SHEREHE ZA KRISMAS
  • Kichwa: SHEREHE ZA KRISMAS
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 22:26:14 6-10-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

SHEREHE ZA KRISMAS

Katika moja ya hotuba zake za swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Omar bin Khattab huko Doha nchini Qatar, Sheikh Yusuf Qardhawi amezungumzia masuala matatu muhimu yanayowahusu Waislamu. Ameanza kwa kuzungumzia kuenea kwa madhihirisho ya sherehe za Kikristo za Krismasi nchini Qatar na kukosoa vikali tabia ya Waislamu ya kujishughulisha na sherehe hizo zisizoambatana na utamaduni wa Kiislamu.

Sheikh huyo amesikitishwa mno na tabia hiyo na kuuliza maswali mengi kwa kusema; Je, sisi tunaishi katika jamii ya Kiislamu au Kikristo? Ni sherehe gani hizi zinazofanyika katika mitaa na maduka kwa jina la sikukuu ya Kikristo au Krismasi, ni kana kwamba sisi tunaishi katika mojawapo ya nchi za Ulaya zinazofuata mafundisho ya Kikristo? Huku akiashiria kumalizika hivi karibuni tu kwa idi kubwa ya Waislamu ya Adh'ha, na kutofanyika sherehe kubwa kama hizo zinazoonekana hivi sasa za Krismasi nchini Qatar, Sheikh Yusuf Qardhawi ameashiria kuwepo hitilafu kubwa miongoni mwa Wakristo wenyewe kuhusiana na iwapo kweli Nabii Isah (as) au kwa jina jingine, Yesu, alizaliwa tarehe 25 Disemba au tarehe 7 Januari.
Alisema hitilafu hizo pia zinahusiana na iwapo Yesu alizaliwa katika msimu wa joto au wa baridi. Hata hivyo ameashiria aya ya Qur'ani Tukufu kuhusiana na uzawa wa Isah Masih (as) na kusema kuwa kwa mujibu wa aya hiyo, mtukufu huyo alizaliwa katika msimu wa joto ambapo tende zilikuwa zikivunwa.

Sheikh Qardhawi ametumia fursa hiyo kuwakosoa vikali baadhi ya Waislamu wenye misimamo ya kupindukia mipaka katika nchi za Qatar, Saudi Arabia na nchi nyinginezo za Kiislamu, wanaopinga kufanyika sherehe za kuadhimisha uzawa wa Mtume Mtukufu (saw) katika tarehe aliyoitaja kuwa ni 12 Rabiul Awwal na kujiuliza ni kwa nini wanazuoni wanaochukua msimamo kama huo mkali hawashughulishwi na sherehe hizo za Krismasi katika nchi za Kiislamu wala kuchukua hatua za kuzuea kuenea kwake katika jamii za Kiislamu?

Aliuliza, ni kwa nini wanaruhusu kufanyika sherehe hizo zisizo za Kiislamu katika nchi za Kiislamu na kuzuia kufanyika sherehe halali za maulidi ya Mtume katika nchi hizo? Sheikh Yusuf Qardhawi ameendelea kusema kuwa tunashuhudia kuenea kwa madhihirsho kama hayo hasi na ya kusikitisha yanayodhoofisha misingi ya imani ya Kiislamu miongoni mwa jamii za Kiislamu na kuongeza kuwa hayo yote yanafanyika katika hali ambayo tunashuhudia nchi za Magharibi zikizuia kujengwa kwa minara ya misikiti katika nchi hizo.
Amesema kuwa hivi karibuni pia tutashuhudia nchi hizohizo zikichukua hatua za hata kuzuia ujenzi wa misikiti katika nchi hizo. Sheikh Qardhawi amehoji, iwapo Waislamu wanaweza kuruhusiwa kufanya sherehe zao kubwa za idi katikati ya miji ya nchi za Magharibi kama wanavyoruhusiwa kufanya Wakristo katika kitovu cha Bara Arabu ambalo ni susu la Uislamu duniani. Sheikh Qardhawi amesema kwamba madhihirisho hayo ya Kikristo katika nchi za Kiislamu ni haramu na aibu na jambo lisilofaa kuonekana kabisa katika nchi za Kiislamu. Amesema kuwa sherehe hizo ni ishara ya fikra finyu, ujahili na jambo linalogongana moja kwa moja na misingi ya Kiislamu.
Katika hutuba zake za swala hiyo ya Ijumaa, Sheikh Qardhawi amefasiri maana ya maneno Bismillah ar-Rahman ar-Raheem na Rab al-Aalamin na kusema kuwa maneno hayo yanaashiria kuwa Mwenyezi Mungu ni wa walimwengu wote na sio kama wanavyodai Mayahudi katika kuhalalisha misimamo yao ya kibaguzi kwamba Mungu ni wao peke yao.

Kama inavyofanyika miaka yote nchini Qatar katika kukaribia siku ya kuzaliwa Nabii Isah (as) au siku ya Krismasi, Doha, mji mkuu wa nchi hiyo, mwaka huu pia imebadlika na kuwa kama moja ya miji ya Kikristo ya Magharibi, ambapo maduka mengi makubwa na madogo katika mji huo yamejaa zawadi, vifaa na miti ya Krismasi iliyopambwa kwa namna tofauti. Mazingira hayo ya uhuru wa kijamii na kidini kwa Wakristo yanameandaliwa sambamba na kuwepo nchini humo kwa idadi kubwa ya wageni na hasa Wakristo kutoka Ulaya, Marekani na Kusini mwa Asia, hali ambayo imepelekea raia wa Qatar kuhisi kuwa ni wachache, kijamii na kidini, katika nchi yao wenyewe.
Kila mwaka baadhi ya wahubiri na mashekhe wa Qatar huzungumzia suala hilo kwa woga na kwa hali isiyoweza kuathiri lolote kupitia magazeti na kisha kusahaulika kabisa. Ni muhimu kuashiria hapa kwamba, licha ya kuwa Qardhawi amezungumzia kwa masikitiko makubwa jambo hilo, lakini hadi sasa hakuna shekhe mwingine yoyote kati ya mashekhe wanaochaguliwa na Wizara ya Wakfu ya Qatar, ambaye amejitokeza na kukosoa hali hiyo.

Kuhusiana na Rais Barrack Obama wa Marekani, Sheikh Qardhawi amewataka watu kutochukua misimamo ya pupa na ya kupindukia mipaka kuhusiana na siasa zake na kuwataka wasubiri na kutathmini rekodi yake kutokana na utendaji wake.

MWISHO