KULINDA UMOJA
  • Kichwa: KULINDA UMOJA
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 14:29:59 3-9-1403


BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

KULINDA UMOJA

Mbinu na mikakati ya Uislamu ya kulinda umoja wa Umma Umoja wa Umma wa Kiislamu si maudhui ambayo imeanza kujadiliwa katika milenia hii ya 21, bali ni jambo la msingi ambalo siku zote limekuwa likisisitizwa na kufuatilia kwa karibu na Uislamu. Huku ikisisitiza umuhimu wa kubainishwa na kuwekwa mipaka kati ya makafiri na maadui wa Uislamu na wafuasi wa dini hii tukufu, Qur'ani Tukufu inatilia mkazo suala la kuwepo mapenzi, usamehevu, umoja na mahaba kati ya Waislamu. Inawasihi Waislamu kushikamana na kuwa na umoja katika msingi wa kamba ya Mwenyezi Mungu na kuutaja udugu na umoja huo kuwa neema Yake kubwa kwa wanadamu. Sira na maisha ya Mtume Mtukufu (SAW) pia yanasisitiza juu ya jambo hilo. Kwa ibara nyingine, tunaweza kusema kuwa tabia na maisha yote ya Mtume Mtukufu yanaakisi moja kwa moja mafundisho hayo muhimu ya Qur'ani Tukufu.
Kuna aya nyingi mno za Qur'ani ambazo zinasisitiza juu ya kuwepo umoja na udugu kati ya Waislamu. Tunaashiria hapa baadhi ya aya hizo: Mwenyezi Mungu anasema hivi katika aya ya 31 ya Surat Aal Imran: "Na shikamaneni kwa kamba (dini) ya Mwenyezi Mungu nyote, wala msiachane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu. (Zamani) mlikuwa maadui; Naye akaziunganisha nyoyo zenu hivyo, kwa neema Yake; mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto (wa Jahannam), naye akakuokoeni nalo. Namna hii Mwenyezi Mungu anakubainishieni aya Zake ili mpate kuongoka." Udugu unaokusudiwa hapa ni udugu wa kidini na imani. Waislamu ni ndugu kwa sababu kila mmoja wao hutafuta na kufuata kile kinachofuatwa na kutafutwa na Muislamu mwenzake. Kushikamana kwa kamba ya Mwenyezi Mungu huandaa njia na uwanja wa waja wa Mwenyezi Mungu kupaa mbinguni pamoja wakiwa kundi moja. Hi ni kwa sababu Mwenyezi Mungu anamuamuru Mtume ambaye anaweza kupaa peke yake, apae na umma wake mzima, ili kwa njia hiyo kuwepo na ushirikiano, udugu, umoja na mfungamano kati ya imam na umma mzima wa Kiislamu. Jambo hilo linawawezesha Waislamu wote kutembea kwenye njia nyoofu, ya haki na saada kuelekea kwa Muumba wao: Na uinamishe bawa lako kwa wale wanaokufuata katika wale walioamini (26-215)."
Kushikamana pamoja, umoja, uratibu na mfungamano kwa msingi wa kamba ya Mwenyezi Mungu huwapelekea Waislamu kuwa na uchangamfu na bidii kubwa katika utekelezaji wa majukumu yao waliyopewa na Mwenyezi Mungu. Aya ya pili inayowahimiza Waislamu kuwa na umoja na mshikamano miongoni mwao ni ile inayosema: "Enyi mlioamini! Ingieni katika hukumu za Uislamu zote, wala msifuate nyayo za Shetani; yeye kwenu ni adui dhahiri (2-208)."
Ibn Abbas ananukuliwa akisema kuwa aya hii iliteremka kuhusiana na Abdallah bin Salam Yahudi na wafuasi wake. Hii ni kwa sababu waliposilimu walihitilafiana na Waislamu wengine kuhusiana na baadhi ya masuala kama vile kuadhimishwa siku ya Jumamosi na kuchukia nyama na maziwa ya ngamia. Kisha wakamtaka Mtume Mtukufu (SAW) kuleta Torati na kutekeleza mafundisho yake. Kisha Mwenyezi Mungu akataremsha aya hiyo akiwataka wote waishi kwa suluhu na amani. Baadhi ya tafsiri za Qur'ani zinasema kuwa Mayahudi hao walimtaka Mtume (SAW) awaruhusu wasome Torati kwenye swala zao, lakini Mwenyezi Mungu akateremsha aya hiyo akiwakataza kumfuata shetani.
Kwa vyovyote vile, kwenye aya hii Mwenyezi Mungu anawasihi waumini kuishi pamoja kwa amani na umoja kwa sababu vitu viwili hivyo ni mfano wa ngome iliyo imara na madhubuti inayolinda na kumkinga mwanadamu kutokana na mabalaa yote maishani. Kwa msingi huo neno la Kiarabu la 'silm' lililotumika kwenye aya hii lina maana ya kuishi kwa umoja, udugu na amani kati ya Waislamu na waumini na sio wito wa kuingia kwenye Uislamu. Kwa msingi huo aya hii inawasihi Waislamu na waumini ambao tayari wamesilimu na kukubali imani ya Uislamu kuishi pamoja kwa amani na udugu bila kuvutana na kuhasimiana miongoni mwao. Nam, kama wito ungekuwa ni kwa watu wote na neno 'nas' lililo na maana ya 'watu' kutumika hapa, ni wazi kuwa maana ingekuwa ni wito wa kuingia kwenye Uislamu kama ambavyo baadhi ya tafsiri za Ahlu Sunna zimejaribu kubainisha.
Aya ya tatu ni aya ya udugu wa imani. Aya inayozungumzia suala hilo ni aya ya 10 ya Surat al-Hujurat inayosema: "Kwa hakika Waislamu wote ni ndugu; basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu, (msipuuze jambo la kupatanisha) ili mrehemiwe."
Aya hii inawasihi Waislamu kuimarisha udugu wa Kiislamu baina yao na kuwataka wajiepushe kabisa na mifarakano ili kwa njia hiyo waweze kuishi pamoja kwa mapenzi, amani, ushirikiano na upendo chini ya mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu na kwa msingi wa aya isemayo: "Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja naye ni wenye nyoyo thabiti mbele ya makafiri na wenye kuhurumiana wao kwa wao (48-9)."
Kwa maelezo hayo, watu wanaodai kuwa ni Waislamu na waumini na kisha kuwaua ovyo Waislamu wenzao na kuzusha fitina na hitilafu miongoni mwao wanapasa kuzuiwa kufanya uovu huo. Kama inavyosema Qur'ani Tukufu, iwapoa waumini wawili watahitilafiana kutokana na mitazamo tofauti, kwanza wanapasa kupatanishwa kupitia mawaidha na nasaha za waumini wenzao. Lakini iwapo wataendelea na ugomvi wao na upande mmoja kutaka kuudhulumu wa pili bila kuzingatia nasaha na upatanishi huo wa Waislamu, kundi au upande unaodhulumu unapasa kudhibitiwa na kulazimishwa kuacha dhulma hiyo dhidi ya upande unaodhulumiwa na kuheshimu sheria za Mwenyezi Mungu. Iwapo makundi mawili hayo yatakubali kusuluhishwa kwa msingi wa sheria hizo, basi upatanishi unapaswa kufanyika baina yao kwa msingi wa uadilifu na sio kwa msingi wa kupatikana suluhu tu.
Hii ni kwa sababu suluhu na amani inayopatikana katika hali hii si jambo zuri wala la kuridhisha. Kwa ibara nyingine ni kuwa, kwa namna yoyote ile haki ya mdhulumiwa inapasa kuchukuliwa kutoka kwa dhalimu na kurejeshewa mdhulumiwa na sio kumlazimisha mdhulumiwa akubali suluhu na hivyo kukanyaga haki yake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba hata kama suluhu na mapatano yatafanyika katika mazingira kama hayo, lakini ni wazi kuwa uadilifu utakuwa haujafanyika: "Na ikiwa makundi mawili katika Waislamu yanapigana, basi fanyeni suluhu baina yao; na likiwa moja kati ya hayo linamdhulumu mwenziwe, basi lipigeni lile linaloonea mpaka lirudi kwenye amri ya Mwenyezi Mungu. Na kama likirudi, basi yapatanisheni baina yao kwa uadilifu. Na hukumuni kwa haki. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaohukumu kwa haki (49-9)."
Umoja wa Kiislamu katika sira ya Mtume (SAW) Uchunguzi wa maisha na sira ya Mtume Mtukufu (SAW) unathibitisha wazi kwamba, sambamba na juhudi zake za kueneza mafundisho ya tauhidi na upwekeshaji wa Mwenyezi Mungu katika jamii, Mtume alikuwa akilipa umuhimu mkubwa suala la kuleta umoja na mshikamano baina ya Waislamu na kuamini kwamba, hakukuwepo na jambo jingine lililokuwa na madhara makubwa kwa umma wa Kiislamu kama mitengano na mifarakano kwenye jamii.
Udugu, nara ya kwanza ya Mtume (SAW) Kwa msingi huo, nara ya kwanza ya Mtume Mtukufu (SAW) alipowasili mjini Madina, hata kabla ya kuanza kufikiria juu ya ujenzi wa msikiti na kutekeleza miradi ya maendeleo, alizungumza na kusisitiza juu ya udharura wa kuimarishwa udugu wa Kiislamu kati ya Waislamu wote. Aliweka mkataba wa udugu kati ya kila Waislamu wawili wawili, wakiwemo Ansar na Muhajirin na pia kati ya makabila mawili ya Aus na Khazraj. Mtume alitangaza udugu huo kati yake na Imam Ali (AS). Nara ya kuimarishwa umoja wa Kiislamu ilitolewa mwanzoni mwa kuasisiwa serikali ya Kiislamu na pia katika kipindi cha kuimarika serikali hiyo mjini Madina. Nara hii ilisikika wakati wa kukombolewa mji mtakatifu wa Makka na Waislamu, kutoka mikononi mwa makafiri na washirikina na vilevile wakati wa hija ya mwisho ya Mtume ambapo alisikika akiwasihi na kuwausia Waislamu walinde umoja na mshikamano miongoni mwao. Alisema: "Waislamu ni ndugu na damu yao ni sawa. Hakuna miongoni mwao aliye na damu yenye thamani kubwa kuliko ya wenzake. Wao ni kitu kimoja dhidi ya adui wao." Kama ambavyo ndugu wa damu wana baba yao wa damu, ndugu katika imani pia wana baba yao wa imani naye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Ali Amirul Mu'mineen (AS).
Kwa msingi huo, Mtume alijiarifisha yeye na Imam Ali (AS) kuwa baba wa imani wa umma wa Kiislamu kwa kusema: "Mimi na Ali ni baba (wawili) wa umma huu (Bihar 95/16)." Licha ya nara ya umoja maisha na sira ya Mtume pia inabainisha wazi umuhimu uliokuwa ukitolewa na mtukufu huyo kuhusu suala la umoja. Masuala yafuatayo yanabainisha wazi jambo hilo:
1- Katika vita na kabila la Bani al-Mustalaq, na kufuatia ushindi wa Waislamu dhidi ya washirikina, kulitokea ugomvi wa maneno kati ya Waislamu wawili mmoja kutoka kundi la Muhajirin na mwingine kutoka Ansar. Wawili hao waligombana na kuomba msaada kutoka kwa makabila yao kama walivyokuwa wakifanya wakati wa ujahili. Sauti ya wito wao wa mfarakano na fitina, tena katika ardhi ya adui aliyeshindwa, ilimfikia Mtume ambapo alikasirishwa mno na jambo hilo.
Mtume aliwataka Waslamu wasiyazingatia matamshi na wito huo mbovu na kusisitiza kuwa hizo zilikuwa ni nara za kijahili tu. Hatimaye, ili kuzima fikra hizo mbovu za kimakundi na kikabila, Mtume aliamuru mara moja jeshi lake lianze mwendo mara moja tena katika joto kali la adhuhuri. Baada ya kukata masafa marefu kuliko kawaida, Mtume alitoa amri msafara huo usimame na wote wakalala usingizi mzito kutokana na machovu walioyokuwa nayo. Kwa kadiri kwamba baada ya kuamka walikuwa wamesahau kabisa tukio hilo chungu. Kwa hatua yake hiyo ya hekima, Mtume (SAW) alifanikiwa kurejesha tena umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu hao (Sirat Ibn Hisham j 3 uk 303).
2- Vijana wa makabila ya Aus na Khazraj ambao kabla ya kuingia Uislamu mjini Madina walikuwa daima wakipigana na kugombana, walikuwa na umoja na mshikamano pamoja na kushirikiana kidugu baada ya kuingia Uislamu katika mji huo. Siku moja vijana hao walikuwa wamekusanyika pembeni ya Msikiti wa Mtume (SAW) mjini Madina huku wakizungumza kwa furaha.
Mmoja wa wakuu wa Kiyahudi kwa jina la Shas alipita mahala hapo na kukasirishwa mno na hali hiyo. Alimtuma kijana mmoja wa Kiyahudi ili aende kwenye kundi la vijana hao na kuvuruga mazungumzo yao. Aliwachochea wahasimiane kwa kuamsha hisia za unafiki na vita vyao vya kale vya kijahili. Kijana huyo alitekeleza vyema jukumu alilopewa na mkuu huyo wa Kiyahudi kwa kadiri kadiri kwamba alifanikiwa kuwagonganisha vichwa vijana hao na kuwapelekea wagombane na karibu wapigane. Wote walishika mapanga na kuwa tayari kupigana.
Ghafla habari hizo zilimfikia Mtume (SAW) ambaye alifanya hima kufika mahala hapo na kupaza sauti kwa kusema: "Mwogopeni Mwenyezi Mungu! Mwogopeni Mwenyezi Mungu! Je, mnahuisha madai ya kijahili, hali ya kuwa mimi niko miongoni mwenu na hali ya kuwa Mwenyezi Mungu amekuongozeni, kukutukuzeni, kukata uhusiano wenu wa zama za ujahili, kukunusuruni kutoka kwenye ukafiri na kufungamanisha nyoyo zenu kwa njia ya Uislamu? Maneno hayo ya Mtume (SAW) yalikuwa mfano wa maji baridi yaliyomwagwa kwenye ndimi za moto. Vijana waliokuwa wakigombana walifahamu mara moja kwamba walikuwa wamehadaika na maneneo ya kijana yule mfitini wa Kiyahudi aliyewapelekea kubadilisha umoja wao kuwa ugomvi. Bila kusita, waliamka na kupeana mikono kama ishara ya udugu baina yao na hivyo kurejea tena kwenye kivuli cha umoja na mshikamano. (Sirat Ibn Hisham j. 2 uk. 250).

MWISHO