UMOJA NI JAMBO LA DHARURA
  • Kichwa: UMOJA NI JAMBO LA DHARURA
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 16:56:36 6-10-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

UMOJA NI JAMBO LA DHARURA

Profesa Burhanu Deen Rabbani, Rais wa zamani wa Afghanistan amesema katika kikao cha 23 cha kimataifa cha Umoja wa Kiislamu mjini Tehran kwamba, umoja katika umma wa Kiislamu si tu kwamba ni wadhifa bali ni jambo la dharura na hitajio muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu.

Akizungumza hapo siku ya Jumanne katika kikao cha ufunguzi wa mkutano huo muhimu wa kimataifa, Bwana Rabbani amemshukuru Ayatullah Ali Taskhiri, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kukurubisha pamoja Madhehebu ya Kiislamu pamoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kudumisha na kuimarisha umoja miongoni mwa Waislamu. Rais huyo wa zamani wa Afghanista amesema kuwa nguzo za Uislamu zimesimama juu ya msingi wa umoja katika umma wa Kiislamu na kwamba Uislamu unauchukulia umoja kuwa msingi muhimu sio kwa ajili ya Waislamu tu bali kwa ajili ya jamii nzima ya mwanadamu.

Amesema jambo hilo ndilo limeleta saada na msisimuko maalumu kati ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu katika kipindi chote cha historia. Rabbani ameongeza kuwa, tunaporejea historia tunatambua wazi kwamba Mtume Mtukufu (SAW)N mwanzoni mwa kuasisi serikali ya Kiislamu katika mji mtakatifu wa Madina kwa uungaji mkono wa Waislamu na Mayahudi, aliwapa wote haki sawa za kiraia na hivyo kusisitiza juu ya msingi wa umoja.

Amesema, Mayahudi waliendelea kunufaika na haki hizo hadi pale walipoamua kuwafanyia hiana Waislamu. Rais wa zamani wa Afghanistan amesisitiza kwamba maendeleo ya Waislamu yalipatikana pale tu walipokuwa na umoja na kwamba matatizo yao yalianza kudhihiri na kuongezeka pale walipoamua kuruhusu hitilafu na migawanyiko kuenea miongoni mwao.

Profesa Rabbani ameongeza kuwa tofauti za madhehebu katika Uislamu si jambo haramu bali jambo linalokemewa ni kuenea ugomvi, hitilafu na migawanyiko, mambo ambayo hayana msingi wowote wa kidini wala kiutu. Amesema kwa masikitiko kwamb, makundi hasimu ambayo hivi sasa yamedhihiri kwa wingi katika nchi za Kiislamu hatimaye yatasababisha umwagikaji bure damu ya Waislamu.

Profesa Rabbani ameongeza kwamba kuna mambo mengi yanayopelekea kudhihiri kwa mivutano na ghasia katika nchi za Kiislamu na kuwataka wanafikra, wanazuoni na wasomi wa Kiislamu katika nchi hizo kuyatafutia ufumbuzi mambo hayo. Amesema kuwa moja ya mambo hayo ni fikra finyu zinazoonekana kuenea miongoni mwa Waislamu na kutozingatiwa kwa kina maana ya aya za Qur'ani Tukufu pamoja na Sunna. Amesema, jambo hilo huwapelekea Waislamu kukabiliana kwa nguvu na makundi ya wenzao wasioafikiana nao kifikra na kiitikadi. Rabbani ameendelea kusema kuwa kwa bahati mbaya, fikra na mitazamo finyu haionekani tu miongoni mwa watu wa kawaida bali hata miongoni mwa baadhi ya wanazuoni.

Kwa kadiri kwamba baadhi yao huwakufurisha wenzao wanapoona kwamba wana fikra au mitazamo inayokinzana na yao. Ranbbani amesema kuwa jambo jingine linalosababisha ghasia na machafuko kati ya makundi mbalimbali katika nchi za Kiislamu ni hatua ya wanasiasa kutumia vibaya tofauti zilizopo kati ya Waislamu kwa manufaa yao wenyewe ya kisiasa. Amesema kuwa tatizo la hitilafu na mivutano kati ya Waislamu linaweza kutatuliwa kwa urahisi iwapo Waislamu wataamua kufuata njia zinazofaa. Amesema mfano mzuri wa jambo hilo ni pale Imam Ali (AS) alipooamua kuamiliana vizuri na kwa heshima na wanafiki katika vita vya Jamal ambapo alikuwa akiwaita kuwa ni ndugu zake katika Uislamu ili kuepuka uwezekano wa kutokea hitilafu na migawanyiko katika Uislamu.

Rais huyo wa zamani wa Afghanistan amesema kuwa kuna mifano mingi katika maisha ya maimamu watoharifu inayothibitsha jinsi walivyokuwa wakiishi na kuamiliana kwa wema na watu mbalimbali. Amesema jambo hilo linabainisha wazi kuwa maimamu maasumu walikuwa na kiwango kikubwa cha huruma na msamaha kwa watu na kamwe hawakuwa wakiwatwisha watu matakwa yao. Amesema mwishoni kwamba, sisi Waislamu tunapasa kutambua vyema kwamba mojawapo ya njama zinazotekelezwa na maadui wa Uislamu ni kutumia vibaya hitilafu zilizopo miongoni mwatu kwa ajili ya kutoa pigo dhidi yetu. Amesema kwa masikitiko kwamba, hitilafu za kifikra kwa bahati mbaya zimeruhusiwa kusababisha umwagikaji damu tukufu ya Waislamu katika ulimwengu wa Kiislamu. MWISHO