YENYE KUHATARISHA NYUMBA (4 )
  • Kichwa: YENYE KUHATARISHA NYUMBA (4 )
  • mwandishi: Ummu Nassra
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 18:55:45 2-10-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

YENYE KUHATARISHA NYUMBA ( 4 )
MCHANGANYIKO WA WANAUME NA WANAWAKE
Moja katika jambo linaloonekana ni la kawaida hasa katika majumba yetu ni michanganyiko ya wanaume na wanawake (Ikhtilaatw). Ni wajibu wa kila Muislamu kuelewa hukumu ya kisheria juu ya jambo hili. Ikhtilaatw ni kuchanganyika kwa wanawake na wanaume waliokuwa sio maharim ima kwa wingi au uchache katika sehemu moja. Hali hii imezoeleka sana majumbani mwetu, katika shughuli zetu zikiwa ni za furaha au misiba au hata siku za kawaida.

Tuelewe kuwa mijumuiko ya aina hii na kudhihirika mapambo ni kitu kilichokatazwa katika sheria kwa sababu huwa ni mzizi wa fitina na ni kichochezi cha maasia mengine kwani shaytwan huwa pamoja nao. Katika hadithi iliyosimuliwa na 'Umar, Radhiya Llahu 'Anhu inatueleza:
Kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Hachanganyiki mwanamume na mwanamke ila shaytwaan huwa ni watatu wao. [At-Tirmidhiy]
Dini yetu imetuwekea adabu maalum; na kama kuna ulazima wa kuchanganyika majumbani, basi ni vyema kuwe na sehemu tofauti kati ya wanaume na wanawake pindi wakikujia kwao. Tunatakiwa tuwe na hadhari tunapotembelewa na mgeni, hata kama ni ndugu wa mume au mke. Mtume Swalla Llahu 'Alayhi wa Ssalaam aliwaeleza maswahaba zake na Waislamu wote kuwa: Tahadharini kuingilia majumbani mwao wanawake; Wakasema: Ewe Mjumbe wa Allaah, je, vipi kuhusu shemeji? Akasema: Shemeji ni mauti Al-Bukhaariy na Muslim]

Pia Allaah Subhanahu wa Taala anatueleza katika Suuratul Al-Ahzaab: 53
Nanyi mnapowauliza (wakeze) waulizeni nyuma ya pazia. Kufanya hivyo kunasafisha nyoyo zenu za zao. Ni jukumu letu kama ni wazazi kuzielewa sheria hizi na kuzidi kuzipamba nyumba zetu katika mandhari nzuri ya kiislam. Hii itasaidia hata na vizazi vyetu kuinukia kwa maadili na tabia njema na kujua mipaka yao. Na kama itatokea kwa mwanamme au mwanamke kutembea au kutembelewa na kukutana na mwenyeji wa jinsia tofauti basi na tumuogope Allaah na kujihifadhi kwa kadiri ya uwezo wetu, bila ya kurefusha mazungumzo.

Allaah Alietukuka Anatufahamisha katika Suuratu Nnuur:30-31

Wambie waumini wanaume wainamishe macho yao (wasitazame yaliyokatazwa) na wazilinde tupu zao hili ni takaso kwao; bila ya shaka Allaah anazo habari za wanayoyafanya. Na wambie waumini wanawake wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao, wala wasidhihirishe viungo vyao isipokuwa vinavyodhihirika.
MWISHO