GHADIR IZINGATIWE
  • Kichwa: GHADIR IZINGATIWE
  • mwandishi: BARAZA
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 19:21:1 1-10-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

GHADIR IZINGATIWE

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alipokutana na maelfu ya wananchi wa matabaka mbalimbali waliokwenda kuonana naye kwa mnasaba wa sikukuu ya Ghadiri Khum (siku Imam Ali bin Abi Twalib alipotawazwa rasmi na Mtume wa Mwenyezi Mungu kuwa Imam na kiongozi wa umma wa Kiislamu baadaye yake) alisema kuwa suala la Ghadir ni kigezo cha milele cha Mwenyezi Mungu kinachoainisha njia sahihi ya umma wa Kiislamu.

Ayatullah Khamenei ameashiria urongo mkubwa unaoenezwa na Wazayuni na nchi za kigeni kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran kwa shabaha ya kupotosha fikra za walimwengu na akasema kuwa urongo huo utawafedhehesha zaidi maadui wa taifa la Iran baada ya kudhihiri ukweli wa mambo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewapongeza wananchi wa Iran na Waislamu wote ulimwenguni kwa mnasaba wa sikukuu ya Ghadir. Akifafanua sababu ya sikukuu hiyo kuitwa sikukuu kubwa zaidi ya Mwenyezi Mungu (Idullahil Akbar), Ayatullah Khamenei amesema, tukio la Ghadiri Khum lilikuwa na maana kubwa zaidi kuliko idi na sikukuu nyingine za Kiislamu, kwani kwa mujibu wa vigezo vya Mwenyezi Mungu, wajibu wa Waislamu kuhusu uongozi na serikali uliainishwa katika siku hiyo.

Ameashiria aya za Qur'ani kuhusu kukamilishwa dini ya Uislamu katika tukio la Ghadir na kukata tamaa na matumaini kwa maadui na makafiri baada ya tukio hilo na akasema, tangazo la uongozi wa Imam Ali bin Abi Twalib na kuchaguliwa kwake kuwa Kiongozi wa Waumini na Khalifa wa Mtume (saw) kwa hakika ulikuwa uteuzi wa Mwenyezi Mungu, na Nabii Muhammad (saw) alikamilisha ujumbe wake kwa kufikisha tangazo hilo kwa walimwengu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amefafanua sababu za kuteremshwa baadhi ya aya za Qur'ani Tukufu na haditi zenye kutegemewa za Kiislamu na akasema kuwa Imam Ali bin Abi Twalib (as) ndiye aliyekuwa mbele na juu zaidi katika elimu, takwa, kujitolea, jihadi, kutoa mali katika njia ya Mwenyezi Mungu na kadhalika katika historia ya Uislamu baada ya Mtume Mtukufu. Ayatullah Khamenei amewataka Waislamu kote duniani kutalii na kusoma kwa kina uhakika huo.

Ayatullah Ali Khamenei amekariri tena wito wa siku zote wa umoja na mshikamano kati ya Wislamu unaotolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akasema: "Hatusisitizi kuwa kundi moja la Kiislamu linapaswa kukubali itikadi za kundi jingine, lakini tuna takwa la kimantiki nalo ni kwamba, Waislamu wote duniani wasome na kutaamali uhakika na ukweli ulioandikwa na maulamaa wakubwa kama Allamah Sayyid Sharafuddin Amili na Allamah Amini kuhusu Amirul Muuminina Ali bin Abi Twalib (as).

Amesema kuwa kipindi cha ujana cha Imam Ali (as) kilichojaa matukufu ni kigezo kamili cha vijana na ameyataka matabaka yote kuiga na kufuata mwenendo wa Imam huyo katika vipindi mbalimbali vya maisha.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa Ushia ni madhehebu inayotokana na itikadi sahihi na halisi ya wahyi wa Mwenyezi Mungu na thamani na vigezo vya Qur'ani. Ameashiria propaganda chafu na tuhuma nyingi zinazodai kuwa Ushia ni madhehebu ya kubuni au ya kisiasa na akasisitiza kuwa suala la Ghadir ambalo ni miongoni mwa masuala yaliyothibitishwa katika historia ya Kiislamu, linabatilisha tuhuma hizo na kueleza waziwazi asili na misingi ya Ushia.

Akieleza sababu za propaganda chafu dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, Ayatullah Khamenei amesema kuwa mabeberu duniani wanaelewa vyema kwamba taifa la Iran linaloshikamana vilivyo na Uimamu, limetimiza ndoto na matarajio ya Waislamu wote na wanafikra wanaojua matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu kwa kuasisi serikali ya Kiislamu, na kwa msingi huo wanafanya jitihada za kuidhihirisha jamii kubwa ya Mashia kuwa si jamii ya Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa Marekani ndiye kinara wa maadui wa taifa na Uingereza ndiye adui habithi zaidi wa Iran. Amesisitiza kuwa Wazayuni, Wamarekani na mabeberu wengine wanakasirika mno kwa kuliona taifa la Iran likiwa kigezo cha kuigwa na vilevile mwamko wa sasa wa umma wa Kiislamu na kwa sababu hiyo wamefanya njama na hila za aina mbalimbali katika kipindi chote cha miaka 30 ya baada ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini kwa lengo la kulitenga taifa hili lakini wameshindwa.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria urongo unaoenezwa na Wazayuni na wageni kuhusu kadhia ya nishati ya nyuklia nchini Iran na kasema: "Maadui wa taifa la Iran wamefikia kiwango cha kutumia uongo kwa ajili ya kupotosha na kuzihadaa fikra za walimwengu lakini hatimaye uongo huo utawadhuru wao wenyewe baada ya kudhihiri uhakika wa mambo na kuwafedhehesha zaidi kama ilivyokuwa huko nyuma.

Ayatullah Khamenei amewausia viongozi wa serikali za Marekani, Uingereza na baadhi ya nchi za Magharibi wajiepushe na kusema uongo na akaongeza kuwa: "Kama tulivyosema mara kwa mara, taifa la Iran linataka kupata elimu inayohitajiwa na nchi katika medani ya nyuklia na linaamini kuwa iwapo halitapata elimu na teknolojia hiyo hivi sasa litakuwa limechelewa kesho wakati uchumi wa dunia nzima utakapokuwa ukiendeshwa kwa kutumia nishati ya nyuklia.

Amesema kuwa wananchi wa Iran leo hii wanafanya jitihada za kupata teknolojia ya nyuklia ili wana wa nchi hii na kizazi kijacho cha Iran kisiwanyooshee mkono wa haja Wamagharibi baada ya miaka 20 au 30 ijayo. Amesisitiza kuwa Wamagharibi wanafanya njama za kulizuia taifa kufikia lengo hilo la kitaifa kwa kutumia makele ya kipropaganda, tuhuma na uongo.

Akijibu nara zilizokuwa zinatolewa na wananchi kwamba "Nishati ya nyuklia ni haki isiyokanushika ya Iran", Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka wananchi kuwa macho na wasiruhusu mabeberu wa dunia kutumia nyenzo mbalimbali za kisiasa na kipropaganda kulinyima taifa la Iran haki yake katika medani ya nishati ya nyuklia.

Ayatullah Khamenei ameeleza siasa zinazotumiwa kwa sasa za mabeberu na akasema kuwa madhalimu wa kimataifa wanaposhindwa kukabiliana na taifa fulani kwa kutumia vitisho vya mashambulizi ya kijeshi na vikwazo, hutumia visingizio mbalimbali kwa ajili ya kuzusha hitilafu na uhasama ndani ya taifa hilo.

Amesema kuwa maadui wameelekeza juhudi zao katika propaganda na michezo michafu ya kisiasa kwa ajili ya kuzusha hitilafu na mifarakano nchini. Ameongeza kuwa tunapaswa kutambua jinsi adui anavyotumia vibaya maneno na mambo yanayozusha hitilafu. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa baadhi ya watu wanapaswa kujibu mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kufanya mambo yanayotumiwa na adui kudai kuwa kuna hitilafu za ndani na kumtia kiburi.

Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa wananchi wa Iran ni wavumilivu, wenye ghera na msimamo imara. Ameongeza kuwa viongozi wa ubeberu wanadai kuwa subira na uvumilivu wao umefika ukingoni japokuwa dunia nzima inaelewa kuwa mabeberu hao hawajawahi kuwa na subira kuhusu Iran na katika kipindi cha miaka 30 iliyopita walifanya kila walilotaka na kutekeleza njama zote za kisiasa, kiuchumi, kijeshi na kipropaganda dhidi ya taifa la Iran.

Ayatullah Ali khamenei amesema kuwa subira na msimamo imara wa taifa la Iran ndio msingi wa kuendelezwa njia ya ustawi na maendeleo ya nchi. Amesisitiza kuwa taifa lenye uvumilivu la Iran linapuuza makelele ya kipropaganda ya nchi za kigeni kama ilivyokuwa huko nyuma na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na hima ya vijana wake, litaendeleza njia lililoonyeshwa na Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu kwa kuwa macho na kujenga mustakbali unaong'ara zaidi.

MWISHO