MTUME WA AMANI
  • Kichwa: MTUME WA AMANI
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 9:8:40 2-10-1403


BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

MTUME WA AMANI  

Qur'ani Tukufu inamuarifisha Mtume Muhammad (SAW) kuwa rehema kwa walimwengu wote. Inasema mtukufu huyo ana akhlaki, maadili na tabia adhimu, na kwamba watu walivutiwa na kukusanyika pembeni yake kutokana na tabia zake njema, maneno yake laini na ya unyenyekevu, kifua kipana na upole wake.
Inaendelea kusema kuwa kama asingelikuwa hivyo na kuwa mkali, basi watu wangejiweka mbali naye na kutomkaribia kabisa. Alikuwa akishughulishwa na kutaabishwa mno na matatizo yaliyokuwa yakiwapata Waislamu na wafuasi wake. Katika aya nyingine, Qur'ani inasema kuwa Mtume alikuwa akishughulishwa mno na hali ya Waislamu kiasi kwamba alikaribia kutoa mhanga roho yake katika njia ya kutaka kuwaongoza Waislamu na kuwaepusha na madhara na upotovu.
Tangu zama za kale, makundi maovu ya kijahili na yenye uadui dhidi ya Uislamu yamekuwa yakitumia hila na upotovu kama chombo cha kujinufaisha na kukariri upotovu huo ili kuudhihirisha kuonekana kuwa ni ukweli halisi. Karne nyingi kabla ya kuanza Vita vya Msalaba dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi, serikali na tawala za nchi hizo zilifanya juhudi kubwa za kupotosha sura halisi na nzuri ya mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW). Zilijaribu kumuonyesha Mtume Mtukufu (SAW) kuwa mtu aliyependa vita na kuwa mbali na misingi ya amani, njama na upotofu ambao hadi leo ungali unaenezwa ulimwenguni na nchi hizo zilizo na chuki kubwa dhidi ya Uislamu.
Licha ya kuwa nchi hizo huzungumzia udharura wa eti kuzingatia usamehevu, kuheshimu imani, matukufu na fikra za upande wa pili, kuishi pamoja kwa amani na hata kuziarifisha serikali na nchi zao kuwa zisizo za kidini, lakini ukweli wa mambo ni kuwa misingi ya kiutamaduni na kifikra za watawala na serikali za nchi hizo, bado haijabadilika na ni ileile ya ubaguzi na uadui dhidi ya imani nyinginezo na hasa Uislamu. Licha ya kuwa hakuna tofauti yoyote ya kimsingi kati ya mitume wa Mwenyezi Mungu na kwamba wote walitumwa kwa ajili ya kufikia lengo moja la kurekebisha jamii na kumuongoza mwanadamu kwenye njia nyoofu, lakini nchi za Magharibi daima zimekuwa zikifanya juhudi za kuwatenganisha mitume hao na kudai kwamba baadhi yao walikuja kuleta amani na upendo hali ya kuwa wengine walikuja kuleta ghasia na machafuko.
Kwa bahati mbaya hali na fikra hiyo imekuwa ikienezwa na hata vyombo vya habari vya baadhi ya nchi za Kiislamu, bila kujua kwamba kwa kufanya hivyo vinatekeleza, kwa njia isiyo ya moja kwa moja, malengo ya maadui wa Uislamu ambao wanadai kwamba Nabii Isa (AS) alikuja kuleta amani na upendo hali ya kuwa Mtume Muhammad (SAW) hakuwa hivyo. Jambo hilo bila shaka linakera na kumuumiza sana kila mtu anayezingatia ukweli, haki na uadilifu kuhusiana na mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW).
Jambo linalobainika wazi ni kwamba, hata baada ya kupita karne nyingi lakini bado kuna fikra za Vita vya Msalaba na uadui wa jadi dhidi ya Uislamu unaotawala miongoni mwa jamii, serikali na watawala wa nchi za Magharibi. Badala ya kufanya juhudi za kuimarisha moyo wa udugu, maelewano, urafiki na ushirikiano, ambao ni msingi muhimu wa pamoja wa mafundisho ya dini zote za mbinguni, nchi hizo zimekuwa zikitekeleza njama za kueneza fitina, unafiki, hitilafu na migawanyiko miongoni mwa wafuasi wa dini hizo na hata baina ya mitume wa Mwenyezi Mungu. Nchi za Magharibi daima zimekuwa zikitekeleza njama za kumzushia Mtume Mtukufu (SAW) mambo yasiyomfaa kwa lengo la kumuharibia jina na kumdharau, na hivyo kuamsha hasira ya mamilioni ya Waislamu ulimwenguni. Licha ya njama na dharau hizo zote, lakini Qur'ani Tukufu inabainisha na kusisitiza wazi kwamba Mtume Mtukufu (SAW) ni Mtume wa Akhlaki na maadili aali, amani, upendo, udugu, rehema na mahaba. Ni wazi kuwa maisha yake yaliyojaa machungu na mashaka yanathibitisha wazi ukweli huo. Kufichwa chuki na uadui wa kijahili katika nyoyo za maadui wa Mtume huyo kunabainisha wazi dhulma kubwa anayofanyiwa mtukufu huyo ambaye ni Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu.
Tunabainisha hapa kwa muhtasari mambo tuliyoyaashiria hapo juu:
1- Qur'ani Tukufu inamtaja Mtukufu Mtume (SAW) kuwa rehema kwa waja wote wa Mwenyezi Mungu na kuwa ana maadili na taabia bora na adhimu. Inasema, watu walikusanyika kando yake na kuvutiwa naye kutokana na tabia njema pamoja na maneno yake laini na ya unyenyekevu, la sivyo wote hao wangemkimbia na kutotaka kuwa karibu naye. Inasifu na kumpongeza Mtume (SAW) kutokana na uwazi pamoja na upana wa kifua chake. Kitabu hicho kitakatifu kinasema kuwa Mtume alikuwa akisikitishwa sana na matatizo yaliyokuwa yakiwapata Waislamu kwa kadiri kwamba alikuwa karibu kutoa muhanga nafsi yake ili kuwaongoza kwenye njia iliyo nyooka.
2- Mtume alisema kuwa alitumwa na Mwenyezi Mungu humu duniani ili kuja kukamilisha majukumu waliyopewa mitume waliomtangulia na katika kukamilisha maadili na tabia njema. Alikuwa akiwaambia watu kwamba alikuja kukamilisha njia ya mitume wa Mwenyezi Mungu waliotumwa kabla yake. Kitabu kitakatifu cha Qur'ani kimejaa aya zinazotambua na kuwaheshimu mitume wengine wa Mwenyezi Mungu. Aya hizo zinatambua risala na vitabu vya mbinguni walivyotumwa navyo mitume hao waliomtangulia Mtume Muhammad (SAW).
3- Sira na kuishi Mtume (SAW) (jambo ambalo pia linaweza kuchukuliwa kuwa ni muujiza) katika jamii iliyopenda vita na baadhi ya wakati kutokuwa na huruma, na kisha kuwavutia watu wengi kiwango cha kumuwezesha kujenga umma mzima kutokana na jamii hiyo, ni jambo lililowashangaza walimwengu wengi. Tabia njema na mafundisho yake ya kupenda amani na upendo yalimfanya aweze kukutanisha pamoja makabila na jamii zilizokuwa na uadui mkubwa na kupigana mara kwa mara. Maadili na mafundisho yake mema yaliyakinaisha makabila hayo kuishi na kushirikiana pamoja na hivyo kusahau kabisa mielekeo na chuki zao za kikabila na kimakundi. Sera na mafundisho ya Mtume Mtukufu (SAW) yaliwapa Waislamu nguvu na uwezo mkubwa wa kuweza kushinda vita katika nyanja mbalimbali dhidi ya maadui wao kama vile vita vya kuikomboa Makka.
Licha ya nguvu hiyo kubwa ya kijeshi lakini Mtume aliyapa kipaumbele masuala ya amani, utulivu na suluhu. Baadhi ya wakati watu waliosilimu karibuni walikuwa wakimuhadithia Mtume baadhi ya ngano na visa vilivyojaa unyama na ukatili wa zama za ujahili, visa ambavyo alikuwa akiwazuia waliokuwa wakivihadidhia kuendelea kuvizungumzia.
Kwa ibara nyingine ni kuwa, Mtume hakuwa na wakati wa kusikiliza hadithi kama hizo zilizokuwa zikishajiisha unyama na ukatilia miongoni mwa Waislamu. Kulia machozi na kuomboleza Mtume (SAW) kwa kumpoteza mwanawe Ibrahim na kuuawa shahidi ami yake Hamza (AS), katika jamii hiyo iliyojaa unyama na ukatili, ambapo kubainishwa hisia na masuala ya kiroho lilichukuliwa kuwa jambo la kushangaza, kuliacha athari kubwa kwa jamii hiyo iliyokuwa ikijaribu kuachana na mielekeo ya kijahili. Mfungamano na ushirikiano wa hisia za kimaumbile aliouanzisha Mtume kati ya Answar, Muhajireen na Waislamu wengine mjini Madina, ulikuwa ujumbe wa wazi kwa wale watu waliotaka kuhifadhi na kuhuisha hisia za ghasia na mabavu zilizotawala katika zama za ujahili. Watu wa aina hiyo walitaka kuhuisha hisia hizo za kijahili hata baada ya kusilimu kwao na kuanza kufuata mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.
Kuwekwa mkataba wa udugu baina ya Waislamu Hakuna shaka kuwa kulitokea mabadiliko makubwa katika sheria na kanuni nchini Saudi Arabia baada ya kudhihiri dini tukufu ya Kiislamu. Mabadiliko hayo yaliyoandamana na sheria mpya za Kiislamu, yaligongana moja kwa moja na itikadi, fikra, mila na mienendo ya majahili. Uislamu ulikuja na sheria nyingi mpya na kubakisha baadhi ya zile zilizokuwa zikitekelezwa katika zama za ujahili, lakini tu baada ya kuzifanyia marekebisho na kuondoa humo madhihirisho ya ujahili. Mfano wa hilo ni amali za hija ambapo licha ya kuwa majahili pia walikuwa wakihiji na kuizunguka al-Kaaba, lakini Uislamu ulipokuja uliondoa nguzo na misingi muhimu ya ujahili katika amali hizo. Katika zama hizo majahili na makafiri walikuwa wakiabudu masanamu kwenye al-Kaaba lakini Uislamu ulipokuja ulifutilia mbali ibada ya masanamu na kuwajibisha ibada ya Mwenyezi Mungu Mmoja tu. Kuna baadhi ya watu wasiofahamu vyema mambo, wanaodai kwamba mkataba wa udugu alioweka Mtume baina ya Waislamu hauna tofauti yoyote na mikataba iliyokuwa ikiwekwa baina ya majahili na makafiri. Watu hao wanaghafilika na ukweli kwamba kuna tofauti kubwa mno kati ya mikataba miwili hiyo na tofauti muhimu zaidi ni kuwa mikataba ya Mtume, yote ilikuwa na uhusiano kati ya Mwenyezi Mungu na waja Wake. Hakutofautisha kwenye mikataba hiyo kati ya watu masikini na matajiri, wenye nguvu na wanyonge bali aliwasawazisha wote mbele ya sheria za Mwenyezi Mungu. Alikuwa akiwasihi Waislamu wapendane na kushirikiana kwa msingi wa mafundisho ya Mwenyezi Mungu.
Kufutwa taasubi za kikabila na kiukoo Uadui, ugomvi na chuki ya kijahili iliyokuwa imebaki katika nyoyo za baadhi ya Waislamu tokea zama za ujahili, na hasa miongoni mwa Answar ni ukweli ambao umeashiriwa wazi kabisa katika kitabu kitakatifu cha Qur'ani. Uadui huo haukuwa mdogo wala wa kidhahiri tu ambao ungeweza kutatuliwa kupitia upatanishi wa watu kadhaa. Ulikuwa mkubwa na kusababisha tatizo kubwa la kijamii kiasi kwamba Mwenyezi Mungu aliashiria jambo hilo kwa kumwambia Mtume Wake (SAW) kwamba, hata kama angetumia utajiri na mali yote iliyoko duniani kwa ajili ya kulitatua tatizo hilo, hangefanikiwa kufanya hivyo.
Kutokana na umuhimu na thamani kubwa ya mafanikio ya mkataba huo, Mwenyezi Mungu amenasibisha mafanikio hayo kwake mwenyewe ili kuthibitisha kwamba kufikiwa kwa lengo muhimu kama hilo hakutimii kupitia juhudi na nara za kisiasa za muda tu. Licha ya kuwepo tofauti kubwa za kijamii, kimakundi na kikabila katika zama hizo, lakini kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu Mtume alifanikiwa kuyaunganisha makundi hayo yote chini ya anwani ya umma mmoja wa Kiislamu na kuwa Waislamu wote ni ndugu. Kuleta mfumo wa nidhamu maalumu katika jamii ya Kiislamu mjini Madina kulitimia kwa namna ambayo maslahi na sifa za mtu binafsi hazikupewa umuhimu mkubwa bali ni maslahi na sifa za umma mzima wa Kiislamu ndizo zilizopewa uzito. Jambo hilo na kupokewa mjini Madina jumbe mbalimbali zilizokuwa zikienda huko kwa lengo la kusilimu na kuukubali Uislamu pamoja na mambo mengine mengi, ni sehemu ya miujiza ya Mtume Muhammad (SAW), miujiza ambayo ilitimia kwa madhumuni ya kuthibitisha kuwa mja huyo bora zaidi wa MwenyeziMungu alikuwa dhihirisho halisi la akhlaki, tabia njema, rehema, mahaba, suluhu, amani, udugu na usawa.

MWISHO