KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA KUMI) A
  • Kichwa: KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA KUMI) A
  • mwandishi: Ramadhani Kanju Shemahimbo
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 20:27:25 13-10-1403

KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA KUMI) A
MLANGO WA 11: MALEZI YA MTOTO
MAMBO 40 JUU YA AKHLAQ (TABIA) KATIKA MAHUSIANO NA MTOTO WAKO:1
1. UTOE ZAWADI KWA MABINTI ZAKO KWANZA.
2. CHEZA NA WATOTO WAKO.2
Hili lina athari muhimu katika kumfundisha na malezi ya mtoto wako. Viongozi wetu katika Uislam wamesisitiza umuhimu wa jambo hili, na wamelipendekeza sana kwa Waislam.
Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwamba: “Mtu ambaye ana mtoto, anapaswa kuwa na tabia kama mtoto aapokuwa pamoja naye.”3 Pia imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s) kwamba : “Yeyote ambaye anaye mtoto, anapaswa kwa ajili ya mafunzo yake kujishusha mwenyewe mpaka kwenye kiwango chake cha utotoni.”4
3. Msiwapige watoto wenu wakati wakiwa wanalia, kwa sababu imes- imuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwamba: “Msiwapige watoto wenu wanapolia kwani kulia kwao kuna maana. Miezi minne ya kwanza ya kulia ni kukiri Upweke wa Allah, miezi minne ya pili ya kulia ni kumtakia rehma na amani Mtume na kizazi chake na miezi minne ya tatu ya kulia ni mtoto kuwaombea wazazi wake.”5
4. Busu watoto wako. Imesimuliwa kutoka kwa mmoja wa Maimam kwamba: “Mbusu sana mwanao kwa sababu kwa kila busu, utapewa cheo kitukufu cha kiungu ambacho vinginevyo itakuchukua miaka 500 kupata cheo hicho!” 6
Imesimuliwa pia kwamba mtu mmoja wakati mmoja alikuja kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na akasema: “Mimi sijawahi kubusu mtoto wangu kamwe.” Mtukufu Mtume akasema: “Kwa kweli mtu kama huyu atakuja kuwa mkazi wa moto wa Jahannam.”
5. Kwa kutoa salaam kwa mwanao, kunajenga hisia yake ya nafsi na tabia. Kama vijana wakitoa salaam ni wajibu kwa wakubwa kujibu; hata hivyo, ilikuwa ni tabia ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kutoa salam kwanza, ama kwa wakubwa au kwa wadogo.7
6. Usivikebehi vitendo vya mwanao, wala usiviite ni vya kijinga.
7. Usimwamrishe au kumkataza sana mwanao, kwani hili linawatia sana hamasa na kuwapelekea kuwa na tabia ya ukaidi watakapokuwa wakubwa.
8. Jenga tabia ya wanao kwa kuwaheshimu. Tunasoma katika hadithi kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alirefusha sajidah yake mpaka wajukuu zake waliposhuka kutoka mabegani mwake, na nyakati zingine aliswali swala za jamaa haraka sana wakati aliposikia watoto wa mama zao wanaoswali wakilia. Kadhalika, Imam Ali (a.s.) alikuwa akiwauliza wanawe maswali kuhusu mambo ya kidini mbele ya wengine, na hata kuy- atoa maswali ya watu kwao ili wapate kuyajibu.
Wakati wazazi wasipotosheleza shauku za asili na matamanio ya mtoto, basi mtoto anakimbilia kwenye njia potovu na mbinu (mara nyingi zinazofananishwa na makosa) ili kujaribu kujipa mwenyewe msukumo muhimu kujenga hisi za nafsi yake na umaarufu. Shaksia, uhuru, dhamira, kujiamini binafsi, na kadhalika udhaifu, uovu na kukosa kujiamini zote ni tabia na desturi ambazo misingi yake ipo mapajani mwa baba yake na kifua cha mama yake. Mtoto ambaye hakufanyiwa kama binadamu wengine au kama mwanafamilia mwenye thamani hawezi kutegemewa kuwa na shaksia iliyojengeka vyema katika utu uzima wake.
9. Timiza ahadi zako. Kutimiza ahadi katika Uislam ni alama ya imani yake mtu, na Mwenyezi Mungu Mtukufu anakutaja huku katika Qur’ani Tukufu:
وَأَوْفُوا بِالْعَهْدِ ۖ إِنَّ الْعَهْدَ كَانَ مَسْئُولًا {34}
“….. Na timizeni ahadi zenu, kwani ahadi ni yenye kuulizwa.” (Bani Israail; 17:34).
وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ {8}
“Na wale ambao kwa amana zao na ahadi zao ni wenye kutekeleza.” (Al-Mu’minun; 23:8).
Kutimiza ahadi ni moja ya nguzo za ustawi wa mwanadamu na moja ya sifa bora kabisa za tabia za mtu, msingi wake ukiwa juu ya malezi na mafunzo yake mtu. Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwamba: “Wapende watoto wako na uwafanyie upendo na upole. Pale unapowaahidi, ni lazima utimize ahadi hizo, kwa sababu wanakuchukulia wewe kama mpaji wao.
10. Na kuhusu kuwafundisha watoto mambo ya kijinsia, wazazi ni lazima kwanza wawafundishe watoto wao kutoingia chumbani kwa wazazi wao bila ya kuomba ruhusa. Mwenyezi Mungu ameelekeza kwenye suala hili muhimu ndani ya Suratun-Nuur; Aya ya 58:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لِيَسْتَأْذِنْكُمُ الَّذِينَ مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ وَالَّذِينَ لَمْ يَبْلُغُوا الْحُلُمَ مِنْكُمْ ثَلَاثَ مَرَّاتٍ ۚ مِنْ قَبْلِ صَلَاةِ الْفَجْرِ وَحِينَ تَضَعُونَ ثِيَابَكُمْ مِنَ الظَّهِيرَةِ وَمِنْ بَعْدِ صَلَاةِ الْعِشَاءِ ۚ ثَلَاثُ عَوْرَاتٍ لَكُمْ ۚ {58}
“Enyi mlioamini! Wakuombeni ruhusa wale iliyowamiliki mikono yenu, na wale wasiofikia balekhe miongoni mwenu mara tatu: Kabla ya swala ya Alfajiri na mnapovua nguo zenu wakati wa adhuhuri na baada ya Swala ya Isha; hizi ni nyakati tatu za faragha kwenu. …..”
(An-Nuur; 24:58).
Inashauriwa pia kuweka uangalizi wa karibu na udhibiti juu ya vitendo vyao pamoja wengine na kuzuia vile vitendo ambavyo vinaongeza hisia za kijinsia (kwa mfano, kwenda kwenye makundi yenye mchanganyiko). Ni muhimu kueleza hapa kwamba udadisi wao unakuwa mkubwa sana katika utoto wao. Kwa nyongeza, wanakuwa na hisia kali sana katika yale wanayoyaangalia na kuyaona, na bila ya woga wakataka kuyaweka katika vitendo na kuyajaribu wao wenyewe bila ya kujua au kufikiri kwamba kile wanachokifanya kinaweza kuwa sio sahihi.
BAADHI YA MAMBO MUHIMU YA KUANGALIWA
a. Akina mama ni lazima wawe waangalifu sana wakati wanapochunga usafi wa watoto wao (kwa mfano kuwaogesha), hata vile vichanga ambavyo ndio kwanza kuzaliwa, kwamba watoto wengine wanakuwa hawapo, hasa wale ambao ni wa jinsia tofauti.
b. Kutokea utotoni, wazazi wasicheze na viungo vya watoto vya uzazi, au hata vifua vyao na mapaja yao.
c. Kamwe usiwaache watoto peke yao au kwenye sehemu za faragha kwa vipindi virefu vya muda na wakati wanapokuwa wanapita kwenye awamu za udadisi. Pia si jambo linaloshauriwa kuwaacha bila kushughulikiwa wakiwa na mtu mwingine katika wakati huu, hasa kaka au dada.
d. Msiwaache wasichana wenye umri wa miaka sita wakae kwenye mapa- ja ya mwanaume asiye maharimu au wapigwe mabusu na wanaume wasio maharimu wao.
e. Msiwaache wasichana wakae uchi mbele ya watu wengine. Hususan vifua vyao na mapaja ni lazima vifunikwe.
f. Jenga mapenzi ya Swala ndani ya watoto wako, kama Mwenyezi Mungu Mtukufu anavyosema ndani ya Qur’ani Tukufu kwamba Swala inamwepusha mbali mtu na vitendo viovu:
إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنْكَرِ ۗ{45}
“….. Hakika Swala huzuia mambo machafu na maovu ….. (Ankabuut; 29:45).
11. Kumharibu mtoto kunasababisha udhaifu, na ukosefu wa nia na dhamira. Watoto wa namna hii huwasumbua wazazi wao katika utoto wao, na huwafanya wapambane na matatizo mengi.
WATOTO WALIOHARIBIKA, WAO BINAFSI HUKABILIWA NA MATATIZO MAWILI:
a. Wanayo matumaini yanayoegemea kwenye matakwa ya jamii, kama wazazi wao, kuwaliwaza na kuwaheshimu kwa hali yoyote ile iwayo, bila ya swali lolote lile. Pale wanapotambua kwamba watu sio tu kwamba hawatafanya hivyo, bali pia watayadhihaki matamaini hayo, wanachanganyikiwa na kujihisi wamefedheheshwa na kushushiwa hadhi yao.
b. Hali kama hizo huunda msingi wa dharau na kuwafanya wachukie, jeuri, wanaokosa subira na wanyonge. Wanakuwa aina ya watu wanaowafikiria wengine kwa uduni na wanawatendea vitendo na maneno makali.
12. Hakuna kinachoweza kuzima hisia za kujiamini binafsi kwa mtoto zaidi kuliko kumlazimisha kufanya mambo wanavyoweza kuwa hawana uwezo wa kuvifanya. Hii hasa ndio hali wakati endapo mtoto hana mafanikio, inafuatiwa na kauli za kukatisha tamaa: “Usijisumbue kujaribu, hutaweza, huna uwezo huo.”
13. Swali kwa ajili ya watoto wako, tangu wakati wa mimba na baada ya kuzaliwa pia.8
14. Ukumbusho na maombi lazima vitolewe kwa upole na uangalifu ili visije vikasababisha kizuizi kati ya wazazi na mtoto. Siku moja, Imam Hasan (a.s.) aliwaita watoto wake na watoto wa ndugu yake pamoja na akawaambia: “Ninyi wote ni watoto wa jamii ya leo, na inategemewa kwamba ni viongozi wa jamii ya kesho. Kwa hiyo, someni, jifunzeni na fanyeni juhudi ya kupata elimu, na yeyote ambaye hana kum- bukumbu nzuri na hawezi kuyahifadhi masomo yanafundishwa na mwalimu wakati wa vipindi vya masomo, (anapaswa) ayaandike na ayaweke nyumbani.” Hivyo tunaona kwamba Imam alisababisha mapenzi ya kupata elimu ndani yao bila kutumia mbinu kama kuwatishia au kuwalazimisha, bali kwa kuwafanya wao waelewe kwamba elimu ndio njia ya kwenye heshima na utukufu.
15. Endapo mtoto wako akiheshimiwa, anao mwelekeo mdogo sana wa kuasi kanuni za nyumbani humo. Heshima na maingiliano mazuri kati ya wazazi na mtoto ndio msingi katika kuunda tabia ya mtoto, imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Waheshimuni watoto wenu na zungumzeni nao kwa desturi nzuri na kwa namna inayopendeza.”
16. Mfano mzuri wa maadili ni mtu ambaye anayerekebisha tamaa za watoto wake kwa hekima sana pamoja na mbinu sahihi.
17. Lea imani ya mtoto wako. Watoto ambao wamekuzwa tangu mwanzoni na imani ya Mwenyezi Mungu Mtukufu wanayo dhamira yenye nguvu na moyo shupavu, na kuanzia miaka yao ya awali kabisa wanakuwa wamekomaa na wajasiri; hili linaonekana kirahisi kwa vitendo na maneno yao. Utayari wa moyo wa mtoto kujifunza imani na akhlaq ni kama ardhi yenye rutuba ambamo aina yoyote ya mbegu inaweza kumea na kukua. Kwa hiyo wazazi ni lazima wawafundishe watoto wao mapenzi juu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na Ahlul-Bayt (a.s.) na viongozi wa Uislam kuanzia kwenye fursa zao za mapema kabisa.
Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.) kwamba: “Wafundisheni hadithi watoto wenu mapema sana iwezekanavyo, kabla wapingaji (wa imani zenu) hawajawafikia kabla yenu.”9
Katika hadithi, wazazi ambao hawazingatii maisha ya baadae (akhera) ya watoto wao wanaonywa vikali. Imesimuliwa kwamba macho ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) yaliangukia kwa watoto fulani na yeye akasema: “Ole kwa watoto wa zama za mwisho (kabla ya kudhihiri kwa Imam wa 12) kwa sababu ya taratibu zisizopendeza za baba zao.” Yeye akaulizwa: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni kwa sababu ya baba zao washirikina?” Yeye akajibu akasema: “Hapana, kwa sababu ya baba zao Waislam ambao hawakuwafundisha watoto wao wajibu wowote wa kidini. Wao waliridhika na mambo ya kimaada yasiyo na thamani kwa ajili yao. Nimechoshwa na watu kama hao na sina haja nao.” 10
Inasemekana kwamba katika Urusi ya kikomunisti, wao walikuwa waki- uondoa uwepo wa Mwenyezi Mungu kutoka kwenye kiwango cha chini kabisa; kwa mfano, wakati watoto walipokuwa na njaa au kiu, wazazi wao wangewaacha walie a kumwaambia, “Muombeni Mwenyezi Mungu aku- ruzukuni.”
Pale watoto walipofanya hivyo, na bado wakabakia na njaa na kiu, wao walikuwa wakiwaambia, “Mnaona, mmemlilia Mungu na hakukupeni chochote! Sasa muombeni Lenin (kiongozi wa Urusi) awape riziki!” Pale watoto walipofanya hivyo, ndipo hapo tu walipoweza kuwa- pa chakula na kinywaji. Matokeo ya hili ni kwamba, walipandikiza ndani ya watoto kuanzia utotoni mwao kwamba hakuna Mungu kupitia njia hii ya udanganyifu. Dhani hii hii inashutumiwa ndani ya Qur’ani Tukufu, Sura ya Yaasiin, Aya ya 47:
قَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلَّذِينَ آمَنُوا أَنُطْعِمُ مَنْ لَوْ يَشَاءُ اللَّهُ أَطْعَمَهُ إِنْ أَنْتُمْ إِلَّا فِي ضَلَالٍ مُبِينٍ {47}
“….. Wale waliokufuru huwaambia wale walioamini: Je, tumlishe ambaye Mwenyezi Mungu akipenda atamlisha? Ninyi hammo ila kati- ka upotevu dhahiri…..” (Surat Yaasiin; 36:47).
Hata hivyo, hili ni soma zuri sana kwetu sisi la jinsi Mwenyezi Mungu Mtukufu anavyopaswa kutambulishwa kwa watoto tangu umri wa utotoni. Wakati wowote watoto wanapofikia kwenye umri ule ambao kwamba wanaelewa kwamba wakati wowote wanapotamani kitu, wanahitajia kuwaomba wazazi wao, basi wazazi wao wanapaswa kuwataka kwanza waombe kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Kisha pale wanapowapatia kile kitu walichokihitaji, wazazi wanapaswa kusisitiza kwamba kimewafikia wao kupitia kwenye rehema za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hivyo, jinsi wanavyoendelea kukua, watakuwa na uwezo wa kumuona Mwenyezi Mungu Mtukufu kama ndiye msingi mkuu nyuma ya kila kitendo.
18. Kaa mbali na tabia ya kukamatana mikono na utawala juu ya watoto.
19. Moja ya wajibu wa wazazi ni kulea ile tabia ya asili ya kusema kweli ndani ya watoto. Tabia zao ndani ya nyumba zinapaswa kuwa za namna ambayo kwamba hii inakuwa ni desturi yao. Hata hivyo, hili ni moja ya maeneo magumu sana ya kumkuza mtoto na uangalifu kwenye elimu na vitendo ni muhimu sana.
Imesimuliwa katika hadithi kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Mwenyezi Mungu awe na huruma kwa mtu yule ambaye anawasaidia watoto wake katika kufanya wema.” Msimuliaji wa hadithi hii aliuliza: “Kwa vipi?” Katika jibu lake, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alitoa maelekezo manne:
a. Chochote kile alichonacho mtoto katika uwezo wake na akawa amekifanya, basi kikubali.
b. Usitarajie kile ambacho ni kigumu kwake.
c. Mkinge kutokana na dhambi.
d. Usimuongopee wala kufanya mambo ya kijinga.
20. Usitumie hofu kama njia ya kumkuzia mtoto wako, kwani hili linasababisha madhara kwenye utu wao na kupelekea kwenye matatizo ya kisaikolojia. Hususan adhabu za kupindukia kutoka kwa mama zinadhoofisha uhusiano na thamani ambayo mtoto anakuwa nayo juu ya mama yake ndani ya moyo wake. Mara nyingi, kutazama au kukaa kimya kunaweza kuwa na nguvu zaidi katika kuwafanya watoto kuelewa makosa yao kuliko kuwapiga au kuwatishia.
21. Kumkumbatia na kumbusu mtoto ni moja ya chakula chao cha roho, na ni muhimu sana kwamba kiasi cha kutosha cha jambo hili kinatolewa kwao. Moja ya sababu ya kwa nini mtoto analia inaweza kuwa kwamba ana kiu juu ya huku kuonyeshwa upendo. Watoto wanaokua kwa upendo mwingi wanakuwa na utu wa kujiamini ambao hauyumbishwi na matatizo yanayojitokeza katika maisha.
Inasimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Kwa hakika Mwenyezi Mungu huonyesha huruma kwa mja Wake ambaye ana mapenzi makubwa kwa watoto wao.”11
Imesimuliwa vile vile kutoka kwa Imam huyo: “Nabii Musa alimwambia Mwenyezi Mungu yafuatayo wakati alipokuwa kwenye mlima Tuur: ‘Ewe Allah! Ni tendo gani lililo bora kwa mujibu Wako?’ Mwenyezi Mungu akamjibu: ‘Kuwapenda watoto ndio tendo bora.’”
22. Wazazi wanao wajibu wa kuwafanya watoto wao kuelewa ubaya wa dhambi na kujenga chuki kwa ajili ya watu wanaoshiriki katika hili, na kadhalika kukemea maovu na kuyatia moyo matendo mema ya mtoto. Hata hivyo, kukemea na kuvutiwa kuna wakati na mahali pake na kusi- fanywe kupita kiasi kwani hili lenyewa linaweza kumpotosha mtoto.
23. Vitanda vya watoto wa miaka sita na zaidi lazima vitengwe mbali na kila kimoja, hata kama wote ni wasichana au wote ni wavulana.12
24. Pamoja na tabia asilia ambazo mtoto anarithi kutoka kwa wazazi wake, mazingira na malezi ya mtoto yana athari kubwa. Ni kutowezekana kukubwa sana kwamba ndani ya familia ambayo haishughuliki sawa- sawa, mtoto wa desturi na kawaida anakuzwa.
Hasa, yale maelekezo ya wazazi yanakuwa na matokeo tu kama wazazi hao wanaongoza kwa mfano. Hatua ya kwanza ya kumkuza mtoto ni malezi ya nafsi.
Mtu ambaye hana tabia nzuri hawezi kumuongoza mwingine kwenye akhlaq nzuri, na kadhalika, wazazi wenye hasira kali kwa kawaida hawawezi kukuza mtoto mtulivu na mwenye subira.
Watoto wanahitaji kufundishwa kwamba tabia kama vile kusema uongo, kusengenya, lugha chafu na kadhalika, ni sifa ambazo hazipendezi, na kwa kawaida, mtoto atajiepusha kutokana na mambo kama hayo pale tu wazazi watakapokuwa wameweka mifano kama hiyo.
25. Ni lazima pawe na tofauti katika taratibu na matarajio ya tabia ya mtoto ndani ya nyumba, na nje pia. Hapo nyumbani, mruhusu mtoto kucheza kwa uhuru.
26. Wakati wote zivumilie tabia zisizotegemewa za mtoto wako kwa kiwango cha ukomo, na usiyachukulie makosa ya mtoto wako wakati wote kuwa ni yasiyosameheka, ili kwamba uwe hulazimiki wakati wote kumuadhibu. Subira, kuvumilia na msamaha ni lazima wakati unapomkuza watoto. Kama mwanao anayo sifa ambayo huipendi, inapaswa kusahihishwa kwa njia ya busara bila kuonyesha kumdharau mtoto, na namna sahihi ya kufanya mambo inapaswa kuonyeshwa wakati uleule kama kumzuia na njia za kizamani.
Pale wazazi wakiwakaripia watoto wakati wote, wanawadhalilisha watoto hao na sio tu kwamba hawatakuwa na mafanikio katika kumrekebisha mtoto, bali pia watawasababishia tabia ya ukaidi. Imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s.): “Makaripio yaliyozidi yanachochea moto wa kiburi. 13
27. Unapokuwa unamwelekeza mtoto, usitaje majina ya watoto wengine kila mara, au kuwalinganisha na wengine.
28. Simulizi za hadithi ni mbinu inayofaa na muhimu sana ya kuhimiza tabia na sifa njema na kukatisha zile mbaya, kama vile haki za marafi- ki, dini na kadhalika. Qur’ani Tukufu inatumia mbinu hii kufanyia hivyo kama ilivyoelezwa katika Surat Yusuf; Aya ya 111:
لَقَدْ كَانَ فِي قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ لِأُولِي الْأَلْبَابِ ۗ{111}
“Bila shaka katika hadithi zao limo fundisho kwa wenye akili …..” (Yusuf; 12:111).
Ni muhimu kuzingatia akilini yafuatayo wakati unapochagua simulizi za hadithi:
a. Hadithi hizo lazima zimtaje Mwenyezi Mungu kwa namna moja au nyingine, na zisimuliwa kwa lengo la kulea utu na tabia za mtoto wako.
b. Umri, akili na hali ya maarifa ya mtoto lazima uzingatiwe wakati wa kuchagua hadithi.
c. Kusiwepo na uzidishaji kiasi, au uongo au uvumi mbali na ukweli ndani ya hadithi hizo.
d. Lazima ziwe na majibu ya maswali ya mtoto.
e. Zichaguliwe hadithi bora, kama vile alivyoeleza Mwenyezi Mungu ndani ya Surat Yusuf, Aya ya 3:
“Sisi tutakusimulieni hadithi zilizo bora zaidi.”
f. Ukweli na uadilifu ni lazima wakati wote viwepo katika hadithi hizo.
g. Mhusika mkuu (ambaye ndiye mfano wa maadili) wa hadithi hizo laz- ima awe hana mikengeuko au tabia mbaya.
h. Hadithi hizo lazima zisiwe ndefu sana au zenye kuchosha juu ya mtoto.
29. Utundu wa mwanao katika miaka ya mwanzoni ni ishara ya akili nyingi inayoongezeka katika miaka ya utu uzima, hivyo usije ukawa na wasiwasi sana au kumuadhibu sana.
30. Wafanye watoto wako waswali kuanzia umri wa miaka saba (7), na kufunga kuanzia miaka 9, ama nusu siku au kiasi kama hicho, kutegemea uwezo wao.
Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Pale watoto wetu wanapofikia umri wa miaka 5, sisi tunawaambia waswali, kwa hiyo waambieni watoto wenu kufanya hivyo pale wanapofikia umri wa miaka 7; na sisi tunawaambia watoto wetu wafunge pale wanapofikia umri wa miaka 7 kwa kiasi chochote cha uwezo wanachoweza kuwa nacho, nusu siku, au zaidi, au pungufu kidogo, na wafunje saumu zao wanapokuwa na njaa au kiu ili waweze kuzoea kufunga na kuendeleza uwezo kwa ajili ya hilo, hivyo waambieni watoto wenu katika umri wa miaka 9 wafunge kwa kiasi chochote watakachoweza kuwa na uwezo nacho, na wakati kiu inapowazidia basi wavunje saumu zao.” 14 na 15
Imesimuliwa vilevile katika hadithi: “Tunawaamrisha watoto wetu kufanya tasbihi ya Hadhrat Fatimah (a.s.) kama vile tu tunavyowaamrisha kuswali. 16
Ni muhimu kukumbuka kwamba katika matendo ya ibada, kama katika jambo jingine lolote, lazima kuwe na kiasi cha wastani. Imesimuliwa kuto- ka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Uislam ndiyo dini madhubuti ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Endeleeni na kufanya wastani wa mambo na msifanye vitu ambavyo vitafanya nyoyo zenu kuona taabu kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu.17
31. Usiwe mwepesi wa kuwashutumu watoto wako kwa kusema uongo kwa sababu hadi miaka 5, kudanganya halisi, au kudanganya kwa sababu ya faida binafsi ni adimu; bali ni kutokana na mawazo yao mashughuli, yanayohusiana na kucheza au kusababisha mshangao ndani ya wengine, au kwa ugunduzi wa mtoto wa kinafsi.
32. Msiwalaumu watoto ambao wamewachosha ninyi na maswali yao, kwa vile hili linadhoofisha hisia zao za udadisi.
33. Jaribuni kugombana, hususan mbele ya mtoto, kwani holi linawasum- bua sana na linaathiri utu wao.
34. Watoto wana hofu maalum juu ya neno kifo, hususan kifo cha mama au baba yao. Kwa hiyo, pale ambapo sio lazima, msizungumzie wakati wote juu ya kifo, au mfano wake. Hata hivyo, wafundisheni watoto wenu juu ya ukweli wa kifo, wazi wazi na kwa utulivu na bila ya kuvu- tia hofu.
35. Chunguza na kutambua juu ya vipaji vya mwanao na uviendeleze hivyo kiasi inavyowezekana.
36. Kuhusu mielekeo ya kidunia, usimkalifishe mwanao kupita kiasi ili asije akaenda kwenye njia ya upotovu, wala usifanye kwa kiwango cha chini mno, kwani njia zote hizo ni hatari.
37. Sababu moja muhimu ya furaha ya mtoto ni upole wa wazazi. Hakuna sifa nyingine inayoweza kusababisha furaha na utulivu kwa mtoto kama upendo, na kadhalika, hakuna sifa nyingine inayoweza kuvuruga na kutatiza mtoto kama kukosa upendo kutoka kwa wazazi.
Watoto wa wazazi ambao wamefanikiwa katika nyanja hii wanajaribu kiasi cha uwezo wao kuwaridhisha wazazi wao na kujiweka mbali na vitendo ambavyo vinawaudhi na kuwasumbua, wakati wa utoto wao na pia pale wanapokuwa wakubwa. Kwa hiyo, mapenzi na upendo sio tu vinakidhi haja za watoto bali pia vinawahakikishia utiifu wao.
Mwenyezi Mungu Mtukufu ameelezea juu ya uzito wa upole huu ndani ya Qur’ani Tukufu, katika Surat al-Imraan; Aya ya 159:
فَبِمَا رَحْمَةٍ مِنَ اللَّهِ لِنْتَ لَهُمْ ۖ وَلَوْ كُنْتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ {159}
“Basi kwa sababu ya rehema ya Mwenyezi Mungu umekuwa laini kwao na kama ungekuwa mkali mshupavu wa moyo, wangekukim- bia…..” (al-Imraan; 3:159).
Ni muhimu kutambua kwamba hapapaswi kuwa na kuzidi kiasi; mapenzi makubwa sana, kama vile tu madogo sana, ni uharibifu kwa mtoto; kwa hiyo, fuata njia ya kati na kati na uwakuze na kuwalea watoto kwa namna ambayo wanaweza kusimama wenyewe kwa miguu yao miwili (kujitegemea) wanapokuwa watu wazima.Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Akina baba wabaya sana ni wale ambao, katika wema na mapenzi yao kwa watoto wao, wanavuka mipaka na kuelekea kwenye kuzidisha kupita kiasi.” 18
38. Ni muhimu kwamba wazazi wawape watoto wao hiari na uhuru kulin- gana na uwezo wao, ili wabadili uzembe wao, na waendeleze uhuru wao wa ndani na kujiamini binafsi. Wakati huo huo, mtu lazima awe mwangal- ifu asivuke mipaka kiasi kwamba watoto wajiletee madhara wao wenyewe.
Baadhi ya wazazi, ama kujipa uhuru wao wenyewe au majukumu yao au kwa sababu ya mapenzi
yaliyopotea njia, wanawaacha kabisa watoto wao kwenye mipango yao wenyewe, hata hivyo, kabla ya
muda mrefu, watoto wanakua bila kujua kitu chochote cha majukumu yao ndani ya nyumba, au vinginevyo.
Ni kufikia hapa ambapo wazazi wanajaribu kuliingiza hili kwa watoto wao, bila kushangaza ikawa bila athari yoyote.
Wazazi wengine hata hivyo, wanafanya kinyume chake na hawawapi watoto wao fursa ya kutosha kuongoza vitendo vyao wenyewe, daima wakiingilia kati katika kile wanachofanya watoto wao na jinsi wanavyofanya. Vyote ni makosa na vina matokeo hasi.
39. Kuwalea watoto wako vizuri inavyostahili ni moja wa wajibu wa mzazi, na kukosa umakini katika wajibu huu ni sababu ya makemeo ya Maimam.19 Mtu anapaswa kujaribu kwa uwezo wake wote kupitia njia mbalimbali kujenga mapenzi ya Mwenyezi Mungu na Ahlul-Bayt (a.s.), ili watoto wafuate njia ya haki. Kwa kiasi ambacho msingi wa mapenzi ni uzoefu na elimu, watu wajaribu kulipandikiza hili ndani ya watoto wao.20
40. Wafundishe watoto wako Qur’ani. Usomaji wa Qur’ani ndani ya nyumba unaeneza maneno bora ya haki na ukweli halisi wa Uislam. Kuwa katika mazingira ambayo mtu ana ufahamiano na Qur’ani, anasikiliza visomo vya Qur’ani Tukufu na anayafanyia kazi maelekezo ya Qur’ani, kunakuwa na athari kubwa kwenye maisha ya mtoto. Kila wakati wazazi wanaposoma Qur’ani, watoto wanashawishika kufanya vivyo na wanafuata katika tabia hii. Hasa hasa, wale watoto ambao wana kumbukumbu nzuri ya asili na wana vipaji, wanaweza kwa urahisi kabisa kuhifadhi Qur’ani, ambayo itawanufaisha daima.21
REJEA:
•    1. Mengi yamechukuliwa kutoka Rayhaaneye Beheshti, Uk. 221 – 241
•    2. Mustadrakul-Wasa’il, Jz. 15, Uk. 171
•    3. Wasa’ilush-Shi’ah, Jz. 21, Uk. 386, hadithi ya 27659
•    4. Wasa’ilush-Shi’ah, Jz. 21, Uk. 386, hadithi ya 27658
•    5. Biharul-Anwaar, Jz. 60, Uk. 381
•    6. Rawdhatul-Waaidhin.
•    7. Mustadrakul-Wasa’il, Jz. 2, Uk. 69
•    8. Dua zinazopendekezwa kwa ajili ya mtoto wa halali zimeelezewa kwa kirefu katika Mlango wa 6 – Mimba: Dua zinazopendekezwa.
•    9. al-Kafi, Jz. 6, Uk. 47
•    10. Mustadrakul-Wasa’il, Jz. 2, Uk. 625
•    11. Biharul-Anwaar, Jz. 103, Uk. 7
•    12. Mustadrakul-Wasa’il, Jz. 2. Uk. 558
•    13. Tuhafal-Uquul, Uk. 84
•    14. al-Kafi, Jz. 3, Uk. 409 hadithi ya 1
•    15. Hadithi hii inawahusu hasa vijana wavulana; maana ya jumla hata hivyo ni kwamba watoto wanapaswa kufundishwa kuswali na kufunga, miaka michache kabla hawajafikia kipindi cha baleghe, ili kwamba waweze kukuza uwezo kwa ajili ya hilo.
•    16. al-Kafi, Jz. 3, Uk. 343
•    17. al-Kafi, Jz. 2, Uk. 86-87
•    18. Ta’rikh Ya’quubi, Jz. 3, Uk. 53
•    19. Mustadrakul-Wasa’il, Jz. 15, Uk. 164
•    20. Hili linaelezewa kwa kina zaidi katika: Njia 14 za kudukiza Mapenzi ya Ahlul-Bayt (a.s.) ndani ya watoto wako katika Mlango huu.
•    21. Hili linaelezewa kwa kina zaidi katika: Uhifadhi wa Qur’ani, katika Mlango huu.
ITAENDELEA KATIKA MAKALA IJAYO