KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA KUMI) B
  • Kichwa: KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA KUMI) B
  • mwandishi: Ramadhani Kanju Shemahimbo
  • Chanzo: www.islam.org
  • Tarehe ya Kutolewa: 20:37:24 13-10-1403

KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA KUMI) B

MLANGO WA 11: MALEZI YA MTOTO

NJIA 14 ZA KUDUKIZA MAPENZI YA AHLUL-BAYT (A.S.) NDANI YA WATOTO WAKO 1

1. Utungaji mimba, na kile kipindi chote cha kuwa na mimba na tabia ya kiakili ya wazazi vyote vina athari juu ya mtoto katika eneo hili. Vilevile na kufuata yale mapendekezo yaliyotajwa katika kitabu hiki, kufuata mambo ambayo yamekokotezwa: kula tabaaruk (chakula kilichobarikiwa) ya Maimam, kuhudhuria kwenye Majalis na kusikiliza hotuba, kuwa mwangalifu juu ya yale mtu anayoyaangalia au kusikia, na kusikiliza Qur’ani, Nauha na Qasidah wakati wa kunyonyesha, na kadhalika.

2. Tumia kunywa maji ya mto Furati na Khakhe Shafaa (udongo kutoka kwenye eneo karibu na kaburi la Imam Husein (a.s.) huko Karbala).

3. Kuza mapenzi na hisia za upendo. Wafunze watoto wako kwamba mapenzi juu ya Ahlul-Bayt (a.s.) yanasababisha wao kupendwa na Mwenyezi Mungu na hao Ahlul-Bayt (a.s.), na kwamba mapenzi juu Allah na Ahlul-Bayt (a.s.) yanakwenda pamoja mkono kwa mkono.

4. Zingatia neema ya Ahlul-Bayt (a.s.) kwa wafuasi wao, Shi’ah.
Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Tunawajua Shi’ah wetu kwa namna ile ile mtu anavyoijua familia yake.” Imesimuliwa vilevile kwamba katika Siku ya Kiyama, Shi’ah wa Imam Ali (a.s.) watatoshelezwa, kuokolewa na kufaulu.

5. Peleka ujumbe wa faida za urafiki na Ahlul-Bayt (a.s.), kama vile, “Fahamu kwamba yeyote anayekufa akiwa na mapenzi na dhuria wa Muhammad anakuwa amekufa shahidi,” na “Fahamu kwamba, yeyote anayekufa na mapenzi juu ya kizazi cha Muhammad, milango miwili ya peponi itafunguka kutoka kaburini mwake.”

Thamani ya mtu ni kulingana na kiasi gani cha mapenzi kilichomo mioy- oni mwao. Jinsi shabaha ya mapenzi ilivyo na thamani zaidi ndivyo anavyokuwa na thamani zaidi yule mwenye kupenda.

6. Fikisha haja ya mapenzi haya. Watu kwa kawaida wanavutiwa na vile vitu ambavyo vinatosheleza mahitaji yao, na sisi kwa kweli ni wahitaji zaidi sana wa hao Ahlul-Bayt (a.s). Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwamba: “Mapenzi juu yangu na mapenzi juu ya Ahlul-Bayt wangu yanamnufaisha mtu katika sehemu 7 ambako kuna wingi wa misukosuko: Wakati wa kukata roho, ndani ya kaburi, wakati wa kufufuliwa kutoka kaburini, wakati wa kupewa kitabu cha matendo, wakati wa hesabu, wakati wa kupimwa kwa vitendo, na wakati wa kuvuka lile daraja – Siraat.”2

7. Onyesha kuthamini kwako, na matumaini yako juu ya vitendo maalum, ili kufanya mfano wa matendo hayo kwa ajili ya baadaye. Imesimuliwa kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alimpa Mwarabu mmoja kipande cha dhahabu ambacho yeye alikizawadiwa, kwa sababu Mwarabu huyo alijiweka kwa unyenyekevu mbele za Allah katika swala yake yenye makusudio mema na ukweli. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Nimekupa dhahabu hii kwa sababu mbele ya Allah, wewe ulimtukuza kwa wema na kwa kustahiki kwake.” Hata hivyo, ni muhimu kwamba kumtia mtu moyo kusiwe katika namna ya kishawishi cha hongo.

8. Tekeleza yale unayoyalingania, kwani ile hali ya utu na vitendo vya mzazi ni walimu wasio wa moja kwa moja lakini muhimu sana kwa mtoto.

9. Sherehekea maadhimisho ya zile wiladat (kuzaliwa) na wafat (vifo) vya Ahlul-Bayt (a.s.), kama vile Muharram, Iddul-Ghadir, wiladat ya Imam wa 12, na kadhalika. Hii inajumuisha, sio tu kwenda msikitini, bali na maadhimisho nyumbani, kwenye Madrassa, na kadhalika. Panapaswa kuwepo na mafungamano baina ya furaha ya maisha ya mtoto na maisha ya Maimam (a.s.), kwa mfano, kufanya maadhimisho ya kuzaliwa kwao kuwa ni tukio la furaha katika kumbukumbu za watoto kwa kufanya tafrija, kutoa peremende, zawadi na hivyo kuwa na athari isiyo ya moja kwa moja juu ya mtoto.

10. Tamaa ya mtoto ya kutaka kukua na kufikia ukamilifu ni ya juu sana katika miaka ya ujana na mwanzoni mwa utu uzima, na hii inawasababishia, bila ya kufikiri, kutafuta (watu) vigezo vya mifano katika maisha. Tamaa hii ya kimaumbie lazima itumike vizuri sana na ombwe (nafasi tupu) hiyo ijazwe na Ahlul-Bayt (a.s.)

Kwa kweli, hao Ahlul-Bayt (a.s.) ndio udhihirisho wa ukamilifu wa uzuri wa Mwenyezi Mungu. Kupokezesha ujasiri wao, maadili, miujiza, ukarimu, uwezo wa kutibu watu na kutatua matatizo yao na daraja yao ya uombezi kwa Mwenyezi Mungu vyote vina matokeo mazuri katika kuleta mfungamano kati ya watoto na wao Ahlul-Bayt (a.s.).

Moja ya mbinu za Qur’ani Tukufu katika malezi na kuelekeza wanadamu pia ni katika kutumia vigezo bora ili kumuongoza mtu kwenye njia ya sawa iliyonyooka, kama ilivyoelezwa katika Surat al-Ahzab, Aya ya 21:

لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِمَنْ كَانَ يَرْجُو اللَّهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّهَ كَثِيرًا {21}

“Bila shaka mnao mfano mwema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na kumtaja Mwenyezi Mungu sana.” (al-Ahzaab; 33:21).

11. Jiepushe na vile vitendo ambavyo vinaondoa mapenzi ya Ahlul-Bayt (a.s.) kutoka kwa watoto; hili liende sambamba na vile vitendo vinavy- ochochea mapenzi. Kwa mfano, kama zile Majlisi nyingi zinazofanyika katika zile siku kumi za mwanzo za mwezi wa Muharram zikiwa zinachosha na kuwafanya watoto kuwa wachovu, au hali ya mazingira ikawa sio nzuri kwa watoto kwa kuwa wao hawatendewi vizuri, au watoto wanalazimishwa kufanya ibada nyingi, yote haya yanaweza kusababisha vikwazo kwenye uhusiano wa karibu na wa mapenzi kwa Ahlul-Bayt (a.s.).

12 Jenga mazingira ya kiroho na ya makusudi. Hata kama watoto wataachwa zaidi kwenye mipango yao wenyewe na hawakuvutwa huku na huko, kama wanawekwa kwa utaratibu maalum katika mazingira hayo, huo mvuto kwa Ahlul-Bayt (a.s.) bila kusukumwa utajitokeza. Kambi za kitamaduni na kiislam, ziyara, kwenda kwenye haraam, kukutana na watu wa maana, kuwa na marafiki wa Ahlul-Bayt wakati wote, shughuli za kijamii na kushiriki kwenye majlisi, yote haya yanaweza kuchangia katika kujenga mazingira kama hayo.

13. Wazoeshe watoto wako vitabu, majarida, michoro ya picha za rangi na mashairi kuhusiana na Ahlul-Bayt (a.s.). Hili linaweza kufanyika kwa idadi kadhaa ya njia kama vile mashindano, majadiliano, kusoma, uan- dishi wa makala, kubadilishana mawazo na kadhalika.

14. Himiza uanzishwaji wa vikundi vya vijana hasa kwa kuadhimisha matukio katika maisha ya Ahlul-Bayt (a.s.) kujumuisha shughuli kama vile azadari, michezo, hotuba, na kadhalika.
UHIFADHI WA QUR’ANI TUKUFU

Hapa 3 chini na baadhi ya mambo ya kuwasaidia wote, wazazi na watoto kuhifadhi Qur’ani, ili kwamba kitendo hiki kitukufu kiweze kuleta manu- faa mfululizo daima, Insha’allah.

1. Anzisha uhifadhi wa Qur’ani kwa watoto katika umri mdogo, kama inavyosemekana kwamba kile kinachojifunzwa katika siku za mapema hakisauliki kamwe.

Kwa kweli, imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s.): “Nyoyo za vijana ni kama ardhi isiyolimwa, inakubali chochote kila kinachopandwa juu yake.”4 Imesimuliwa pia kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Elimu utotoni ni kama kuichonga juu ya jiwe.”

2. Hifadhi Qur’ani kwa uaminifu. Vitendo vyote lazima viwe ni kwa kutafuta ukaribu na ujamaa na Mwenyezi Mungu peke Yake. Kwa vile hili sio jambo rahisi kulihamishia kwa watoto, ni lazima waangaliwe kuona kwamba ni nini motisha yao au hamasa juu ya kuhifadhi Qur’ani. Hakuna ubaya katika kuwapa watoto zawadi ili kuwatia moyo pale mwanzoni, na kisha, jinsi vile wanavyokua wakubwa, taratibu na kwa kufaa sana kuwafanya watambue lile lengo halisi nyuma ya vitendo vyao.

3. Hifadhi kila Aya, kifungu au Sura kwa nia ya Ma’sumin (r.a.) au shahidi, na muwasilishie mtu huyo hizo thawabu baada ya kuhifadhi. Sio tu kwamba kufanya hivyo kunamuongezea mtu malipo bali watu hawa vilevile watakuwa waombezi wetu. Hivyo mtu Insha’allah atakuwa mwenye kupokea rehema za ziada, neema na tawfiiq ya Allah Azza wa Jallah, na Aya hizo zitahifadhika haraka na kwa ubora zaidi.

4. Amini katika uwezo wa milele wa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

5. Kamwe usikadirie kwa upungufu nguvu ya Dua na maombi. Kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Suratul-Furqaan; Aya ya 77:

قُلْ مَا يَعْبَأُ بِكُمْ رَبِّي لَوْلَا دُعَاؤُكُمْ ۖ{77}

“Sema: Mola Wangu asingekujalini kama sio kule kuomba kwenu …..” (al-Furqaan; 25:77).

6. Kuwa shupavu, mwenye lengo, uvumilivu na matumaini. Kufanikisha lengo hili, na vilevile tamaa na shauku, jitihada na dhamiri ni lazima viwepo.
7. Kula vyakula rahisi, halali na halisi kwani hivi ni venye athari sana katika kuiandaa akili na kumbukumbu.

8. Kuwa na ratiba sahihi. Bila ya ratiba sahihi, itakuwa nihatua ndefu na ngumu, na pengine hata isiyowezekana kulifikia lengo hilo tukufu.

Kwa ajili ya kuhifadhi, ainisha muda maalum kila siku, kipindi maalum cha muda na vile vile kiwango maalum (kwa mfano idadi ya kurasa kwa siku). Usingojee fursa zijitokeze, bali weka kwa bidii sana masharti muhimu yanayotakikana, na jaribu kutokosa hata siku moja ya kutekeleza ratiba hiyo.

9. Tumia Qur’ani ambayo ni rahisi, yenye maandisi ya wazi, ambayo ni rahisi kusomeka na yenye kanuni za tajwiid ndani yake. Kama huna ufahamu wa tafsiri ya Qur’ani Tukufu, ni bora kutumia nakala yenye tafsiri chini yake (au pembeni mwake), ambayo ni fasaha na nyepesi kusomeka, kwani kule kusoma na tafsiri yake pia kutasaidia kuhifadhi. Ni lazima kwamba uwekwaji wa namba za aya ndani ya Qur’ani ni sahihi na wakuaminika. Upande wa nyuma wa kurasa hizo zisije zikawa nyeupe kabisa kwani hilo linapelekea uchovu wa macho.

10. Sahihisha matamshi yako kwa kujifunza chini ya usimamizi wa mso- maji hodari mwenye uwezo, au kumsikiliza msomaji mzuri. Matumizi ya mikanda ya sauti, video na CD yanafaa kwa kazi hii vile vile.5

11. Rudia kile ulichokwisha kujifunza, kwa kughani na mara kwa mara.

Usiende kwenye fungu jingine la Aya au Surah mpaka lile fungu la nyuma liwe limekamilishwa. Soma mbele ya watu wengine ili kisahi- hisha na kujaribu ule uhifadhi, na wakati wote rudi kwenye kile kilichohifadhiwa ili kukidumisha.

12. Wakati wa kuhifadhi, kuwa na umakini kamili na akili huru kutokana na mawazo ya aina zote. Hiki ni kimoja cha vipengele kinachoongezea kwenye hifadhi yenye mafanikio. Kuondoa aina zote za vivurugaji, kama vile njaa, kiu, wasiwasi, uchovu ni muhimu sana, kama kulivyo kuchagua kwa muda na mahali panapofaa.

Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Msomaji wa Qur’ani tukufu anahitaji mambo matatu: moyo mnyenyekevu, mwili huru (kutokana na usumbufu) na mahali pa faragha.”

13. Kuwa na udhuu wakati wa kuhifadhi Qur’ani tukufu na elekea Qibla kwa kiasi kinachowezekana.

14. Himiza ushiriki katika mashindano na programu za kuhifadhi na kuso- ma.

15. Soma Dua ifuatayo kabla ya kuanza:

“Ewe Allah! Nipe rehma Zako kwa kuniwezesha mimi kuacha vitendo visivyo vya utii Kwako daima kwa kiasi utakachonibakisha kuwa hai, na unirehemu kwa (kunikinga) kujikalifu na yale ambayo hayanihusu.

Na uniruzuku na mawazo mazuri juu ya yale yote ambayo ni lazima niyafanye ili kukufanye uwe radhi nami. Na uufanye moyo wangu ugandamane kati- ka kukifadhi Kitabu Chako kama ulivyonifundisha, na uniruzuku niweze kukisoma katika namna itakayokufany uridhike nami. Ee Mungu! Nitie nuru katika kuona kwangu kupitia Kitabu Chako, nikunjulie kifua changu, ufurahishe moyo wangu, ufanye ulimi wangu kuwa fasaha na mwili wangu kushughulika. Nitie nguvu kwa Kitabu hiki, unisaidie mimi ndani yake. Hakika hakuna msaidizi kwa ajili yake hicho ila Wewe; hakuna mungu ila Wewe.”6
MANENO YA HEKIMA KUTOKA KWA IMAM ALI IBNUL-HUSEIN; ZAINUL-ABIDIIN (A.S.)

“Haki ya mama yako ni kwamba, utambue kwamba alikubeba wewe mahali ambapo hakuna mtu anayembeba mtu mwingine, alikupa wewe lile tunda la moyo wake ambalo hakuna mtu anayempa mwingine, na alikulinda wewe kwa viungo vyake vyote. Hakuwa akijali kama ana njaa alimradi wewe ulipata kula, wala kama alikuwa na kiu alimradi wewe ulikunywa, kama hakuvaa ilimradi wewe ulivaa, kama alikuwa juani ilimradi wewe ulikuwa kivulini. Alisamehe usingizi wake kwa ajili yako na alikukinga kutokana na joto na baridi, yote hayo ili uweze kuwa wake.

Hutaweza kumuonyesha yeye shukurani, isipokuwa kupitia msaada wa Mwenyezi Mungu Mtukufu na Yeye kukupa mafanikio.”

“Haki ya baba yako ni kwamba, unajua kwamba yeye ndiye mzizi wako. Bila ya yeye, wewe usingekuwepo. Wakati wowote unapoona jambo lolote ndani yako ambalo linakufurahisha, ujue kwamba baba yako ndie chanzo cha neema hiyo juu yako. Hivyo mtukuze Mwenyezi Munguna umshuku- ru Yeye kwa kiwango hicho. Na hakuna nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu.”

“Haki ya mwanao ni kwamba, unapaswa kujua kwamba yeye anatokana na wewe na atahusishwa na wewe – kupitia vitendo vyake vyote, vizuri na vibaya – katika mambo ya karibuni ya dunia hii. Unawajibika kwa kile ambacho kimedhaminiwa kwako, kama vile kumsomesha katika tabia njema, kumwonyesha kwenye mwelekeo kwa Mola Wake.

Hivyo fanya vitendo kuelekea Kwake kwa vitendo vya mtu anayejua kwamba atalipwa thawabu kwa kufanya mema kuelekea Kwake, na ataadhibiwa kwa kufanya makosa au dhambi.”

Yamechukuliwa kutoka – Makala ya Haki – (ar-Risalatul-Huquq)
MANENO YA HEKIMA KUTOKA KWA IMAM ALI IBNUL-HUSEIN; ZAINUL-ABIDIIN (A.S.)

“Ewe Mungu! kuwa na huruma juu yangu kupitia kuendelea kuishi kwa wanangu, uwaongoze kwenye haki kwa ajili yangu, na kuniruhusu mimi kuwafaidi wao!”

“Mola Wangu, yafanye maisha yao kuwa marefu kwa ajili yangu, ongeza vipindi vyao, unikuzie yule mdogo kabisa kwa ajili yangu, mpe nguvu yule dhaifu kwa ajili yangu; rekebisha miili yao kwa ajili yangu, kujitolea kwao katika dini, na tabia zao za kimaadili, wafanye wazuri katika nyoyo zao, viungo vyao, na kila kitu ambacho kinanihusu mimi katika mambo yao, mimina kwa ajili yangu na juu ya mikono yangu riziki zao!

Wafanye kuwa wachamungu, wenye kuhofia, wenye utambuzi, wasikivu, na watiifu Kwako, wenye upendo na mwelekeo mwema kwa marafiki Zako, na wap- inzani shupavu na wenye chuki kwa maadui Zako wote! Amiin!

“Ewe Allah, imarisha mkono wangu kupitia kwao, unyooshe mgongo wangu uliolemewa; nizidishie idadi yangu; pendezesha mahudhurio yangu, dumisha utajo wangu, nitosheleze ninapokuwa sipo nyumbani; nisaidie katika mahitaji yangu; na wafanye wenye mapenzi kwangu, upendo, walio karibu, waadilifu, watiifu, wasiwe wakaidi kamwe, wasio na hes- hima, wapinzani au wakosaji!

“Nisaidie katika kuwalea kwao, kuwaelimisha kwao, na upendo wangu kwao, nipatie miongoni mwao, kutoka Kwako, watoto wanaume, lifanye hilo liwe wema kwa ajili yangu, na wafanye wawe msaada kwa ajili yangu katika kile ninachoomba kutoka Kwako!

“Nipatie mimi pamoja na kizazi changu kinga kutokana na Shetani aliye- laaniwa, kwani Wewe umetuumba sisi, umetuamuru sisi, na umetukataza sisi, na umetufanya sisi kutamani malipo ya kile ulichoamrisha, na kuhofia adhabu yake!

Umetuwekea adui anayepanga dhidi yetu, ukampa mamlaka juu yetu kwa namna ambayo kwamba hukutupa sisi mamlaka juu yake, ukamruhusu yeye kukaa katika vifua vyetu na ukamfanye atembee katika mishipa yetu ya damu; yeye hajali kitu, ingawaje sisi tunajali, yeye hasau, ingawaje sisi tunasahau, anatufanya sisi tujihisi kuwa salama kutokana na adhabu Yako na anatujaza hofu kwa wengine wasiokuwa Wewe.”

Dua kwa ajili ya watoto wema na waadilifu,
as-Safinatul-Kamilatul Sajjadiyah.

REJEA:

    1. Nyingi zimepatikana kutoka Rayhaaneye Beheshtii, Uk. 244-247
    2. Mizan al-Hikmah, Jz. 2, Uk. 237
    3. Nyingi zimechukuliwa kutoka kwenye Rayhaaneye Beheshti, Uk. 235-238
    4. Nahjul-Balaghah, Barua ya 31
    5. Wasomaji wanaopendekezwa ni pamoja na Muhammad Siddiq Menshawi, Khaleel Hussari, Muhammad Jibrail, Abu Bakr Shaatri, hawa pamoja na wengineo wanaweza kupatikana katika mtandao http://www.hidayahonline.org/7page=audio.
    6. al-Kafi, Jz. 2, uk. 577

MWISHO WA MSURURU WA MAKALA HIZI ZA: KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI