KUKOMBOLEWA QUDS
  • Kichwa: KUKOMBOLEWA QUDS
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 17:51:38 19-9-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

KUKOMBOLEWA QUDS

Abdallah Fahd, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kuwait amesisitiza kwamba kukombolewa kwa Quds Tukufu kutoka kwenye makucha ya utawala ghasibu wa Israel kunahitajia muamko, azma na irada thabiti ya Waislamu wote duniani.
Akizungumza katika kikao cha kimataifa cha "Quds katika Dhamiri ya Waarabu" kinachofanyika mjini Kuwait na ambacho kimefunguliwa na Nasir Muhammad Ahmad Swabah, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Fahd amesema kuwa nchi za Kiislamu zinapasa kuwa na mikakati madhubuti na ya pamoja kwa ajili ya kuikomboa Quds kutoka mikononi mwa walowezi wa Kizayuni. Amesema kuwa jambo hilo litathibiti tu iwapo nchi za Kiislamu zitaamua kushirikiana na kuwa na umoja pamoja na urafiki miongoni mwao.
Amesema nchi za Kiislamu na Kiarabu zina majukumu mazito kuhusiana na suala la Palestina. Amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona kwamba utawala ghasibu wa Israel umewafukuza mamilioni ya Wapalestina kutoka kwenye ardhi zao za jadi na kuwafanya waishi kama wakimbizi katika ardhi zao wenyewe na kwingineko huku ukiharibu kabisa sura ya mji wa Quds Tukufu ambao zamani ulikuwa nembo ya umoja na kuishi pamoja kwa amani wafuasi wa dini tofauti.
Akizungumza katika kikao hicho, Raif Najm, Waziri wa zamani wa Wakfu na Masuala ya Kiislamu wa Palestina pia amesema kuwa inasikitisha kuona kwamba taasisi na jumuiya mbalimbali za kimataifa zimepitisha maazimio mengi ambayo hadi sasa hayajawahi kutekelezwa na utawala haramu wa Israel. Wazungumzaji mbalimbali katika kikao hicho wamesema kuwa kuchaguliwa mji wa Quds kuwa makao makuu ya kiutamaduni ya nchi za Kiarabu ni fursa nzuri kwa ajili ya kuhuisha na kulinda utambulisho wa Kiislamu na Kikristo wa mji huo mtukufu. Wataalamu, wasomi na watafiti wengi wa masuala ya Palestina kutoka pembe mbalimbali za dunia wanashiriki katika kikao hicho cha siku mbili.

MWISHO