & 164. Na waulizeni habari za mji ambao ulikuwa kando ya bahari, (watu wa mji huo) walipokuuwa wakivunja (sheria ya) Jumamosi (ambayo waliambiwa wasifanye kazi katika sikuu hiyo, wafanye ibada tu. Na kazi yao ilikuwa uvuvi). Samaki wao walipowajia juu juu siku za Jumamosi zao; na siku isiyokuwa Jumamosi hawakuwa wakiwajia (hivyo). Basi namna hivyo tuliwatia mtihani kwa sababu ya kuasi kwao.

Na (wakumbushe wakati) baadhi ya watu katika wao waliposema (kuwaonya waliovunja hishima ya Jumamosi kwa kuvua, na hali yakuwa wamekatazwa; waliposema): "Pana faida gani kuwaonya watu ambao Allah swt atawaua au atawaadhibu kwa adhabu kali ( papa hapa)?" Wakasema:"Tupate kuwa na udhuru mbele ya Mola wenu (kuwa tumewaonya lakini hatukusikilizwa) na huenda wakaogopa." Mtume Musa mwana wa Imran aliwahubiri wana wa Isra'il kuwa wawe na siku moja maalum katika juma kwa ajili ya kumwabudu Allah swt ili wao wasijishughulishe na kazi zinginezo mbali na ibada ikiwemo kuuza na kununua bidhaa za aina zote.

Siku hiyo ilikuwa makhsusi ya Ijumaa lakini wana wa Isra'il waliiomba siku ya Jumamosi kama ndiyo siku maalumu ya kufanya ibada ya Allah swt na hivyo siku ya Jumamosi ikawa ndiyo siku Kuu ambamo biashara za aina zote zilikatazwa. Hivyo kila Jumamosi Mtume Musa alikuwa akiwahutubia mkusanyiko maalum wa wana wa Isra'il. Ilipita miaka na watu waliichukulia Jumamosi kama siku njema na maalum kwa ajili ya ibada za Allah swt. Baada ya kuaga dunia kwa Mtume Musa a.s. kulianza kutokea mabadiliko mengi katika jamii ya wana wa Isra'il, hata hivyo wao waliendelea kuiheshimu siku ya Jumamosi kama ndiyo siku maalum kwa ajili ya ibada za Allah swt. Lakini ulipofika zama za Mtume Daud a.s., kikundi kimoja cha wana wa Isra'il waliokuwa wakiishi ukingoni mwa bahari, mji wa Ela,walipuuza utukufu wa siku hiyo ya Jumamosi na hivyo wakajishughulisha kuvua samaki.

Habari kamili ya matukio hayo ni kama ifuatavyo: Wakati uvuaji wa samaki ulipokuwa umepigiwa marufuku katika siku za Jumamosi, samaki walibuni njia yao, walikuwa wakijitokeza kwa wingi ufuoni mwa bahari katika siku hizo na kwa siku zilizobakia walikuwa wakiondoka kwenda mbali kabisa katika maji mengi ili wasiweze kuvuliwa na wavuvi. Watu wa Bani Isra'il ambao walikuwa wakitilia maanani maslahi yao ya kidunia, walikusanyika na kulizungumzia swala hili na kutoa kauli yao: "Sisi hatuna budi kubuni mikakati ya kuweza kudhibiti swala hili la uvuaji wa samaki. Katika siku za Jumamosi samaki wengi mno huonekana ufuoni kuliko siku zinginezo. Hivyo itatuwia rahisi mno kuvua samaki siku hiyo kwani siku zingine tunambulia kapa kwani wao wanakwenda katika maji yenye kina kikubwa mno hivyo kutuwia vigumu uvuvi."

Katika kikao hicho kuliafikiwa kuwa wabuni taratibu za kuvulia samaki. Hivyo wakaafikiana kuchimba mito na mifereji midogo midogo ili samaki wanapokuja ufuoni katika siku za Jumamosi waweze kupitiliza katika mifereji hiyo hivyo kuwawia rahisi katika kuwanasa. Hivyo wao walitekeleza mpango wao huo na wakachimba mito kutokea baharini. Katika siku za Jumamosi samaki wengi mno walikuwa wakiogelea kwa furaha hadi ukingoni mwa bahari na kupenya katika mito hiyo. Katika nyakati za usiku wakati samaki hao walipokuwa wakitaka kurudi baharini, hao walikuwa wakiziba midomo ya mito hiyo ili samaki hao wasiweze kurudi baharini na badala yake wabakie katika mito hiyo. Siku iliyofuatia wao walikuwa wakiwanasa samaki wote waliokuwa katika mito hiyo.

Hata hivyo watu wenye busara na fahamu waliwakanya watu hao wasijifanye wajajnja mbele ya amri za Allah swt. Wao waliwaonya na kuwabashiria adhabu na maangamizo makubwa yaliyokuwa yakija kwao, lakini haya pia hayakufua dafu. Hata hivyo watu hao wema waliendelea na juhudi zao za kuwakanya kwa njia mbalimbali kuhusu adhabu na maangamizo ya Allah swt, lakini walafi hao hawakuwasikiliza na badala yake waliwapuuza na kuwadharau. Hao waovu waliwaondoa wale wenye hekima na busara na badala yake wakaanza kuwafuata wale waliokuwa wakisema: "Jee kwa nini nyinyi munawa hubiri watu ambao watateremshiwa adhabu kali kabisa za Allah swt na hatimaye watateketezwa kabisa ? Hivyo muwaache katika hali yao walivyo."

Kikundi cha waja wema wakawaambia hao kuwa: "Sisi tunawahubiria ubashiri mwema hawa watu ambao hawapo katika fahamu zao kamili ili kwamba na Allah swt aone kuwa kwa kweli hawa watu ni masikini mbele ya macho ya Allah swt ." Hao wapotofu walikuwa wameshughulika mno na unasaji wa samaki kwa wingi mno bila kujali nasiha za kundi la kwanza la watu wema katika Bani Isra'il na walikuwa wakijionea ufakhari na majivuno juu ya ufanisi wao katika mipango yao hiyo. Baada ya maonyo ya siku chache, hao wapotofu walipokithiri katika kutotii amri ya Allah swt , waliteremshiwa adhabu kutoka kwa Allah swt kwamba nyuso zao ziligeuka kuwa za wanyama na baada ya kupita siku tatu, Allah swt aliwateremshia adhabuu kali kiasi kwamba wote kwa pamoja wakateketea.

MWISHO