KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA PILI) B
  • Kichwa: KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA PILI) B
  • mwandishi: Ramadhani Kanju Shemahimbo
  • Chanzo: www.islam.org
  • Tarehe ya Kutolewa: 20:59:45 13-9-1403

KUANZIA NDOA HADI KUWA WAZAZI (SEHEMU YA PILI)
MLANGO WA 2: TARATIBU ZA KUJAMIIANA KATIKA UISLAM NO: 2
VITENDO VISIVYOPENDEKEZWA KATIKA TENDO LA NDOA
VITENDO VINAVYOLETA KARAHA (MAKRUUH)
1. LIWATI!

Kuna baadhi ya Wanavyuoni wanaosema kuwa Liwati inaruhusiwa kwa ridhaa ya mke, lakini ni kauli zisizo na nguvu, na pia ni kitendo kinachochukiwa sana!

Zayd ibn Thabit anasimulia kwamba mtu mmoja alimuuliza Imam Ali (a.s.): “Je, unaweza kumsogelea mkeo nyuma kwake?” Imam Ali (a.s.) akajibu akasema: “Likatae, lichukie hilo liwe kinyaa kwako! Mwenyezi Mungu anakushusha kwa njia hii (ya kumwingilia mwanamke). Hukuyasikia maneno ya Mola Wako kwamba imesimuliwa kutoka kwa Lut ambaye alisema kuwaambia kaumu yake:

وَلُوطًا إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ أَتَأْتُونَ الْفَاحِشَةَ مَا سَبَقَكُمْ بِهَا مِنْ أَحَدٍ مِنَ الْعَالَمِينَ {80}

“Kulikoni! Mnafanya uchafu ambao hajakutangulieni yeyote kwa (ufasiki) huo katika walimwengu? (Al-A’araf; 7:80). 1

Kuna baadhi ya watu wanaolihalalisha tendo hili kwa kutumia aya ya Qur’ani Tukufu ifuatayo:

نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ ۖ {223}

“Wanawake ni mashamba yenu, basi yaendeeni mashamba yenu kwa namna muitakayo …”
(Al-Baqarah; 2:223).

Hata hivyo, Imam as-Sadiq (a.s.), katika tafsiri yake juu ya aya hiyo ya Qur’ani hapo juu anasimulia kwamba: “Madhumuni ya aya hii ni kwamba kujamiiana hakuna budi kufanyika kutokea mbele, kwani sababu ambayo kwamba mwanamke katika aya hii amefananishwa na shamba linalotoa mavuno (kutokea juu ya udongo) ambao ni kama tu kule mbele kwa mke kwa sababu huku ndiko ambako kwamba mtoto hutokea kupatikana na kuja ulimwenguni humu.”2
Abuu Basiir anasimulia kwamba yeye alimuuliza Imam kwamba ni nini hukmu ya mtu anayemwendea mke wake nyuma. Imam alilichukulia tendo hili kutokubalika na akasema: “Kaa mbali na nyuma kwa mkeo, na maana ya aya hii tukufu ya Surat al-Baqarah hapo juu sio kwamba unaweza kumwingilia mkeo kutokea popote unapotaka, bali haswa ni kwamba huna budi kufanya ngono, na kwa hiyo maana ya aya hiyo ni kumkurubia mkeo kwa wakati wowote uupendao kufanya hivyo.”3
2. KUWA NA QUR’ANI AU MAJINA YA ALLAH (S.W.T.) MWILINI MWAKO

Imesimuliwa kutoka kwa Ali, mtoto wa Imam as-Sadiq (a.s.): Nilimuuliza ndugu yangu Imam Kadhiim (a.s.): “Je, mtu anaweza kujamiiana na akaenda bafuni wakati akiwa na pete mkononi mwake yenye jina la Allah au aya ya Qur’ani iliyoandikwa juu yake?” Imam alijibu akasema: “Hapana – hilo ni makuruhu.”4
3. KUFANYA MAPENZI (NGONO) KWA KUSIMAMA WIMA

Inasimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Mume na mke wasije wakajamiiana kama punda wawili waliong’ang’aniana pamoja, kwa sababu kama ikiwa namna hiyo, malaika wa rehma watakaa mbali nao na neema ya Mwenyezi Mungu itaondolewa kutoka kwao.5
4. KUJAMIIANA WAZI (BILA KUJIFUNIKA NGUO)

Imesimuliwa kwamba Muhammad ibn al-Ais alimuuliza Imam as-Sadiq (a.s.): “Je, inaruhusiwa kumwendea mke wangu nikiwa uchi kabisa (yaani kujamiiana bila kujifunika)?” Imam alijibu akasema: “Hapana, usifanye jambo kama hilo…..”6
5. KUSHUGHULIKA NA NGONO CHINI YA ANGA

Imesimuliwa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.): “Allah anazichukia tabia 24 kwa ajili yenu, enyi watu, na amekukatazeni kutokana nazo; moja ya tabia hizi ni kujamiiana chini ya anga.”7
6. KUSHUGHULIKA NA KUJAMIIANA PANAPOKUWA NA WATU WENGINE (NA WANAWEZA KUWASIKIA NA/AU KUWAONA) NDANI YA NYUMBA

Imesimuliwa kutoka kwa Imam al-Baqir (a.s.): “Ni makuruhu kwamba mtu ashughulike katika kujamiiana na mke wake kama, pamoja na kuwepo kwao, kuna mtu mwingine pia ndani ya nyumba hiyo.8

Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Twaeni tabia tatu kutoka kwa kunguru; kujamiiana kwa siri, kwenda kutafuta riziki mwan- zoni mwa asubuhi, na akili na hadhari dhidi ya hatari zinazoweza kujitokeza.” 9
7. KUJISHUGHULISHA NA KUJAMIIANA MBELE YA MTOTO MDOGO

Imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s.): “Mtume amekataza kwamba mtu amwendee mke wake (kwa ajili ya kujamiiana) na mtoto katika susu lake anaweza kuwaona. 10

Imesimuliwa kutoka kwa Imam al-Baqir (a.s.): “Epukana na kujamiiana katika sehemu ambayo panaweza kuwa na mtoto anayeweza kuwaoneni.11

Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Jiepushe na kwenda kulala (kwa ajili ya kujamiiana) na mke wako wakati ambapo mtoto anaweza kuwaoneni, kwani Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alijua sana hasa kwamba kitendo hiki ni Makruhu na cha kuaibisha sana.”12
8. KUSHUGHULIKA NA KUJAMIIANA NDANI YA JAHAZI, UFUKWENI 63AU BARABARANI

Imesimuliwa katika hadithi kwamba kujamiiana ndani ya jahazi au barabarani kunaishia kwenye laana ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na ya Malaika kuwa juu yako mtu.13

Imesimuliwa katika hadithi nyingine kutoka kwa as-Sakuni kwamb Imam Ali (a.s.) aliwapita wanyama wawili waliokuwa wakijamiiana mahali njia ya watu wengi. Imam aligeuka mbali nao.

Ikaulizwa: “Ewe Amirul-Mu’minin, kwa nini uligeukia pembeni mbali nao?” Imam (a.s.) akajibu akisema: “Sio sahihi kwamba mkaribiane katika njia ya watu kama wanyama hawa; kitendo kama hicho kimekatazwa na kifanyike mahali ambapo si mwanaume au mwanamke awezaye kuona.” 14
9. KUELEKEA, AU MTU KUKIPA MGONGO QIBLAH

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amekataza watu kujamiiana wakati wakiwa wameelekea Qiblah, au mtu mgongo wake kuelekea Qiblah, na amesema kwamba endapo kitendo kama hicho kikifanyika, kinaleta matokeo ya laana ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na Malaika na wanadamu wote kuwa juu yako mwenye kufanya hivyo.15

Dokezo: Ikiwa pale unapokaa wima kutoka kwenye hali ya kulala, uso wako unaelekea Qiblah, hii inafahamika kama kuelekea Qiblah, na kinyume chake (yaani na mgongo pia).
10. KUKATAA KUJAMIIANA (KWA SABABU MBALIMBALI)

Imesimuliwa kutoka kwa Imam al-Baqir (a.s.): Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alisema kuwaambia wanawake: “Msirefushe Swala zenu kiasi kwamba ikawa ni kisingizio cha kutokwenda kulala (kwa ajili ya kujamiiana) na waume zenu.”16
NYAKATI ZINAZOPENDEKEZWA
NYAKATI ZA WAJIBU
1. IKIWA KUNA HOFU YA HARAMU (ILIYOKATAZWA)

Endapo mtu anahofia kwamba anaweza kushindwa na tamaa zake za kingono na minong’ono ya Shetani na akaweza kujiingiza katika vitendo vya haramu, ni wajibu kwamba wajichunge na wajilinde nalo hili.17

Kama mtu yuko peke yake, ni lazima afunge ndoa na hivyo kujiweka mbali na vitendo vyovyote vinavyowezekana kuwa vya haramu (vilivyokatazwa).

Imesimuliwa kutoka kwa Ayatullah Khomeini (r.a.) “Ni faradhi kwa mtu ambaye, kwa sababu ya kutokuwa na mke ataangukia kwenye haram, afunge ndoa.” 18
2. MARA MOJA KWA KILA MIEZI MINNE

Mtu ni lazima apate kujamiiana na mkewe kijana angalau mara moja katika miezi minne. Hii ni moja ya haki za ndoa za mke na wajibu huo unabaki kufanya kazi isipokuwa ima kama una madhara kwa mume, unahusika na kutumia jitihada za ziada zisizo za kawaida, au mke kusamehe haki yake au masharti ya awali kama hayo yalikuwa yamewekwa na mume wakati wa kufunga ndoa. Haina tofauti kama mume yuko mbali safarini ama yupo nyumbani.

Safwan ibn Yahya alimuuliza Imam ar-Ridhaa (a.s.): “Mtu anaye mke kijana na akawa hajamkaribia kwa kiasi cha miezi, au hata mwaka. Sio kwa sababu anataka kumtaabisha yeye (kwa kukaa mbali naye), bali hasa ni janga fulani limewashukia. Je, hili linahesabiwa kama ni kosa?”

Imam akajibu akasema: “Endapo atamwacha kwa kiasi cha miezi minne, hilo linahesabiwa kama
ni dhambi.”19
NYAKATI ZINAZOPENDEKEZWA (MUSTAHAB)

Kujamiiana, kama kutafanywa katika namna inayoruhusiwa, basi wakati wote kunakuwa ni mustahabu. Hata hivyo, kuna nyakati ambazo kunapendekezwa zaidi.

1. Wakati mke anapokuhitaji kutoka kwa mumewe.
2. Wakati mume anapokuwa amevutiwa na mwanamke mwingine.20

Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.) “Mtu yoyote atakayeona mwanamke na akavutiwa naye ni lazima aende kwa mke wake na aka- jamiiane naye, kwa sababu kile ambacho yule mwanamke mwingine ana- cho, na mke wako pia anacho, na mtu asimwachie nafasi Shetani katika moyo wake.

Na endapo mtu hana mke, ni lazima aswali Swala ya rakaa mbili, amtukuze sana Allah (s.w.t.). na kumswalia Mtume – kumtakia rehma yeye na kizazi chake na amuombe Mwenyezi Mungu amjaalie kumpa mke muumini na mchamungu, na kwamba Yeye Allah (s.w.t.). amfanye asiwe mwenye kuhitaji yaliyoharamishwa.21
NYAKATI ZISIZOPENDEKEZWA
NYAKATI HARAM – ZINAZOKATAZWA

1. WAKATI WA HEIDHI (SIKU ZA MWEZI ZA MWANAMKE):

Allah (s.w.t.). anaeleza ndani ya Suratul-Baqarah, aya ya 222 kama ifuatavyo:

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ ۖ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ ۖ {222}

“Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie: Huo ni uchafu, basi jitengeni na wanawake (wakiwa) katika hedhi. Wala msiwaingilie mpaka watakapotoharika …..” (Al-Baqarah; 2:222).

Endapo mtu anayejamiiana na mke wake akagundua kwamba kipindi chake cha hedhi kimeanza, basi na ajiondoe na kujitenga naye mara moja.

Ndani wa kipindi cha hedhi, vitendo vingine, mbali na kujamiiana vinaruhusiwa kufanyika kama inavyoonyeshwa na hadithi ifuatayo hapa chini:

Mu’awiyah ibn Umar anasimulia kwamba, yeye alimuuliza Imam as-Sadiq (a.s.): “Ni nini kinachoruhusiwa kwa mwanaume wakati mwanamke anapokuwa kwenye hali ya hedhi?”
Imam akajibu akasema: “Mbali na sehemu zake za siri (yaani, mwili wote uliobakia isipokuwa sehemu zake za siri tu). 22

Imran ibn Qanzali anasimulia kwamba yeye alimuuliza Imam as-Sadiq (a.s.): “Ni vipi mwanaume anavyoweza kufaidika kutoka kwa mwanamke ambaye yuko kwenye hali yake ya hedhi?” Imam akajibu akasema: “Yale mapaja mawili (ya mwanamke huyo).” 23

Hata hivyo, ingawa mwili wote uliobakia, wa mwanamke (ukiachilia mbali sehemu zake za siri) unaruhusiwa kwa mume, lile eneo tokea kitovuni hadi magotini ni makuruhu (haipendekezwi kufikiwa);24 kwa hiyo inashauriwa sana kwamba mume azikwepe sehemu hizi vile vile.

Ni muhimu kutambua kwamba haipendekezwi kujishughulisha na ngono baada ya kwisha kwa hedhi. Hata hivyo, kama ni lazima, mwanamke anapaswa kuoga kwanza.25

Mwenyezi Mungu analieleza hili katika muen- delezo wa aya hiyo hapo juu: “Na wanapokuwa tohara, basi waingilieni kama alivyokuamuruni Mwenyezi Mungu.” (Al-Baqarah; 2:222).

2. Wakati wa Nifaas 26

3. Wakati wa kufunga katika mwezi wa Ramadhani.27

4. Wakati katika hali ya Ihraam na kabla ya kuswali swala ya Tawafun Nisaa.28

5. Pale ambapo inaweza kusababisha madhara makubwa kwa amma mwanaume au mwanamke. Kujamiiana kunaruhusiwa endapo hakuwezi kuleta madhara makubwa.29

REJEA:

    1. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 144, namba 25258
    2. Wasailush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 134, numba 25253
    3. Wasailush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 147, namba 25266
    4. Wasailush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 148, namba 25271
    5. Ibid., Juz. 20, Uk. 120, namba 25190
    6. Ibid., Juz. 20, Uk. 137, namba 25238, na uk. 138, namba 25239
    7. Niyazha wa Rawabith Jinsii was Zanaashuii, Uk. 61
    8. Wasailush-Shi’a, Juz. 12, Uk. 380, namba 16565
    9. Wasailush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 133, namba 25227
    10. Wasailush-Shi’a, Juz. 12, Uk. 382, namba 16568
    11. Wasailush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 134, namba 25229
    12. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 132, namba 25222
    13. Ibid., Juz. 20, uk. 138, namba 25240
    14. Ibid., Juz. 20, Uk. 133, namba 25226
    15. Ibid., Juz. 20, Uk. 138, namba 25240
    16. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 20, Uk. 164, namba 25317
    17. Hili limethibitishwa pamoja na ofisi ya Ayatullah Sistanii, Qum
    18. Niyaazhaa wa Rawabith Jinsii was Zanaashuii, uk. 71
    19. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 21, Uk. 458 namba 27573
    20. Niyaazhaa wa Rawabith Jinsii was Zanaashuii Uk k. 71
    21. Niyaazhaa wa Rawabith Jinsii was Zanaashuii, Uk. 48-49
    22. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 2, Uk k. 321, hadith namba 2249
    23. Wasa’ilush-Shi’a, Juz. 2 Uk k. 322, hadith namba 2254
    24. Halliyatul-Muttaqin, uk. 109
    25. Niyaazhaa wa Rawaabith Jinsii was Zanaashuii, Uk. 72
    26. Islamic Laws (Shari’ah ya Kiislam) Kanuni namba 520
    27. Islamic Laws (Shari’ah ya Kiislam) Kanuni namba 1593
    28. Hajj Manaasik, Kanuni ya 219
    29. Imethibitishwa na ofisi ya Ayatullah Sistani, Qum.

ITAENDELEA MAKALA IJAYO