UMOJA KWA WAISLAMU
  • Kichwa: UMOJA KWA WAISLAMU
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 14:21:19 3-9-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

UMOJA KWA WAISLAMU

Umoja wa Kiislamu

Ayatulllah Taskhiri amesema kwa masikitiko kuwa, ukufurishaji wa Waislamu ni kizuizi kikubwa zaidi kinachozuia kukurubiana madhehebu ya Kiislamu na hii ni katika hali ambayo Uislamu umeweka wazi mipaka ya kuamini na kukufuru. Umoja wa Kiislamu ni lengo muhimu na tukufu ambalo wanafikra, viongozi, wasomi na wanazuoni wa Kiislamu wamekuwa wakilifuatilia kwa juhudi kubwa na kwa miaka mingi tokea mwanzoni mwa Uislamu. Ulimwengu wa Kiislamu unazijumuisha nchi ambazo kwa kawaida zina mifungamano mikubwa ya kijografia na kiutamaduni. Kutokana na utajiri mkubwa wa mafundisho yake, dini ya Kiislamu ilianzisha utamaduni na ustaarabu mkubwa pamoja na kuandaa mazingira bora ya kuwepo ushirikiano wa kidini na kiutamaduni kati ya mataifa mbalimbali. Lakini umoja na mshikamano wa ulimwengu wa Kiislamu katika kipindi ha historia umekuwa ukikabiliwa na hujuma ya kigeni na mara nyingine vitisho vya ndani. Moja ya mbinu zinazotumiwa na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu ni kuzifanya baadhi ya tofauti za kimadhehebu na kifikihi za Waislamu kuonekana kuwa kubwa zaidi kupita kiasi.
Katika hali kama hii, kufanyika juhudi za kuyakurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu kwa kuzingatia masuala ya pamoja yaliyopo kati ya madhehebu hayo ili yaweze kukabiliana na njama za maadui ni jambo la dharura kabisa. Ni wazi kuwa umoja kama huo hauwezi kupatika ila kupitia juhudi za kunyanyua uelewa na muamko kati ya Waislamu. Kwa kuandaliwa vikao mbalimbali vya umoja wa Kiislamu, wanafikra wasomi na wanazuoni wa Kiislamu kutoka kila pembe ya dunia hukusanyika na kujadili pamoja na kubadilishana mawazo kuhusiana na changamoto nyingi zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu na kutafuta njia zinazofaa za kuzitatua ili kuimarisha mshikamano wa Kiislamu. Katika kikao cha 23 cha kimataifa kilichoandaliwa hivi karibuni mjini Tehran kwa mnasaba wa kuzaliwa Mtume Mtukufu (SAW), zaidi ya nchi 45 za dunia ziliwakilishwa na wasomi wa Kiislamu. Kwa kutilia maanani matukio mengi makubwa ambayo yametokea katika ulimwengu wa Kiislamu na hasa katika nchi za Palestina, Iraq na Afghanistan, washiriki wa kikao hicho walijadili njia mbalimbali za kuweza kutatua matatizo yanayowakabili Waislamu katika nchi zao.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho, Ayatullah Muhammad Ali Tashkhiri , Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Kukurubisha pamoja Madhehebu ya Kiislamu, taasisi ambayo ndiyo inayohusika na uuandaaji wa vikao hivyo, alisema kuandaliwa vikao vya ndani ya nchi, kieneo na kimataifa vya kukurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu ni moja ya majukumu muhimu ya taasisi hiyo. Amesema tokea kuanzishwa kwa taasisi hiyo ya kukurubisha madhehebu ya Kiislamu, imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kuwakutanisha pamoja wanafikra na wasomi wa Kiislamu ili waweze kujadili kwa pamoja matatizo yanayowakabili Waislamu katika sehemu tofati wanazoishi. Taasisi hiyo imetekeleza mipango muhimu ya kutatua matatizo ya kisiasa, kiutamaduni na kimadhehebu yanayotokea katika ulimwengu wa Kiislamu. Imetumia njia za usuluhishi wa pamoja unaopatikana katika vitabu, sunna na sera za viongozi wa kidini ili kuweza kukubalika na kila upande. Huku akikosoa taasubi za kikabila, kimadhehebu na ufahamu finyu kuhusiana na dini, Ayatullah Taskhiri amesema kwamba njama za maadui wa Uislamu za kuzusha fitina na migawanyiko miongoni mwa Waislamu ni mbinu kongwe ambayo imekuwa ikitumiwa na maadui hao katika kipindi chote cha historia ya Kiislamu.
Ayatulllah Taskhiri amesema kwa masikitiko kuwa, ukufurishaji wa Waislamu ni kizuizi kikubwa zaidi kinachozuia kukurubiana madhehebu ya Kiislamu na hii ni katika hali ambayo Uislamu umeweka wazi mipaka ya kuamini na kukufuru. Ameongeza kwamba juhudi za kufanya yaonekane kuwa makubwa kuliko kiasi, mashambulio dhidi ya matukufu ya Kiislamu na kudharauliwa watu wengine ni baadhi ya mambo yanayozuia kuungana kwa madhehebu ya Kiislamu, na kwamba juhudi maradufu zinapasa kufanyika ili kuondoa mambo hayo na hivyo kuandaa uwanja wa kukurubiana Waislamu wa madhehebu tofauti katika kipindi hiki tata.
Kama tulivyosema mwanzoni, kuna udharura mkubwa wa kuungana Waislamu katika kipindi hiki nyeti kwa kutilia maanani kwamba maadui wanatekeleza njama kubwa na zilizopangwa kwa mpangilio maalumu dhidi ya Waislamu. Miongoni mwa mbinu zijulikanazo za maadui dhidi ya Waislamu ni kuwatenganisha kwa misingi ya kimadhehebu. Huku akibainisha hali ya hivi sasa ya ulimwengu wa Kiislamu, Ayatullah Hashimi Rafsanjani, Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran alisema katika kikao cha Umoja wa Kiislamu mjini Tehran kwamba inasikitisha kuona kuwa Waislamu ambao wanaunda zaidi ya watu bilioni moja na milioni 600 katika karibu nchi huru 60 za dunia, hawawezi kuungana kwa msingi wa nguzo muhimu inayojenga na kumuongoza mwanadamu, yaani Qur'ani Tukufu. Amesema matunda ya umoja na madhara ya mtengano ni jambo lililo wazi kwa kila mtu. Huku akisema kuwa tofauti za kimadhehebu ni jambo la kawaida kabisa, Ayatullah Rafsanjani amesisistiza kuwa uzingatiaji wa misingi ya maadili na akhlaki kama vile takwa na kumtegemea Mwenyezi Mungu ni mojawapo ya njia bora za kuleta umoja na mshikamno kati ya Waislamu.
Abdul Wahid Petersen mwandishi na mwanafikra wa Kiislamu kutoka nchini Denmark ni mzungumzaji mwingine aliyehutubia kikao hicho cha Tahran. Alisema kuwa Mwenyezi Mungu anasema katika kitabu kitakatifu cha Qur'ani kuwa aliwaumba wanadamu katika makabila na rangi tofauti ili kuwajaribu na kuwapa mtihani. Amesisitiza kwamba ubaguzi wa rangi hauna nafasi yoyote katika Uislamu. Amesema, Mwenyezi Mungu hazingatii rangi wala kabila katika kuwachagua waja wake wema. Wakati huohuo Dakta Muhammad as-Sayyid ad-Dasuqi mhadhiri katika Chuo Kikuu cha al-Azhar mjini Cairo alisisitiza katika kikao cha Tehran, udharura wa kuwepo umoja kati ya Waislamu na kuongeza kuwa utamaduni wa mazungumzo ya kuleta umoja miongoni mwa Waislamu yana athari kubwa. Amesema, mitazamo na nadharia za kifikihi hazipasi kuzusha taasubi na migawanyiko kati ya Waislamu bali jambo hilo linapasa kuwa ishara njema ya uhai wa mafundisho ya Kiislamu na utajiri wake wa kiutamaduni na kifikra. Alisema ni jambo bora kwa wanazuoni na wanafikra wa Kiislamu kuwa na umoja na sauti moja kwa shabaha ya kuleta ukurubiano kati ya madhebeu ya Kiislamu.
Hii leo njama za maadui wa Uislamu zimelenga fikra za Waislamu. Akifafanua suala hilo, Dakta Abdul Raheem As-Sayeh, Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Qatar amesema katika kikao hicho kwamba hujuma ya kiutamaduni ya nchi za Magharibi dhidi ya thamani za Kiislamu ndiyo hujuma kubwa zaidi ambayo inahatarisha ulimwengu wa Kiislamu kwa njia ambayo si ya moja kwa moja. Amesema, hujuma hiyo imeratibiwa kwa njia madhubuti na mpangilio maalumu, lengo lake likiwa ni kuyadhoofisha mataifa ya Kiislamu na kuyafanya yaachane na misingi yao ya kidini na kiustaarabu. Ameongeza kuwa baadhi ya changamoto zinazohatarisha ulimwengu wa Kiislamu ni zile zinazotekelezwa na maadui kwa njia ya moja kwa moja na mara nyingine kwa njia za siri.

Ufinyu wa fikra kuhusiana na masuala ya kidini ni jambo jingine linalodhuru umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu. Profesa Burhanu Deen Rabbani, rais wa zamani wa Afghanistan akizungumza katika kikao hicho cha Umoja wa Kitaifa alisema kuwa kuna mambo mengi yanayosababisha mivutano na migawanyiko katika nchi za Kiislamu na kwamba wanafikra na wanazuoni wa Kiislamu wa nchi tofauti wanapasa kufanya juhudi za kuondoa hitilafu na tofauti zinazotawala miongoni mwa Waislamu. Amesema moja ya mambo yanayosababisha matatizo katika ulimwengu wa Kiislamu ni fikra finyu na kutozingatia kwa kina tafsiri ya Qur'ani. Amesema, inasikitisha kuona kwamba ufinyu huo wa fikra pia unaonekana miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu. Bi Wilda Agobot, mwakilishi wa televisheni ya Hilal ya nchini Uturuki ambaye alishiriki katika kikao cha Tehran alisema kuwa Waislamu wanapasa kuzingatia nukta za pamoja kama vile Mtume, Kitabu na kibla na kujiepusha na misimamo ya kihamasa na kishabiki ili kuimarisha umoja miongoni mwao. Wanawajibika kujiweka mbali na masuala ya kihisia na kihamasa na kukabiliana kwa muamko na uangalifu mkubwa na njama za maadui wa Uislamu. Amesisitiza kwamba matatizo mengi yanayowakumba Waislamu hii leo yanatokana na fikra finyu kuhusiana na Uislamu na kuwataka wote washikamane vilivyo na kamba ya Mwenyezi Mungu ili kuweza kuleta umoja na mshikamano miongoni mwao.
Sayyid Ali Fadhlullah, mmoja wa washiriki wa kikao cha Umoja wa Kiislamu mjini Tehran kutoka nchini Lebanon alisema kuwa mkusanyiko huo mkubwa wa wanazuoni na wanafikra wa Kiislamu unatokana na juhudi za umoja wa Kiislamu za Imam Khomeini (MA) pamoja na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei. Amesema, hakuna tatizo lolote la kuwepo madhehebu tofauti ya Kiislamu lakini akaongeza kuwa, jambo hilo hugeuka na kuwa hatari kubwa linapopelekea wafuasi wa madhehebu hayo kuchukua misimamo inayokwenda kinyume na mafundisho ya Kiislamu. Amesisitiza kwamba Waislamu wanalazimika kutumia uwezo wao wote katika kukabiliana na adui. Amesema, Waislamu wanapasa kushirikiana kwa karibu na kuwa na umoja katika kukabiliana na utawala haramu wa Israel ambao unakanyaga matukufu ya Kiislamu huku taasisi muhimu za kimatifa, na hasa Umoja wa Mataifa, zikiwa zimekaa kimya na kutochukua hatua yoyote ya kukabiliana na dharau hiyo dhidi ya Uislamu.
Mwishoni, washiriki wa kikao cha 23 cha kimataifa cha Umoja wa Kiislamu mjini Tehran walisisitiza katika taarifa yao ya mwisho juu ya udharura wa Waislamu kuimarisha umoja, kusisitiza juu ya masuala ya pamoja, kuheshimiana wafuasi wa madhehebu mbalimbali na kudumishwa mazungumzo kati yao.

MWISH