KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA TANO)
  • Kichwa: KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA TANO)
  • mwandishi: Ramadhani Kanju Shemahimbo
  • Chanzo: www.isalm.org
  • Tarehe ya Kutolewa: 11:50:10 14-9-1403

KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA TANO)
MLANGO WA 4: UPANGAJI WA FAMILIA
UZAZI WA MPANGO KATIKA UISLAM:
Uzazi 1 wa mpango kama hatua ya binafsi kupanga au kudhibiti ukubwa wa familia kwa sababu za kiafya au kiuchumi zinazoruhusiwa katika Uislam. Hakuna ama aya ya Qur’ani au hadithi dhidi ya udhibiti wa uzazi, wala sio wajibu wa lazima kupata watoto katika ndoa. Aidha, kuna hadithi kadhaa ambazo bila shaka zinathibitisha kwamba kupanga uzazi kunaruhusiwa.
Imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s.) kwamba: “Moja ya njia mbili za ukwasi ni kuwa na wategemezi wachache.2
Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.) kwamba: “Imam Ali ibn al- Husein (a.s.) hakuona tatizo katika kukatiza kujamiiana na kumwagia nje na alikuwa akiisoma aya ya kwamba: ‘Na (kumbuka) Mola wako alipowaleta katika wanadamu kutoka migongoni mwao kizazi …..’ 3
Hivyo kutoka kwenye mbegu yoyote Mwenyezi Mungu amechukua ahadi, ina uhakika wa kuzaliwa hata kama (imemwagwa) juu ya jiwe gumu.4
Kwa kulingana na hadithi hiyo hapo juu, uumbaji upo mikononi mwa Mwenyezi Mungu Mtukufu pekee. Tupange ama tusipange uzazi, kama Mwenyezi Mungu Mtukufu akihukumu, mtoto huyo atatungwa kwenye mimba.
Kwa kuhitimisha ni kwamba hadithi hiyo hapo juu inaonyesha kwamba kupanga uzazi kunaruhusiwa.
MBINU ZA KUZUIA MIMBA
Kuna idadi kadhaa ya mbinu au njia za uzuiaji wa mimba. Zile ambazo kwa kawaida ni zenye kutumika sana tutazichunguza hapo chini ili kufahamu iwapo kutumika kwake kunaruhusiwa katika Uislam au hapana.
Uruhusiwaji umetambulika kwa ufafanuzi wa uanzaji wa ujauzito kwa mtazamo wa Kiislam, ambao ni wakati yai la uzazi linapopandikizwa kwenye ukingo wa mji wa mimba tumboni mwa mwanamke.
Kwa hiyo, chochote kinachozuia upandikizaji huo kinaruhusiwa na chochote kinachokatisha mimba, baada ya upandikizaji, huko ni kutoa au kuharibu mimba nako ni haraam (hakuruhusiwi).
Ni muhimu kutambua kwamba mbinu hizi zimechunguzwa kutokana na mtazamo wa fiqhi tu. Kwa maoni ya kiuganga kuhusu kuaminika na uwezekano wa athari za mbinu hizi, tafadhali muone daktari.
MBINU ZINAZORUHUSIWA
Mbinu zifuatazo hazihusishi upasuaji kiganga na pia zinageuzika na kutu- mika kwa njia zaidi ya moja. Mwanaume au mwanamke anayetumia mbinu hizi anaweza kuacha kuzitumia wakati wowote ili kuweza kutunga mimba.
1. KINGA YA VIDONGE (VYA KUMEZA)
Vidonge vya kudhibiti uzazi huzuia kushika mimba kwa kuzuia utengenezwaji wa mayai ya uzazi. Vidonge hivyo hubadilisha viwango vya homoni na huzima dalili za homoni kutoka kwenye tezi kwa ajili ya ovari kutoa yai la uzazi. Vidonge hivi vinatumiwa kwa njia ya kunywa kwenye ratiba sahihi kwa siku 20 au zaidi wakati wa kila mzunguko mmoja wa hedhi.
Kwa vile aina zote za vidonge kama hivyo huwa vinazuia utengenezwaji wa mayai, basi vinaruhusiwa; hata hivyo, mhusika lazima amuone daktari kuhusu athari ambazo zinawezekana kutokea.
Kuna baadhi ya vidonge ambavyo vinafanya kazi baada ya kujamiiana kukishatokea, kwa mfano, kile ‘kidonge cha asubuhi ya baada’ – (morning- after pill), au kile kilichoendelezwa hivi karibuni, kidonge cha RU486. Halafu tena, kwa vile matumizi ya vidonge kama hivyo yanazuia upandikizwaji wa mayai, basi yanaruhusiwa. Kwa hiyo, vidonge kama vile ‘morning-after pills’ na RU486 vinaweza kutumika baada ya kujamiiana LAKINI sio baada ya kuhisi au kutambua kwamba mimba tayari imekwishatungika.
2. SINDANO YA DEPO-PROVERA
Depo-Provera inafanya kazi sawasawa kabisa kama vidonge, bali badala ya kuinywa huwa inapigwa sindano mara moja kila baada ya miezi mitatu. Hii na njia za kuzuia uzazi nyingine kama hii kwa njia ya sindano zinaruhusiwa.
3. KITANZI (INTRAUTERIE DEVICES IUD)
IUD ni kitanzi cha plastiki au metali, katika aina mbalimbali za maumbo, ambacho kinapachikwa ndani ya mji wa mimba (uterasi). Wataalam wa uganga hawajui hasa jinsi IUD inavyofanya kazi.
Kwa wakati huu kuna maoni namna mbili: namna moja inasema kwamba IUD inazuia urutubishaji wa mayai; na ile nyingine inasema kwamba inazuia yai lililoru- tubishwa kupandikizwa kwenye mji wa uzazi.
Kwa vile mimba inaanzia kwenye upandikizaji kwa mujibu wa mtazamo wa Kiislam, matumizi ya IUD kama mbinu ya kudhibiti uzazi yanaruhusiwa, bila kujali tofauti hizo hapo juu miongoni mwa wataalam wa tiba.
4. MBINU YA KIZUIZI
Mbinu za kizuizi zote zinazuia mbegu ya kiume kupenya na kuingia kwenye mji wa uzazi. Hizi zinafanyika kwa kuifunika dhakari kwa kondomu, au kwa kufunika mlango wa tumbo la uzazi kwa kiwambo, finiko ya mlango wa uzazi, au sponji ya ukeni. Matumizi ya viini vya kuulia ambavyo vinaua mbegu za kiume kabla ya hazijafika kwenye mji wa uzazi vilevile ni mbinu ya kuzuia. Zote ni namna za kudhibiti uzazi.
5. KUJIZUIA WAKATI WA KIPINDI CHA RUTUBA
Kuna taratibu aina tatu za kimsingi za kutabiri utayari wa mayai ya mwanamke, ili kuweza kujiepusha na kujamiiana wakati wa takriban siku sita za kipindi cha uwezo mkubwa sana wa kushika mimba wa mwanamke cha kila mwezi..
NJIA HIZO TATU NI KAMA ZIFUATAZO:
a.) Mbinu ya kutagwa kwa yai: Mwanamke anajifunza kutambua kile kipindi cha rutuba, yaani utayari wa yai kwa kukagua ile tofauti katika uanzaji wa kutoka kwa ute wa mlango wa uzazi.
Kutoka kwa ute wa mlango wa uzazi kunaashiria kile kipindi cha mbolea kabisa, na hivyo kujiepusha na ngono katika wakati huu kunazuia ushikaji wa mimba.
b.) Mbinu ya mfuatano maalum: Hii ni mbinu inayofanana na ile ya kwan- za, bali inategemea katika kuchunga ile mizunguko ya kila mwezi kwa mwaka mzima ili kutambua zile siku za hatari (za kuweza kushika mimba).
c.) Hali ya Joto: Katika mbinu hii, mbali na kuweka rekodi ya kalenda ya mzunguko wake, mwanamke pia anapima joto lake kila siku ili kugundua utayari wa yai. Anaweza kutambua wakati wa utayari wake wa yai wakati wowote joto lake muhimu la mwili linapoongezeka.
ANGALIZO: Njia nyingine ya kisasa zaidi ni kutabiri utayari wa mayai kwa kutumia kipimia utayari wa yai (ovulation test) ambacho kimeundwa ili kutabiri zile ziku za mbolea zaidi za kuweza
kuwa mjamzito.
6. KUTOA NA KUMWAGIA NJE (COITUS INTERRUPTUS):
Hii ina maana ya kuchomoa dhakari mara tu kabla ya kumwaga manii. Hii ilikuwa ndio mbinu ya kawaida kabisa ya kudhibiti uzazi kabla ya kugunduliwa kwa mbinu za kisasa.
Imesimuliwa kwamba Muhammad ibn Muslim na Abdur-Rahman bin Abi Abdillah Maymun walimuuliza Imam as-Sadiq (a.s.) kuhusu uchomoaji. Imam akasema: “Ni juu ya mwanaume; anaweza akamwagia popote anapotaka yeye.5
Hata hivyo, katika hadithi nyingine, Muhammad bin Muslim anasimulia kutoka kwa Imam wa tano au wa sita (a.s.) kama ifuatavyo: “Kwa upande wa mtumwa wa kike hiyo imeruhusiwa, hata hivyo, kwa upande wa mwanamke huru, mimi nalichukia hilo isipokuwa kama lilikuwa limeamuliwa hivyo wakati wa kufunga ndoa.6
Kwa kutegemea hadithi hiyo hapo juu, wengi wa Mujitahid wetu wanaami- ni kwamba kuchomoa na kumwagia nje kunaruhusiwa bali ni makruh iwapo ni bila ridhaa ya mkewe mwenyewe. 7
7. KUFISHA MBEGU (ZA UZAZI) – STERLIZATION:
Kufisha mbegu kunahusisha upasuaji kiuganga. Kufisha mbegu kwa wanaume, kunakojulikana kama kuhasi, kunahusisha utenganishaji au ufungaji wa bomba katika njia ya uzazi ya mwanaume. Bomba hili au mchirizi unapitisha manii kutoka kwenye korodani kwenda kwenye kibofu cha masalia na viungo vingine vya uzazi.
Kufisha mbegu kwa mwanamke, kunakojulikana kama kufunga kitanzi, kunahusisha uzibaji au utenganishaji wa mirija ya uzazi inayosafirisha yai.
Kufisha mbegu hakuko huru kutokana na vipingamizi, ingawaje kunaruhusiwa kama hakuambatani na mbinu zilizokatazwa zilizoonyeshwa hapo chini.8
MBINU ZILIZOKATAZWA
Mbinu yoyote ya uzazi wa mpango au kudhibiti uzazi inakatazwa chini ya mazingira yafuatayo:
a.) Pale inapoleta madhara makubwa kwenye afya ya mwanamke, kama vile kuondoa viungo fulani kama vile mifuko ya mayai ya uzazi.
b.) Wakati inapohusisha kitendo haramu, kama vile mwanaume kugusa au kuangalia kwenye sehemu za siri za mwanamke ambazo zimekatazwa au kuharamishwa juu yake kuzitazama, hapo inakatazwa.
Masharti haya yanaweza kupuuzwa tu katika mazingira yaliyozidi mno, inapokuwa ni muhimu kabisa.
MARIDHIANO KATI YA MUME NA MKE
Kwa mujibu wa mwelekeo wa kisheria wa shari’ah ya kiislam, mke anayo haki kamili ya kutumia mbinu za kudhibiti uzazi (contraceptives), hata bila kuridhia na kuruhusiwa na mume wake.9
Hata hivyo, mke huyo asije akatumia mbinu ambayo inaweza kuingilia kati haki za ndoa za mume wake. Kwa mfano, hawezi kumlazimisha kutumia kondomu au kufanya njia ya kumwagia nje au kukatiza kujamiiana.
Kanuni hii imeegemea kwenye msingi kwamba kadiri ya haki za kindoa za mume juu ya mkewe ni kwamba tu anapaswa kupatikana kwa kujinsia, mwenye kuelekea na mwenye ushirikiano.
Haki hii haiendelei kufikia ile ya kumzalia watoto. Kuzaa watoto au kutozaa ni uamuzi binafsi wa mwanamke, na kwa hiyo, anaweza kutumia njia za kuzuia uzazi kama vile vidonge, sindano au uoshaji wa uke wake baada ya kujamiiana, kwani hizo haziingilii haki za kindoa za mume wake.
Kinyume chake, mume hana haki ya kumlazimisha mke wake asibebe mimba kama akitaka kufanya hivyo, kwa kumlazimisha matumizi ya vidonge, sindano au kitanzi IDU. Hata hivyo, anaweza kutumia kondomu maadamu awe amepata ridhaa ya mkewe juu ya hilo. Kwa nyongeza, anayo haki ya kufanya hivyo kwa kutumia kumwagia nje wakati wa kujamiiana.
Kwa busara ya sawa hata hivyo, maamuzi kama hayo yanafanywa kwa ubora zaidi kwa mashauriano ya pamoja baina ya mume na mke; vinginevyo, inaweza kusababisha kutokuelewana na kutoaminiana.
Mtazamo wa kisheria ni kulinda hame za mwanamke, lakini katika dunia yenyewe, mwanaume na mwanamke lazima waweke msingi wa maisha yao juu ya upendo, huruma na ushirikiano kama ilivyoelezwa katika Surat ar-Rum; 30:21, “Naye amejaalia mapenzi na huruma kati yenu.”
KUHARIBU MIMBA (ABORTION)
Mtazamo wa Uislamu kwenye suala la kudhibiti au kupanga uzazi na kuharibu mimba ni wa sawasawa kabisa. Unawaruhusu wanawake kuzuia mimba lakini unawakataza kuikatisha. Kuharibu au kutoa mimba baada ya kupandikizwa yai la mbolea (uzazi) kwenye tumbo la uzazi kumekatazwa kabisa na kunachukuliwa kuwa ni uhalifu dhidi ya sheria ya Mwenyezi Mungu, na vile vile kosa dhidi ya hicho kijusi (foetus).
Kwa mtazamo wa kimaoni wa Uislam, uharamu wa kutoa kijusi hautegemei juu ya suala la kwamba kijusi hicho kina hali ya binadamu au hapana. Ingawa Uislam haukitambui kijusi kama binadamu kamili, bado unatoa ile haki ya uhai unaowezekana.
Utoaji mimba huwa unafikiriwa kwa sababu mbalimbli. Hizi zitajadiliwa, na mtazamo wa Kiislam katika kila sababu utaangaliwa.
1. NI UCHAGUZI KATI YA MTOTO NA KAZI NA/AU MTINDO WA MAISHA YA ANASA
Sababu hiyo hapo juu inaakisi hali ya asili ya ubinafsi wa jamii hii ya kimaada, na haichukuliwi kuwa ni sababu ya halali au yenye kukubalika kwa ajili ya utoaji wa mimba. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُمْ مِنْ إِمْلَاقٍ ۖ نَحْنُ نَرْزُقُكُمْ وَإِيَّاهُمْ ۖ {151}
“Wala msiwaue watoto wenu kwa sababu ya umasikini, Sisi tutakupeni riziki ninyi na wao …..”
(Al-An’aam; 6:151).
وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُمْ خَشْيَةَ إِمْلَاقٍ ۖ نَحْنُ نَرْزُقُهُمْ وَإِيَّاكُمْ ۚ إِنَّ قَتْلَهُمْ كَانَ خِطْئًا كَبِيرًا {31}
“Wala msiwaue watoto wenu kwa kuogopa umasikini, sisi ndio tunaowaruzuku wao na ninyi pia, kwani kuwaua ni kosa kubwa. (Al- Israa; 17:31)
Naam, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu hakutuambia sisi kuwa: “Sisi hatuikalifishi nafsi ila kwa yale iliyo na uwezo nayo.” (al- An’aam; 6:172).
2. MTOTO ANATUNGWA MIMBANI KINYUME CHA SHERIA
Haya ni matokeo ya mahusiano haramu ya kingono ambayo Uislam unayashutumu kwa nguvu zote, bali hayachukuliwi uhalali unaokubalika wa kuharibu au kukitoa kijusi.
3. MTOTO NI WA JINSIA ISIYOPENDELEWA
Sababu hii haina tofauti yoyote ya ubaya na ukatili na ile desturi ya kiarabu ya kabla ya Uislam ya kuwazika watoto wa kike wakiwa hai, na vilevile sio sababu halali ya kukubalika kwa ajili ya kutoa au kuharibu mimba.
4. MTOTO NI MATUNDA YA UBAKAJI
Wakati mwanamke anapokuwa amebakwa, anapaswa kutumia vile vidonge vya ‘asubuhi ya baada’ au RU486 mara moja tu baada ya shambulio hilo la kingono ili kuzuia uwezekano wa upandikizwaji wa mbegu ya uzazi. Hata hivyo, mara tu mimba itakapoanza, basi Uislam hauruhusu kuitoa.
Katika sababu kama hiyo, Uislam hauwezi kuhalalisha utoaji mimba ya mtoto kwa ajili ya dhambi au kosa la baba. Na kuhusu heshima ya mwanamke huyo, Uislam unawashutumu sana wale watu wanaomdharau mwathirika wa ubakaji; badala ya kumshutumu na kumtukana, wanapaswa kuwa wenye huruma juu yake.
5. MTOTO ANA MAPUNGUFU
Kwa matumizi ya vipimo vya mawimbi ya sauti (ultrasounds) na tekinolojia nyingine za kisasa kama hiyo, inawezekana kujua iwapo kama mtoto anayo mapungufu mapema kabisa kabla hajazaliwa. Watu wengine wanahalalisha kuharibiwa kwa kijusi chenye hitilafu.
Hata hivyo, Mujtahid wa wakati huu wa sasa hawaruhusu utoaji mimba wa namna hiyo, hata kama hitilafu hizo ni kubwa na mbaya sana kiasi kwamba hazitibiki baada ya kuzaliwa mtoto, na kwamba mtoto anaweza asiishi baada ya kuzaliwa isipokuwa kwa muda mfupi na kwa maumivu makali.
Wazazi wanapaswa kuomba na kutumainia afya njema ya mtoto huyo. Naam, wakati kuna bahati kwamba kijusi kinaendelea kinyume na utabiri wa kiganga. Bahati hii, kwa vyovyote itakavyokuwa finyu na isiyo na umuhimu, bado inatun- yima sisi haki ya kukatiza uhai.
6. MIMBA HIYO NI HATARI KWA MWANAMKE
Mfano pekee unaoruhusiwa, wa kutoa au kuharibu mimba ni iwapo kijusi hicho kina umri chini ya miezi minne pungufu (kabla roho haijaingia ndani yake) na madaktari wakaamua kwa uhakika wenye mantiki kwamba uendeleaji wa mimba hiyo utamdhuru mwanamke huyo, au kumsababishia matatizo kwa kiwango ambacho kwa kawaidi hakivuliki. Haiwezekani kukitoa au kukiharibu kijusi hicho baada ya miezi minne bila hata kujali sababu ya utoaji mimba yenyewe.
MALIPO YA FIDIA
Kama utafanyika utoaji mimba, yeyote atakayefanya utoaji mimba huo atakuwa anawajibika katika ulipaji wa fidia. Hii ni bila ya kujali iwapo utoaji mimba huo unafanyika kwa hiari, kwa makubaliano ya wazazi wote ama la.
Malipo hayo ya fidia yanafanya sehemu ya mali ya mtoto huyo na itak- wenda kwa warithi wake, yaani wazazi wake hata ingawa inawezekana wakawa washiriki kwenye uamuzi huo. Hata hivyo, ni jambo ambalo, wazazi wake, kama warithi wake, wanaweza kusamehe haki zao, hivyo kuondoa uwajibikaji wa malipo hayo kutoka kwa yule mtu anayefanya utoaji mimba huo.Malipo hayo ni kama ifuatavyo:10
KAMA KIJUSI HICHO NI:
Chenye umri hadi kufikia siku 40 – gramu 70 za dhahabu
Chenye umri hadi kufikia siku 80 – gramu 140 za dhahabu
Chenye umri hadi kufikia siku 120 – gramu 210 za dhahabu
Chenye umri hadi kufikia siku 160 – gramu 280 za dhahabu
KIJUSI CHENYE UMRI HADI KUFIKIA SIKU ZAIDI YA HAPO:
Kama mimba ya mtoto wa kiume inatolewa – gramu 350 za dhahabu
Kama mimba ya mtoto wa kike inatolewa – gramu 1750 za dhahabu
Kwa nyongeza, mtu lazima afanye istighfar na kuomba msamaha wa Mwenyezi Mungu Mtukufu ili kwamba ule uhai uliotolewa (kwa kuharibu mimba) usije ukatafuta kudai kurudishiwa uhai wake tena.
•    1. Sehemu kubwa imechukuliwa kutoka Mariage and Morals in Islam, Sayyid Muhammad Rizvi, Contemparary Laws cha Ayatullah Sistani, na A Code of Practice for Muslims in the West
•    2. Nahjul-Balaghah, hotuba ya 141
•    3. Suratul-A’raf; 7:172
•    4. Wasa’ilush-Shi’ah, Jz. 14, Uk. 105.
•    5. Wasa’ilush-Shi’ah, Jz. 14, uk. 105
•    6. Wasa’ilush-Shi’ah, Jz. 14, uk. 106
•    7. Sharh Lumu’ah, Jz. 2, uk.28
•    8. al-Mustahdathat min al-Masa’il al-Shar’yyah, uk. 19-20; swali la 26
•    9. Minhaj as-Salihin, Jz. 2, uk. 276
•    10. Kama ilivyotafsiriwa na Marhum Mulla Asgharali M.M. Jaffer.
ITAENDELEA KATIKA MAKALA IJAYO