UKHALIFA
  • Kichwa: UKHALIFA
  • mwandishi:
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 9:41:50 2-10-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

UKHALIFA

JAWABU KWA SHEIKH MAZRUI

Baada ya kifo cha mtume
Suala la Ukhalifa ni suala nyeti sana, sina budi kabla ya kumjibu Bwana Juma Mazrui niwaletee habari muhimu zilizotokea kabla ya tukio la Ukkhalifa na kama zilivyoelezwa na Hadithi sahihi na masimlizi ya Historia katika Vitabu tunavyovitegemea:
Sina budi kumshukuru Bwana Juma Mazrui kwa jitihada zake za kutaka kuwaelewesha watu kuwa Seyyidna Ali hakuwa Khalifawa Kwanza wa Waisilamu, pia nawaomba wasomaji pia wawe na subira katika kusikiliza Upande wa pili wa maoni ya Waisilamu Huru usiotaka kushutumu yo yote kati ya Shia na Sunni juu ya suala hili.

Kwanza kabisa, Mtume Muhammad alikufa mwaka 632 AD, alikufa kutokana na ahadi yake kufika na baada ya kupewa sumu kule Khaybar baada ya kuiteka ngome ya wayahudi wa Khaybar. Mtume Muhammad (s) baada ya ushindi wake dhidi ya Mayahudi wa Khaybar alikubaliana nao na kuwapa sharti ya kulipa jizya, walilipa nusu ya mazao wanayovuna hapo Khaybar kwa Dola ya Kiislamu ya Madina.

Baada ya kufa kwa Mtume Muhammad (s) mayahudi waliobakia Khaybar waliondolewa na kufukuzwa kutoka madina na Khalifa wa pili Omar Bin al-Khattab ®.

Tukirudi nyuma kwenye ushindi wa Mtume juu ya Mayahudi wa Khaybar na sababu ya kifo chake, tunasoma katika Historia kuwa, mwanamke wa kiyahudi alitayarisha chakula na kumkaribisha Mtume (s) ambaye hakujuwa kuwa ndani yake mlikuwa na sumu na akafa baada ya miaka mitatu tangu kula kwa sumu hiyo!

Tunaambiwa na Imam Muhammad Bin Ismail Al-Bukhari kuwa: Imepokewa kutoka kwa Anas ® kuwa; " Mwanamke Myahudi alileta nyama ya mbuzi iliyopikwa na kutiwa sumu kwa Mtume (s) na Mtume akala nyama hiyo. Kisha mwanamke huyo aliletwa mbele ya Mtume, akaulizwa Mtuem na masahaba, "jee, tumwuwe mwanamke huyu? Mtume akasema, hapana. Basi nikawa naendelea kuona athari ya sumu kwenye midomo ya Mtume wa Allah.(hadi alipokufa"). Sahiih al- Bukhari,juzuu ya 3, Hadithi namba 786… Pia tazama Sahiih al-Bukhari,juzuu ya 4 Hadithi namba 394, hadithi iliyosimliwa na Sahaba Abu Hurayra. Pia tazama Tabaqaat, ya Ibnu Saad, uk. Wa 249-252, na mwisho tazama Tariikh at- Tabari, ya Imam At-Tabari, jalada la 8, uk. wa 123, 124.

Pia kabla ya kufa kwake Mtume alisema kumwambia mke wake na mama yetu bibi Aisha ® maneno haya: "Ewe Aisha, mpaka sasa hivi nahisi athari ya sumu ile niliyoila kule Khaybar, na hivi sasa nahisi kama kwamba mshipa wangu wa moyo unakatika kutokana na sumu hile" Sahiih al-Bukhari, juzuu ya 5. uk. Wa 713.

KABLA NA BAADA YA KIFO CHAKE
Imam al-Bukhari anasema kwenye juzuu yake ya 5, uk. Wa 713 wa sahihi yake kwenye hadithi iliyosimliwa na Ibnu Abbas ® kuwa, "Omar bin al- Khattab ® alikuwa akimwacha Ibnu Abbas siku zote kukaa karibu na ubavu wake, basi mara moja Abdulrahmani Bin Awf ® akamwambia Omar, "sote tuna watoto kama huyo Ibnu Abbas" Omar akajibu kwa kusema,"hakika namheshimu kutokana na cheo chake ambacho wakijuwa" kasha Omar akamtaka Ibnu Abbas amweleze fahamu yake juu ya surat al- nasr (Idha jaa, sura ya 110), Ibnu Abbas akasema: Sura ii yaonyesha kuwa kifo cha Mtume wa Mwenyezi Mungu kimekaribia, kasha Omar naye akasema sikuifahamu sura hii isipokuwa kama wewe ulivyoifahamu".

BAADA YA KIFO CHAKE

Palitokea mshtuko mkubwa sana baina ya masahaba, watu walikuwa kama wenda wazimu, hawakujuwa la kufanya, mapenzi yao juu ya Mtukufu Mtume (s) yalidhihiri na nyoyo za masahaba zilikuwa na majonzi makubwa sana. Jamii ya masahaba ya Madina ilipata mtihani mwengine wa suala la Ukhalifa, mgogoro ulitokea, khitilafu za masahaba juu ya suala la ukhalifa zilitokea na hili si jambo lililozushwa. Ndugu yangu Juma Mazrui anaona suala hili ni kama mas-khara, anaweza kuandika atakavyo na kuandika mara moja hadi kufikia makala saba hivi jambo ambalo chimbuko lake ni maisha yote ya Mtume Muhammad (s).

Suala la Ukhalifa si suala la kuandikiwa watu waliokuwa hawakusoma Hadithi wala historia ya Uislamu, ni suala ambalo linahitaji kuzungumzwa na wasomi wa Dini ya Kiislamu, mada kama hii ambayo ni nyeti ukiwatupia watu wasiojuwa hata hilo dhehebu wanalilifata ni kuwaletea kasumba itakayowapa chuki,bugdha na hata kuwaona waisilamu wenzao kuwa ni makafiri, wakati ambapo kinachotakiwa ni huko kuzipeleka fikra za waisilamu kutambuwa kuwa kweli khitilafu zilitokea katika jambo hili la Ukhalifa na hapakuwa na huko kubadilika kwa madaraka katika hali ya amani na usalama kama rafiki yangu Juma Mazrui anavyotaka kuwafahamisha wasiokuwa na elimu ya kutosha juu ya masuala haya.

Hivyo, si kila sahaba alidhani kuwa Seyyidna Abubakar ® angekuwa Khalifa wa waisilamu, bali kuna wale waliopinga jambo hilo, na haki hii haikukatazwa katika Uislamu.Palitokea watu kutoka katika sehemu mbali mbali waliopinga kuchaguliwa kwa Seyyidna Abubakar kuwa Khalifa wa Waisilamu ingawa baadaye palipatikana huko kwa wengi kuunga mkono jambo hilo ingawa nguvu, hadaa pia ilitumika katika kutetea ukhalifa na kuchaguliwa kwa Seyyidna Abubakar, haya si mageni kwa wale waliosoma historia ya Kiislamu katika Vitabu Sahihi vya Historian a vile vya Hadithi.

Inavyoonyesha ni huko kwa Seyyidna Ali (k) kukataa kumpa kura yake Seyyidna Abubakar ®, hayoni kwa sababu Ali alidhani ya kuwa yeye ndiye angestahiki kuwa Khalifawa Waisilamu badala ya Abubakar, haya yamenakiliwa na Imam Tabari katika Tariikh yake kwa kusema:"Mtume amekufa na nimeona kuwa hakuna yo yote aliyebora kwa Ukhalifa kuliko mimi lakini watu wamemchaguwa Abubakar, nami nikawafata. Kisha Abubakar naye akafa bado nilihisi kuwa hakuna aliyekuwa bora kwa jambo hilo kuliko mimi, lakini watu wakamchanguwa Omar, nami nikawafata. Kisha Omar naye akauwawa bado niliona kuwa hakuna aliyefaa kwa jambo hilo kuliko mimi, bali walimchaguwa Othman badala yangu nami tena nikawafata" Tar-iikh At-Tabari,jalada la 16, uk. Wa 51.

Mtu mwengine aliyepinga Ukhalifa wa Abubakar ® alikwua ni saad Bin Ubadah ®, yeye ni katika waliofika kwanza katika jumba la Saqifa Bani Saidah akifatwa na wajumbe wengi wa kabila la Aws na Khazraji inawa baadaye alishindwa kwa hoja na baada ya kutokea kurushiana maneno kati ya Omar na Habbab Bin Mundhir! Hapa kuna baadhi yamasahaba waliotowa hata wazo la kuuliwa kwa Saad bin Ubadah! Maneno kama Qaatalaka-llah! (Allah akulani) yalisikika yakitamkwa na baadhi ya wajumbe waliohudhuria katika tukio la uchaguzi wa Khalifa mpya (Tariikh at-Tabari, jalada la 9, uk.wa 194), vipi basi tuambiwe kuwa Ukhalifa wa Seyyidna Abubakar ® ulikuja na kutokea kwa njia isiyo na mashaka wala kibiru? Kwa ufupi hapakuwa na makubaliano ya moja kwa moja juu ya aliyefaa kuwa Khalifa baada ya Mtume isipokuwa baada ya hayo majadiliano marefu na yaliyojaa fujo na hatimaye kukubaliana kuchaguliwa kwa Seyyidna Abubakar kuwa Khalifa.

HABARI MUHIMU

1.Mtume wa Mwenyezi Mungu alikufa adhuhuri ya jumatatu, mwezi pili Mfungo sita, na Seyyidna Abubakar alichaguliwa kura Khalifa siku hiyo hiyo ambayo Mtume alikufa.Tariikh at-tabari, juzuu ya 9 uk. Wa 184.

2.Omar ® alisimama huku anasema "nani miongoni mwenu ataacha kumbai Abubakar ambaye Mtume mwenyewe alimpa kipa umbele? Kisha Omar akampa mkono wake Abubakar, baadhi ya watu wakamfata Omar, lakini Ansaar (watu wa Madina) wakasema, hatutompa kura zetu yo yote isipokuwa Ali (Tariikh tabari, juzuu ya 9 uk. Wa 186.)

3.Ali na Zubeir hawakuwepo katika uchaguzi huo wa Abubakar. Ali na Zubeir ni katika masahaba kumi waliobashiriwa pepo kwa mujibu wa Hadithi zinazokubaliwa, Zubeir alitowa Upanga wake na kusema kuwa hatompa kura yake mtu yo yote isipokuwa Ali Bib Abu talib (k), bali habari hizi zilipomfikia Seyyidna Abubakar alisema, mpigeni Zubeir kwa mawe na mnyang'anyeni Upanga wake" (Tariikh At-tabari, juzuu ya 9, uk. Wa 188-189).

1)Ali aliogopa kutokea kwa fitna mara tu baada ya fitna ya kifo cha Mtume, fitna ambayo ingeung'owa Uislamu, hivyo, alikataa mapendekezo mengi yaliyoletwa kwake na baadhi ya waliomtaka awe Khalifa. Huyu hapa Ali anamkatalia Abu Sufiyan ambaye alimjuwa kuwa bado alikuwa athari za kijahiliyyah na wazo lake la kukusanya majeshi ya Makuraishi chini ya amri ya Ali dhidi ya kupambana na Abubakar! (Tariikh At-tabari, jalada la 9, uk. Wa 198). )

TANBIIH

Tariikh ya Imam al-Tabari, niliyoitumia kwenye utafiti huu ni ile nuskha yake ya kiengereza.

MWISHO