KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA NANE) A
MLANGO WA 8: BAADA YA KUJIFUNGUA
VYAKULA VINAVYOPENDEKEZWA
1. TENDE SAFI
a) Imesimuliwa kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Kitu cha kwanza mwanamke anachopaswa kula baada ya kujifungua kiwe ni ratb (aina ya tende freshi), kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu alimwambia Hadhrat Maryam baada ya kumzaa Nabii Isa ale ratb.” 1
Alipoulizwa, “Je kama sio msimu wa ratb iweje?” Yeye akajibu akasema: “Basi ale tende tisa kutoka Madina, na kama hizo nazo hazi patikani, basi tende zozote tisa zitatosha. Hakika Mwenyezi Mungu amesema: “Naapa kwa Heshima na Utukufu Wangu, kwamba mwanamke yeyote ambaye amezaa hivi punde na akala ratb, nitamfanya mwanawe kuwa mwenye subira.’”
b) Imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s.) kwamba lisha tende aina ya Birmi kwa mwanamke baada ya kuzaa mtoto wake ili kwamba mtoto huyo awe jasiri na mwenye subira.
c) Kula tende sio tu kwamba kuna manufaa kwa mama huyo bali kuna athari kwenye maziwa ya kifuani vilevile, na pia ni kwenye manufaa zinapolishwa watoto.2 Kwa vichanga vinavyoanza kuzaliwa, imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s.) kwamba weka kajipande kadogo katika kinywa cha kitoto hicho, na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alifanya hivyo kwa Imam Hasan na Imam Husein (a.s.).
2. MAJI YA MTO FURATI NA KHAKHE SHAFAA
a. Imesimuliwa kwamba maji ya Furati na khakhe shafaa yawekwe kwenye mdomo wa mtoto, na kama maji ya mto Furati hayapatikani, basi maji ya mvua badala yake.3Na4
b. Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.) kwamba khakhe shafaa inapaswa kuwekwa kwenye kinywa cha mtoto, kwani hii inamkinga na maumivu na majonzi.5
c. Katika riwaya nyingine kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.), inasimuliwa kwamba yeye amesema: “Hakuna mtu ambaye anakunywa maji ya mto Furati na akayaweka kwenye mdomo wa mtoto isipokuwa kwamba yeye ni rafiki yetu, kwa sababu Furati ndio mto wa mu’min.6
3. NYINGINEYO
Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.) kwamba wakati mtoto anapozaliwa, chukua kiasi cha maziwa kutoka kwa mama yake (kipimo cha mbegu ya adesi), yachanganye na maji na uweke matone mawili katika tundu ya pua ya kulia ya mtoto huyo, na kisha ya kushoto, na usome Adhana katika sikio lake la kulia na Iqaamah katika sikio lake la kushoto, kabla hawajakata kiunga mwana kutoka kitovuni mwake. Kama hili likifanyika, hofu haitamfika mtoto huyo kamwe na Umm Sabyaan (jinni subiani) hatamsumbua kamwe.7
MATENDO YANAYOSHAURIWA
1. UKUBALIKANAJI WA MTOTO, AWE WA KIUME AU WA KIKE
Kwa bahati mbaya, hata leo hii, wengi bado wanayo ile kasumba kwamba watoto wa kike hawafai na kuwashughulikia watoto wa kiume na wa kike kwa tofauti. Ambapo, iko wazi kabisa ndani ya Qur’ani Tukufu kwamba mtoto ni kiumbe cha Mwenyezi Mungu Mtukufu na Yeye anajaalia mtoto wa kiume kwa yeyote amtakaye na mtoto wa kike kwa amtakaye. 8
Inasimuliwa kwamba wakati pale Imam Zainul-Abidiin (a.s) alipobashiriwa habari njema za kuzaliwa kwa mwanawe, yeye hakuuliza iwapo kama alikuwa wa kiume au wa kike, bali hasa kwanza aliuliza, maumbile (umbo) yake yako sawasawa?
Kisha alipoambiwa kwamba mtoto huyo alikuwa mwenye afya njema na hakukuwa na dosari yoyote katika maumbile yake, yeye alisoma haya: “Alhamdulillahi al-ladhiy lam yakhluq miniy shaiyaan mushawwahaan”
“Sifa zote ni za Mwenyezi Mungu ambaya hakuumba kutoka kwangu kitu chenye umbo lisilo sawa.”9
Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Ni jambo la neema kwa mwanamke kwamba mtoto wake wa kwanza awe ni wa kike.”10
Imesimuliwa kwamba mabinti ni wema na neema na vijana ni fadhila. Mtu ataulizwa kuhusu fadhila alizopewa, ambapo wema na neema vitaongezwa.11
2. KUSOMA ADHANA NA IQAAMAH
Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ameeleza kwamba yeyote ambaye atazaliwa mtoto, anapaswa kumsomea Adhana kwenye sikio lake la kulia na Iqaamah kwenye sikio la kushoto, kwani hili ni ulinzi kutokana na uovu wa Shetani.12
Kwa kuongezea, katika simulizi nyingine imeelezwa kwamba mkunga au mtu mwingine lazima aambiwe amsomee Iqaamah katika sikio la kulia ili jinni asije akamsumbua mtoto, wala asije akawa mwendawazimu. 13
Imesimuliwa vilevile kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alithibitisha kwamba zilisomwa Adhana na Iqaamah kwenye masikio ya Imam Hasan (a.s.) na Imam Husein (a.s.), na pia Suratul-Fatiha, Ayatul-Kursi, mwisho wa Suratul-Hashir, Suratul-Ikhlaas, Suratul-Falaq, na Suratun-Naas.14
3. NGUO ZA MTOTO
Kutoka kwenye hadithi wakati wa kuzaliwa Imam Hasan (a.s.) na Imam Husein (a.s.), ni dhahiri kwamba ni makuruhu kumfunga mtoto kwenye nguo ya manjano mara tu baada ya kuzaliwa; bali inapendekezwa kumfunika kwenye nguo nyeupe.15
4. JOSHO (GHUSL)
Imeelezwa katika kitabu Fiqh al-Ridhaa kwamba moja ya mambo yanay- opendeza (mustahab) lililosisitizwa sana (wengine wanadiriki hata kuliita la wajibu) baada tu ya kuzaliwa kwa mtoto ni kumpatia mtoto huyo Ghusl. Mtu lazima aweke nia kwamba ninampa mtoto huyu ghusl kwa ajili ya radhi za Mwenyezi Mungu Mtukufu na halafu kwanza aoshe kichwa chake, kisha upande wa kulia na halafu upande wa kushoto.16
Hata hivyo, inapasa ifahamike kwamba hili linapaswa kufanyika tu iwapo lina usalama kiafya na sio lenye madhara kwa mtoto huyo.
5. KUNYOA NYWELE 17
Hii inahusisha unyoaji wa nywele zote za mtoto (anayetoka tumboni) mara tu baada ya kuzaliwa, na kutoa dhahabu au fedha kulingana na uzito wa nywele hizo kama sadaqah. Halafu nywele hizo zizikwe ardhini. Inapendekezwa kulifanya hili katika siku ya saba baada ya kuzaliwa mtoto.
Nywele ni lazima zinyolewe zote kabisa bila kuacha kishungi au shole (sokoto) la nywele kwenye paji.Imesimuliwa kwamba mtoto mwenye kishungi aliletwa karibu ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.); kisha Mtume hakumswalia mtoto huyo na akasema kwamba kishungi chake kinyolewe kiondoke.
Inashauriwa kwamba baada ya kunyolewa kwa nywele hizo, inapaswa akandwe kwa zafarani kichwani mwake. Ukandaji wa damu ya aqiqah hata hivyo unakataliwa kwa nguvu kabisa na umeitwa ni kitendo cha kijahilia.
6. ‘AQIQAH 18 NA 19
Hii inahusisha uchinjaji wa mnyama kwa jina la mtoto kwa ajili ya ulinzi wake. Aqiqah ni sunna iliyokokotezwa sana kwa yeyote yule mwenye uwezo (baadhi wamediriki hata kuiita ni wajibu), na ni bora kama itafanyi- ka katika siku ya saba baada ya kuzaliwa mtoto.20
ANGALIZO: Inashauriwa kwamba huo unyoaji wa nywele, utoaji wa dhahabu/fedha kama sadaka na Aqiqah vifanyike kwenye sehemu moja hiyohiyo na kwa wakati mmoja, ingawaje ni sunna kwamba unyoaji wa nywele ndio ufanyike mwanzo.
ANGALIZO: Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.) kwamba Aqiqah sio sawa sawa na kafara (qurbaanii)
7. UTAHIRIWAJI WA WAVULANA21
Kutahiri ni wajibu juu ya wavulana, na pamoja na kunyoa na Aqiqah, inapendekezwa kwamba yafanyike yote katika siku ya saba baada ya kuzaliwa kwa mtoto, ingawaje hili likifanyika kabla ya hapo hakuna madhara.22
Kama haikufanyika wakati huo, ni sunna kwamba ifanyike hadi wakati wa balehe ya mtoto huyo, ambapo baada ya hapo ni wajibu juu ya kijana huyo mwenyewe kuifanya. Hata hivyo, wanavyuoni wengine wameeleza kwamba pale mtoto anapokaribia kubalehe, ni wajibu juu ya mlezi kumfanyia. Hasa imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s.) kwamba mtu anayekuwa muislam anapaswa kutahiriwa, hata kama ana umri wa miaka 80.
Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.) kwamba watoto wanapaswa kutahiriwa kwani kunafanya mwili kuwa msafi zaidi, kunafanya nyama za mwili kukua haraka, na ardhi inachukia sana mkojo wa mtu asiyetahiriwa.
Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwamba ardhi inakuwa najisi kwa siku arobaini kutokana na mkojo wa mtu asiyetahiri- wa, na katika riwaya nyingine, imesimuliwa kwamba ardhi inatoa mkoromo wa huzuni kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa sababu ya mkojo wake mtu asiyetahiriwa.
Imesimuliwa vilevile kwamba endapo utamtahiri kijana, na ile ngozi ya kifuniko ikakua tena na kufunika dhakari, mtahiri tena, kwa sababu ardhi inalalamika kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa muda wa siku arobaini kwa sababu ya kufunikwa kule kutahiriwa kwake.
Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Mtu yeyote ambaye hajatahiriwa asiongoze swala, na ushahidi wake haukubaliki, na endapo atafariki (katika hali hiyo) basi msimswalie kwa vile ameacha sunna kubwa sana ya Mtukufu Mtume, isipokuwa kama ameiacha kwa hofu ya kifo ambacho kingetokana na kutahiriwa kwake.” Inashauriwa kusoma du’a ifuatayo wakati wa kutahiri:23
“Ewe Mungu! Hakika (hili tunalofanya) limo katika njia ya Sunnah Yako na Sunnah ya Mtume Wako (s.a.w.w.) kukutii Wewe na dini Yako na kutimiza amri Yako, nia na kutekeleza sheria ambazo umeamua kuzifanya zifuatwe bila masharti. Kwa hiyo umempa muonjo wa joto la chuma kupitia kutahiriwa kwake na kufikwa na jambo ambalo kwa hakika Wewe unalijua vizuri zaidi kuliko mimi. Ewe Allah! basi mtakase na dhambi zake; umuongezee umri; na umuondolee kutoka mwilini mwake magonjwa ya mlipuko na maumivu; na uongeze utajiri wake; na umlinde kutokana na umasikini; kwani kwa hakika Wewe unajua zaidi na sisi hatujui kitu.”
8. KARAMU (WALIMAH)
Hii inahusisha kuwalisha waumini juu ya kuzaliwa mtoto na kwa ajili ya kutahiriwa kwa mtoto huyo (hizi zinaweza kukusanywa na kufanywa kwa pamoja wakati mmoja). Inashauriwa kuwakaribisha ndugu na marafiki mnamo siku ya saba baada ya kuzaliwa kwa mtoto (au karibu na siku hiyo) kushiriki katika tukio adhimu la kuzaliwa kwa kichanga hicho. Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Sherehe na karamu katika siku ya kwanza ni wajibu, kwenye siku ya pili ni vizuri, na kwenye siku ya tatu hiyo ni riyaa (yaani, ni kwa ajili ya watu wengine na sio kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu).” 24
Ni makuruhu kwa waalikwa wote kuwa ni matajiri, bali mchanganyiko wa matajiri na masikini sio tatizo.
Ni mustahab pia kwamba waalikwa waitikie huo mwaliko wa kwenye walimah huo
9. KUTOGA (KUTOBOA) MASIKIO
Kutoga masikio ya mtoto huyo ni jambo linalopendekezwa.25
10. KUGUSANA KWA MAMA NA MTOTO NA KUNYONYESHA26 NA27
Moja ya vitendo bora baada ya kuzaa ni kuogesha mtoto huyo na kisha kumrudisha karibu na ngazo ya mama yake na kuwafunika na blanketi. Nusu saa baada ya kuzaliwa, mtoto anakuwa anatambua kabisa na mchangamfu, na ndio wakati muafaka wa kujizoesha kunyonya na mguso wa mama yake.
Zile siku chache za mwanzo maziwa hayatengenezwi kwa wingi; hata hivyo, kiasi kile kinachotoka kinatosha, kinafaa na muhimu kwa mtoto aliyezaliwa punde. Ni muhimu sana kwamba kuchoka kwa mama na kukosa maziwa (kwa wingi) kusije kukatumiwa kama ni sababu ya kumlisha mtoto kwa chupa kwa hili linasababisha kucheweza kutengeneza maziwa kutoka kwa mama na mtoto kutokuwa na uwezo wa kunyonya sawa sawa. Vile vile kunaongeza uwezekano wa maambukizi kwa mtoto.
AQIQAH - MTAZAMO WA KARIBU ZAIDI 28
UMUHIMU WA KUFANYA AQIQAH
Imesimuliwa kwamba maisha ya mtoto yameambatishwa na Aqiqah,30 na endapo kama haikufanyika, inamuanika mtu kwenye taabu na kifo. Kama ikicheleweshwa, ni sunnah juu ya baba mpaka kubalekhe kwa mtoto, na baada ya balehe, inakuwa ni sunnah juu ya mtoto mwenyewe.29
Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.) kwamba Aqiqah ni muhimu kwa mtu yeyote tajiri, na kama mtu ni masikini, anapaswa kufanya Aqiqah mara tu anapopata pesa, na kama hatapata pesa yoyote, basi ni sawa tu. Endapo mtu hakufanya Aqiqah, na akawa alifanya kafara (qurbaani), hii itatosha.
Imesimuliwa kwamba mtu mmoja alimuuliza Imam as-Sadiq (a.s.): “Tumeomba kondoo kwa ajili ya Aqiqah lakini hatuwezi kupata hata mmoja, je, unashauri nini? Je, tunaweza kutoa thamani ya kondoo huyo kama sadaka badala yake?” Imam alijibu akasema: “Hapana, ombeni mpaka mpate mmoja kwani Mwenyezi Mungu anapenda ulishaji wa wengine …”
Umar ibn Yazid anasimulia kwamba yeye alimuuliza Imam as-Sadiq (a.s.): “Mimi sijui kama baba yangu alinifanyia Aqiqah au hapana.” Imam akajibu akasema: “Itekeleze wewe,” na hivyo akafanya Aqiqah katika umri wa utu uzima wake.
Katika riwaya nyingine imesimuliwa kwamba mtu mmoja alimuuliza Imam as-Sadiq (a.s.) kwamba endapo mtoto atafariki katika siku ya saba, je, Aqiqah bado inapaswa kufanyika? Imam akajibu kwamba ikiwa mtoto atafariki kabla ya swala ya Adhuhuri, Aqiqah inakuwa sio lazima, bali endapo mtoto huyo atafariki baada ya Adhuhuri, basi itekeleze Aqiqah.
REJEA:
1. Surat Maryam, 19:25
2. Israar Khuuraakiihaa, Uk . 96
3. Udongo mtakatifu wa Karbala, Iraqi.
4. Hii inashauriwa tu kwenye maeneo ambapo mtu ana hakika kwamba maji ya mvua hayakuchafuliwa
5. Al-Kafi, Jz. 6, Uk. 24 hadithi ya 4
7. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 145-146
6. Biharul-Anwaar, Jz. 104, Uk. 114, hadithi ya 33
7. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 126
8. Surat al-Shuraa (42:49)
9. al-Kafi, Jz. 6, Uk. 21
10. Biharul-Anwaar, Jz. 104, Uk. 98, hadithi ya 64
11. al-Kafi, Jz. 6, Uk. 6, hadithi ya 8
12. al-Kafi, Jz. 6, Uk. 24, hadithi ya 6
13. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 126
14. Biharul-Anwaar, Jz. 104, Uk. 126, hadithi ya 86
15. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 146
16. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 130
17. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 132
18. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 120 - 133
19. Aqiqah itakuja kuelezewa kwa kirefu chini ya - Aqiqah: Uchunguzi makini katika mlango huu
20. Mustadrakul-Wasa’il, Jz. 15, Uk. 145, hadithi ya 17807
22. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 134-135
23. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 134
24. Kitabu, ‘A Mother’s Prayer’
25. Wasa’ilush-Shi’ah, Jz. 16, Uk. 455
26. Wasa’ilush-Shi’ah, Jz. 16, Uk. 134
27. Rayhaaney-e Behesht, Uk. 167
28. Hili limeelezwa kwa kina zaidi katika Mlango wa 9: Kunyonyesha
29. Hilliyatul-Muttaqin, Uk. 130 - 133
30. al-Kafi, Jz. 6, uk. 25, hadithi ya 3
31. Hilliyatul-Muttaqin, Uk. 150
ITAENDELEA KATIKA MAKALA IJAYO