MBINU ZA MAADUI KUZUSHA FITINA
  • Kichwa: MBINU ZA MAADUI KUZUSHA FITINA
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 22:38:50 6-10-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

MBINU ZA MAADUI KUZUSHA FITINA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo amehutubia umati mkubwa wa maelfu ya wanafunzi wa vyuo vya kidini, maulamaa, walimu na maimamu wa swala za jamaa wa misikiti ya Tehran kwa mnasaba wa kukaribia mwezi wa Muharram akisema kuwa ulinganiaji sahihi ni kuwazindua wananchi na kuwawezesha kumaizi mambo katika jamii hususan katika kipindi cha fitina.

Ayatullah Khamenei ameashiria matukio ya baada ya uchaguzi wa Rais hapa nchini hususan hatua ya hivi karibuni ya maadui wa taifa la Iran ya kumvunjia heshima Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu na akawashukuru wananchi kwa kuwa macho na kujitokeza kwa wingi kupinga kitendo hicho.

Vilevile amewataka wananchi wote kuwa watulivu hususan tabala la wanafunzi wa vyuo vikuu. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa jengo hili imara ambalo uhandisi wake ni wa Mwenyezi Mungu, umetayarishwa na rijali wa Mwenyezi Mungu na litabakia kwa himaya ya taifa linalomwamini Mwenyezi Mungu, litabakia imara daima na maadui hawatafikia malengo yao.

Ayatullah Ali Khamenei ameashiria matukio ya baada ya uchaguzi wa Rais hapa nchini na akasema inasikitisha kwamba baada ya uchaguzi huo baadhi ya watu walivunja sheria na kuanzisha ghasia na kutayarisha uwanja uliowapa matumaini maadui waliokuwa wamekata tamaa kiasi cha kuthubutu kumvunjia heshima Imam Khomeini mbele ya macho ya wanafunzi wa vyuo vikuu wafuasi wa Imam, Mapinduzi na mfumo wa Kiislamu hapa nchini.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa kitendo hicho cha kumuvunjia heshima Imam ni matokeo ya ukiukaji huo wa sheria na kuridhishwa na uungaji mkono wa vyombo vya habari vya wageni, na baada ya makosa hayo kutukia zinafanyika jitihada za kuyaficha kwa kutoa visingizio mbalimbali.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa visingizio hivyo vinavyotolewa baada ya makosa ya mara kwa mara ndio sababu kuu ya fitina na machafuko. Amesema baadhi ya watu wachache wanatoa madai ya kuheshimu sheria na wakati huo huo wanakiuka sheria. "Kundi hilo linatoa nara za kumuunga mkono na kumfuata Imam Khomeini lakini linafanya mambo ambayo yanapelekea kutendwa uhalifu mkubwa wa kumvunjia heshima Imam na kuwafurahisha maadui wanaochukua maamuzi dhidi ya maslahi ya kitaifa na taifa la Iran kutokana na kuchambua hali hiyo", amesisitiza Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa mtu anayefanya kazi kwa ajili ya Uislamu, Mapinduzi na Imam anapotambua kuwa maneno na harakati zake zinawapa fursa maadui huzinduka mara moja na kurekebisha mwelekeo wake.

Amehoji kwamba, ni kwa nini mabwana hawa hawazinduki? Amesema kuwa wakati kipengee cha Uislamu kinapotolewa kwenye kaulimbiu kuu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yaani "Kujitawala, Uhuru, Jamhuri ya Kiislamu" mabwana hawa wanapaswa kuzinduka na kuelewa kwamba wamekwenda mrama; na wakati zinapozotolewa kauli zinazodhamini maslahi ya utawala ghasibu wa Israel na dhidi ya Palestina katika Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo ilianzishwa kwa lengo la kutetea Palestina na kukabiliana na utawala wa Kizayuni, mabwana hawa wanapaswa kuamka na kujitenga kabisa na mrengo huo.

Kiongozi Muadhamu ameendelea kuhoji kuwa, ni kwa nini mabwana hawa hawaamki wakati viongozi wa dhulma na ubeberu ambao kielelezo chake ni Marekani, Ufaransa na Uingereza, wanapowaunga mkono? Ni kwa nini hawazinduki wanapoungwa mkono na mafuska waliokimbia nchi na wanaotaka kurejesha utawala wa kifalme na wala hawaelewi kwamba wameingia katika njia ya makosa?

Ayatullah Khamenei amewataka mabwana hao kufungua macho na kujitenga na mrengo huo. Amesema kuwa kupuuza ukweli huo ni kinyume cha akili na mantiki. Amesisitiza kuwa akili na mantiki inahukumu kwamba badala ya kukanusha asili ya tukio la kuvunjiwa heshima Imam Khomeini wanapaswa kulaani hatua hiyo na kuelewa vyema malengo ya adui.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa ndugu zetu hawa wa zamani ambao walipata majina na umashuhuri kutokana na Mapinduzi ya Kiislamu, ni kwa nini hawafungui macho na kuona jinsi maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu na Imam Khomeini wanavyofurahishwa na maneno na hatua zao na kuwapongeza kwa kuwapigia makofi huku wakibeba juu picha zao?

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa uchaguzi wa Rais wa Juni 12 ulifanyika kwa mujibu wa sheria na haukuwa na tatizo lolote na kusisitiza kuwa kushikamana na sheria kunatulazimisha kwamba hata kama hatumkubali Rais aliyechaguliwa na wananchi lakini tunapaswa kuheshimu sheria.

Akiashiria matukio ya kujitenga baadhi ya waliokuwa wafuasi wa Imam Khomeini katika kipindi cha uhai wake na kutupiliwa mbali kwao na taifa, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema masuala hayo yanapaswa kuwa ibra na mafunzo kwetu sote. Amesisitiza tena juu ya udharura wa kufanyika juhudi za kuwaunganishwa zaidi wananchi wa matabaka yote na kujiepusha na mfarakano na akasema kuwa hata hivyo inaonekana kuwa baadhi ya watu wanataka wenyewe kujitenga na mfumo wa Kiislamu na kutupiliwa mbali.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa idadi ndogo ya watu waliochochewa na matamshi na harakati za baadhi ya wengine na kupata ujasiri wa kusimama dhidi ya mfumo wa Kiislamu si lolote wala chochote mbele ya adhama ya taifa la Iran. Amesema mfumo wa Kiislamu hapa nchini ni utawala uliosimama kwenye misingi ya mafundisho ya Mwenyezi Mungu na katika kipindi chote cha miaka 30 iliyopita Mwenyezi Mungu Muweza ameonyesha rehema na nusura yake kwa mfumo huu wa Kiislamu. Amesisitiza kuwa: "Iwapo tutakuwa pamoja na Mwenyezi Mungu basi hapana shaka Yeye pia atakuwa pamoja nasi".

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema maadu wa mfumo wa Kiislamu na mabeberu wanaotaka kuidhibiti dunia kwa kutumia mantiki isiyokuwa sahihi watapata kipigo kutoka kwa taifa hili na mataifa mengine huru. Amesisitiza kuwa maadui hawa bado hawajayatambua vyema Mapinduzi ya Kiislamu, hayati Imam Khomeini, taifa shujaa la Iran na vijana wa taifa hilo na akasema kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu wa sasa ni miongoni mwa wanafunzi bora zaidi katika masuala ya kielimu na kiroho na daima wamekuwa macho katika medani mbalimbali na kutekeleza vyema maukumu yao.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hasira na kuchikizwa matabaka mbalimbali ya wananchi kutokana na kuvunjiwa heshima Imam Khomeini na akapongeza hatua yao ya kulaani na kukemea kitendo hicho. Hata hivyo amesisitiza juu ya udharura wa kulindwa utulivu na amani na kuelewa kwamba wale wanaosimama mkabala wa taifa la Iran hawana msingi na asili na wala hawana ubavu wa kuendelea kukabiliana na adhama ya taifa la Iran na Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa iwapo italazimu viongozi na walinzi wa sheria watatekeleza wajibu wao. Amesema, pamoja na hayo wanafunzi wa vyuo vikuu wanawajibika kuwatambua watu ambao ndio vyanzo na sababu za maovu na uhalifu na kuwaarifisha kwa wenzao lakini kazi zote hizo zinapaswa kufanyika kwa utulivu.

Ayatullah Khamenei amesema wadhifa mkubwa kwa hivi sasa ni kulinda amani na usalama na akaongeza kuwa maadui wanaozusha ghasia na machafuko wanakabiliana na wananchi, na vyombo vya sheria vinawajibika kuchukua hatua. Ameongeza kuwa maadui wa taifa la Iran na utawala wa Kiislamu ni mithili ya povu juu ya maji ambalo hatimaye litatoweka na mfumo wa Kiislamu utabakia hai.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia matukio matatu muhimu ya Mubahala, mwezi wa Muharram na siku ya umoja wa vyuo vya kidini na vyuo vikuu na akasema kuwa ujumbe mkuu wa mambo hayo matatu ni kulingania uhakika na kuwaelimisha wananchi. Amesema kuwa katika siku ya tukio la Mubahala (ambapo Mtume alifanya mdahalo na Manasara wa Najran) mtukufu huyo alifuatana na watu azizi na vipenzi vyake kwa ajili ya kuwaelimisha watu na kumaizi baina ya haki na batili. Vileve katika siku ya Ashura, Imam Hussein amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake aliingia katika medani ya vita akiwa pamoja na vipenzi vyake azizi kwa lengo hilo hilo na akalingania haki na kweli kwa maneno na matendo na kwa kutoa gharama kubwa mno.

Ayatullah Khamenei amesema lengo la umoja kati ya vyuo vikuu vya kidini (hauza) na vyuo vikuu vingine ni kujenga mshikamano halisi na kutumia uwezo wa kimaada na kimaanawi wa majmui hizo mbili zenye taathira kubwa. Amesisitiza kuwa lengo kuu la mnasaba huo pia ni kulingania ujumbe wa Mwenyezi Mungu na kufikisha hakika kwa watu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa misingi mikuu ya ulinganiaji ni kuwa na maarifa, yakini na matendo na akaongeza kuwa katika suala la kulingania haki kuna udharura wa kuwa na maarifa, imani na yakini kwa ujumbe unalinganiwa ili uweze kufanyiwa kazi na ulinganiaji huu hutambuliwa kuwa ni amali njema.

Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa mwezi wa Muharram ni fursa nzuri ya ulinganiaji sahihi na kuweka vigezo katika jamii hususan katika zama za fitina. Amesema kuwa katika dunia ya sasa ambako msingi wa kazi za maadui wa haki na hakika ni kuzusha fitina, msingi wa kazi za wafuasi wa kweli na hakika unapaswa kuwa juu ya maarifa na kuongoza watu.

Akibainisha masharti mawili makuu ya ulinganiaji, Ayatullah Khamenei amesema, ulinganiaji na kubainisha ukweli unapofanyika katika njia ya Mwenyezi Mungu, kwa ikhlasi na bila ya kumuogopa asiyekuwa Mola Muumba kama watawala waovu na wenye nguvu, hapana shaka kwamba utakuwa na matunda mazuri. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewausia mahatibu katika mwezi wa Muharram kuzingatia maelekezo ya Imam Khomeini kuhusu jinsi ya kuzungumzia tukio hilo na kubainisha masaibu ya Imam Hussein (as) kwa kutumia mbinu za kijadi.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa kuzungumzia masaibu yaliyompata Imam Hussein na wafuasi wake katika siku ya tarehe kumi Muharram ni kujenga mfungamano wa kiroho na mawalii wa Mwenyezi Mungu na msingi wa thamani wa uhusiano wa kifikra na kimatendo na maarifa ya kidini. Amesema kuwa mfungamano huo wa kiroho kwa hakika ndiyo mapenzi yaliyozungumziwa katika Qur'ani Tukufu na iwapo mapenzi hayo hayatakuwapo basi uongozi wa Kiislamu na utiifu kwa kiongozi pia hautakuwapo; na katika hali hiyo yumkini maafa yaliyoupata umma wa Kiislamu katika zama za awali kutokana na kutupilia mbali mapenzi hayo, yakatukia tena.

Amesisitia tena juu ya udharura wa kuzungumzia tukio la Ashura na mauaji ya Imam Hussein (as) na kuwakosoa wale wanaohoji umuhimu wa suala hilo na kulia kwa sababu ya masaibu yaliyowapata watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw). Hata hivyo amewataka wananchi kujiepusha na baadhi ya ada mbaya na zisizokuwa sahihi katika kuhuisha tukio hilo la kuuawa shahidi Imam Hussein na wafuasi wake kama kujiumiza kwa visu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ameendelea kuzungumzia umuhimu wa kulingania dini na kueleza ukweli na uhakika akiashiria matukio ya kipindi cha Mtume Muhammad (saw) na zama za Khalifa wake wa haki Imam Ali bin Abi Twalib (as). Amesema kuwa katika kipindi cha Mtukufu Mtume juhudi kubwa zaidi za kuwazindua watu zililenga kundi la wanafiki, na changamoto kubwa zaidi ya zama za Imam Ali bin Abi Twalib ilikuwa kukabiliana na watu waliodai kuwa ni Waislamu ambao walipotoka njia sahihi kutokana na kuweka mbele matamanio yao ya kinafsi.

Ayatullah Khamenei amesema hali hiyo huwa ngumu na ya kutatanisha na watu wa kawaida hushindwa kubaini ukweli wa mambo huku kundi la wasomi na tabaka makhsusi likipatwa na shaka. Amesisitia kuwa shaka hiyo ya wasomi na watu wa tabaka makhsusi hutafuna nguzo za harakati ya jamii ya Kiislamu kama anavyofanya mchwa.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa suala hilo ni moja ya matatizo ya sasa ya jamii ya kimataifa na kuongeza kuwa maadui wanatumia nyenzo zote kwa ajili ya kutia tashwishi katika fikra za watu katika uga wa kimataifa ikiwa ni pamoja na kutoa madai ya kuheshimu sheria, kutetea haki za wanadamu na kuwatetea wanaodhulumiwa.

Ayatullah Khamenei ameashiria hotuba iliyotolewa siku chache zilizopita na Rais wa Marekani akidai kwamba nchi zinazokiuka sheria zinapaswa kuwajibika na akahoji: "Ni serikali ipi inayokiuka sheria zaidi kuliko Marekani ambayo iliivamia Iraq kwa kutumia urongo na kuwasababishia wananchi wa nchi hiyo masaibu makubwa? Ameuliza kwamba serikali ya Marekani inatumia sheria ipi kuendeza uvamizi na kuikalia kwa mabavu Iraq, na ni kwa kutumia sheria gani inazidisha idadi ya askari wake huko Afghanistan na kuendelea kuua wananchi wasiokuwa na hatia wa nchi hiyo?

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa serikali ya Marekani ndio kielelezo halisi cha ukiukaji wa sheria duniani japokuwa kidhahiri inatenda kwa namna nyingine. Amesema kuwa hii ndiyo maana ya fitina. Amesema kwamba njia pekee ya kukabiliana na mwenendo huu wa uozo na uvundo wa maovu ambao unafanya jitihada za kupenya katika fikra za walimwengu kwa kutumia nyenzo mbalimbali, ni kuwazindua watu na kubainisha ukweli na uhakika wa mambo. Amesisitiza kuwa kazi hiyo ni nzito na ngumu.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa moja ya mbinu zinazotumiwa kuzusha hitilafu kati ya Waislamu ni kueneza hitilafu za kimadhehebu na amesisitiza kuwa njia pekee ya kuzuia hitilafu za kimadhehebu ni kuwa na maarifa, kuwazindua wananchi, ulinganiaji sahihi na kutotumbukia katika mtego wa adui.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Muqtadai, Mkuu wa Hauza na Chuo Kikuu cha Kidini cha Qum ametoa hotuba fupi akisema kuwa kulingania maarifa ya Ahlubaiti wa Mtume Muhammad (saw) Uislamu sahihi na njia ya Imam Khomeini ndio nguzo kuu za harakati na shughuli za vyuo vikuu vya kidini.

MWISHO