UMOJA WA KIISLAMU
  • Kichwa: UMOJA WA KIISLAMU
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA LIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 16:31:21 19-9-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

UMOJA WA KIISLAMU
Baada ya kutekwa ardhi za Palestina na Uingereza pamoja na Wazayuni katika miaka ya baada ya Vita vya Kwanza na Pili vya Dunia, na kufuatia kushindwa kijeshi nchi za Kiarabu na utawala ghasibu wa Israel, wasiwasi wa kutekwa na kudhibitiwa nchi hizo na utawala huo uliongezeka maradufu.

Kwa msingi huo suala la kuimarishwa umoja kati ya madhehebu ya Kiislamu liliwasilishwa na wanazuoni wa Kiislamu kuwa moja ya njia za kukabiliana na hatari hiyo ya Wazayuni. Kutokana na kuwa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar katika zama hizo ndicho kilichokuwa kituo mashuhuri cha elimu ya kidini na pia cha zamani zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu, kilikuwa cha kwanza kutoa wito wa kuwepo umoja miongoni mwa Waislamu ili kukabiliana na hatari ya Wazayuni dhidi ya uliwengu wa Kiislamu. Ukaribu wa kimazingira na kijografia wa chuo hicho na pia kuwepo kwa manazuoni mashuhuri wa Kiislamu kama vile Sayyid Jamal ad-Deen Asadabadi.

Sheikh Muhammad Abdou na wanafunzi wao ambao wote walikuwa walinganiaji wa umoja wa Kiislamu na vilevile kushiriki kwao katika vita dhidi ya Israel, ni jambo jingine lililoimarisha wito wa kuwepo umoja wa Kiislamu katika chuo hicho kuliko vituo vingine vyote vya Kiislamu. Wito huo ulipokelewa na kuungwa mkono mara moja na wanazuoni wengine wa Kiislamu katika pembe mbalimbali za ulimwengu wa Kiislamu. Ayatullah Burujerdi wa nchini Iran alikuwa miongoni mwa wanazuoni hao mashuhuri waliopokea kwa moyo mkunjufu wito huo wa kuimarishwa umoja miongoni mwa Waislamu na kuwataka wafanye hima ili kuhakikisha kwamba lengo hilo la umoja linafuatiliwa kwa karibu na Waislamu wote bila kujali madhehebu zao.

Akiwa mwanzoni mwa umar'ja wake, Ayatullah Burujerdi alilipa umuhimu mkubwa suala la umoja wa madhehebu ya Kiislamu na kuamini kwamba, suala hilo lilikuwa moja ya majukumu muhimu ya kila mwanazuoni wa Kishia. Akisema kuwa mjadala kuhusiana na suala la 'nani aliyepasa kuwa khalifa au ni jambo gani la haki na lipi la batili,' si mjadala unaofaa kujadiliwa katika jamii ya Kiislamu ya hivi sasa.

Alikuwa akiwaambia wanazuoni wa Kishia kwamba suala hilo si hitajio muhimu la jamii ya Kiislamu katika zama hizi kwa sababu husababisha ugomvi na mvutano kati ya ya Waislamu. Ayatullah Burujerdi alikuwa akisema kuwa jambo lenye umuhimu kwa Waislamu hivi sasa ni kwa wao kutambua vyema vyanzo vya sheria zao za kidini. Kuhusiana na hamu kubwa aliyokuwa nayo Ayatullah Burujerdi kuhusiana na suala la umoja baina ya Waislamu, Shahid Murtadha Muttahari, msomi na mwanafalsafa mashuhuri wa Kiislamu anasema:
"Moja ya sifa njema za Ayatullah Burujedi ni uzingatiaji wake mkubwa kuhusiana na suala la umoja wa Waislamu na maelewano pamoja na ukuruba baina ya madhehebu ya Kiislamu. Kutokana na kuwa mtu huyu alifahamu vyema historia ya Kiislamu na madhehebu ya Kiislamu, alitambua madhara makubwa yaliyosababishwa na watawala wa zamani dhidi ya Uislamu kwa kutumia vibaya hitilafu na tofauti za Waislamu. Alitambua vyema pia kwamba katika zama hizi ukoloni unatumia vibaya hitilafu na tofauti za Waislamu kwa ajili ya kutoa pigo dhidi ya ulimwengu wa Kiislamu. Alifahamu pia kwamba, kutokana na Mashia kuwa mbali na kutofahamika vyema na wafuasi wa madhehebu mengine ya Kiislamu, walikuwa wakidhaniwa vibaya na wafausi wa madhehebu hayo kinyume kabisa na ukweli wa mambo ulivyo.

Kwa msingi huo, alikuwa na hamu kubwa ya kuona kwamba umoja na mshikamano unaimarishwa miongoni mwa Mashia na Masuni kupitia umoja wa Kiislamu, ambalo ni lengo muhimu zaidi la dini hii tukufu. Alitaka Ushia na fik'hi ya Kishia kuarifishwa kama ilivyo kwa Masuni, ambao ndio wanaounda idadi kubwa zaidi ya wafuasi wa Uislamu, ili wapate kuujua vyema. Akiwa mjini Burujerd alianzisha Taasisi ya Kukurubisha pamoja Madhehebu ya Kiislamu kwa ushirikiano wa wanazuoni kadhaa wa Kishia na Kiislamu na kuimarisha, kadiri ya uwezo wake, fikra ya umoja wa Kiislamu kupitia taasisi hiyo. Kwa mara ya kwanza na baada ya kupita mamia ya miaka, mwanazuoni huyo wa Kishia alianzisha uhusiano wa kidugu na kirafiki na kuandikiana barua na mwanazuoni wa Kisuni Sheikh Abdul Majid Salim na baada ya kuaga kwake dunia akawa na uhusiano kama huo na Sheikh Mahmoud Shaltut, Mufti na Mkuu wa hivi sasa wa Chuo Kikuu cha al-Azhar….. Muadhamu alikuwa na hamu kubwa kuhusiana na maudhui hii na moyo wake ukidunda kwa ajili ya kufikia lengo hilo. Jambo la kushangaza ni kuwa, tumesikia kutoka kwa vyanzo viwili vya kuaminika kwamba, katika tukio la hivi karibuni la mushtuka wa moyo lililompelekea kuaga dunia, alipata mshutuko wa kwanza uliompelekea kupoteza fahamu kwa muda. Kisha baadaye alipata fahamu na hata kabla ya kuzungumzia mkasa uliompata, alianza kuzungumzia suala la kukurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu na umoja baina ya Waislamu na kusema kuwa ana matumaini makubwa katika uwanja huo."

Ayatullah Burujerdi tokea mwanzoni aliunga mkono kuasisiwa kwa Daru at-Taqrib na kuendelea kuwa na msimamo huo katika kipindi chote cha shughuli za taasisi hiyo. Katika darasa zake za Fik'hi, Ayatullah Burjerdi mara nyingine alikuwa akibainisha fatuwa za wanazuoni wa Kisuni na kusema kuwa mwenendo wa historia ya fik'hi ya Kiislamu hubainika zaidi kwa kusoma na kutalii fatuwa za wanazuoni wa Kisuni. Kwa msingi huo, alimtuma Sheikh Muhammad Taqi Qumi nchini Misri kama mwanazuoni wa Kishia na mjumbe wake katika kituo hicho muhimu cha kielimu cha Masuni. Kwa njia hiyo, aliweza kudumisha mawasiliano na kuandikiana barua na wanazuoni pamoja na wasimamizi wa Chuo cha al-Azhar kupitia mjumbe huyo. Kupitia mjumbe wake huyo, Ayatullah Burujerdi alimwandikia barua Haj Sheikh Abdul Majid Salim, naye kwa upande wake akashukuru na kujibu kwa heshima barua hiyo kwa kuandika:
"Nauchukulia ushirikiano wako kwenye jihadi hii kubwa ya Mwenyezi Mungu kuwa muhimu mno. Hii ni kwa sababu kutokana na elimu, nafasi na ushawishi mkubwa ulionao nchini Iran na sehemu nyinginezo, daima umekuwa ukifanya juhudi za kurekebisha mambo katika umma wa Kiislamu. Fikra ya kukurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu imeimarika mno kutokana na uzingatiaji wako kwa suala hili. Fikra hiyo imekuwa ikiimarika kutokana pia na misaada na miongozo yako yenye thamani kubwa katika vipindi tofauti."

Kwa kutambua vyema hali ya ulimwengu wa Kiislamu, Ayatullah Burujerdi alifanya juhudi kubwa za kuzuia jambo lolote ambalo alihisi kwamba lingehatarisha umoja wa Kiislamu katika jamii. Kwa mfano wakati mmoja licha ya kuwa alikuwa mgonjwa mahututi, lakini alitumia uwezo wake wote kujaribu kurudisha katika hali ya kawaida uhusiano wa Iran na Misri ambao katika kipindi hicho cha utawala wa Shah nchini Iran na Jamal Abdu an-Nasir wa Misri ulikuwa umekatwa kutokana na tofauti za pande mbili. Alifanya juhudi kubwa kujiepusha kutumia vibaya nafasi yake ya uongozi na ushawishi kwenye dini kuleta hitilafu na migawanyiko miongoni mwa Waislamu. Wakati mmoja mwanazuoni mmoja wa mjini Qum aliandika kitabu kimoja cha fik'hi kilichokuwa cha juu mbili. Mwandihi wa kitabu hicho alimtumia nuskha moja Ayatullah Burujerdi ambapo katika kitabu hicho mlikuwa mmeandikwa beti moja ya shairi ambayo ilikuwa ikiwadharau makhalifa. Baada ya kusoma beti hiyo kwa makini, Ayatullah Burujerdi alikasirishwa nayo na kusema kuwa huo haukuwa wakati wa kuandikwa beti kama hizo, tena kwenye kitabu cha Kishia. Aliamuru beti hiyo irekebishwe mara moja kwa gharama yake mwenyewe.

Hatimaye juhudi za siku nyingi za Ayatullah Burujerdi za kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu zilizaa matunda, ambapo Sheikh Shaltut Mufti Mkuu na Mkuu wa Chuo Kikuu cha al-Azhar alitoa fatuwa tarehe 9/10/1958 akiutambua rasmi Ushia kuwa mojawapo ya madhehebu muhimu ya Kiislamu. Alisema kwenye fatuwa hiyo kama ifuatavyo: "Uislamu haumlazimishi mfuasi wake yoyote kuafuata madhehebu maalumu, bali kila Muislamu anaweza kufuata madhehebu yoyote ambayo imepokelewa kwa njia sahihi na sheria zake kuandikwa katika vitabu maalumu vya madhehebu hiyo. Kila mtu anayefuata madhehebu nne za Kisuni anaweza kufuata madhehebu nyingine yoyote ile.

Madhehebu ya Jaafari, mashuhuri kwa jina la madhehebu ya Maimamu Kumi na Wawili, ni madhehebu ambayo inasihi kufuatwa kisheria kama ambavyo inasihi kufuatwa madhebeu nne za Ahlu Sunna. Kwa msingi huo inafaa Waislamu kutambua hakika hiyo na kuachana na vilevile kujiweka mbali na taasubi zisizofaa kuhusiana na madhehebu fulani. Hii ni kwa sababu dini ya Mwenyezi Mungu na sheria zake hazifuati madhehebu fulani na wala hazitahodhiwa na madhehebu maalumu. Waanzilishi wa madhehebu, wote walikuwa ni mujtahid na ijtihadi yao inakubaliwa na Mwenyezi Mungu. Watu wasiofikia daraja ya ijtihadi, wanaweza kufuata madhehebu yoyote wanayoipenda na kutekeleza sheria zake, na wala hakuna tofauti yoyote katika hili kuhusiana na masuala ya ibada na miamala."

Fatuwa hiyo ilitolewa katika kipindi ambacho Mawahabi na Masalafi wenye taasubi ya kupindukia wa Saudi Arabia walikuwa wakiwakufurisha wazi Mashia. Kwa msingi huo, fatuwa hiyo ya Mahmoud Shaltut iliacha athari kubwa katika kukubalika rasmi Ushia katika ulimwengu wa Kiislamu.