LENGO LA SHARAFU DIIN
  • Kichwa: LENGO LA SHARAFU DIIN
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 14:7:10 3-9-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

LENGO LA SHARAFU DIIN

Umoja wa Umma wa Kiislamu, lengo kuu la uandishi wa Sharafu Deen.

Hata kama, kama walivyokuwa wanazuoni wengine muhimu katika historia ya Kiislamu, Sayyid Sharafu Deen alipambana na ukoloni, lakini alikuwa akiamini kwamba changamoto na matatizo muhimu zaidi ya Ulimwengu wa Kiislamu, ni ya ndani na wala hayatokani na madui wa nje, na wakati huohuo kusisitiza kwamba utatuzi wa matatizo hayo unahitajia mbinu za kielimu na kimantiki.

Kwa kawaida fikra, umashuhuri, kiwango cha elimu, ubunifu na kina cha fikra cha kila mwandishi hujulikana kupitia maandishi yake. Ni maandishi hayo ndiyo huwafanya wasomaji kutambua elimu kubwa na maarifa aliyonayo msomi fulani katika uwanja unaomuhusu wa kielimu na hivyo kumpa majina na lakabu kama vile 'ensaiklopidia', 'allama' au majina mengine yanayoonyesha mtu aliye na kipaji kikubwa cha elimu.

Amma, kuna waandishi wachache mno ambao katika vitabu vyao hujishughulisha na masuala maalumu na kuchukua misimamo mahususi kuhusiana na utatuzi wa matatizo yanayoikabili jamii. Ni wazi kuwa waaandishi kama hao wana thamani na umuhimu mkubwa zaidi katika jamii kwa sababu huongoza na kuielekeza katika upande maalumu, ikiwa inafuatilia maalengo maalumu pia.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa, waandishi kama hao huyachukulia maisha humu duniani kuwa na malengo maalumu. Huyatazama maisha ya kijamii ya Waislamu pia katika mtazamo huohuo. Suala hilo bila shaka hufungamana na jambo linalochukuliwa na waandishi hao kuwa muhimu na nyeti katika zama zao na kwamba jamii inahitajia swali, jibu na utatuzi wake wa haraka. Huenda likawa ni jambo la busara kuwaita waandishi kama hao kuwa ni wasomi warekebishaji wa jamii. Marekebisho bila shaka hufanyika katika masuala ya kijamii au mara nyingine ya kisiasa, ambayo huishughulisha jamii kifikra. Ni kutokana na hali kama hiyo ndipo wasomi kama hao wa Kiislamu huamua huchukua misimamo na kufuata njia maalumu katika kuwaongoza wafuasi wao kwenye njia nyoofu.

Allama Tabatabai na Shahid Murtadha Mutahhari, Mwenyezi Mungu awareemu, waandishi na wanafikra wawili muhimu wa Kiislamu waliokuwa na vipaji vikubwa vya kielimu katika karne ya hivi karibuni, ni miongoni mwa wasomi, waandishi na wanafikra wa aina hiyo. Kama watu wote wanavyojua, katika uandishi wake na hasa katika tafsiri yake muhimu ya Qur'ani ya al-Mizaan, ambapo kwa uvumbuzi wake mwenyewe, alitumia mbinu ya kutarjumu na kufasiri Qur'ani kwa Qur'ani, Allama Tabatabai alijaribu kadiri ya uwezo wake, kuanzisha na kuimarisha mbinu hiyo ya tafsiri ya Qur'ani katika vituo muhimu vya kidini nchini.

Aliwataka wakufunzi na wanafunzi wa vyuo vya kidini kuzingatia kwa kina maana na mafundisho ya Qur'ani Tukufu pamoja na kuelewa na kisha kufundisha vyema maana halisi ya aya za kitabu hicho kitakatifu. Pia aliwataka wachambue kielimu na kuwasilisha fikra sahihi ya kimantiki kuhusiana na falsafa ya umaada wa Magharibi.

Amma kuhusiana na Ustadh Shahid Mutahhari, masuala ya kielimu na kiakili ya jamii ya Kiislamu yalikuwa tofauti kabisa. Licha ya kuwa aliwasilisha na kukamilisha mambo mengi katika uwanja wa falsafa ikiwa ni katika kukamilisha fikra za mwalimu wake kuhusiana na masuala ya kiakili kwenye Uislamu, lakini vitabu vyake vingi muhimu vinachambua masuala yanayowasilisha dini tukufu ya Kiislamu kama mfumo kamili wa kielimu na wa maisha ya mwanadamu kwenye jamii. Vitabu vyake vingi vikiwemo vile vinavyohusiana na masuala ya hijabu, haki za mwanamke katika Uislamu, hatima ya wanadamu, sababu za kuimarika mielekeo ya umaada, vyote hivyo vinathibitisha kwamba lengo kuu la Shahid Mutahhari lilikuwa ni kujibu matatizo na changamoto za kijamii zilizoibuka katika zama zake. Alitekeleza jukumu lake kwa kutetea kielimu na kimantiki dini tukufu ya Kiislamu.

Wanazuoni wa Lebanon Wanazuoni wa Kiislamu na hasa wa Kishia wa nchini Lebanon wametoa chango mkubwa katika kuimarisha, kutetea na kueneza dini tukufu ya Kiislamu duniani. Mmoja wa wanazuoni mashuhuri na muhimu katika uwanja huo ni Allama Ayatullah Sayyid Abdul Hussein Sharafu Deen. Aliandika vitabu vingi akijadili matatizo makuu yanayoukabili ulimwengu wa Kiislamu. Alizingatia na kulipa umuhimu mkubwa suala la kuondoa tofauti na kuyakurubisha pamoja madhebu mawili makuu ya Kiislamu yaani, Ushia na Usuni.

Vitabu vingi vya Ayatullah Sharafu Deen vinazingatia suala la kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu na vinajaribu kukurubisha pamoja nyoyo na fikra za Waislamu katika ulimwengu wa Kiislamu. Uzingatia wa Sharafu Deen juu ya suala hili si jambo dogo. Alitilia mkazo umuhimu wa kuwepo ushirikiano na umoja wa kisiasa kati ya serikali za Kiislamu kwa madhumuni ya kupambana na njama za maadui wa kikoloni dhidi ya ulimwengu wa Kiislamu. Alisema kuwa jambo muhimu linaloharibu nguvu ya Waislamu na vipaji vyao ni kuwepo chuki na mivutano ya kimadhehebu katika ulimwengu wa Kiislamu, suala linaloharibu na kuvuruga kabisa malengo yao matukufu.

Hata kama Sayyid Sharafu Deen alipigana na ukoloni kama walivyofanya wanazuoni wengine wengi wa Kiislamu, lakini alichukulia tatizo kuu la ulimwengu wa Kiislamu kuwa ni matatizo na tofauti za ndani na kuhimiza kutatuliwa kwa matatizo hayo kwa njia za kielimu na kimantiki. Aliamini kwamba, sehemu kubwa ya matatizo hayo ni taasubi isiyo na msingi kuhusiana na masuala ya kidini. Anasema iwapo fikra na taasubi hiyo kavu na potofu itaruhusiwa kuenea kwenye jamii ya Kiislamu, jamii hiyo itapata madhara makubwa kutokana na taasubi hiyo.

Sayyid Sharafu Deen alikuwa akiamini kwamba kutokuwepo kwa mazingira ya maelewano ya kidini na kutawala taasubi katika jamii na wakati huohuo kutokuwepo uamuzi sahihi unaotegemea misingi iliyo wazi ya akili na mantiki, ni tatizo muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu. Aliwataka Waislamu kufanya juhudi kubwa za kielimu kutatua tatizo hilo ambalo linaoonekana kati ya wafuasi wa madhehebu yote mawili muhimu ya Kiislamu ya Shia na Suni. Kwanza alipendekeza kutumiwa njia ya mijadala bora na kufahamishwa wafuasi wa pande mbili misingi ya fikra, hoja, mantiki na imani ya upande wa pili. Kisha baada ya hapo alipendekeza kuwepo na umoja wa kisiasa wa nchi zote za Kiislamu.

Juhudi zisizo na kikomo Sayyid Sharafu Deen tokea utotoni aliishi na kukulia katika jamii iliyokuwa na madhehebu mengi ya Kiislamu. Kutokana na mazingira yaliyomzunguka, mwanazuoni huyo muhimu wa Kiislamu alihisi kuwepo na udharura wa Waislamu kuwa na umoja na mshikamano wa kijamii miongoni mwao. Alitaka hatua za dharura zichukuliwe kwa ajili ya kuondoa kila aina ya mifarakano na kuimarishwa umoja na mshikamano miongoni mwao.

Alisema ufunguo wa kufikiwa lengo hilo ulipaswa kutafutwa kwenye masuala na utambulisho wa pamoja wa madhehebu zote mbili muhimu za Kiislamu. Kwa msingi huo, katika siku ya kuzaliwa Mtume Mtukufu (SAW) katika mwezi Mtukufu wa Rabiul Awwal, Sayyid Sharafu Deen alikuwa akiandaa sherehe kubwa ya maulidi huko katika mji wa Sur, kusini mwa Lebanon Kusini, ambapo alikuwa akiwaalika wanazuoni na wafuasi wengi wa madhehebu ya Kisuni ili washerehekee pamoja siku hiyo adhimu. Baada ya kumalizika sherehe hizo, alikuwa akienda katika misikiti ya Masuni na kuwapa mkono wa pongezi na fanaka ndugu zake hao wa kidini kwa mnasaba wa kuadhimishwa siku tukufu ya kuzaliwa Mtume (SAW), ambapo alipokelewa kwa moyo mkunjufu na wenyeji pamoja na wasimamizi wa misikiti hiyo.

Sayyid Sharafu Deen alilipa umuhimu mkubwa suala hilo kwa kutilia maanani kwamba, aliamini kuwa kutokuwepo maelewano kati ya Waislamu kungesababisha tofauti kubwa za kifikra na kimadhehebu kati yao na hivyo kuwaangamiza. Aliamini kwamba jambo hilo pekee lilitosha kuhatarisha usalama wao na hivyo kuwaaangamiza kabisa. Bila shaka suala hilo lina umuhimu mkubwa kuliko umoja na muungano wa kisiasa ambao hutimia kupitia mapatano na mikataba inayoandikwa kwenye makaratasi kwa ajili ya kuleta ushirikiano na mshikamano wa kidhahiri tu katika kupambana na adui wa pamoja.

Ni wazi kuwa njia bora zaidi ya kuleta umoja na mshikamano kati ya makundi mawili muhimu ya Kiislamu ni kuimarisha mwenendo wa mazungumzo kati yao ambapo kila moja ya makundi hayo hupata fursa ya kutoa madukuduku na mitazamo yake kuhusiana na masuala tofauti yanayouhusu ulimwengu wa Kiislamu pamoja na itikadi zake. Katika mazingira kama hayo, kila upande hupata nafasi ya kujieleza na kutoa hoja zake na wakati huohuo kusikiliza na kufahamu hoja za upande wa pili kwa msingi wa mantiki na akili.

Ni wazi kuwa iwapo mazingira kama hayo yatampelekea mtu mwenye taasubi kubadili mwenendo wake na kukubali hoja za mantiki pamoja na kuustahamili upande wa pili, hayo yatakuwa ni mafanikio makubwa katika juhudi za kuleta umoja na mshikamano kati ya Waislamu. Si jambo dogo kuweza kuandaa mazingira mazuri ambapo kila Muislamu anaweza kuachana na mienendo yake ya kitaasubi na kuweza kuzungumza kwa uhuru kamili na wenzake ambao amekuwa akiwaachukulia kuwa maadui kutokana na misingi potovu ya imani na itikadi yake.

Dalili za Sharafu Deen kuchagua njia hiyo Marehemu Sharafu Deen amebainisha dalili zilizompekekea kusisitiza na kuchagua njia hiyo ya kuimarisha mazungumzo, maelewano na mshikamano miongoni mwa Waislamu, katika utangulizi wa kitabu chake 'al-Fusul al-Muhimma', ambacho ni kitabu chake cha kwanza katika uwanja huo. Anasema:
1- Sharti la kupatikana uhuru ni kufikiwa mshikamano wa kitaifa
Sayyid Sharafu Deen alikuwa akiamini kwamba, sharti la kwanza la kujiondoa jamii ya Kiislamu katika minyororo ya ukoloni na utumwa, ni kufanyika juhudi kubwa kwa shabaha ya kuleta umoja na mshikamano wa kitaifa katika jamii. Alisema, jamii mwanzo inatakiwa kuboresha miundombinu yake na kisha baadaye kushughulikia haki ya uhuru wake.
2- Athari mbaya na hatari za mgawanyiko
Ayatullah Sharafu Deen alikuwa akiutahadharisha sana umma wa Kiislamu dhidi ya athari pamoja na madhara makubwa ya kuwepo migawanyiko na mifarakano miongoni mwao. Aliwataka wanazuoni na viongozi wa kidini kufanya juhudi zisizo na kikomo katika kutafutia ufumbuzi tatizo hilo hatari kwa mshikamano wa Waislamu.

3- Sababu ya tatu aliyotoa Sharafu Deen katika kutetea na kuchagua njia hiyo ni kuandaa mazingira ya kuwepo uhuru wa kifikra na kuepuka mnyororo wa taasubi pofu ambayo hukandamiza fikra za mwanadamu na kumuweka mbali na utukufu wake wa dhati. Taasubi ya aina hiyo humuletea mwanadamu matatizo na kumzushia mabalaa mengi maishani. Sayyid Sharafu Deen alifanya juhudi kubwa ya kuondoa taasubi hiyo pouf katika ulimwengu wa Kiislamu, taasubi ambayo ilikuwa imejenga uadui mkubwa kati ya madhehebu mbili muhimu ya Shia na Sunni. Taasubi hiyo hata imewafanya baadhi ya Waislamu kuchoma misikiti ya wenzao wanaowachukulia kuwa maadui na kuzifanyia maskhra itikadi zao.

Ufumbuzi Kuna udharura wa kutafutwa njia za kimantiki za kufumbua na kutatua matatizo yaliyojitokeza kati ya wafuasi wa dini tukufu ya Kiislamu katika kipindi chote cha historia, matatizo na hitilafu ambazo zimepelekea kuzuka maelfu ya vita, ugomvi na mivutano kati yao. Utatuzi huo unapasa kutatua taratibu hitilafu kongwe zilizopo kati ya Waislamu na hivyo kurejesha tena utulivu na amani katika jamii ya Kiislamu. Jambo hilo linapasa kuwasaidia Waislamu kusahau hitilafu na chuki zao na kuzingatia fahari na utukufu wao wa kiutamaduni na kielimu katika historia. Ni wazi kuwa hatua ya kwanza inayopasa kuchukuliwa katika kutatua hitilafu hizo ni kuimarisha kuaminiana kati ya pande hasimu ili kuandaa mazingira mazuri ya wanazuoni kuzungumza na kujadiliana na wenzao wa upande wa pili bila kuwa na woga wala chuki mioyoni mwao. Sayyid Sharafu Deen alichukua hatua kama hiyo katika juhudi zake za kuleta mageuzi na mabadiliko katika jamii ya Kiislamu. Alifanya juhudi hizo zote kwa lengo la kuunganisha ulimwengu wa Kiislamu katika masuala ya pamoja na kuandaa mazingira bora ya Waislamu kukaa pamoja na kujadiliana masuala yanayowahusu.

Kuaminiana Kama tulivyosema hapo juu, hatua ya kwanza inayopasa kuchukuliwa kwa ajili ya kuondoa hitilafu na tofauti kati ya Waislamu ni kujenga mazingira ya kuaminiana na kuondoa kila aina ya jambo linaloweza kuzusha fitina kati ya wafuasi wa madhehebu mbalimbali ya Kiislamu. Ni wazi kuwa alama na dalili za kuaminiana ni kuheshimiana na kuepuka mambo yanayozusha chuki na ugomvi miongoni mwa Waislamu. Hiyo ndiyo hatua ya kwanza ya kuandaa mazingira ya kufanyika mazungumzo ya kielimu na kisiasa kati ya pande mbili zinazohasimiana. Tunapochunguza barua alizowatumia wafalme na watawala wa nchi mbalimbali, tunaona kwamba Mtume Mtukufu (SAW) pia alitumia mbinu hiyo katika kuwaita na kuwaalika watawala hao katika Uislamu. Kwa ibara nyingine ni kwamba, Mtume alikuwa akiandaa mazingira ya kufanyika mazungumzo na watawala hao kabla ya kuwaalika kwenye dini. Alikuwa akianza barua zake kwa kuwaita kwa majina ya heshima.

Kwa mfano alikuwa akianza barua zake kwa kusema, "kwa Kasra, Mkuu wa Fars" na "kwa Kaisari, Mkuu wa Roma." Na hasa ikitiliwa maanani kwamba katika barua zake kwa Watu wa Kitabu, alikuwa akibainisha nia yake njema kwao kwa kuwatajia aya isemayo: "Sema: "Enyi watu mliopewa Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Mayahudi na Manasara)! Njooni kwenye neno lililo sawa baina yetu na baina yenu; ya kwamba tusimwabudu yoyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe (Mwenyezi Mungu) na chochote; wala baadhi yetu tusiwafanye baadhi yetu wengine kuwa waungu badala ya Mwenyezi Mungu (au pamoja na Mwenyezi Mungu). Wakikengeuka, semeni: "Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu, (tumenyenyekea amri za Mwenyezi Mungu) (Aal Imraan: 64)."

Katika mihadhara, mijadala, midahalo na vitabu vyake, Sayyid Sharafu Deen alitumia njia na mbinu hiyo ya busara kwa madhumuni ya kuimarisha maelewano, umoja na udugu baina ya Waislamu. Swala hilo linaonekana wazi katika barua yake ya mdahalo wa kielimu kati yake na Sheikh Salim al-Bashri, Mufti wa Misri.

MWISHO