IBADA YA HIJA
  • Kichwa: IBADA YA HIJA
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 18:37:12 2-10-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

IBADA YA HIJA

Hija ni ibada kubwa inayokusanya ibada kadhaa. Umuhimu wa ibada ya hija umo katika ahadi iliyowekwa baina ya mja na Mola wake Muumba. Imepokelewa katika hadithi zinazotaja utukufu wa ibada ya hija kwamba "Mtu anayefariki dunia hutamani kwamba laiti angetoa dunia na yaliyomo kwa ajili ya kufanya hija walau mara moja katika maisha yake.

Imam Ja'far Sadiq (as) ambaye ni miongoni mwa Watu wa Nyumba tukufu ya Mtume wetu Muhammad (saw) amesema: "Watu wanaofanya hija au umra ni wageni wa Mwenyezi Mungu. Kama watakuwa na haja basi atawakidhia, na kama watamuomba, atajibu maombi yao, na iwapo watanyamaza kimya na wasimuombe chochote, basi Yeye Mwenyezi Mungu atawapa bila ya wao kumuomba."

Hija ni ibada inayokusanya mambo mengi yanayomkurubisha mja kwa Mola wake Karima. Ni shule ya kutoa malezi na maarifa kwa waja kwa msingi wa tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Safari hiyo ya hija huanza kwa kuwekwa nia safi na ikhlasi na kukamilika kwa ibada na amali makhsusi. Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu huanza ibada hiyo kwa kufanya ihram katika maeneo maalumu yanayojulikana kwa jina la Miqaat na hapo huvaa vazi la ihram.

Ihram ni nini?
Ihram ni mwanzo wa harakati ya maarifa na safari ya ndani ya nafsi ya kutaka kujitambua vyema na kwa undani kwa shabaha ya kufikia nafasi ya juu kabisa ya kiumbe mwanadamu. Baada ya Nabii Adam (as) kuhadaiwa na iblisi mlaanifu na kuteleza, alipoteza nafasi na hadhi yake katika pepo alipokuwa. Nabii huyo ambaye alikuwa amezama katika huzuni na majonzi makubwa kutokana na tukio hilo, aliusiwa na Malaika wa wahyi Jibril (as) avae ihram kwa ajili ya ibada ya hija. Alilia mno akitubu na kumtaradhia Mola wake na kuanza safari ya kudhihirisha uja na ikhlasi yake kwa Mola Muumba. Katika ibada hii ya hija, mahujaji humuiga Nabii Adam na Ibrahim (as) kwa kuvaa vazi la ihram na kuelekea kwenye nyumba ya Allah kwa ajili ya kusafisha roho na nafsi zao.

Kwa vazi hilo la ihram la aina moja na rangi moja, mahujaji hufanya jitihada za kukata mahusiano yao yote ya kimaada, kama vyeo, kazi, mali, hadhi na daraja zao za kidunia na kidhahiri. Mahujaji hao hufanya jitihada za kutaka kutambua hakika ya dhati zao mbali kabisa na mapambo ya kidhahiri ya kidunia. Kwa maana kwamba, mwanadamu ambaye ameghafilika na hakika ya dhati yake kutokana na kuzongwa na masuala ya kimaada, huweza kuona hakika ya nafsi yake katika kioo cha ihramu na kuvua nguo za kidhahiri za kidunia na pia kutambua nakisi na mapungufu yake. Haji anayevua nguo zake za kawaida na kuvaa vitambaa viwili vyeupe vya ihram, hutambua kwamba anapaswa kuvua na kutupilia mbali vazi la kiburi, ghururi, maasi na mapambo ya kidhahiri ya kidunia.

Baada ya haji kuhirimu anapaswa kuchunga harakati na mwenendo wake na kujiepusha na mambo kadhaa. Mtu aliyehirimu anapaswa kujiepusha na baadhi ya matakwa na matamanio yake ya halali na kujishughulisha na kazi ya kuijenga na kuitakasa nafsi. Hutakiwa kuwa na akhlaki na mwenendo mzuri katika matendo na maneno yake na kujizoesha subira na uvumilivu. Kwa hakika amri zote za Mwenyezi Mungu kwa mtu aliyehirimu huimarisha azma na irada ya mwanadamu mbele ya matakwa na matamanio yake ya kinafsi. Miongoni mwa mambo hayo ni kama kukatazwa kuwinda na kuwaudhi wanyama, kujiepusha na urongo, matusi na maneno machafu na kukutana kimwili na mkewe. Hali hiyo inayopatikana katika kipindi hicho cha ihramu humrejesha hujaji katika njia ya ubinadamu halisi na kuanza safari ya ukamilifu.

Labeka ewe Mola labeka
Baada ya ihram, mahujaji wa nyumba ya Mwenyezi Mungu huanza kumuitikia Mola wao Mlezi kwa sauti kubwa wakisema "Labbaika Allahumma Labbaik", kwa maana ya Mola Wangu Mlezi! Nimeitikia wito wako. Sauti hizo za Labbaik ambazo huitwa talbiya, hujaza anga ya Makka kwa wito wa tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Hii ndiyo dhikri pekee ya wajibu katika ibada ya hija na humkumbusha mwanadamu kwamba, harakati na juhudi zake zote zinapaswa kuanza kwa kumtaja Mola Muweza. Kwa hakika maana ya talbiya ni tangazo la mwanadamu kurejea katika nafasi yake tukufu na ya kibinadamu.

AL-KAABA
Al Kaaba na nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu
Baada ya mahujaji kuacha mji na nchi zao na kukata masafa marefu wakielekea Makka, hatimaye hufika katika eneo la haram tukufu. Haram ni eneo lenye mipaka maalumu katika mji wa Makka. Eneo hilo liliainishwa na Nabii Ibrahim (as) kwa msaada wa Malaika Jibril. Imepokelewa katika hadithi kwamba, Mwenyezi Mungu SW ana haramu na maeneo matakatifu mawili. Kwanza ni ardhi ya eneo hilo la Makka ambako ibada ya hija hufanyika, na pili ni roho ya muumini. Kwa msingi huo, kama ambavyo nyumba ya al Kaaba imesafishwa na kutakaswa na shirki na uchafu wote na kuwa nembo ya tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, vivyo hivyo, roho na moyo wa muumini unapaswa kutakasika na kung'ara kama kioo na kujiepusha na kitu chochote ghairi yake Mola Muumba.

Mahujaji sasa wanawasili katika mji mtakatifu wa Makka, mji wa tauhidi, kibla na maelekeo ya walimwengu wote. Anaingia katika mji alikozaliwa Mtume Muhammad (saw), mahala wahyi ulipokuwa ukiteremshwa na Malaika kushuka. Siku za ibada ya hija huwa siku za amani na usalama kamili kiasi kwamba hata ndege wa mji huo huwa katika amani. Jambo hilo huonesha mwelekeo wa dini ya Kiislamu wa kueneza uadilifu na amani kote duniani. Uadilifu huo wa Kiislamu wakati wa ibada ya hija hutekelezwa hata kwa mimea na wanyama ambao haki zao zinapaswa kuheshimiwa na mahujaji.

Imepokelewa kwamba wakati Mtume Muhammad (saw) alipokuwa akiondoka mjini Makka alikuwa akisema: "Mji mtakatifu ulioje na ninaoupenda mno. Kama si kaumu yangu kunifukuza katika mji huu kamwe nisingeishi isipokuwa katika Makka." Nyumba ya Mwenyezi Mungu katika mji wa Makka ni jengo kubwa lenye mvuto wa aina yake ambalo lilikarabatiwa na kujengwa upya na Nabii Ibrahim akishirikiana na mwanae Ismail. Jengo hilo hadi sasa limekarabatiwa mara kumi, na mara ya mwisho kufanyiwa ukarabati ilikuwa mwaka 1040 Hijria baada ya kuharibiwa na mafuriko. Imepokelewa kwamba ardhi ya dunia imetandazwa kutokea chini ya nyumba ya al Kaaba, suala ambalo lina maana kwamba, nyumba hiyo takatifu ndiyo kituo na kitovu cha sayari ya ardhi.

Katika upande mwingine, Qur'ani Tukufu inasema waziwazi kwamba al Kaaba ndiyo nyumba ya kwanza iliyojengwa kwa ajili ya wanadamu na kutambuliwa kuwa mahala patakatifu penye amani na usalama. Aya za 96 na 97 za suratu Aali Imran inasema:

إِنَّ أَوَّلَ بَيْتٍ وُضِعَ لِلنَّاسِ لَلَّذِي بِبَكَّةَ مُبَارَكًا وَهُدًى لِّلْعَالَمِينَ* فِيهِ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ مَّقَامُ إِبْرَاهِيمَ وَمَن دَخَلَهُ كَانَ آمِنًا

"Kwa yakini nyumba ya kwanza iliyowekwa kwa ajili ya watu (kufanya ibada) ni ile iliyoko Makka yenye baraka na uongozi kwa ajili ya walimwengu wote. Humo zimo ishara zilizowazi. Miongoni mwa hizo ni mahala alipokuwa akisimama Ibrahim, na anayeingia humo (ardhi hiyo) huwa katika salama (amani)". Hija za Manabii adhimu wa Mwenyezi Mungu katika eneo hilo tukufu kama Nabii Ibrahim al Khalil na Mtume wa mwisho wa Allah Muhammad mbora wa viumbe zinalipa hadhi na utukufu makhsusi eneo hilo. Kwa msingi huo, safari ya hija na kuzuru nyumba tukufu ya al Kaaba huwa safari ya kiroho na kimaanawi ambayo inapasa kufanyika kwa ikhlasi na maarifa ili mwanadamu apate kuelewa adhama ya ardhi tukufu, historia yake, na muhimu zaidi, tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu.

TAWAFU
Twawafu na kuzunguka nyumba ya habibu kipenzi
Baada ya ihram na kumwitikia Mola kwa sauti za labbaika, hujaji huanza kutufu nyumba ya al Kaaba kwa ikhlasi na shauku kubwa na kuzunguka nyumba hiyo kongwe mara saba. Twawafu ina maana ya kuzunguka kitu ikiwa ni ishara ya kilele cha upendo na mahaba kwa kinachozungukwa. Ni ishara kwamba mtu anayetufu yuko tayari kuzunguka mahbubu na mpenzi wake kama kipepeo anavyozunguka kandokando ya mshumaa na hatimaye kujitoa mhanga kwa ajili ya kipenzi chake. Imepokelewa kwamba, kabla ya Adam (as) kuondolewa katika pepo, Malaika walikuwa wakifanya twawafu wakimsabbih na kumhimidi Mola Mlezi. Baada ya kujengwa nyumba ya al Kaaba, Malaika walimfunza Nabii Adam jinsi ya kutufu na tangu wakati huo ibada hiyo imekuwa ikifanywa na wanadamu kandokando ya nyumba ya Mwenyezi Mungu hadi hii leo ikiwa ni ishara ya kuonesha mahaba, upendo na kilele cha unyenyekevu kwa mwenye nyumba aliyetakasika na kila nakisi.

Kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndilo lengo kuu la twawafu. Kutufu huko ni kwenda sambamba na viumbe vingine vya dunia hii ambavyo vimo katika harakati ya daima ya kumsabbih na kumtukuza Mwenyezi Mungu mtukufu. Mwanazuoni na arifu mkubwa wa Kiislamu Muhyiddin bin Arabi anasema kuhusu siri ya twawafu kwamba: Mtu anayetufu kandokando ya al Kaaba anapaswa kujiona kana kwamba anatufu na kuzunguka arshi ya Mwenyezi Mungu na anakwenda sambamba na wanaozunguka arshi hiyo kama inavyosema aya ya 75 ya suratuz Zumar kwamba:

وَتَرَى الْمَلائِكَةَ حَافِّينَ مِنْ حَوْلِ الْعَرْشِ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ

Na utawaona Malaika wakizunguka pembeni mwa arshi (kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu) wakimtukuza na kumsifu Mola wao. Ibada ya twawafu ina siri nyingi. Moja ya siri na hikima hizo ni kuhudhuria katika mkusanyiko wa watu wenye lengo moja. Kwa msingi huo Waislamu katika siku za hija hujiondoa katika hali ya upweke, mifarakano na kujitenga na wenzao na kujiunga na jamii kubwa ya watu wanaomwendea Mola wao Mlezi. Katika ibada zake nyingi, dini ya Kiislamu imetoa kipaumbele kikubwa katika suala la umoja na mshikamano na kujiepusha na mifarakano na mtengano. Suala hilo lina maana kwamba, ili kuweza kufikia malengo makubwa, mwanadamu anapaswa kujiunga na kuungana na bahari kubwa ya wenzake kama yalivyo matone ya maji na hatimaye kufikia umoja na mshikamano halisi.

MWISHO