KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA KWANZA)
  • Kichwa: KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA KWANZA)
  • mwandishi: Ramadhani Kanju Shemahimbo
  • Chanzo: www.islam.org
  • Tarehe ya Kutolewa: 21:12:6 10-10-1403

KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA KWANZA)
MLANGO 1: USIKU WA HARUSI (NDOA)
A’MALI ZA USIKU WA HARUSI
Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwamba: “Milango ya Peponi kwa ajili ya rehema itafunguliwa katika hali nne: Wakati inaponyesha mvua; wakati mtoto anapoangalia kwa huruma usoni kwa mzazi wake; pale mlango wa Ka’ba unapokuwa wazi, na wakati wa (kutokea) harusi.”1
Kama inavyoonyeshwa na hadithi hiyo hapo juu, dhana ya harusi katika Uislam ni tukufu mno na yenye kuthaminiwa, kiasi kwamba milango ya rehema ya Mwenyezi Mungu inafunguliwa katika tukio hili.
Naam, hili halishangazi pale mtu anapochukulia kwamba ndoa inahifadhi sehemu kubwa ya imani ya mtu na kuilinda na uovu wa Shetani, kama ilivyosimuliwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.): “Hakuna kijana yeyote atakayefunga ndoa katika ujana wake, isipokuwa kwamba shetani wake anapiga makelele akisema: ‘Ole wake, ole wake, amezikinga sehemu mbili ya tatu ya imani yake kutokana na mimi;’ kwa hiyo mwanadamu lazima awe na taqwa (mwenye kumcha Mungu) kwa Mwenyezi Mungu ili kulinda sehemu moja ya tatu ya imani yake iliyobakia.2
Ni muhimu kwa hiyo, kwamba wawili hao, pale wanapoingia kwenye hatua hii, wachukue hadhari ya hali ya juu kulinda usafi wa muungano huu mtukufu na wala wasiutie doa tangu mwanzoni mwake kwa kuruhusu lile tukio la sherehe ya harusi kuwa ni chanzo cha madhambi na israaf.
Hususan ule usiku wa harusi ndio usiku wa kwanza ambao mwanaume na mwanamke wanakuja pamoja kama mume na mke, na imekokotezwa sana kwamba wanaunda muungano huo kwa nia ya kupata ukaribu na radhi za Mwenyezi Mungu Mtukufu na kufanya zile A’amali zilizopendekezwa kwa ajili ya usiku huo.
Wakati huu ni muhimu kuangalia ni hali gani yule ‘Bibi wa wanawake wote wa ulimwengu,’ Hadhrat Fatimah (a.s.) aliyokuwa nayo ule usiku wa harusi yake, na ni vipi alianza maisha yake na mume wake, Imam Ali (a.s.): Katika ule usiku wa harusi Imam Ali (a.s.) alimuona Hadhrat Fatimah (a.s.) alikuwa amefadhaika na akitokwa na machozi, na akamuuliza kwa nini alikuwa kwenye hali ile.
Yeye alijibu akasema: “Nilifikiria kuhusu hali yangu na vitendo na nikakumbuka mwisho wa uhai na kaburi langu; kwamba leo nimeondoka nyumbani kwa baba yangu kuja nyumbani kwako, na siku nyingine nitaondoka hapa kwenda kaburini na Siku ya Kiyama.
Kwa hiyo, namuapia Mungu juu yako; njoo tusimame kwa ajili ya swala ili kwamba tuweze kumuabudu Mwenyezi Mungu pamoja katika usiku huu.”3
A’AMALI ZIFUATAZO ZINAPENDEKEZWA KWA AJILI YA USIKU HUU
A’amali Zifuatazo Zinapendekezwa Kwa Ajili Ya Usiku Huu4
1. Jaribu kuwa katika Udhuu kwa kiasi kirefu kinachowezekana cha usiku huo, na hususan wakati wa A’amal zifuatazo hapa chini.
2. Anza kwa kumtukuza Mwenyezi Mungu Mtukufu halafu useme “Allahu Akbar,” ikifuatiwa na Swala ya Mtume – Allahumma swali ‘alaa Muhammadin wa aali Muhammad).
3. Swali rakaa mbili, kwa nia ya ‘Mustahab Qurbatan ilallah’ – kujisogeza karibu na Allah (s.w.t.). (Swala inayopendekezwa kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu) ikufuatiwa na Swala
ya Mtume.
4. Soma Dua ifuatayo, ikifuatiwa na Swala ya Mtume. Kwanza bwana harusi aanze kuisoma, baada yake ambapo bibi harusi atapaswa kusema: Ilahi Amin (Mwenyezi Mungu aitakabalie Dua hii).
“Allahumma rzuqniy ilfahaa wa wudhahaa wa ridhwaahaa wa radhwiniy bihaa thumma j’ma’u bayinanaa bi-ahsani j’timaa’in wa asarri itilaafin fainnaka tuhibbul-halaala wa takrahul-haraam.”
“Ewe Allah! Nijaalie na upendo wake, mapenzi na kunikubali kwake mimi; na nifanye mimi niridhike naye, na tuweke pamoja katika namna bora ya muungano na katika muafaka kamilifu, hakika Wewe unapenda mambo ya halali na unachukia yale ya haram.”5
5. Hata kama wawili hao hawadhamirii ushika mimba katika usiku huo wa harusi, inapendekezwa kwamba Dua zifuatazo zisomwe kwa ajili ya watoto wazuri (wakati wowote itakapotunga mimba):
a. Bwana harusi anapaswa aweke kiganja cha mkono wake wa kulia kwenye paji la uso la bibi harusi kwa kuelekea Qibla na asome:
“Allahumma bi-amaanatika akhadhtuhaa wa bikalimaatika stahlaltuhaa fain qadhwayta liy minhaa waladaan faaj’alhu mubaarakaan taqiyyan min shiy’ati aali Muhammad wa laa taj’al lil-shaytwaani fiyhi shirkaan wa laa naswiybaan.
“Ewe Allah! Nimemchukua (binti) huyu kama amana Yako na nimemfanya halali juu yangu mwenyewe kwa maneno Yako. Kwa hiyo, kama umenikadiria mtoto kutokana naye, basi mfanye mbarikiwa na mchamungu kutoka miongoni mwa wafusi wa familia ya Muhammad; na usimfanye Shetani kuwa na sehemu yoyote ndani yake.”6
b. Dua ifuatayo pia inapaswa kusomwa:
“Allahumma bi-kalimaatika stahlaltuhaa wa bi-amaanatika akhadhtuhaa. Allahumma-j’alhaa waluwdaan waduwdaan laa tafraku taakulu mimmaa raaha wa laa tas-alu ‘ammaa saraha.”
“Ewe Allah! Nimemfanya awe halali juu yangu kwa maneno Yako, na nimemchukua katika amana Yako. Ewe Allah! Mjaalie awe mwenye kuzaa na mwenye upendo.”7
6. Bwana harusi aioshe miguu ya bibi harusi na anyunyize maji hayo katika pembe zote nne za chumba na nyumba. Mwenyezi Mungu Mtukufu ataondoa aina 70,000 za umasikini, aina 70,000 za neema zitaingia ndani ya nyumba hiyo na neema 70,000 zitakuja juu ya bibi na bwana harusi. Bibi harusi atakuwa salama kutokana na wendawazimu, vidonda vya tumbo na ukoma.8
MAMBO KADHAA KUHUSU ‘AQD NA NDOA
Mambo Kadhaa Kuhusu ‘Aqd Na Ndoa 9
1. Mtu anapaswa kujiepusha na kufanya Aqd au ndoa wakati wa Qamar dar Akrab – pale mwezi unapopita kwenye eneo la ng’e (scorpio). **
**Kanuni hii haiungwi mkono na Shi’a wote – Mtarjuma.
2. Mtu sharti ajiepushe kutokana na kufanya Aqd au ndoa nje chini ya mwanga wa jua.
3. Inapendekezwa kwamba Aqd na ndoa zifanywe wakati wa usiku.
Dokezo: Ni muhimu kukumbuka kwamba lengo kuu la ndoa ni kumuun- ganisha mwanaume na mwanamke. Mara nyingi sana harusi zinazofanyi- ka leo hii huwa ni ndefu sana na zenye kuchosha kwa bibi na bwana harusi; wanafika chumbani kwao usiku sana wakiwa hawana nguvu za kufaa kwa ajili ya A’amali zilizopendekezwa kwa ajili ya usiku huu mtukufu, wala nyingine zaidi. Kwa hiyo, inapendekezwa kwamba taratibu za usiku huu zinawekwa rahisi na kwa kiwango kidogo kabisa. Kama sherehe nyingine zinahitajika, basi zipaswe kufanyika katika usiku uliotangulia au unaofuata ule wa harusi.
BAADHI YA MAMBO KWA AJILI YA BIBI NA BWANA HARUSI
1. Sio lazima kwamba kujamiiana kwa kutimiza ndoa kufanyike katika ule usiku wa harusi; bali unaweza kuchukua siku chache au hata majuma machache.
2. Uchovu, wasiwasi na fadhaa vinaweza kufanya hilo liwe gumu zaidi; hivyo ni muhimu kwamba mume na mke wachukue muda wa kutosha kuweza kuwa wametulizana na kuzoeana na kwenda kwa mwendo wao wenyewe.
3. Mafuta ya kulainishia yanaweza yakahitajika kwa siku zile chache za mwanzo au majuma ili kufanya kule kujamiiana kuwa rahisi zaidi na kwenye starehe zaidi.10
4. Kumaliza mapema au kusikotarajiwa kunaweza kuwa ni tatizo kwa mara chache za mwanzoni; hata hivyo, hili linapaswa kutatuliwa baada ya kupita muda na kupatikana uzoefu.
5. Kizinda (cha bikra) kinaweza kivuje au kisivuje damu. Unyegereshano, upole na kuingiliana tena mara tu baada ya hapo kunaweza kupunguza maumivu ya uchanikaji wa hicho kizinda.
6. Baada ya kujamiiana (wakati wowote itakapokuwa), bibi harusi asije akatumia maziwa, siki, giligilani, tuhafa chungu au tikitimaji kwa kiasi cha juma moja, kwani vinasababisha tumbo la uzazi kukauka na kuwa la baridi na gumba. Kula siki wakati huu vilevile kunatokezea kwa mwanamke kutokuwa msafi (tohara) kutokana na damu ya hedhi, giligilani (na tikitimaji) kunasababisha matatizo ya wakati wa uchungu na tuhafa linasababisha kusimamisha ukawaida wa hedhi, na yote haya yanaishia kwenye kuleta maradhi.11
7. Watu wanaweza wakatoa maoni fulani juu ya siku chache zinazofuatia. Ni muhimu sana kufanya hilo lisikuathiri wewe, na usivutike kwenye mazungumzo yao.
8. Usizungumze kuhusu mambo yako ya ndani kwa watu wa nje, chunga heshima kwa mwenza wako na kwenye uhusiano wenu.
HARUSI YA IMAM ALI (A.S.) NA HADHRAT FATIMAH (A.S.)
‘AQD (MKATABA WA NDOA)
Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipenda hotuba ya ndoa isomwe msikitini na mbele ya mahudhurio ya watu. Imam Ali (a.s.) alikwenda pale msikitini kwa furaha sana, na Bwana Mtume (s.a.w.w.) vilevile akaingia msikitini mle. Muhajirina na Ansari wakakusanyika kuwazunguka. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akenda juu ya mimbari na baada ya kumtukuza na kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema:
“Enyi watu! Jueni kwamba Jibril amenishukia mimi na kuniletea ujumbe kutoka kwa Allah (s.w.t.). kwamba sherehe za ndoa ya Ali (a.s.) zimefanyika mbele ya Malaika huko ‘Bait al-Ma’mur.’
Mwenyezi Mungu Mtukufu ameamuru kwamba mimi nifanye sherehe hizi hapa duniani na niwafanye nyote nyie kuwa mashahidi.” Kufikia hapa, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasoma hotuba ya ndoa (‘Aqd).
Halafu Mtume (s.a.w.w.) akamwambia Imam Ali: “Simama na utoe hotuba.” Imam Ali (a.s.) aliianza hotuba yake na akaonyesha kufurahi na kuridhika kwake kwa ndoa yake na Hadhrat Fatimah (a.s.).
Watu wakamuombea yeye na wakasema: “Mwenyezi Mungu Mtukufu aibariki ndoa hii, na aweke mapenzi na usuhuba ndani ya nyoyo zenu.”12
HARUSI YENYEWE
Sherehe za harusi zilifanyika mnamo mwezi mosi Dhul Hijjah, mwaka wa pili Hijiria13 (au tarehe 6 ya Dhul Hijjah, 2 A.H.)14 mwezi mmoja baada ya hotuba ya ndoa.
Muda kati ya hotuba ya ndoa na sherehe za harusi, Imam Ali (a.s.) alikuwa ana haya ya kuongea kuhusu mke wake kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Siku moja, kaka yake, Aqiil, alimuuliza: “Kwa nini humleti mke wako nyumbani ili tuweze kukupongeza kwa ajili ya shughuli ya kufunga ndoa kwako?” Jambo hili lilimfikia Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), ambaye alimwita Imam Ali (a.s.) na kumuuliza: “Je, uko tayari kwa kufunga ndoa (kuoa)?”
Imam Ali (a.s.) alitoa jibu la kukubali. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Insha’allah, leo usiku au kesho usiku, mimi nitafanya maandalizi kwa ajili ya harusi.” Wakati huo, yeye Mtume (s.a.w.w.) akawaambia wake zake wamvalishe Hadhrat Fatimah (a.s.) na kumtia manukato na kuweka mazulia kwenye chumba chake ili kujiandaa kwa ajili ya sherehe za harusi.15
Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akamwambia Imam Ali (a.s.): “Hapawezi kuwa na harusi bila ya wageni.” Mmoja wa viongozi wa Ansari aliyeitwa Sa’ad akasema: “Mimi nakuzawadia kondoo mmoja,” na kikundi cha Ansari nao vilevile wakaleta kiasi16 cha nafaka,17 na maji ya maziwa yaliyoganda, mafuta na tende pia vililetwa kutoka masokoni. Nyama hiyo ilipikwa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) pamoja na usafi wake alichukua jukumu la kupika kwa ajili ya harusi hiyo, na kwa mikono yake iliyobarikiwa, akavichanganya (viungo) na akaanza kutengeneza aina ya chakula cha kiarabu kinachoitwa Habis au Hais.18
Hata hivyo, ingawa chakula kilitayarishwa, mwaliko ulikuwa wa jumla. Idadi kubwa ya watu ilishiriki na kwa baraka za mikono ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), kila mmoja alikula na akashiba kutokana na chakula hicho, na kulikuwa na kingine kamwe kilichobakia kwa ajili ya masikini na wenye shida; sinia la chakula vile vile liliwekwa kwa ajili ya bibi na bwana harusi.19
Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliwaambia wake zake waandae sherehe kwa ajili ya Hadhrat Fatimah (a.s.). Baada ya chakula, wanawake hao walijiku- sanya karibu na Hadhrat Fatimah (a.s.) na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akamsaidia kupanda juu ya farasi wake Mtume mwenyewe.
Salman al- Farsi alizikamata hatamu za farasi huyo na kwa sherehe hiyo maalum, wanaume majasiri kama vile Hamza na idadi kadhaa ya wana familia na maharimu wa Hadhrat Fatimah (a.s.) wakajikusanya karibu ya farasi huyo wakiwa na panga zilizochomolewa. Wanawake wengi walisubiri nyuma ya bibi harusi na wakasoma Takbira.
Farasi akaanza kutembea, na wale wanawake wakaanza kusoma Takbira na sifa za Mwenyezi Mungu Mtukufu Kwa wakati ule, mmoja baada ya mwingine, walisoma qaswidah nzuri na, tamu ambazo zilikuwa zimetung- wa kwa utukufu na shangwe, wakampeleka bibi harusi nyumbani kwa bwana harusi. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) vilevile alilikuta kundi hilo na akaingia chumbani kwa maharusi.
Aliitisha karai la maji, na wakati lilipo- letwa, yeye akanyunyiza kiasi juu ya kifua cha Hadhrat Fatimah (a.s.) na akamwambia atawadhe na kuosha kinywa chake kwa yale maji yaliyobakia. Alinyunyiza kiasi juu ya Imam Ali (a.s.) pia na akamwambia atawadhe na kuosha kinywa chake.
Kisha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akachukua mkono wa Hadhrat Fatimah (a.s.) na akauweka kwenye mkono wa Imam Ali (a.s.) na akasema: “Oh, Ali! Ubarikiwe wewe; Allah (s.w.t.). amemuweka juu yako binti ya Mtume wa Allah, ambaye ndiye mbora wa wanawake (wa ulimwengu).”
Kisha akaongea na Hadhrat Fatimah (a.s.) na akasema: “Oh, Fatimah! Ali ni kutoka kwa wabora wa waume.”20
Kisha akawaombea Dua juu yao: “Ewe Allah, wafanye wazoeane (wakaribiane) na kila mmoja wao! Ee Allah, wabariki hawa! Na weka neema kwa ajili yao katika maisha yao.”
Wakati alipokaribia kuondoka, yeye akasema: “Mwenyezi Mungu Mtukufu amekufanyeni ninyi na kizazi chenu kuwa tohara. Mimi ni rafiki wa marafiki zenu, na ni adui wa maadui zenu. Sasa nakupeni mkono wa kwaheri na kukukabidhini kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu”21
Asubuhi iliyofuata, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alikwenda kumuona binti yake. Baada ya kuwatembelea huku, yeye hakwenda tena nyumbani kwao kwa muda wa siku tatu, bali akaenda katika siku ya nne.22
MATAKWA YA HADHRAT KHADIJA (A.S.)
Katika ule usiku wa harusi ya Hadhrat Fatimah (a.s.), Asma bint Umais (au Umm Salama) ambaye alikuwa miongoni mwa wanawake hao, aliomba ruhusa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kama angeweza kukaa karibu na Hadhrat Fatimah ili aweze kutekeleza mahitaji yoyote atakay- oweza kuwa nayo. Alimwambia Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Wakati wa kifo cha Hadhrat Khadija ulipofika hapo Makkah, mimi nilikuwa karibu naye na niliona kwamba Khadija alikuwa analia.
Nilimuuliza: “Wewe ni ‘Bibi wa wanawake dunia zote’ na mke wa Mtume (s.a.w.w.) na licha ya yote hayo bado unalia ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu amekupa habari njema za peponi?”
Hadhrat Khadija alijibu: “Silii kwa sababu ya kifo; bali mimi ninalia kwa ajili ya Fatimah ambaye ni msichana mdogo, na wanawake katika usiku wa harusi wanahitaji mwanamke kutokana na ndugu zao na wale wa karibu (maharimu) watakaoweza kuwaambia wao siri zao zilizofichika, na nina- hofia kwamba usiku huo, kipenzi changu Fatimah hatakuwa na mmojawapo.”
Kisha nilimwambia Khadija kwamba: ‘Ninaapa kwa Mola wangu kwamba kama nitabakia kuwa hai mpaka siku hiyo, usiku huo mimi nitakaa ndani ya nyumba hiyo mahali pako (badala yako).’ Sasa ningeomba ruhusa kutoka kwako kwamba unisamehe ili niweze kutimiza ahadi yangu.’”
Baada ya kuyasikia haya, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alianza kulia na aka- nipa ruhusa kubakia na akaniombea Dua. 23
SUTI YA HARUSI YENYEWE
Katika ule usiku wa harusi ya Imam Ali (a.s.) na Hadhrat Fatimah (a.s.), Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimpa binti yake suti (vazi) ya harusi ya kuvaa usiku ule. Wakati Hadhrat Fatimah (a.s.) alipokuwa amekwenda kule kwenye nyumba ya harusi na pale alipokuwa ameketi kwenye mkeka wa kuswalia ili kumuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu mara akatokea mtu mwenye shida kwenye mlango wa nyumba ya Hadhrat Fatimah (a.s.) na kwa sauti kubwa akasema: “Kutoka kwenye mlango wa nyumba ya utume, mimi ninaomba suti ya zamani, chakavu.”
Kwa wakati ule, Hadhrat Fatimah (a.s.) alikuwa na suti mbili, moja iliyochakaa na nyingine bado mpya. Yeye alitaka kutoa ile suti ya zamani kulingana na maombi ya yule mtu mwenye haja wakati ghafla alipokum- buka aya inayosema: “Humtapata uchamungu mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda mno…..”24 Hadhrat Fatimah (a.s.) ambaye alijua kwamba anaipenda ile suti mpya zaidi, alifanya kulingana na aya hii na akatoa ile suti mpya kumpa yule mtu mwenye haja.
Siku iliyofuata, wakati Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipoiona ile suti ya zamani mwilini mwa Hadhrat Fatimah (a.s.), yeye alimuuliza: “Kwa nini hukuvaa ile suti mpya?”
Hadhrat Fatimah akajibu: “Niliitoa kumpa mtu mwenye haja.” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Kama ungevaa ile suti mpya kwa ajili ya mumeo ingekuwa vizuri na yenye kufaa sana.” Hadhrat Fatimah (a.s.) ali- jibu akasema: “Hili nimejifunza kutoka kwako.
Wakati mama yangu Khadija alipokuja kuwa mke wako, alitoa utajiri wake wote kwenye mkono mtupu uliokuwa kwenye njia yako, ilikuwa haina kitu, hadi ikafikia mahali wakati alipokuja mtu mwenye shida kwenye mlango wa nyumba yako na kuomba nguo. Kukawa hamna nguo ndani ya nyumba yako hivyo ukavua shati lako na ukampatia yeye, na ndipo ikashuka aya hii: “Wala usiufanye mkono wako kama uliofungwa shingoni mwako, wala usiukunjue kabisa, usije ukakaa hali ya kulaumiwa (na) kufilisika ukajuta.”25
Akiwa amezidiwa na mshangao kwa upendo na uaminifu wa binti yake Zahraa (a.s.), Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) yalimdondoka machozi kutoka machoni mwake, na kama ishara ya upendo, yeye alimshikilia Hadhrat Fatimah (a.s.) kifuani kwake (s.a.w.w.).26
•    1. A Bundle of flowers, Uk. 149
•    2. Muntakhab Mizan al-Hikmah, Jz.. 1, Uk.457
•    3. Kitab al-Irshad, Jz. 1, Uk. 270
•    4. Halliyatul-Muttaqin, uk. 116-117
•    5. Al-Kafi, Jz. 3, uk. 481
•    6. Al-Kafi, Jz. 5, uk. 500
•    7. Al-Kafi, Jz. 5, Uk. 501
•    8. Wasail ash-Shi’a, Jz. 20, Uk. 249, hadithi ya 25555
•    9. Halliyatul-Muttaqin, uk. 108-109 (nukta ya 1-3)
•    10. Pasukh be Masa’il-e Jinsii wa Zanashuii, Uk.235
•    11. Wasa’il ash-Shi’a, Juz. 20, Uk. 250 hadithi ya 25556
•    12. Bihar al-Anwar, Juz. 43, Uk.. 120 na 129
•    13. Bihar al-Anwar, Juz. 43, Uk.. 92
•    14. Baadhi wamesimulia kwamba ule wakati baina ya ndoa na harusi kuwa ni mwaka mmoja)
•    15. Bihar al-Anwar, Juz. 43, Uk. 130-131
•    16. Takriban ratili 8
•    17. Bihar al-Anwar, Juz. 43, Uk 137
•    18. Bihar al-Anwar, Juz. 43, Uk 106 na 114
•    19. Manaqib ibn Shahr Ashub, Juz.3, Uk. 354
•    20. Izdawaaj Maktab Insaan Saazi, Juz. 2, Uk. 300
•    21. Manaqib ibn Shahr Ashuub, Juz. 3, Uk. 3554-355
•    22. Manaqib ibn Shahr Ashuub, Juz. 3, Uk. 356
•    23. Sar Guzashthaaye Hadhrat Ali (a.s.) wa Fatimah (a.s.), Uk.30
•    24. Surat al-Imran; 3:92
•    25. Surat al-Isra; 17:29
•    26. Sar Guzashthaaye Hazrat Ali wa Fatimah (a.s.), uk. 31

ITAENDELEA KATIKA MAKALA IJAYO