UHUSIANO ULIOPO BAINA YA HAKI NA DINI
  • Kichwa: UHUSIANO ULIOPO BAINA YA HAKI NA DINI
  • mwandishi: SALIM SAID AL-RAJIHIY
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 16:31:29 6-10-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

UHUSIANO ULIOPO BAINA YA HAKI NA DINI

SEHEMU YA KWANZA

UTANGULIZI

Kwa jina la Muumba wa Mbigu na Ardhi na Viumbe wote. Ninamshukuru Muumba Mkamilifu kwa kunipa uwezo wa kuandika Makala hii, kwani mara nyingi ninapotaka kushika kalamu na kuandika kitu fulani, huwa ninapatwa na uvivu wa kufanya hivyo kwa kukhofia mambo mbali mbali, lakini leo Mola Mtukufu amenipa uwezo wa kuandika Makala hii ambayo iko mbele yenu. Makala hii iegawika katika sehemu mbili, sehemu ya kwanza inazungumzia masuala ya Haki na Dini pamoja na tofauti za kimaana zilizomo katika vitu viwili hivi, na sehemu ya pili ya Makala hii itazungumzia zaidi upande wa Haki pamoja na kugusia aina mbali mbali za Haki, ili kuweza kupata tafsiri sahihi ya neno hilo. Ifuatayo basi ni sehemu ya kwaza ya Makala hii.

Sehumu hii ya kwanza ya Makala hii, ina dhamira ya kutoa changamoto kwa wale wote wapendao Haki, kwani Haki ndiyo ufunguo pekee wa mafanikio ya Wanaadamu. Hakuna jamii katika Ulimwengu huu isiyo furahia Haki, au hata kutangaza vita dhidi ya wapinga Haki. Lakini bila ya mtu kujifahamu pamoja na kuielewa nafasi aliyonayo katika jamii anayoishi, huwa ni vigumu kuweza kuifahamu Haki yake. Wengi leo katika jamii mbali mbali huwa ni wenye kugombea nyadhifa tofauti kwa kudhania kuwa wao ndiyo wenye kustahiki nyadhifa hizo, laiti wanajamii wangaliweza kuwafahamu watu hao kiundani zaidi, basi wangaliweza kuelewa kuwa, ni nani mwenye Haki zaidi ya kupewa nyadhifa hizo. Ni mara chache mno kuweza kupatikana jamii isiyo na baadhi ya viongozi wadanganyifu, lakini tatizo huwa haliko kwa viongozi hao, bali tatizo huwa liko kwenye upanda waliyowachagua viongozi hao.

Muokozi pekee awezaye kuziokoa jamii zetu, ni chaguo letu wenyewe, kwani iwapo wana jamii watazielewa nafasi zao, huku wakizifahamu Haki walizonazo katika jamii zao, hapo ndipo watapoweza kugombania Haki zao za kijamii pamoja na kibinafsi, huku wakimuelewa ni nani awafaaye kuwaongoza. Kuna njia nyingi zinazoweza kutumika huku zikionekana kuwa ndiyo ngao za jamii katika kutetea Haki za jamii fulani, lakini si njia zote huwa ni sahihi na ni zenye kuleta mafanikio kamili ya jambo hilo.

Kwa mtazamo wangu mimi ni kwamba: njia pekee iwezayo kutoa mafanikio tosha katika kuzitambua Haki zetu, pamoja na kutupa uwezo wa kuzitetea Haki hizo ni elimu, elimu ambayo kwanza kabisa itazifunua Akili zetu pamoja na kutupa sisi thamani tunayostahiki kupewa ndani ya Ulimwengu huu tunaoishi, kwani leo katika dunia hii kila asiye na elimu huwa ndiye gurudumu zuri liwezalo kutumiwa na waovu mbali mbali, katika kuzinyakua nyadhifa mbali mbali kwa manufaa ya waliyo kidogo ndani ya jamii zetu zilizonyongeka kimaarifa.

Dini ni moja kati ya vyombo vikuu viwezavyo kutowa miongozo mbali mbali kwa wanajii, pamoja na kuwafanya Waumini wake kuwa ni imara katika kugombea haki zao za kijamii pamoja na zile za kibinafsi, na kama tulivyosema hapo mwanzo kwamba, silaha muhimu katika jamii ni elimu ya waliyonayo wana jamii wa jamii hiyo, kwa msingi huu basi, Dini bora zaidi itakuwa ni ile Dini iwezayo kutowa taaluma zilizo bora zaidi kwa Waumini wake, taaluma ambazo zitaweza kutumika kuwa ni kama silaha kuu za kuwatetea na kuwalinda Waumini hao. Bila shaka chaguo huru, huwa ndiyo Haki ya kila mwana jamii katika kujichagulia Dini aitakayo, mwenye Akili zaidi basi katika jamii, huwa ni yule awezaye kujichagulia Dini iwezayo kumpa maendeleo ya Kiroho na Kimwili, maendeleo ambayo yatazingatia nafasi aliyo nayo mtu huyo katika jamii yake, huku ikimzindua kwa kumpigia honi ya tahadhari kutokana na madhara mbali mbali yawezayo kumuelekea kutoka upande fulani, iwapo yeye atakwenda kinyume na mafunzo ya dini hiyo.

Kengele ya tahadhari haitaacha kulia kwenye kila sikio la jamii iliyokubali kufuata miongozo ya Dini sahihi, lakini kuisikiliza au kuto isikiliza sauti hiyo ya tahadhari, huwa ni hiyari ya kila mmoja wetu, lakini lililo muhimu kulifahamu ni kwamba, madhara yaingiapo katika jamii fulani, huwa hayana ubaguzi katika kusibu kwake, bali madhara hayo humsibu au kumgusa kila mwana jamii anayeishi katika jamii hiyo.
Ninamuomba Muumba Mtukufu azifunguwe jamii zetu, na atupe elimu iwezayo kutuletea manufaa ndani ya jamii zetu, Aamin.

UHUSIANO BAINA YA HAKI NA DINI
Kuna maswali mengi yanayoweza kuulizwa kuhusiana na Dini na Haki, au kuhusiana na fungamano lililopo baina ya vitu viwili hivyo, na miongoni mwa maswali hayo ni kama ifuatavyo:
Jee Dini ndiyo Haki, au Haki ndiyo Dini?
Jee Dini ndiyo inayoihitajia Haki ili iwe Dini ya Haki, au Haki ndiyo inayoihitajia Dini ili iwe ni Haki?
Jee fungamano la Haki na Dini, ndilo linaloifanya Dini kuwa ndiyo chimbuko la kudhihiri kwa Haki mbali mbali?
Jee watu huwa wanaikubali Haki, kwa kuwa Haki hiyo imetiwa saini na Dini, au watu huwa wanaikubali Dini kwa kutokana na kuwa Dini hiyo inaendana na Haki?
Ili papatikane ufahamu mzuri kuhusiana na maswali haya, pamoja na kuwafanya watu wayaelewe vizuri makusudio ya Makala hii, inanibidi niyageuze maswali haya katika mtindo ufuatao: Jee Haki ndiyo inayotakiwa kuwa ni kipimo cha kuzitambua Dini za Haki na za kweli, au Dini ndiyo inayotakiwa kuwa ndiyo kigezo cha kuzitambua Haki mbali mbali?

Jee Dini ndiyo kigezo cha mambo mbali mbali, au Haki ndiyo kigezo cha mambo hayo?
Jee Haki ndiye mdhamini wa Dini katika kuyapasisha na kuyakubali masuala ya Dini, au Dini ndiyo inayoidhamini Haki katika kiufanya Haki iwe ni Haki?

Ikiwa Haki tutaichukua kuwa ndiyo kigezo, hapo basi Dini itahitajika kuifuata Haki na kuto toka nje ya mipaka ya Haki, lakini iwapo Dini ndiyo itakayokuwa kigezo, hapo basi Haki haitakuwa na uhuru wa kutoka nje ya mipaka ya Dini. Mtafaraka wa masuala mbali mbali kama haya, ni lazima upate jawabu madhubuti ili kuweza kupata muongozo sahihi utakaoweza kutuondoa katika njia panda, kwani iwapo mtu atashindwa kupata jawabu sahihi kuhusiana na maswali haya, Akili ya mtu huyo haitaacha kutangatanga bila ya kuwa na mashiko ya kuyashika, huku ikitafuta muokozi wa kumuelekeza njia iliyo sahihi na salama katika maisha yake.

NATIJA MBALI MBALI
Natija mabali mbali zinaweza kupatikana kutokana na maswali tofauti yaliyoulizwa hapo juu, na aina za natija hizo zitategemea namna ya mtu atakavyo yajibu maswali hayo. Miongoni mwa natija zinazoweza kupatikana kutokana na maswali hayo ni kama ifuatavyo:
1- Kipimo na kigezo cha Dini ni Dini yenyewe, na wala sisi hatuna haja ya kutafuta kigezo chengine, ama kigezo cha Haki siyo Haki yenyewe, bali kigezo cha kuitambua Haki ni Dini.

2- Kigezo na kipimo cha Haki ni Haki yenyewe, na sisi hatuna haja kuzitafuta sababu zilizoifanya Haki kuwa ni Haki, lakini Dini katika kukubalika kwake, inahitajia vigezo maaalumu, na vigezo vya kuikubali Dini ni Haki. Kwa ibara nyengine ni kwamba, Haki hujitegemea wenyewe katika kuthibiti kwake na wala haihitajii mdhamini yeyote wa kumdhamini na kumpa ithibati, ama Dini haiwezi kusimama wenyewe bila ya kuwa na mdhamini wa kuithibitisha Dini hiyo kwa kutoa ithibati maalumu kuhusiana na Dini hiyo.

3- Kila kimoja kati ya Dini na Haki, huwa ni vyenye kujitegemea wenyewe, yaani Dini haihitajii ithibati kutoka upande wa Haki katika kuthibiti kwake, na wala Haki haihitajii ithibati kutoka upande wa Dini katika kuthibiti kwake. Katika hali kama hii huwa hakupatikani mgongano wa aina yeyoye ile baina ya pande mbili hizo, hivyo basi kila kimoja miongoni mwa vitu viwili hivi, huwa ni chenye kushika njia yake bila ya utata wowote ule. Msingi huu huwa unakifanya kila kimoja kisimdhuru mwenziwe, na vile vile kila kimoja hakitokuwa na msaada wowote ule kwa mwenziwe katika kuthibitika kwake, jambo ambalo huwa halionyeshi fungamano la aina yeyote ile lililopo baina ya pande mbili hizo.

Iwapo hali itakuwa ndiyo kama hiyo, hapo basi Dini itakua inanadi upande wa Dini, na Haki nayo itakuwa ikinadi upande wa Haki, na hapo ndipo kila kimoja kati ya Dini na Haki kitapoonekana kujitangazia sera zake peke yake, bila ya kuuegemea mgongo wa mwenziwe. Hali ambayo itamfanya Mwanaadamu ashughulishwe na minada miwili hiyo, kiasi ya kwamba hatojua ashike lipi aache lipi, kwani bila shaka kutatokea watu watakaopenda kuwa na Dini huku wakiwa wameshikamana na Haki, hali ya kuwa kufanya hivyo kutakuwa ni jambo la muhali na lisilowezekana kwa watu hao, kwani iwapo mtu fulani ataamua kushikamana na Haki, hapo basi itambidi aachane na Dini, kwani Dini ni yenye kwenda kinyume na Haki.

Na kwa upande wa pili tunaweza kuwagawa watu katika makundi mawili, kundi lenye kufuata Haki na kundi lenye kufuata Dini, kitu ambacho kitasababisha ugomvi baina ya makundi mawili hayo, kwani kutakuwa hakuna mizani ya kulitetea kundi lolote lile iwapo kutatokea ugomvi katika kugawa kazi na nyadhifa mbali mbali za jamii. Na mambo hayatoweza kuishia hapo tu, kwani katika jamii kunaweza kukatokea kundi la tatu ambalo halitokubaliana na upande wowote ule miongoni mwa pande hizo mbili, na kundi hili halitoacha kuvutia upande wake katika kuchukua nyadhifa na haki mbali mbali za kijamii, na hapo basi ndipo ugomvi utapowaka moto zaidi iwapo hapatopatikana muamuzi atakaye uamua ugomvi huo, huku akiwa huyo yuko nje ya makundi matatu hayo, kwani Hakimu hatotakiwa kufungamana na upande wowote ule wa makundi hayo yanayogombana.

4- Najita nyengine tunayoweza kuipata, ni natija isemayo kuwa, Dini na Haki vyote viwili havina uwezo wa kujithibitisha wenyewe au kimoja kukisaidia chegine katika kutibitika kwake, bali kuthibitika kwa vitu viwili hivi, huwa kunahitajia kitu chengine cha tatu ambacho kitachukua nafasi ya Hakimu mkuu atakayeweza kukithibisha kila kimoja kati ya Dini na Haki bila ya matatizo, yaani Hakimu huyo atatakiwa kutupa sisi vigezo maalumu vitakvyoweza kuithibitisha Dini katika kukubalika kwake, pamoja na kutupa mizani na vigezo maalumu vya kupimia Haki katika kukubalika kwake.

Katika hali kama hii, itabidi tuulize swali lisemalo kua: je kigezo cha tatu ambacho kitakuja na kukithibitisha kimoja kati ya Dini au Haki, kitatumia kigezo gani katika kusimamisha ithibati zake? na suali hili halitaweza kumalizikia hapo, kwani Hakimu atakayekuja kutupa vigezo hivyo, ima atakua ametegemea Dini, au atakua ametegemea Haki katika kutoa vigezo hivyo, la si hivyo atakua ametegemea kitu chengine kilichuwa nje ya vitu viwili hivi, hapo basi suali litakuja katika kitu hicho kilichotegemewa, kuwa je kitu hicho kinalenga upande gani katika kukipa uzito kila kimoja kinachothibishwa? Na hali ndiyo kama hiyo.

Kuna masuli mengi yanayoweza kujitokeza katika hali moja au nyengine itakayo kadiriwa na Mwanaadamu katika kuyajibu maswali yaliyoulizwa hapo mwanzo.

BAYANA
Iwapo tutaamini kua, Dini ni yenye kufuata Haki, hapo basi tutajikutia tukishikamana na moja katika ya misingi ya kifikra na misingi hiyo ni kama ifuatavyo:
1- Dini ndiyo chemchem ambayo kwayo hudhihirika Haki mbali mbali, lakini si makusudio yetu kusema kua, Haki zote Duniani zina vyanzo vitokanavyo na Dini, kama vile Haki zinazothibiti katika Falsafa au elimu nyengine mbai mbali.

Lakini kuna ulazima gani unaotufanya sisi tuseme kuwa ukweli wote unaopatikana katika elimu tofauti unatokana na Dini? Jee hivi sisi tunatakiwa kuwa na Itikadi isemayo kuwa: aina zote za uhakika mbali mbali unaopatikana kutokana na elimu tofauti, pamoja na utafiti mbali mbali, vyote hivyo vinatokana na Dini?

Na je Aya isemayo:
{Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinacho bainisha kila kitu, na ni uwongofu,na rehema, na bishara kwa Waislamu.} 1
Hivi Aya hii inakusudia kusema kua, Muumba Mkamilifu amekileta Kitabu kinachobainisha Haki zote zenye fungamano na malengo ya kumuongoza Mwanaadamu kuelekea kwa Mola wake? au Aya hii inakusudia kusema kuwa Kitabu hichi kimekusanya kila aina za Haki ndani yake, zikiwemo Haki zinazofungamana na Elimu za Majaribio na Elimu za Kiakili, bila ya kuzingatia kuwa je elimu hizo zina mchango wowote katika kumuongoza Mwanaadamu katika suala la kuelekea kwa Mola wake, au hazina mchango?
Je hivi kuna Hesabati au Chemistry inayohusiana na Dini na ile isiyo husiana na Dini?

Lililo Haki na sawa ni kwamba, masoma kama kama haya yanaweza kuwa na aina mbili za mitazamo, hivyo basi iwapo tutakizingatia kuwa, Dini inatutaka kujifunza masomo hayo katika njia iliyo shihi na kuyatumia katika njia iliyo sahihi, nasi tukafanya kama tulivyo amrishwa, na kuyatumia masomo hayo kama tulivyo amrishwa, hapo basi masomo hayo yatakua na fungamano la Kidini, na kwa mtazamo mwengine, masomo haya tunaweza kuyahesabu kuwa si masomo ya Kidini, kwani masomo haya hayana chimbuko la moja kwa moja na masuala ya Maamrisho au Makatazo pamoja masuala ya Kiitikadi au Kimaadili.

Tukitupia macho upande wa elimu za Kiakida, tutakutia kuwa suala hili huwa lina picha nyengine kabisa, kwani Dini huwa ina fungamano la moja kwa moja baina yake na baina ya fikra na Itikadi sahihi za Wanaadamu. Katika masuala ya Kiakida Dini huwa haiachi kutoa mchango wake, hii ni kwa kutokana na haja walionayo Wanaadamu ya kutaka kupata muongozo utakao wasaidia kuwaelekeza katika Itikadi iliyo salama.

Kwani iwapo Wanaadamu watashidwa kupata picha halisi ya Mola wao pamoja na kuzitambua Sifa za Mola huyo, Wanaadamu hao hawataacha kutumbukia katika aina mbali mbali za Shirki zitakazo wazorotesha katika kujipatia maendeleo yao.

Lakini iwapo mtu atakosea katika masuala yanayohusiana na elimu kama vile Baiolojia, makoseo hayo hayatoweza kuleta madhara katika Dini na Imani yake, kwa mfano mtu akiwa anakubaliana na nadharia ya Mwana Sayansi fulani katika mitazamo ya Kijografia, hali ya kuwa mitizamo hiyo haiko sawa, huku akiwa mtu huyo ana Imani kamili kuhusiana na Muumba Mkamilifu pamoja na kuwa na Imani ya kuwa Muumba Huyo Ndiye Mpangaji wa nidhamu ya Dunia hii, jambo hilo hailitamfanya yeye kutoka nje ya Dini au kuhesabiwa kuwa yeye yuko kinyume na Dini yake. Suala hili linatakiwa kufahamika vizuri, ili watu waweze kuelewa makusudio ya maelezo yaliopita hapo juu.

UFAFANUZI WA ZIADA
Katika mitizamo mbali mbali ya Kielimu, Dini inaweza kutoa mtizamo wake ili kuweza kuwaongoa Wanaadamu na kuwatoa katika utatanishi, lakini Dini huwa inagusia zaidi yale mambo yawezayo kumsaidia Mwanaadamu katika kuongoka na kushikamana kwake na Mola wake, hivyo basi kama Dini itaona kuwa kuna umuhimu wa kutowa mtizamo wake kuhusiana na suala fulani la kielimu, hapo basi Dini hiyo itaelezea mtazamo wake kuhusiana na suala hilo.

Tukiutupia macho mtazamo wa Mwana Sayansi maarufu ajulikanaye kwa jina la (Darwin), uzungumziao suala la maendeleo ya viumbe katika kinyanganyiro na mieleka ya kimaisha, tutakutia kuwa mtazamo huu hauko sawa na mtazamo wa Dini zitokazo Mbinguni, kwani mtazamo wa bwana Darwin unasema kuwa umbile la mwanzo la Mwanaadamu lilikuwa likifanana na kima, au kwa lugha nyengine tunaweza kusema kua, kwa mtazamo wa bwana Darwin ni kwamba, Mwanaadamu alipitia katika hatua mbali mbali hadi kuufikia Ubinaadamu aliyonao leo, lakini Dini mbali mbali ni zenye kupingana na Mtazamo huo, na Uislamu nao hauendani sawa na mtazamo wa bwana Darwin. Kwani Uislamu unamuheshimu Mwanaadamu wa mwanzo kama unavyo muheshimu Mwanaadamu wa zama hizi za leo, na Uislamu unawahesabu Wanaadamu wote kuwa ni wenye uwezo wa Kiakili wa kuweza kupambanua mabo mbali mbali, na unamuhesabu Mwanaadamu wa mwanzo aliyekuja katika Ulimwengu huu kuwa ni Mtume, naye alikuwa ni Nabii Aadamu (a.s).

Kwa hiyo Uislamu unaweza ukawa umegusia na kutoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo mbali mbali yanayohusiana na elimu mbali mbali za Sayansi, lakini malengo huwa si kuzamia zaidi katika elimu hizo bali ni kutoa baadhi ya milekeo itakayoweza kumsaidia Mwanaadamu katika kuongoka kwake, kwani malengo hasa ya Qurani na Sheria ya Kiislamu, ni kumuelekeza Mja kwa Mola wake na kumpa Nuru isiyozimika.

Suala jengine ambalo tunaweza kulizungumzia hapa ni kwamba, je kuhusiana na elimu za matendo na tabia, hivi Mwanaadamu katika masuala ya kimatendo na kitabia, ni mwenye kuhitajia maelekezo ya Dini? na je Akili ya Mwanaadamu haidiriki na kufahamu aina yeyote ya matendo mazuri ua mabaya, au inadiriki kwa kiasi fulani? na je amri za Dini huwa zote ni amri za Wajibu au Zote ni amri za Kutoa muongozo tu, au ndani yake mna amri za Wajibu na baadhi yake huwa ni amri za kutoa muongozo tu bila ya kuwa na uzito wa Wajibu? Mwanaadamu ameumbwa na Akili, na kuna masuala mbali mbali ambayo kuyafahamu kwake huwa kunahitajia kuwa na Akili tu pasi na kuwepo msukumo wa Dini, na miongoni mwa masuala hayo ni kama vile: "Kuiba ni kubaya, kusema uongo ni kubaya, kutesa ni kubaya". Masuala kama haya huwa hayahitajii miongozo ya Kidini katika kuufahamu ubaya wake, bali kila mtu mwenye Akili huwa anafahamu ubaya wa mambo kama hayo. Kwa hiyo Akili inaweza kudiriki na kuifahamu misngi mbali mbali ya Uanaadamu, lakini bado Mwanaadamu huwa ni muhitaji wa Dini katika kuikamilisha misingi hiyo, hapa basi ndipo unapokuja ulazima wa Mwanaadamu kushikamana na Dini, ukweli ni kwamba Mwanaadamu hujengeka kwa kupitia njia mbili kuu, nazo ni Akili pamoja na maelekezo Dini itokayo kwa Mola wake.

Kuhusiana na Amri za Dini, baadhi ya amri hizo huwa ni za Wajibu na nyengine huwa si za Wajibu, bali huwa ni zenye kutoa muongozo tu. Amri za Wajibu huwa hazikubaliki kuepukwa, hii ni kwa sababu ya uzito wa faida zinazoweza kupatikana ndani ya amri, iwapo Mja atazitekeleza amri hizo, kama vile amri ya kutoa zaka, amri hi huwa inauzito wa kutoweza kuepukika kwani nchi huwa inahitajia mali katika sekta mbali mbali za kimaendeleo, kama vile kupiga vita ufakiri, kujenga Mashule, kuhifadhi watoto yatima na mengineyo, hivyo basi ni lazima Wananchi wenye uwezo watowe zaka kwa ajili ya kuimarisha nchi yao.

Amri zenye kutoa muongozo hali zikiwa si za Wajibu, ni amri ambazo huwa zinatowa mchango wa kumuendeleza Mwanaadamu kwa kiasi fulani, kiasi ya kwamba iwapo atazipuuza amri hizo basi maendeleo yake yanaweza kuzorota kwa kiasi fulani, kama vile amri ya kuondoa mwiba au vizuwizi katika njia. Ukiangalia kwa makini utakutia kuwa, kuondoa vizuwizi katika njia kunaweza kuwasaidia wanajamii kupita kwa haraka katika njia hizo na hatimaye kutochelewa Maofisini au kutochelewa katika sehemu za kazi zao, na kuto ondoa vizuwizi hivyo kutazizorotesha kazi za jamii tu na hakutoweza kuzisimamisha kabisa kazi hizo, ndiyo maana jambo hili likapewa uzito wa daraja ya chini kidogo katika kuamrishwa kwake.

2- Mtazamo wa Kiislamu unaihesabu Haki kuwa ndiyo kigezo na mizani ya kila kitu, na hakuna mizani ya kuipimia Haki isipokua ni Haki yenyewe. Mtafutaji wa Haki siku zote huwa ni mwenye thamani hata kama mtu huyo atakuwa hakuifikia Haki aitafutayo, na mtafutaji wa Batili hawezi kuwa na thamani katika jamii yeyote ile ya watu wenye Akili. Kwa kutokana na thamani aliyonayo yule mtafutaji wa Haki, hata kama mtu huyo hataifikia Haki aitafutayo, Imamu Ali (a.s) anasema: {Msiwauwe Makhawaarij baada ya mimi kuiaga Dunia, kwani yule mtafutaji wa Haki akawa hakuifikia Haki aitafutayo, huwa hawi sawa na yule mtafutaji wa Batili aliyeifikia Baliti aitafutayo} 2

Kuna tofauti kubwa ilioko baina ya wafuasi wa Muaawia na Makhawaariji, kwani Makhawaariji walikua ni watu Wacha Mungu na wenye wivu wa Dini yao, lakini wafuasi wa Muaawia hawakuwa na Ucha Mungu wala wivu wa Dini yao, na walikuwa wakifahamu vizuri kuwa wao wamo katika Batili, lakini Makhawaariji walikanganishwa na fitina mbali mbali ukiwemu Ubilisi wa Nafsi zao, jambo ambalo liliwasababisha kutengana na kiongozi wao (Imamu Ali (a.s)) na mwishowe kutangaza vita dhidi ya Imamu wao.

Katika vita vya Jamal kuna watu waliopigwa na butwaa pale walipowaona Masahaba wakubwa wakubwa, kama vile Talha na Zubeir pamoja Aaisha abaye ni Ummul- Muuminiina, wakiwa wanakabiliana na Ali (a.s) katika vita hivyo. Mmoja katika watu waliyo kangazwa na suala hilo alishindwa kustahamili, hivyo basi alimwendea Imamu Ali (a.s) akamwambia: "Hivi yawezekana Talha na Zubeir pamoja na Aaisha wawe katika Batili?"

Imamu Ali alimjibu kwa kumwambia: "wewe mambo yamekukangaza; tambua kuwa watu na vyeo vyao huwa si vipimo vya kupimia Haki na Batili. Kwanza unatakiwa uielewe Haki, hapo ndipo utapomuelewa aliyeshikamana na Haki, na utapoielewa Batili ndipo utapowaelewa waliyoishikamana na Batili". Mwandishi wa Kimisri ajulikanaye kwa jina la Dokta Taha Husein katika kitabu chake anasema: "Tangu Wahyi wa Mbinguni kumalizika, hakujawahi kusikika Sentesi nzito kimaana kama ilivyo Sentensi hii". 3

Mwenye Akili na busara ni yule ambaye Haki huiweka mbele, na huwa si mwenye kuburuzwa na vugu vugu la Kimadhehebu, Vikundi, pamoja na mwenendo wa jamii bila ya kutumia mizani ya Haki katika kuyapima mambo hayo. Wazee, Waalimu pamoja na Viongozi mbali mbali waliyotupa maarifa mbali mbali, ni wenye kustahiki heshima na shukurani, lakini tusije kuwageuza kuwa wao ndiyo bendera ya Haki, au kuyahesabu yote yatokayo midomoni mwao, kuwa ni Hekima zitokazo kwa Mola wetu, kwani Wanaadamu wa kawaida huwa ni wenye kusibu na kukosea. Basi itakuwa si busara kwa mtu fulani, kubeba mabahasha ya fikra za yule aliyemsomesha, kwa dalili tu ya kuwa yeye alikua ni Mwalimu wake, kwani bado mpaka leo Haki itabakia kuwa ndiyo kigezo pekee cha kuzipima fikra mbali mbali. Mwana Falsafa maarufu ajulikanaye kwa jina la "Aristotle", alipokuwa akiitoa makosa baadhi ya mitazamo ya Mwalimu wake ajulikanaye kwa jina la "Plato", alisema: "Kwa hakika Mwalimu wangu Aristotle ninampenda, lakini Haki ninaipenda zaidi kuliko Aristotle" 4

Sadrul-Mutaallihiin katika juzuu ya sita ya kitabu chake kiitacho "Al-Asfaarul-Arba-a", akizungumzia masuala ya Itikadi ya Mola Mtukufu anasema: "Mtu mwenye Hekima huwa haangalii wengi wape, na aigunduapo Haki huwa hakhofii kuzipinga kauli za waliyo wengi, vile vile yeye huwa haangalii msemaji ni nani, bali huangalia nini kilichosemwa? Kama ilivyopokewa kutoka kwa Imamu wa Wacha Mungu Ali (a.s) kuwa amesema: "Haki haitambuliwi kwa kupitia nyuso za watu, bali kwanza itambue Haki, hapo ndipo utapowatambua walioshikamana na Haki" Nasi huwa hatuna malengo mengine pale tunapozichunguza na kuzipekua kauli mbali mbali, isipokuwa tunafanya hivyo kwa kutaka kujitakasa na kujikaribisha kwa Mola wetu. Hivyo basi iwapo kauli za Watafiti tunazozitafiti zitaendana na Haki, basi tutashikamana nazo, lakini iwapo kauli hizo zitakuwa zinapingana na Haki kwa sababu ya maradhi ya Nafsi zao, hapo hatutakubaliana na na kauli zao zipingazo Haki" 5

Mpaka hapa tulipofika, tutakuwa tumeshatoa picha kamili ya mtazamo wetu kuhusiana na suala la Dini na Haki, na mtazamo wetu umeweza kufikia natija isemayo kuwa: "Haki ndiyo kigezo pekee cha kila kitu na hakuna kigezo cha kuipima Haki isipokuwa ni Haki yenyewe". Sina budi sasa kuchukua wasaa niliyonao kwa ajili ya kutoa ufafanuzi zaidi, pamoja na kusimamisha dalili kuhusiana suala hili.

Bila shaka ili suala hili lieleweke kwa vizuri zaidi, kwanza kabisa tunatakiwa kuitaarifisha Dini pamoja na Haki kwa kupitia taarifa iliyo sahihi na isiyo na mkangazo wa aina yeyote, kwani iwapo hakutapatikana tafsiri sahihi ya neno Dini na Neno Haki, hakutaweza kupatikana ufumbuzi na jawabu sahihi kuhusiana na kuwa je Dini ni Haki au Haki ndiyo Dini?

Je ni wadhifa wetu kuzitetea Dini mbali mbali, kama vile Dini ya Kiyahudi au Kikristo? Je kuna umuhimu wowote kwa mtu mweye kutaka kuutetea Uislamu, kuzungumzia fungamano lililopo baina ya Haki na Dini nyenginezo kama vile Ubuda Umajusi Uhindu na Nyenginezo?

Neno Dini katika tafsiri ya ujumla, huwa linazikusanya Dini mbali mbali, na hata kuabudu masanamu katika tafsiri hii ya kiujumla pia huhesabiwa kuwa ni Dini, na hilo linaonekana wazi katika Qurani pale Muumba Mkamilifu aliposema: "nyinyi mna Dini yenu na Mimi nina Dini yangu" 6

Kuna masafa marefu yaliopo baina ya Dini ya Uislamu na Dini ya Washirikina, lakini Dini zitokazo Mbinguni huwa ni zenye fungamano moja, kwani shina la mti huu ni moja. Dini ya mwisho iliyokuja kutoka Mbinguni, ndiyo Dini iliyokamilika kuliko Dini zilizopita kabla yake. Dini zote zilizokuja kutoka Mbinguni ni Dini zilizokuwa zikikamilika hatua baada ya hatua, yaani kila Dini iliyokuja baadaye ilikuwa ikiikamilisha Dini iliyopita kabla yake, kwa hiyo sheria zote zilizokuja katika Dini zilizopita, huwa zinapatikana katika Dini ya Kiislamu kwa ukamilifu zaidi. Hapa sitaki kusema kua kila kitu kilichokuwepo katika Dini zilizopita ni lazima kiwepo katika Dini ya Uislamu, la hasha! kwani kila Dini huwa ina Misingi mikuu na Misingi midogo, Misingi mikuu ya Dini za Mbinguni huwa haitofautiani, lakini misingi midogo yaweza kuwa na tofauti fulani, kwa jinsi ya hali ya jamii zilivyo.

Kuzitetea Dini mbalili mbali hakuwezi kuwa ni msaada wa kuisaidia jamii, bali huwa ni msaada wa kuzisambaratisha jamii mbali mbali, hii ni kwa kuzingatia kuwa, haiwezekani Dini zote zikawa ni Dini za haki, hasa hasa tukizingatia kuwa Dini hizo ni zenye kupingana katika baadhi ya mafunzo yake. Kuzitetea Dini mbali mbali huwa kunamaanisha kuwa hakuna Dini yenye kwenda sawa na Haki, kwani kungalikuwapo Dini yenye kwenda sawa na Haki, basi kungelipaswa kuitetea Dini hiyo na kuachana na zile Dini zisizofungamana na Haki. na kwa kutokana na kuwa kila mmoja hudai kuwa Dini yake ndiyo Dini ya Haki, hivyo basi ni lazima kupatikane uchunguzi wa kina katika kuutambua ukweli na uhakika wa Dini mbali mbali.

Kuna ulazima kwa mtu mwenye kutaka kuutetea Uislamu, kuzungumzia fungamano lililopo baina ya Haki na Dini, kwani ni lazima watu wafahamishwe kuwa Dini ni yenye kuhitajia Haki katika kusadikika kwake. Iwapo watu wataielewa Haki na kuifahamu vizuri, na kwa upande mwengine wakawa wameyaelewa mafunzo ya Dini kwa vizuri, hapo basi wao wataweza kuwa huru katika chaguo lao la kuichagua dini waitakayo.

Ufafanuzi tuliyo utowa katika Makala hii kuhusiana na Haki, waweza ukawa si ufafanuzi tosha utakaomkinaisha kila mmoja wetu, bali kuna wengine wanaoweza kutosheka na ufafanuzi huu huku wengine wakawa bado wanataka nyongeza zaidi, lakini kutosheka kwao hakotonitoa mimi shaka ya kuwepo wengine watakaotaka ufafanuzi wa kina zaidi. Kwa hiyo dhana yangu ya kuwepo watu wanaohutajia nyongeza inanilazimisha kuendelea na utafiti zaidi kuhusiana na suala hili la ufafanuzi juu ya Haki. Mimi basi nitaijaalia Makala hii kuwa ni kama ufunguo wa kuufungua mlango wa utafiti wangu juu ya suala la Haki, na ninawataka wasomaji wapenzi wafuatilie sehemu ya pili ya Makala hii, sehemu ambayo itaendelea kutowa ufafanuzi na uchambuzi juu ya suala hili. Ninamuomba Muumba Mkamilifu akukamilisheni nyinyi pamoja namimi kielimu kwa baraka na fadhila za Mtume wetu (s.a.w.w) pamoja na Aali zake.
Aamin.
Mwisho wa sehemu ya kwanza ya Makala hii.

MAREJEO YA VITABU
1 - Suratu- Nahli Aya ya 89 .
2 - Nahjul-Balagha Hotuba ya 59 .
3 - Rejea kitabu Ali wa Banuuhu ukurasa wa 40 .
4 - Kamusi ya Kipashia ya Deh Khodaa Neno