WAISLAMU NA UMOJA WAO
  • Kichwa: WAISLAMU NA UMOJA WAO
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 21:49:17 6-10-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

WAISLAMU NA UMOJA WAO

Kikao cha 23 cha kimataifa cha Umoja wa Kiislamu ambacho kinawashirikisha wasomi, wanafikra na wanazuoni wa Kiislamu wapatao 500 kutoka pembe mbalimbali za dunia kilicho anza Machi Pili mjini Tehran Iran na kuendelea hadi Alkhamisi Machi Nne, ikiwa ni katika siku za kuadhimisha Wiki ya Umoja wa Kiislamu.

Kikao hicho kilifunguliwa rasmi kwa hotuba ya Ayatullah Hashimi Rafsanjani, Mkuu wa Majlisi ya Kumchagua Kiongozi Mkuu wa mfumo wa Kiislamu wa Iran ambaye pia ni Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu nchini Iran. Kikao hicho cha siku tatu ambacho kinawajumuisha wanafikra na wasomi wa Kiislamu kutoka humu nchini na pembe nyinginezo za dunia kitajadili masuala na changamoto mbalimbali zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu na hasa kuhusiana na suala la kuimarisha umoja na mshikamano kati ya wafuasi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu chini ya anwani isemayo: "Umma wa Kiislamu, Tokea Madhehebu Tofauti hadi Mielekeo ya Kimakundi."

Tunaashiria hapa kuwa, ushirikiano wa kimadhehebu, mitazamo tofauti, ushirikiano wa wafuasi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu, masuala yanayochangia kutokea madhehebu tofauti, athari za mielekeo ya kimakundi, dhamana za kuendelea ushirikiano wa madhehebu ya Kiislamu ikiwemo ijtihadi, kudumishwa moyo wa udugu na umoja, njia za kuondokana na migawanyiko ya kimakundi, kuimarishwa utamaduni wa umoja kutoka kwa wasomi wa umma wa Kiislamu na njia za kufikiwa lengo hilo pamoja na mifano ya kihistoria ya kudhihiri makundi katika umma wa Kiislamu ni miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa na washiriki wa kikao hiki cha Tehran.

Profesa Burhan ad-Deen Rabbani, Rais wa zamani wa Afghanistan, Maulawi Is'haq Madani, Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Taasisi ya Kimataifa ya Kukurubisha pamoja Madhehebu ya Kiislamu, Dakta Adil Fallah, Naibu Waziri wa Masuala ya Wakfu wa Kuwait, Dakta Nur Ali Adam, Waziri wa Wakfu wa Somalia, Abdul Hadi Avang, Mkuu wa Chama cha Kiislamu cha Malaysia na Hujjatul Islam wal Muslimeen Muhammad Hassan Akhtari, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Ahlul Beit (as) ni miongoni mwa shakhsia na wanafikra mashuhuri wa Kiislamu wanaoshiriki katika kikao hicho. Ujumbe wa Dakta Abdul Aziz Tuweijiri, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Sayansi, Elimu na Utamaduni ya Umoja wa Nchi za Kiislamu Isesco pia itasomwa katika kikao hicho.

Mwishoni mwa kikao hicho, Muhammad Ali Tashkhiri, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Kukurubisha pamoja Madhehebu ya Kiislamu pia amepangiwa kuzungumzia athari na matokeo ya kikao hiki kinachoendelea mjini Tehran.

MWISHO