HIJA NA UMUHIMU WAKE
  • Kichwa: HIJA NA UMUHIMU WAKE
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 19:7:0 2-10-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

HIJA NA UMUHIMU WAKE
Msimu wa Hija ni machipuo ya umaanawi na kung'ara kwa tauhidi katika upeo wa dunia; na ibada ya Hija, ni chemchemi safi inayoweza kuwatakasa mahujaji na uchafu wa madhambi na mghafala, na kurejesha ndani ya nyoyo na nafsi zao atia ya Mwenyezi Mungu ya nuru ya fitra na maumbile. Kulivua vazi la majivuno na la kujipambanua na wengine katika makutano ya Hija, na kuvaa vazi la pamoja na la rangi moja la Ihramu, ni alama na nembo ya kuwa na hali moja umma wa Kiislamu, na ni hukumu ya dhihirisho la umoja na kuwa kitu kimoja Waislamu wa sehemu zote duniani.

Msimu wa Hija ni machipuo ya umaanawi na kung'ara kwa tauhidi katika upeo wa dunia; na ibada ya Hija, ni chemchemi safi inayoweza kuwatakasa mahujaji na uchafu wa madhambi na mghafala, na kurejesha ndani ya nyoyo na nafsi zao atia ya Mwenyezi Mungu ya nuru ya fitra na maumbile. Kulivua vazi la majivuno na la kujipambanua na wengine katika makutano ya Hija, na kuvaa vazi la pamoja na la rangi moja la Ihramu, ni alama na nembo ya kuwa na hali moja umma wa Kiislamu, na ni hukumu ya dhihirisho la umoja na kuwa kitu kimoja Waislamu wa sehemu zote duniani. Upande mmoja wa Sha'ar ya Hija ni

فَإِلَهُكُمْ إِلَهٌ وَاحِدٌ فَلَهُ أَسْلِمُوا وَبَشِّرِ الْمُخْبِتِينَ

"Basi Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Jisalimishieni Kwake tu, na wabashirie wanyenyekevu." Na upande wake wa pili ni

وَالْمَسْجِدِ الْحَرَامِ الَّذِي جَعَلْنَاهُ لِلنَّاسِ سَوَاء الْعَاكِفُ فِيهِ وَالْبَادِ

"Na Msikiti Mtakatifu, ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawasawa, kwa wakaao humo na wageni." Na ndivyo hivyo, kwamba al Kaaba, mbali ya kuwa ni kiwakilishi cha kalima ya tauhidi, ni dhihirisho pia la tauhidi ya kalima, udugu na usawa wa Kiislamu.

Waislamu waliokusanyika hapa kutoka pembe nne za dunia wakiwa na shauku kubwa ya kutufu al Kaaba na kuzuru Haram ya Mtume Muhammad SAW wanapaswa kuithamini na kuitumia ipasavyo fursa hii kwa ajili ya kuimarisha mfungamano wa kidugu baina yao, ambao ni dawa ya masononeko makubwa uliyo nayo umma wa Kiislamu. Leo hii tunajionea waziwazi jinsi mkono wa wasioutakia mema ulimwengu wa Kiislamu unavyofanya kazi zaidi ya ulivyokuwa huko nyuma, ya kuwafarakanisha Waislamu. Na hii ni katika hali ambayo leo hii umma wa Kiislamu unahitajia mshikamano na kuwa kitu kimoja, zaidi ya ilivyokuwa huko nyuma.

Leo makucha yaliyoroa damu ya maadui, yanaonekana hadharani yakiendelea kuleta maafa katika sehemu mbali mbali za ardhi za Kiislamu; Palestina iko kwenye mateso na madhila yanayoongezeka kila uchao, ya ukandamizaji wa kikhabithi wa Wazayuni; msikiti wa al Aqsa unakabiliwa na hatari kubwa; baada ya mauaji yale ya kimbari yasiyo na mfano, wananchi madhulumu wa Gaza wangali wanaendelea kuishi katika hali ngumu kabisa; Afghanistan iliyoko chini ya ukandamizaji wa kijeshi wa wavamizi, kila siku inapatwa na maafa na masaibu mengine mapya; wananchi wa Iraq wamekuwa hawana raha kutokana na machafuko na kukosekana amani nchini humo; na mauaji baina ya ndugu na ndugu nchini Yemen yameutia jeraha jengine jipya moyo wa umma wa Kiislamu.

Waislamu wa dunia nzima wakae na kutafakari, fitna na vita hivi, na milipuko na mauaji haya ya kigaidi na ya kiholela, ambayo yamekuwa yakijiri katika miaka ya hivi karibuni katika nchi za Iraq, Afghanistan na Pakistan yanatokea vipi na yanapangwa na kuratibiwa wapi? Kwa nini hadi kabla ya uingiaji wa kijeuri na wa kujifanya wamiliki, wa majeshi ya Magharibi katika eneo hili wakiongozwa na Marekani, wananchi wa mataifa haya hawakushuhudia misiba na masaibu yote haya? Kwa upande mmoja wavamizi wanazipa harakati za mapambano za wananchi wa Palestina, Lebanon na maeneo mengine jina la magaidi, na kwa upande mwingine wanaratibu na kuongoza ugaidi wa kinyama wa kimapote na kikaumu kati ya mataifa ya eneo hili. Katika kipindi kirefu, na kwa zaidi ya miaka mia moja, nchi za eneo la Mashariki ya Kati na la Kaskazini mwa Afrika zilikuwa katika madhila, uvamizi na unyonyaji wa madola ya Magharibi, ya Uingereza, Ufaransa na mengineyo, na baadaye Marekani; maliasili zao ziliporwa, moyo na hisia za kujihisi kuwa ni binadamu huru zilizimwa, na wananchi wao wakafanywa mateka wa uchu na tamaa za madola machokozi ya kigeni.

Na mara baada ya madhalimu wa kimataifa kung'amua kwamba haiwezekani tena kuendeleza hali hiyo kutokana na mwamko wa Kiislamu na harakati za mapambano za mataifa, na baada ya kuona kuwa suala la kuwa tayari kufa shahidi na katika njia ya Mwenyezi Mungu limeingia tena katika damu ya Jihadi ya Kiislamu likiwa ni fikra madhubuti isiyo na mithili, (madhalimu hao wa kimataifa) waliamua kutumia mbinu za hila na ujanja, na hivyo ukoloni mamboleo ukachukua nafasi ya mbinu za huko nyuma.

Lakini leo hii zimwi lenye nyuso kadhaa la ukoloni, limeamua kutumia nguvu na uwezo wake wote ili kuupigisha magoti Uislamu kwa kutumia vikosi vya kijeshi, mkono wa chuma na uvamizi wa waziwazi, mlolongo wa kazi za kishetani za propaganda, maelfu ya mifumo ya uenezaji uwongo na uvumi; kuandaa makundi ya kufanya ugaidi na mauaji ya kikatili, kusambaza vitu vya kushamirisha ufuska na maovu ya kiakhlaqi; kueneza mihadarati na kuharibu azma, nyoyo na akhlaqi za vijana, kuanzisha mashambulio na hujuma za kisiasa za kila upande dhidi ya ngome za mapambano, kuamsha na kuchochea ghururi za kikaumu na taasubi za kimapote, pamoja na kuanzisha uadui baina ya ndugu wa Kiislamu. Ikiwa upendo, dhana njema na masikilizano yatatawala baina ya mataifa ya Kiislamu, madhehebu za Kiislamu na kaumu za Waislamu, badala ya dhana mbaya na kutizamana kwa jicho la uadui ambayo ndiyo matakwa ya maadui, Waislamu wataweza kuzima sehemu kubwa ya njama na mipango ya wale wasiowatakia mema, na kutibua mipango yao miovu ya kutaka kuendelea kuuweka umma wa Kiislamu chini ya udhibiti wao.

Hija ni mojawapo ya fursa bora kabisa kwa ajili ya kufikia lengo hili tukufu.
Waislamu waelewe kwamba kwa kushirikiana na kushikamana na misingi yao mikuu ya pamoja ambayo imeelezwa na Qur'an na Sunna wataweza kuwa na nguvu na uwezo wa kukabiliana na shetani hili lenye nyuso kadhaa na kulishinda kwa imani na irada zao. Iran ya Kiislamu ni mfano dhahiri wa istikama iliyofanikiwa kutokana na kushikamana kwake na mafunzo ya Imam Khomeini (MA). Wameshindwa katika Iran ya Kiislamu. Kwa miaka thelathini sasa maadui hao wanafanya njama mbali mbali dhidi ya Iran ya Kiislamu. Kuanzia kujaribu kufanya mapinduzi hadi vita vya miaka minane vya kujihami kutakatifu. Kuanzia vikwazo na kutaifisha mali hadi vita vya kisaikolojia na kipropaganda vinavyofanywa na vyombo vyao vya habari vilivyojipanga safu moja. Kuanzia njama zao za kuizuia Iran isipate maendeleo ya kisayansi na teknolojia za kisasa kama vile teknolojia ya nyuklia hadi kufanya uchochezi na kuingilia waziwazi katika masuala ya uchaguzi uliofana kabisa wa hivi karibuni nchini Iran. Lakini njama na vitimbi vyote hivyo vya maadui vimeshindwa na hivyo kuwalazimisha maadui hao wachanganyikiwe na wachukue maamuzi ya hasira na pupa. Kwa mara nyingine ile aya ya Qur'ani tukufu inayosema:

إِنَّ كَيْدَ الشَّيْطَانِ كَانَ ضَعِيفًا

Hakika vitimbi vya shetani ni dhaifu… imethibiti kivitendo na kwa uwazi kabisa mbele ya macho ya Wairani. Katika sehemu nyingine yoyote pia, ambako istikama iliyotokana na azma na imani imewawezesha wananchi kusimama na kukabiliana na Waistikbari wenye majigambo, ushindi umewaendea waumini, na kipigo na fedheha imekuwa ndiyo hatima ya uhakika iliyowafika madhalimu. Ushindi wa dhahiri wa vita vya siku 33 nchini Lebanon na jihadi ya kujivunia na ya ushindi ya Gaza katika miaka mitatu ya hivi karibuni, ni shahidi hai wa kuthibitisha uhakika huo.

Nasaha zangu ninazozitilia mkazo kwa mahujaji wote waliopata saada , hususan maulamaa na makhatibu wa nchi za Kiislamu ambao wamehudhuria katika makutano haya matukufu, na makhatibu wa Ijumaa wa Haramain tukufu, ni kwamba wawe na uelewa sahihi wa hali halisi, na kulitambua leo hii jukumu walilo nalo linalohitaji kutekelezwa kwa haraka. Kwa uwezo wao wote wawabainishie wasikilizaji wao njama za maadui wa Uislamu, na kuwalingania watu wito wa upendo na umoja.

Wajihadhari sana na kila kinachosababisha Waislamu kudhaniana dhana mbaya; na kwa kadiri ya motisha waliyo nayo, na kwa kiasi wawezavyo kupaza sauti zao, wafanye hivyo dhidi ya Waistikbari, maadui wa umma wa Kiislamu na viranja wa fitna zote, yaani Uzayuni na Marekani na wadhihirishe kwa maneno na matendo yao kujibari na kujiweka mbali kwao na washirikina. Kwa unyenyekevu, ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atupe mimi na nyinyi nyote uongofu, taufiki, msaada na rehma Zake. Wassalaamu Alaykum
Sayyid Ali Husseini Khamenei
3 Dhilhijjatul Haram 1430 Hijria

MWISHO