DU’A YA MWEZI WA RAMADHANI (SEHEMU YA 8)
اللّهُمَّ فُكَّ كُلَّ أَسِيرٍ
Ewe Allah! Muachie Kila Mfungwa
MAANA YA ASIIR
Neno Asiir linatokana na neno al-asr, ambalo lina maana ya:
الشًّدُّ بِالْقَيْدِ
“Kufungwa kwa pingu.”
Raghib, muandishi mashuhuri wa kamusi, katika kamusi yake ‘al- Mufradat’1 anasema:
“Mtu ambaye alifungwa kwa pingu alikuwa anajulikana kuwa ni asiir, kwa hiyo neno hili lilikusudiwa kila kitu ambacho kilishikwa na kufungwa, hata kama hakikufungwa na kitu chochote…kwa mfano:
أَنَا أَسِيْرُ نِعْمَتِكَ
“Nimefungwa kwa fadhila zako.”
Kutokana na ufafanuzi huo hapo juu, upana wa mafuhumu ya neno ‘asr’ unakuwa wazi. Hadithi za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na Ahlul- Bayt wake, vilevile huonyesha ukweli huu. Ifuatayo ni mifano kwa ufuatiliaji wake:
(a) Imamu Abu’l Hasan al-Thalith2 (Ali al-Naqi a.s.) amenukuliwa akisema:
وَالْجَاهِلُ أَسِيْرُ لِسَانِهِ
“Mtu mjinga ni mfungwa wa ulimi wake.”
b) Katika maombi31 kutoka kwa Yusha bin Nun (a.s.) tunapata maelezo yafuatayo:
إِلهِيْ أَنْتَ مَلِكَ الْعطَايَا وَ أَنَا أَسِيْرُ الْخَطَايَا
“Ewe Allah! Wewe ni Mfalme wa wenye kutoa, ambapo mimi ni mfungwa wa makosa yangu.”
c) Katika Ziyarat moja ya Arba’in4 ya Imamu al-Husain (a.s.) ambayo husemwa kwamba ameifundisha Imamu al-Sadiq (a.s.), tunamsalimu Imamu al-Husain (a.s.) kama ifuatavyo:
الَسّلاَمُ عَلى أَسِيْرِ الْكُرُبَاتٍ
“Amani iwe juu ya mfungwa wa huzuni kubwa.”
d) Katika barua zake zijulikanazo sana aliyomtumia Malik al-Ashtar, Imamu ‘Ali anasema:
...فَإِنَّ هَذَا الدِّين قَدْ كَانَ أَسِيْراً فِي أَيْدِي الأشْرَار يُعْمَلُ فِيْهِ بِالْهَوَى وَتُطْلَبُ بِهِ الدُّنْيَا...
“Kwa vile kwa hakika dini hii ilikuwa mfungwa katika mikono ya watu waovu, kwa ajili ya visingizio vyao, watafuata muelekeo wao na kupata mapato ya kiduniya…”5
e) Katika Nahjul Balagha wakati anaelezea tabia za Malaika, Imamu ‘Ali (a.s.) amenukuliwa akisema:6
...فَهُمْ أُسَيرَآءُ إِيْمَانٍ...
“…kwa vile ni wafungwa wa imani…”
Kadhalika neno ‘asr’ lina maana ya kuwiana; wakati ambapo kikundi cha watu chaweza kuwa wafungwa wa muelekeo wa maovu yao lakini wasiteseke kimwili kifungo cha jela. Kundi laweza kustarehe uhuru wa kiroho, lakini wakawa katika hali ya ufungwa wa kimwili.
UPANA DHAHIRI WA NENO ASIIR
Kwa hakika, kipengele hiki cha du’a ni mojawapo ya vipengele vyenye kuumiza moyo. Watu wengi wasio na hatia ulimwenguni pote leo hii wanateseka vifungoni. Wakati ambapo kundi miongoni mwao ni waathiriwa wa ukandamizaji na uvunjaji wa sheria zilizotengenezwa na binadamu, kuna tabaka ambalo kwa kutokuwa kwao kabisa na hatia kumewafanya kuwa magerezani.
Kuwa magerezani ni sehemu moja tu ya hadithi. Ukandamizaji na mateso ambayo wafungwa hawa wasio na hatia huyapata ni makali mno yasiyoelezeka. Aina hii ya utesaji husababishwa na aina ya mtazamo walionao maasikari wa magereza tofauti, ambao hupokea nguvu ya kuamua watakavyo kutoka kwa wakubwa zao, ambao nao wana mamlaka kutoka kwenye serikali zao. Maelezo yafuatayo kutoka shirika la kimataifa la haki za binadamu (Amnesty international) yanazungumzia ukweli huu:
“Utesaji hautokei katika ombwe. Jamii na mazingira ya kisiasa, na usambazaji wa zana na mbinu kwa ajili ya kusababisha maumivu, hutegemea juu ya kushindwa kwa ridhaa ya kisiasa. Kama serikali za ulimwenguni zingelikuwa na ridhaa ya kisiasa kusimamisha mateso, zingelifanya hivyo.”7
Ili kuelewa uzito wa jambo hili, mtu anaweza kurejelea maandishi makhususi yanayopatikana, juu ya mateso gerezani katika Internet kutoka mashirika ya haki za binadamu, kama vile Human Rights Watch [hrw.org] na mfano kama hayo. Hata hivyo, kwa sababu ya ufupi wa ufafanuzi huu tutataja mifano mifupi ya hali ilivyo ya magereza ya ulimwenguni hapa:
WAFUNGWA WANAOUMIA KWA MATESO
1) Wanaume, Wanawake Na Watoto “...lakini mateso yanaendelea na hayakuishia kwenye serikali za kidikteta za kijeshi au tawala za kimabavu; mateso yanafanywa pia kwenye serikali za kidemokrasia. Ni wazi pia kwamba waathiriwa wa mateso ni watuhumiwa wa makosa ya jinai na wafungwa wa kisiasa, watu wa kipato cha chini halikadhalika na wapinzani, watu wanaolengwa kwa sababu ya mitazamo yao hali kadhalika na imani zao. Wao ni wanawake na wanaume, watoto na watu wazima pia.”8
2) Wanawake: “ Amnesty International (AI) imeandika matukio mengi yasiyo na idadi ya wanawake kuteswa katika mahabusi. Katika maelezo yake ya mizozo ya kijeshi, imetoa taarifa ya mfumo unaotumika wa unyanyasaji wa kijinsia kama silaha ya kivita.”9
3) Watoto: Ukweli kwamba watoto wanaweza wakateseka kwa mateso, lazima kiwe ni kitu kibaya mno cha kusitusha. Utegemezi wao na kutokuwa kwao salama lazima kuwape wao kinga kutokana na maovu ya wakubwa wanayopeana wenyewe kwa wenyewe. Kutokuwa kwao kabisa na hatia lazima kuwaweke mbali na kufikiwa na maovu hayo. Bado mateso dhidi ya watoto yameenea; watoto wanateswa na polisi na mjeshi ya usalama…”10
NJIA ZA UTESAJI
“Utafiti umeonyesha kwamba kupiga ndio njia zaidi ya kawaida ya utesaji na ukatili unaofanywa leo na mawakala wa dola, ambao umetaarifiwa katika nchi zaidi ya 150. Watu wanapigwa kwa ngumi, fimbo, vitako vya bunduki, viboko, mabomba ya vyuma, magongo ya besiboli, kamba za umeme. Waathiriwa hupata michubuko, kuvuja damu kwa ndani, kuvunjika mifupa, kung’oka meno, kupasuka viungo na baadhi hufa.
Kubaka na unyanyasaji wa kijinsia wa wafungwa umeenea. Njia nyingine zijulikanazo kwa wote za utesaji na ukatili ni pamoja na mishituko ya umeme (iliyotaarifiwa katika nchi zaidi ya 40), uning’inizwaji wa mwili (zaidi ya nchi 30), usongaji wa koo (zaidi ya nchi 30), mwigo wa kunyonga au kutishia kuuawa (zaidi ya nchi 50) na kutengwa kwa muda mrefu (zaidi ya nchi 50).
Njia nyingine ni pamoja na kuzamishwa ndani ya maji, kuchomwa na moto wa sigara mwilini, kufungwa kwenye gari na kutupwa nyuma yake kisha mtu anaburuzwa, kukoseshwa usingizi na kukoseshwa fahamu…
Aina za adhabu za kimwili zisizo za haki zijulikanazo zaidi kwa wote ni pamoja na ukataji wa viungo na utandikaji wa viboko. Baadhi ya njia nyingine kama vile ukataji wa viungo hufanywa kwa makusudio ya kuulemaza mwili wa mwanadamu. Hata hivyo, adhabu zote hizi zinaweza kusababisha maumivu ya muda mrefu au ya kudumu.”11
Hata hivyo, msimamo wa sheria ya ki-Islamu ambayo chanzo chake ni Muumba Mwenyewe wa viumbe, ni wa tofauti kubwa mno sana. Kuipitia pitia historia ya uongozi wa ki-islamu kuanzia wakati wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) mpaka sasa tunakuja kufahamu ukweli wa ushindani huu. Ifuatayo ni mifano kwa ajili ya ufuatiliaji wako:
1) Vita vya kwanza ambavyo waislamu walipigana kishujaa vilikuwa vya Badri. Wakati wakiwa wamewashinda makafiri, Waislamu waliwakamata makafiri wengi na kuwachukuwa mateka. Hata hivyo, Mtume (s.a.w.w.) aliwachukulia ‘mateka’ kama binadamu na aliamini kwamba wao pia wanazo haki fulani. Hakuna mtu aliyeruhusiwa kuwatesa. Badala yake njia za kuwaacha huru zilipendekezwa kwao. Kwa hiyo wengi waliachwa huru kwa malipo ya fidia. Historia inatuambia kwamba:
وَكَانَ يُفَادِيْ بِهِمْ عَلَى قَدْرِ أَمْوَالِهِمْ
“Na Mtume (s.a.w.w.) alichukuwa malipo ya fidia kutoka kwao kutokana na hali zao kifedha.”12
Na baadhi ya mateka hawana mali lakini walijua ustadi wa kuandika. Mtume (s.a.w.w.) aliwaambia kila mmoja wao kuwafundisha watu kumi kutoka Madina kama fidia.
2) Imeelezwa kwamba baada ya Ibn Muljam kumpiga Imamu ‘Ali (a.s.) dharuba la kufisha, Imamu aliwaambia watoto wake wawili (a.s.):
إِحْبِسُوْا هَذَا الأَسِيْرَ وَ أَطْعِمُوْهُ وَاسْقُوْهُ وَ أَحْسِنُوْا إِسَارَهُ
“….Mfungeni mfungwa huyu, na mpeni chakula na maji, na mshughulike naye kwa njia iliyo nzuri katika ufungwa wake.”13
Na katika hadithi nyingine alisema maneno yafuatayo kuhusu Ibn Muljam:
إنَّهُ أَسِيْرٌ، فَأَحْسِنُوْا نُزْلَهُ وَأَكْرِمُوْا مَثْوَاهُ ، فَإنْ بَقِيْتُ قَتَلْتُ أوْ عَفَوْتُ ،وَإنْ مِتُّ فَاقْتُلُوْهُ قَتْلَتِيْ وَلاَ تَعْتَدُوْا إنَّ اللهَ لاَ يُحِبُّ الْمُعْتَدِيْنَ
“Hakika yeye ni mateka; kwa hiyo mpeni chakula na sehemu nzuri; na kama nitabakia hai , basi ima nitamuuwa au nitamsamehe; na kama nikifariki, basi muuweni kwa njia ile ile aliyonipiga dharuba [kwa pigo moja], na msichupe mipaka, kwani kwa hakika Allah (s.w.t.) hawapendi wale ambao wanachupa mipaka.” [2: 190]14
Hatari hii ya kiutendaji iliyomkabili Imamu ‘Ali (a.s.) katika nyakati hizo nyeti, huonyesha mfano wa mtazamo wa moyo mzuri wa Uislamu. Chuki na kisasi havibakii katika moyo wa ‘Ali (a.s.) kwani kila kitu katika mwili wake ni chombo cha Allah (s.w.t.)
1) Kama mtu kwa uangalifu angechunguza haki za wafungwa kwa mujibu wa Uislamu, angefahamu vipi ilivyo mbali sheria zilizotungwa na wanadamu na sheria za Mwenyezi Mungu. Sheikh Najm al-Din Tabbasi katika kitabu chake ‘Mawāridal-Sijjin’ [Matukio ya Jela] ametaja baadhi ya haki za wafungwa kama ifuatavyo:
“…Wafungwa waumini wanaweza kuhudhuria Sala za Ijumaa na Idd chini ya uangalizi, na kisha kurudi Gerezani haraka, wafungwa wanaweza kukutana na jamaa zao wa karibu na pia wako huru kupokea chakula na nguo kutoka kwao, wafungwa lazima wafungwe katika mazingira mazuri ya kiafya na waruhusiwe kutoka nje nyakati mahususi chini ya uangalizi, mtu ambaye anaumwa hafungwi, msaada ambao mfungwa hutoa kwa familia yake ni lazima utolewe kutoka kwenye hazina ya umma (baytu’l māl) ya waislamu nk…”15
Hata hivyo, maelezo hayo hapo juu yasije yakamchanganya mtu akaamini kwamba wafungwa lazima waachwe bila kuhojiwa au ushawishi wa kutubia. Mfungwa anatendewa kwa mujibu wa kosa ambalo amelitenda. Wafungwa wa kisiasa vile vile wanashughulikiwa katika njia iliyo tofauti. Hata hivyo, mfungwa hatendewi kama mfungwa au kuteswa au kubakwa au hata kutishwa kisaikolojia au kufanyiwa mchezo. Haya ni kinyume na kanuni za Shari’ah ya ki-islamu. Bali wao hutendewa kama wanadamu na hakuna mtu anaruhusiwa kuchupa mipaka iliyowekwa na Allah (s.w.t.). Hivyo endapo tukisikia au kuona tabia isiyo ya kibinadamu kutoka kwa asikari magereza wa dola zinzoitwa za ki-islamu, hayo yasitufanye tufikiri kwamba hayo ndiyo ambayo waislamu wanaamini. Kuna tofauti kubwa kati ya kigezo cha kuwa Mwislamu na kigezo cha kuwa mtawala wa ki-islamu asiyetekeleza shari’ah.
Tazama hadithi ifuatayo kwa uangalifu:
Imamu Ja’far al-Sadiq (a.s.) amenukuliwa akisema:
اِنَّ عَلِيًّا (ع) كَانَ يُطْعِمُ مَنْ خُلِّدَ فِي السِّجْنِ مِنْ بَيْتِ مَالِ الْمُسْلِمِيْنَ
“Hakika ‘Ali (a.s.) angelimlisha mfungwa ambaye anatumikia kifungo cha maisha kutoka kwenye hazina ya waislamu.”
Imamu ‘Ali (a.s.) amenukuliwa akisema:
إِطْعَامُ الأَسِيْرِ وَالإِحْسَانُ إِلَيْهِ حَقٌّ وَاجِبٌ وَ إِنْ قَتَلْتَهُ مِنَ الْغَدِ
“Kulisha mfungwa na kumtendea wema, ni haki ya lazima, hata kama ni wa kuuliwa [kwa mujibu wa sheria za ki-islamu] kesho.”16
HAWA AL-NAFS: MOJA YA MAANGAMIZI YA UFUNGWA
1) Qur’an Tukufu [surat al-Qasas 28: 50] inasema:
فَإِنْ لَمْ يَسْتَجِيبُوا لَكَ فَاعْلَمْ أَنَّمَا يَتَّبِعُونَ أَهْوَاءَهُمْ ۚ وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّنِ اتَّبَعَ هَوَاهُ بِغَيْرِ هُدًى مِنَ اللَّهِ ۚ إِنَّ اللَّهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ
“…..Na nani aliye potea zaidi kumshinda anayefuata pumbao lake bila uwongofu utokao kwa Allah. Hakika Allah hawaongoi watu wenye kudhulumu.”
2)Imam ‘Ali (a.s.) amenukuliwa akisema:
كَمْ مِنْ عَقْلٍ أَسِيْرٍ عِنْدَ هَوَىً أَمِيْرٍ
“Ni ukubwa ulioje wa idadi iliyopo ya wenye akili waliyo chini ya ufungwa wa hawa!”17
3) Imamu ‘Ali (a.s.) amenukuliwa akisema:
إِنَّ أَخْوَفَ مَا أَخَافُ عَلَيْكُمْ إِثْنَتَانِ: اتِّبَاعُ الْهَوَى وَ طُوْلُ الأَمَلِ
“Hakika kuna vitu viwili ambavyo navihofia zaidi kwenu: Kufuata mitizamo yenu miovu na kuwa na matumaini marefu.”18
Moja ya maangamizi makubwa ya ufungwa ni ufungwa wa kiroho kwa mitazamo ya uovu. Katika lugha ya Qur’an inaitwa “al-hawa,” ni kikwazo kikubwa katika njia yetu ya kuelekea kwa Mwenyezi Mungu. Takriban kila tatizo la kidunia leo hii huanzia kabisa kutoka kwenye asili hii ya maangamizi. Bali, historia yote ya viumbe imejaa mifano ambayo huonyesha jinsi aina hii ya ufungwa ilivyokuwa inaangamiza: Kwa sababu ya ufungwa huu haswa, Ibilis hakumsujudia Adam ingawa aliamrishwa kufanya hivyo, Kain (Qabil) alishawishika kumuua Habil pamoja na kwamba yeye ni kaka yake mwenyewe, mtoto wa Nuh (a.s.) alimuacha baba yake hata ingawa yeye (Nuh) alikuwa Mtume wa Allah (s.w.t.), na orodha inaendelea.
Chunguza sababu za vita mbali mbali na migogoro iliyopita na ya sasa utatambua kwamba chanzo cha sababu kabisa ni aina hii ya ufungwa. Wakati Rais anapokuwa na maradhi ya ufungwa huu, huua raia wengi wasio na makosa; wakati waziri wa fedha anapofungwa na ufungwa huu, hufuja mamilioni ya fedha; wakati mtu asiye na dini na mwanadamu asiye na malengo anapougua maradhi haya ya ufungwa, hujiingiza katika aina mbali mbali za uovu. Kwa kifupi yeyote yule anaye faidi mamlaka hufanya uharibifu kwa kadiri ya mamlaka aliyo nayo.
Hata hivyo, uhuru kutokana na ufungwa huu uko kwenye mikono yetu. Allah (s.w.t.) ametupa funguo za mlango wa jela na akatushauri tutoke, lakini mvuto wa uzuri wa jela inaelekea umetufanya kimya na bila kuchukuwa hatua.
HAWA AL-NAFSI HUSHUSHA HADHI YA MTU NA KUWA MFANO WA MBWA!
Qur’an [sura ya 7, Al-Aáraf, aya ya 175-176] inasema:
وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ الَّذِي آتَيْنَاهُ آيَاتِنَا فَانْسَلَخَ مِنْهَا فَأَتْبَعَهُ الشَّيْطَانُ فَكَانَ مِنَ الْغَاوِينَ .وَلَوْ شِئْنَا لَرَفَعْنَاهُ بِهَا وَلَٰكِنَّهُ أَخْلَدَ إِلَى الْأَرْضِ وَاتَّبَعَ هَوَاهُ ۚ فَمَثَلُهُ كَمَثَلِ الْكَلْبِ إِنْ تَحْمِلْ عَلَيْهِ يَلْهَثْ أَوْ تَتْرُكْهُ يَلْهَثْ ۚ ذَٰلِكَ مَثَلُ الْقَوْمِ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا ۚ فَاقْصُصِ الْقَصَصَ لَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ .
“Wasomee habari ya yule ambaye Tulimpa Ishara Zetu, lakini akajivua nazo. Basi shetani akamuandama akawa miongoni mwa waliopotea. Na lau tungelitaka tungelimtukuza kwa Ishara Zetu lakini yeye alishikilia ulimwengu na akafuata pumbao lake. Mfano wake ni mfano wa mbwa. Ukimhujumu hupumua na kutoa ulimi au kama ukimuacha pia hupumua na kutoa ulimi…..”
Aya hii, kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa na ‘Allāma Tabātabā’i katika kitabu chake ‘Al-Mizān’ na kusimuliwa na ‘Tafsir al-Burhān’, anasimulia kuhusu Bal’am bin Bā’ūrā. Alikuwa ni mtu aliyeishi wakati wa Mtume Musa (a.s.) na alifaidi hali ya juu ya kiroho, kwani kwa mujibu wa hadithi iliyonukuliwa kutoka kwa Imamu al-Ridha (a.s.) alijua ism al-a’dham (Jina Tukufu la Allah lenye siri ya mambo). Baadae, kwa muelekeo wake muovu, aligeuka akawa msaidizi wa Firauni na akawa asiyeheshimika kiroho. Imamu al-Ridha (a.s.) alinukuliwa akisema:
“Hakika Bal’am bin Bā’ūrā alipewa jina Tukufu la Allah na wakati wowote alipotaka kuomba kwa Jina hilo, maombi yake yalikubaliwa. Kisha alielekea upande wa Firauni. Wakati fulani Firauni alikuwa anamtafuta Mtume Musa (a.s.) na wafuasi wake alikutana na Bal’am na akasema: ‘Muombe Mola wako amtupe Musa na wafuasi wake kwenye mtego wetu.’ Baadae alipanda punda wake kumtafuta Musa (a.s.) na wafuasi wake. Hata hivyo, punda wake hakusogea. Hivyo alianza kumchapa. Baadaye Allah (Asiyeshindwa na Mtukufu) alimuwezesha yule punda kusema na akasema [kumuambia Bal’am]:
‘Ole wako! Kwani wanipiga kwa kosa gani? Unataka mimi nikufuate ili kwamba uombe dhidi ya Mtume Musa (a.s.) Mtume wa Allah na taifa linaloamini?’ [Bal’am hakusikiliza] na aliendelea kumpiga yule punda mpaka akamuua. Kuanzia pale Bal’am alisahau lile Jina Tukufu la Allah.”19
Aya hii ni fundisho kwa wale watu wote wasomi ambao wamepata daraja ya uchamungu. Kama mtu hakuwa na tahadhari katika vita yake dhidi ya nafsi yake ovu, kuna hatari ya yeye kuangukia katika hali ya udhalili na kuangamia kiroho. Tunaomba kinga kutoka kwa Mola Mwingi wa rehema kutokana na kila aina ya fedheha ambayo hututenganisha sisi kutoka kwenye ujirani Wake.
Aya ya 176/7 sura ya 7, Al-Aáraf, huoneshana mfano wa Bal’am kama mfano wa mbwa:
فَمَثَلُهُ كَمَثَلِ الْكَلْبِ إِنْ تَحْمِلْ عَلَيْهِ يَلْهَثْ أَوْ تَتْرُكْهُ يَلْهَثْ ۚ ذَٰلِكَ مَثَلُ الْقَوْمِ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا ۚ فَاقْصُصِ الْقَصَصَ لَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ سَاءَ مَثَلًا الْقَوْمُ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَأَنْفُسَهُمْ كَانُوا يَظْلِمُونَ
“…Basi mfano wake ni mfano wa mbwa. Ukimhujumu hupumua na kutoa ulimi, na ukimuacha pia hupumua na kutoa ulimi. Huu ni mfano wa wale ambao wanazikanusha Ishara Zetu; kwa hiyo simulia hadithi hii ili kwamba waweze kutafakari.”
UPENDELEO WA UFUNGWA WA NJE JUU YA UFUNGWA WA NDANI
Qur’an Tukufu [12: 33] inamnukuu Yusufu (a.s.) akiomba:
قَالَ رَبِّ السِّجْنُ أَحَبُّ إِلَيَّ مِمَّا يَدْعُونَنِي إِلَيْهِ ۖ وَإِلَّا تَصْرِفْ عَنِّي كَيْدَهُنَّ أَصْبُ إِلَيْهِنَّ وَأَكُنْ مِنَ الْجَاهِلِينَ
“Ewe Mola wangu ! kifungo nakipendelea zaidi kuliko haya wanayoniitia…”
Habari ya Mtume Yusufu (a.s.) katika Qur’an Tukufu ni fundisho la fikira kwa kila mwanadamu ambaye anatamani kuishi maisha ya uhuru na ufanisi.
Baada ya Zulaykha kumshawishi Yusufu (a.s.) lakini akajikuta ameshindwa, alijaribu kumlaumu kwamba amemtongoza. Lawama zake zilithibitishwa na mashahidi kwamba ni za uwongo. Habari za tukio hili zilienea katika mji na Zulaykha alilaumiwa kwa kushawishi ‘mfano halisi wa usafi’. Ili kuzima moto wa kadhia hii, aliwaalika wanawake wale ambao wamemlaumu na kumpa kila mmoja tunda [aina ya chungwa] na kisu, akawambia wamenye matunda wakati Yusufu akipita mbele yao. Badala ya kukata matunda walijeruhi mikono yao. Walifungwa kwa uzuri wa kimwili wa Yusufu (a.s.).
Qur’an Tukufu inasema:
1. Habari zilienea na wanawake wakaanza kuzungumza:
وَقَالَ نِسْوَةٌ فِي الْمَدِينَةِ امْرَأَتُ الْعَزِيزِ تُرَاوِدُ فَتَاهَا عَنْ نَفْسِهِ ۖ قَدْ شَغَفَهَا حُبًّا ۖ إِنَّا لَنَرَاهَا فِي ضَلَالٍ مُبِينٍ
“Hakika wanawake ambao walikuwa mjini walisema, mke wa Gavana anataka kumshawishi mtumishi wake kimapenzi kinyume cha nafsi yake (safi)! Hakika amesalitika kwa mapenzi; hakika sisi tunamuona yumo katika upotovu ulio dhahiri.” [Surat Yusuf 12: 30]
Wakati ambapo mwanzoni wanawake walimhesabu Zulaykha kuwa katika kosa lililo dhahiri, wao wenyewe baadae walimkaribisha Yusufu (a.s.) ili kuwa na uhusiano naye.
2) Zulaykha anawakaribisha wanawake:
فَلَمَّا سَمِعَتْ بِمَكْرِهِنَّ أَرْسَلَتْ إِلَيْهِنَّ وَأَعْتَدَتْ لَهُنَّ مُتَّكَأً وَآتَتْ كُلَّ وَاحِدَةٍ مِنْهُنَّ سِكِّينًا وَقَالَتِ اخْرُجْ عَلَيْهِنَّ ۖ فَلَمَّا رَأَيْنَهُ أَكْبَرْنَهُ وَقَطَّعْنَ أَيْدِيَهُنَّ وَقُلْنَ حَاشَ لِلَّهِ مَا هَٰذَا بَشَرًا إِنْ هَٰذَا إِلَّا مَلَكٌ كَرِيمٌ
“Aliposikia yule bibi masengenyo yao aliwaita, na akampa kila mmoja wao kisu. Akamuambia Yusufu, tokeza mbele yao. Walipo muona waliona ni kitu kikubwa kabisa, na [katika mshangao wao] wakajikata mikono yao wakisema: Hasha lilLah! Huyu sio mwanadamu. Hakuwa huyu ila ni Malaika Mtukufu.”[Surat Yusuf 12: 31]
3) Zulaykha akakiri kwamba waliyosema ni kweli na akatishia kumfunga Yusufu:
قَالَتْ فَذَٰلِكُنَّ الَّذِي لُمْتُنَّنِي فِيهِ ۖ وَلَقَدْ رَاوَدْتُهُ عَنْ نَفْسِهِ فَاسْتَعْصَمَ ۖ وَلَئِنْ لَمْ يَفْعَلْ مَا آمُرُهُ لَيُسْجَنَنَّ وَلَيَكُونًا مِنَ الصَّاغِرِينَ
“Yule bibi akasema: Huyu basi ndiye huyo mliye nilaumia! Na kweli nilimshawishi kimapenzi kinyume cha nafsi yake (safi), lakini alikataa kabisa; na sasa kama hafanyi ninacho muamrisha, basi hakika atafungwa gerezani, na atakuwa miongoni mwa walio chini kabisa." [Surat Yusufu 12: 32]
Pamoja na kumlaumu Yusufu (a.s.) mwanzoni kwa kujaribu kumtongoza, bibi huyu kwa uwazi alikiri kwamba ni yeye ambaye alijaribu kumshawishi.
Aidha, alisema kwamba; amma atasalimu amri kwenye matamanio yangu, au ataishia gerezani [na hivyo yeye vile vile kuonekana kama mtu mwenye makosa].
4) Wanawake wangelitaka kuwa na uhusiano na Yusufu (a.s.):
قَالَ رَبِّ السِّجْنُ أَحَبُّ إِلَيَّ مِمَّا يَدْعُونَنِي إِلَيْهِ ۖ وَإِلَّا تَصْرِفْ عَنِّي كَيْدَهُنَّ أَصْبُ إِلَيْهِنَّ وَأَكُنْ مِنَ الْجَاهِلِينَ
“Yusufu akasema: Ewe Mola wangu naipendelea zaidi jela kuliko haya wanayoniitia (yadu’nani ilayhi); na usiponiondoshea vitimbi vyao nitawaelekea, nakuwa miongoni mwa wajinga.”
[Surat Yusuf 12: 33]
Katika hadithi ndefu iliyosimuliwa na Abu Hamzā al-Thumāli,20 Imamu Zayn al-’Abidin (a.s.) amenukuliwa akisema kwamba, baada ya kuondoka katika mkusanyiko ambao ulipangwa na Zulaykha, kila mmoja wa wanawake wale alituma ujumbe kwa Yusufu kwa siri [bila ya Zulaykha kuwepo] na kumuambia kwamba wangelitaka kukutana naye. Lakini Mtume Yusufu (a.s.) alikataa na akaomba kutoka kwa Allah:
قَالَ رَبِّ السِّجْنُ أَحَبُّ إِلَيَّ مِمَّا يَدْعُونَنِي إِلَيْهِ ۖ وَإِلَّا تَصْرِفْ عَنِّي كَيْدَهُنَّ أَصْبُ إِلَيْهِنَّ وَأَكُنْ مِنَ الْجَاهِلِينَ
“…Kama hutaniondoshea vitimbi vyao, nitawaelekea, na nitakuwa miongoni mwa wajinga.” (12:33)
Kwa mujibu wa wafasiri wa Qur’an neno ‘yad’ūnani ilayhi (naipendelea sana kuliko “wanayoniitia”) ambalo liko katika tensi isiyotimilifu (mudhari) huonyesha kwamba walikuwa wameshikilia kumkaribisha Yusufu (a.s.) kuelekea kwao. Hata hivyo, Mtume Yusufu (a.s.) alilia:
قَالَ رَبِّ السِّجْنُ أَحَبُّ إِلَيَّ مِمَّا يَدْعُونَنِي إِلَيْهِ ۖ وَإِلَّا تَصْرِفْ عَنِّي كَيْدَهُنَّ أَصْبُ إِلَيْهِنَّ وَأَكُنْ مِنَ الْجَاهِلِينَ
“Ewe Mola wangu! Jela naipendelea zaidi kuliko haya wanayo niitia; na kama usiponiondoshea vitimbi vyao nitawaelekea na kuwa miongoni mwa wajinga” [Surat Yusuf 12:33]
Aya hii kwa uwazi inaonyesha kwamba Mtume Yusufu alikuwa na matamanio ya kijinsia, na alikuwa anaelewa hatari ya mtego aliotegewa. Kwa hiyo alimuomba Allah (s.w.t.) amlinde kutokana na uhaini wanaomfanyia. Alipendelea kufungwa jela na kukubali udhilifu [wa kuhusishwa kiuwongo kuwa ni mwenye makosa] lakini asithubutu kumuasi Mola wake. Na Mola Mwingi wa rehema akamjibu:
فَاسْتَجَابَ لَهُ رَبُّهُ فَصَرَفَ عَنْهُ كَيْدَهُنَّ ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ
“Basi Mola wake akamwitikia dua yake, na akamuondeshea vitimbi vyao; hakika Yeye ni Msikizi, Mjuzi.” [Surat Yusuf 12:34]
Hizi ni hali ambapo sura ya kweli ya mu’umini inafunguliwa. Mtume Yusufu (a.s.) alipendelea kuwa mfungwa wa nguvu za nje kuliko kunaswa ndani na nguvu za kiasherati, ambazo humuangamiza mwanadamu na maisha yake yote ya baadae. Jela hapa ni sehemu ya usalama na ukombozi. Ni sehemu ya hifadhi kwa moyo huu, ambao unaungua kwa mapenzi ya Allah (s.w.t.). Yuko tayari kupatwa na machungu na shida za kufungwa jela na udhalili, lakini hawezi kustahamili mateso ya kumuasi Mpendwa Pekee, ambaye amemlea mpaka kuwa hivyo alivyo. Na itawezakana vipi kwa mtu ambaye moyo wake umejazwa kabisa kwa mapenzi ya Allah kufikiri hata kuutia doa mkono wake kwa dhambi?
REJEA
• 1. Rāghib Isfahāni, al-Mufradāt, uk. 76. chapa mpya.
• 2. Allāma Majilisi, Bihār al-Anwār, j. 78, uk. 368, tr. 3.
• 3. Allāma Majilisi, Bihār al-Anwār, j. 94, uk. 93, tr. 8.
• 4. Allāma Majilisi, Bihār al-Anwār, j. 101, uk. 331, tr. 2.
• 5. Imamu ‘Ali (a.s.), Nahj al-Balāgha, barua ya 53.
• 6. Imamu ‘Ali (a.s.) Nahj al-Balāgha, khutuba ya 91.
• 7. http://www. stoptorture.org, tawi la Amnesty intenational.
• 8. Ibid.
• 9. Tawi la Amnesty International htt:// www.Stoptorture.Org/report/ index.htm.
• 10. Ibid.
• 11. Ibid.
• 12. Hayāt al-Nabi wa Siratuhu, j. 2 uk. 60, Uswa Publications.
• 13. Muhammad al-Rayy Shahri, Mawsū’at al-Imam ‘Ali bin Abi Talib, j. 7, uk.250, tr. 2949s.
• 14. Mawsū’at al-Imām ‘Ali bin Abi Tālib, j. 7, uk. 250, rt. 2950.
• 15. Shaykh Najm al-Din Tabasi, Muwārid al-Sijn, uk. 493 na kuendelea.
• 16. Muhammadi al-Rayy Shahri,Mizān al-Hikma, j. 1, uk. 76.
• 17. Marhum Āmadi, Mu’jamu Ghurari’l Hikam, uk. 34.
• 18. Imām ‘Ali (a.s.), Nahjul Balāgha, khutuba ya 28.
• 19. Sayyid Hāshim, Bahrāni, Al-Burhāni Fi Tafsri’l Qur’an, j. 3, uk. 246 – 247.
• 20. Allāma Tabātabāi, Tafsir al-Mizān, j. 11, uk. 164 – 165.
MWISHO