DU’A YA MWEZI WA RAMADHANI 1
  • Kichwa: DU’A YA MWEZI WA RAMADHANI 1
  • mwandishi: al-islam.org
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 18:41:34 1-9-1403

DU’A YA MWEZI WA RAMADHANI (SEHEMU YA 1)

DU’A NA KANUNI YA SABABU NA MATOKEO

اللّهُمَّ أَدْخِلْ عَلَى أَهْلِ الْقُبُورِ السُّرُورَ

Ewe Allah Ingiza Furaha Kwenye Roho Za Wakazi Wa Makaburini

Du’a ndiyo njia bora zaidi ya mtu kupata mwisho wenye maana. Kanuni ya sababu na matokeo inatuhimiza kuomba msaada kutoka kwa Msababishaji Mkuu – ambaye ni Mwenyezi Mungu (s.w.t.), hivyo basi hata kwenye mazingira ambayo vitu vyaweza kupatikana kwa njia za kawaida haipasi mtu kujiona ya kwamba hahitaji dua. Na baadhi kwa upande mwingine wanaweza wakafikiri kwamba dua peke yake inatosha na hakuna haja ya kutumia njia zilizoko kwenye uwezo wetu ili kufikia malengo yetu. Kwa uwazi njia hii pia ni ile ya ujinga, kwani Mwenyezi Mungu pia ameweka mfumo wa sababu na matokeo na akamhimiza mwanadamu kuutumia (mfumo) huo kwa mwishilizo wake mwema. Maneno yafuatayo ya hekima kutoka kwa Imamu al-Sadiq (a.s.) yanathibitisha hilo.
فَجَعَلَ لِكُلِّ شَيْءٍ سَبَبًا, أَبَى اللَّهُ أَنْ يُجْرِيَ الأَشْيآءَ إلاّ بِأَسْبَابِهَا
“Mwenyezi Mungu hayaruhusu mambo kufanyika ila kwa kupitia sababu zake hivyo basi kila kitu amekifanyia sababu.”1

KUTAFUTA SABABU ZA KUWAINGIZIA FURAHA WALIO MAKABURINI

Baada ya kufahamu yaliyo tangulia, tutaona ya kwamba yeyote mwenye kufahamu anapoomba dua, bila ya shaka atatafuta njia na sababu ziwezazo kuzifanya nyoyo za walio fariki zifurahike, mbali na kuziombea dua.
Riwaya zilizopokewa kuhusiana na jambo hili (ambazo zinatuzidishia muangaza) zinatueleza namna ya kuwafurahisha walio fariki. Hadithi zifuatazo zinafaa kutafakari:
1. Imam al-Sadiq (a.s.) aliulizwa, “Je, yawezekana mtu aswali kwa niaba ya aliyekufa?” “Ndio” alijibu Imamu (a.s.) na akaongeza:
إنَّ الْمَيِّتَ لَيَفْرَحُ بِالتَّرَحُّمِ عليهِ وَالإسْتِغْفَارِله،كما يَفْرَحُ الْحَيُّ بِاالْهَدِيَّة تهدى إليه
“Hakika maiti anafurahi anapohurumiwa na kuombewa msamaha kama anavyo furahi aliye hai kwa kupewa zawadi.”2
2. Siku moja Mtume (s.a.w.w.) alipita karibu na kaburi la mtu aliezikwa jana yake, ambapo aliiona familia yake ikimlilia, alipoona hivyo aliwaambia;
لَرَكْعَتَانِ خَفِيْفَتَانِ مِمّا تَحْتَقِرُوْنَ أَحَبُّ إِلَى صَاحِبِ هَذَا الْقَبْرِ مِنْ دُنْيَاكُمْ كُلَّهَا
“Rakaa mbili zilizo nyepesi ambazo mwazidharau ni bora kwa huyu aliyezikwa kushinda dunia yenu yote.”3
3. Imepokewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.) kwamba:
إِنَّ الْهَدَايَا لِلأَمْوَاتِ الدُّعَآءُ وَ الإِسْتِغْفَارُ
“Hakika zawadi (za walio hai) kwa walio fariki ni dua na kuwaombea msamaha”.4
4. Vile vile tumepokea kutoka kwa Imam Ali bin Musa Ridha (a.s.) kwamba:
ما مِنْ عَبْدٍ زارَ قَبْرَ مُؤْمِنٍ فَقَرَأ عليهِ إنَّا أنْزلْنَاهُ في لَيْلَةِ الْقَدْرِ سَبْعَ مَرَّاتٍ إلّا
غَفَرَ اللهُ لَهُ وَلِصَاحِبِ الْقَبْرِ
“Yeyote katika waja wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anapolizuru kaburi la mu’umin halafu akasoma Suratu’l Qadr mara 7 juu ya kaburi hilo, Allah atamsamehe yeye na mkazi wa kaburi hilo.”5
5. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amenukuliwa akisema:
مَنْ مَرَّ عَلَى الْمَقَابِرِ وَقَرَأ قُلْ هُوَ اللهُ أحَدٌ إحْدَى عَشْرَةَ مَرَّةً ثُمَّ وَهَبَ أجْرَهُ لِلْأمْوَاتِ
أُعْطيَ مِنَ الأَجْرِ بِعَدَدِ الأَمْوَاتِ
“Yeyote apitae karibu na makaburi na akasoma Qul Huwallahu Ahad mara 11 na akatoa thawabu zake kwa maiti, malipo yake hulingana sawa na idadi ya maiti (waliozikwa hapo).”6
6. Imamu Ja’far al-Sadiq (a.s.) amenukuliwa akisema:
تَدْخُلُ عَلَى الْمَيِّتِ فِي قَبْرِهِ الصَّلاةُ وَالصَّوْمُ وَالْحَجُّ وَالصَّدَقَةُ وَالدُّعَاءُ وَالبِرُّ وَيُكْتَبُ
أَجْرُهُ لِلَّذِي فَعَلَهُ وَلِلْمَيِّتِ
“Sala, Saumu, Hajj, Sadaka, matendo mema na Du’a humfikia maiti katika kaburi lake, na malipo ya matendo hayo huandikiwa (wote), mtendaji na maiti.”7
7. Imamu Ja’far al-Sadiq (a.s.) amenukuliwa akisema:
مَنْ عَمِلَ مِنَ الْمُسْلِمينَ عَن مَيِّتٍ عَمَلَ ( عَمَلاً ) خَيْرٍ أضْعَفَ الله
لَهُ أجْرَهُ وَنَفَعَ الله بِهِ الْمَيِّتَ
“Yeyote yule miongoni mwa waislamu afanyaye tendo jema kwa niaba ya mtu aliyekufa, Allah humlipa malipo maradufu na kumfanya maiti anufaike nalo.”8
Kwa hiyo, tunapowaombea dua waliofariki ili wapate furaha katika barzakh, lazima vile vile tujitahidi kutumia njia za furaha zao tulizo wekewa, na tumuombe Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu azikubali amali zetu.
Marehemu Ayatollah Shahabudin Mar’ashi katika wasia wake wa mwisho alimpa mwanawe ushauri wa mawazo, moja katika ushauri huo ni huu:
“Nilimshauri (mwanangu) kusoma Qur’an Tukufu na kupeleka baraka za kisomo hicho kwa roho za wafuasi wa Ahlul-Bayt (a.s.) ambao wamefariki na hawakujaaliwa kuwacha kizazi nyuma yao.”9
Kwa hiyo, katika Mwezi huu Mtukufu wa rehema, tusiwasahau wale waliomo makaburini wakiwemo wale tusio wajua. Vile vile tuwaombee dua njema wale wanaoonekana dhahiri kuwa makafiri lakini waliompwekesha Mwenyezi Mungu na wakasilimu kabla ya kufariki kwao.
Katika kitabu chake ‘Chehl Hadith’ (Hadithi Arbaini), Imam Khomeini (Allah atukuze roho yake) anasimulia ushauri wa mawazo kutoka kwa mwalimu wake wa Irfani (elimu ya kiroho) Ayatullah Shah Abadi (r.a.) akisema:
“Shekhe wangu ambaye ni arif mkubwa, moyo wangu uwe ni fidia kwake alikuwa akisema: ‘Usimlaani yoyote japokuwa ni kafiri ikiwa hujui alikuwa katika hali gani ila tu ikiwa umejulishwa na walii aliye Ma’asum kwa kuwa yawezekana kwamba alisilimu kabla ya kufa kwake.’ Kwa hivyo usiwe na mazowea ya kulaani laani bila ya kujua hakika ya unayemlaani.”10
Mahali pengine pia Imam amesema kuwa:
Mwalimu wetu mkuu ‘Arif Shah Abadi, roho yangu iwe fidia kwake alikuwa akisema: ‘Usije ukamdharau yoyote hata kama ni kafiri, kwa kuwa kuna uwezekano wa yeye kuongoka kutokana na nuru iliyoko kwenye nafsi yake. Na ubaya na dharau zako, zikakusababishia hali mbaya na ya kuhuzunisha katika maisha ya akhera.11
Bila shaka kuamrisha mema na kukataza maovu ni tofauti na kudharau. Kwa hivyo ni bora kutowalaani makafiri kwa kuwa haijulikani mtu atafariki akiwa katika hali gani. Na lau utamlaani mtu kisha akafariki akiwa kwenye uongofu, hali yake hii yaweza kuwa kizuizi kwa maendeleo yako ya kiroho.
Hivyo basi tunapokisoma kifungu hiki cha dua, yatakiwa tujishughulishe kutenda matendo mema kwa ajili ya waislamu waliofariki kwa hali halisi ya kuwatakia furaha waliokufa.

•    1. Allāma Majlisi, Bihār al-Anwār, j. 2, uk. 90.
•    2. Mawlā Fayd Kāshāni, al-Mahajjat al-Baydā’, j. 8, uk. 292.
•    3. Tanbihu ‘l Khawātir, uk. 453.
•    4. Mawla Fayd Kashani, al-Ma¦ajjatu ‘l Bayda’, j. 8, uk. 291.
•    5. Shaykh Saduq, Man la Yahduruhu’l Faqih, j. 1, uk.181.
•    6. al-Hajj Mirza Husayn al-Nuri al-Tabrasi, Mustadrak al-Wasa’il, j.2, uk. 483.
•    7. al-Shaykh Muhammad bin al-Hasan al-Hurr al-Āmili, Wasā’il al-Shi’a ilā Tahsili Masā’il al- Shari ‘a, j. 8, uk. 279.
•    8. Ibid.
•    9. Ayatullah al-’Udhma Mar’ashi al-Najafi, Wasiyyatnameye Ayatullah al-’Udhma Mar’ashi.
•    10. Imam al-Khumayni, Chehel Hadith, hadithi ya 28.
•    11. Imam al-Khumayni, Chehel Hadith, hadithi ya 3.

MWISHO