GHADIR NA SUALA LA UMOJA
  • Kichwa: GHADIR NA SUALA LA UMOJA
  • mwandishi: NDUGU ZETU WA KIISLAMU
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 17:39:32 20-10-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

GHADIR NA SUALA LA UMOJA

Kitabu cha 'al-Ghadir' kilizusha wimbi kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Kitabu hicho kimewapelekea wasomi na wanafikra wa Kiislamu kukichambua katika mitazamo mbalimbali ya fasihi, historia, itikadi, hadithi, tafsiri na jamii. Jambo linaloweza kuzingatiwa kwa uwazi zaidi katika mtazamo wa kijamii kuhusiana na kitabu hicho ni uzito wa umoja wa Kiislamu unaotiliwa mkazo na kitabu hicho muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu.

Wahubiri, wasuluhishi, wanafikra na wasomi wa Kiislamu, kwa karne nyingi sasa wamekuwa wakichambua na kuzungumzia umuhimu wa kuwepo umoja na mshikamano kati ya mataifa, jamii na makabila mbalimbali ya Kiislamu na hasa katika zama hizi ambapo maadui wa Waislamu wanawahujumu kutokea kila upande na kwa kutumia zana na silaha mbalimbali hatari.

Kwa kuendesha hujuma hiyo, maadui wana lengo la kuwatawanya na kuwasambaratisha Waislamu kupitia uchochezi wa hitilafu kongwe na nyingine zinazozushwa katika zama hizi. Kwa kuzingatia ukweli huo, wanafikra wa Kiislamu wanaamini kuwa kuna udharura mkubwa wa kuimarishwa umoja na mshikamano kati ya Waislamu hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote ule.

Kuhusiana na suala hilo, baadhi ya watu wamekuwa wakijiuliza swali hili kuwa je, kuandikwa na kuchapishwa kwa kitabu kama 'al-Ghadir' ambacho kinazungumzia suala kongwe zaidi ambalo limekuwa likizusha hitilafu miongoni mwa Waislamu, hakuzuii kufikiwa lengo muhimu na tukufu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu, ambalo ni kuwepo umoja miongoni mwa Waislamu? Katika kujibu swali hili, kwanza ni bora tujadili suala muhimu hapa, yaani maana halisi ya maneno 'umoja na umoja wa Kiislamu', na kisha tujadili nafasi ya kitabu hicho na mwandishi wake mtukufu, Allama Amini (Mwenyezi Mungu Amrehemu).

Umoja wa Kiislamu Je, nini maana ya Umoja wa Kiislamu? Je, maana yake ni kuchaguliwa madhehebu moja tu kati ya madhehebu zote za Kiislamu na kisha kutupilia mbali madhehebu nyingine zote, au kusudio lake ni kuzingatiwa masuala yote ya pamoja yanayoyakutanisha madhehebu hayo na kupuuzwa mambo yanayoyatenganisha? Je, jambo kama hilo linapasa kuletwa na madhehebu nyingine mpya ambayo haitakuwa na uhusiano na moja ya madhehebu za hivi sasa?

Je, ni kweli kuwa umoja wa Kiislamu hauhusiani kwa vyovyote vile na suala la madhehebu, bali linalokusudiwa hapa ni umoja wa Waislamu wote, bila kujali tofauti zao za kimadhehebu, katika kukabiliana na maadui wa kigeni? Wanaopinga kuwepo umoja miongoni mwa Waislamu wanatoa maana isiyo ya kimantiki wala kielimu ya umoja huo kwa kusema kuwa umoja unaopasa kuwepo kati ya Waislamu ni wa kimadhehebu, ili umoja kama huo uliojengeka kwenye misingi dhaifu uweze kuporomoka na kusambaratika bila kupiga hatua yoyote ya maana. Bila shaka kusudio la wanazuoni na wanafikra wa Kiislamu kuhusiana na umoja wa Kiislamu si kuyabana madhehebu yote ya Kiislamu katika dhehebu moja, wala kuzingatia tu masuala ya pamoja na kufutilia mbali tofauti zilizopo kati ya madhehbu hayo.

Ni wazi kuwa jambo hilo si la kiakili, kimantiki, kielimu na wala haliwezi kukubalika. Lengo la wanafikra hao ni kujiunga Waislamu wote katika safu moja ya kupambana na maadui wanaopiga vita masuala na imani yao ya pamoja. Wanafikra na wanazuoni hao wanaamini kwamba, Waislamu wana masuala mengi ya pamoja na yanayofanana ambayo yanaweza kutumiwa kama msingi muhimu wa kubuni umoja na muungano imara wa kuwawezesha kukabiliana na maadui wao. Waislamu wote wanamwabudu Mwenyezi Mungu mmoja na kumwamini Mtume mmoja wa mwisho.

Kitabu chao wote ni Qur'ani Tukufu na wana kibla kimoja ambacho ni al-Kaaba Tukufu. Hufanya hija, kuswali, kufunga swaumu, kujenga familia, kufanya miamala, kulea watoto na kuzika wafu wao kwa mbinu na njia zinazofanana. Licha ya kuwepo tofauti ndogondogo na zisizo na maana kubwa, Waislamu hao hawatofautiani sana katika vitendo hivyo.

Waislamu wote wana mtazamo mmoja kuhusiana na dunia, wana utamaduni na ustaarabu mmoja mkubwa na mkongwe. Umoja katika mtazamo wa ulimwengu, utamaduni, ukongwe wa ustaarabu, mtazamo na mwenendo, imani za kidini, maombi na dua na tamaduni pamoja na tabia za kijamii ni mambo yanayoweza kuwafanya Waislamu kubuni taifa moja lenye nguvu kubwa ambalo linaweza kuyalazimisha mataifa makubwa ya dunia kuliogopa na kulinyenyekea, na hasa ikitiliwa maanani kwamba, jambo hilo limesisitizwa mno katika mafundisho ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'ani Tukufu ni kuwa, Waislamu wote ni ndugu na wanaunganishwa na haki na nyadhifa maalumu. Kwa maelezo hayo, swahili hili linajitokeza hapa kuwa, je, ni kwa nini Waislamu hawanufaiki na suhula, utajiri na baraka nyingi hizo walizopewa na Uislamu katika kufikia malego yao? Kwa mtazamo wa wanazuoni hao wa Kiislamu, hakuna udharura wowote unaowalazimu Waislamu kuachana na misingi ya mafundisho ya madhehebu zao ili kufikia umoja wa Kiislamu.

Kwa ibara nyingine ni kuwa, umoja wa Kislamu unaweza kufikiwa bila wafuasi wa madhehebu za Kiislamu kuachana na mafundisho ya madhehebu zao. Wakati huohuo, umoja huo wa Kiislamu hauwazuii Waislamu kujadiliana wala kuandika kwa hoja, vitabu kuhusiana na tofauti za kimsingi na zisizo za kimsingi zilizopo baina yao. Jambo la pekee linalosisitizwa katika kuleta na kuimarishwa umoja wa Kiislamu ni kuwa Waislamu wanapasa kujiepusha na mambo yanayozusha chuki miongoni mwao. Wanapasa kuheshimiana, kutotusiana wala kushutumiana, kutotuhumiana wala kuzuiana uongo, kutofanyia maskhara mantiki za wenzao, kutodhuru hisia za wenzao na hatimaye kutotoka nje ya mipaka ya mantiki na hoja.

Kwa uchache wanapasa kuchunga na kuheshimu mipaka ya chini kabisa ambayo Uislamu umeiweka katika kuwaita watu wasiokuwa Waislamu kwenye dini hii tukufu; Waite (watu) kwenye njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora (16:125).

Baadhi ya watu wanadhani kwamba, madhehebu yanayoweza kuungana chini ya kivuli cha udugu ni yale tu yanayotofautiana katika matawi na sio kwenye misingi kama yalivyo madhehebu ya Shafi' na Hanafi. Wanasema kuwa madhehebu yanayotofautiana kwenye misingi kamwe hayawezi kuwa ndugu wala kuunda muungano na umoja unaohitajika kati ya Waislamu. Kwa imani ya kundi hilo, misingi ya kimadhehebu ni mjumuiko wa mambo yanayofungamana kwa karibu sana kwa kadiri kwamba iwapo moja ya misingi hiyo utadhurika basi madhara yake huiathiri misingi mingine yote.

Kwa mfano, kwa mujibu wa imani ya kundi hilo, msingi kama vile 'uimamu' unapodhurika, misingi mingine yote ya kimadhehebu hudhurika na hivyo kutokuwepo maana ya umoja kati ya wafuasi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu. Kwa msingi huo, hakuna wakati ambao Washia na Wasunni wanapasa kupeana mkono, kama ndugu wamoja wa Kiislamu, wala kuwa katika medani moja ya vita dhidi ya adui wao wa pamoja.

Ni wazi kuwa, fikra hii si sahihi, na sira, yaani mwenendo wa maisha ya Imam Ali (as), ndilo somo na mfano bora zaidi wa kuigwa na sisi sote kuhusiana na suala hilo. Mtukufu Imam Ali (as) alichukua njia bora na ya kimantiki zaidi kuhusu jambo hili.

Licha ya kuwa alifanya juhudi zote alizoweza kwa jaili ya kuhuisha nafasi na msingi wa uimamu katika jamii, lakini wakati huohuo hakutekeleza nara ya 'ima kufuata misingi yote au kuiacha yote.' Kinyume na msimamo huo alifuata na kutekeleza majukumu yake ya kila siku kwa msingi wa kanuni ya 'jambo lisilodirikiwa (fahamika, patikana, eleweka, wezekana, tambulika) lote haliachwi lote.'

Katika moja ya barua zake kwa Malik al-Ashtar (gavana wake nchini Misri-barua nambari 62 katika Nahjul Balagha), Imam Ali (as) anasema: "Nilijizuia kutoa mkono wangu hadi pale nilipoona kwamba watu wanaritadi na kuwaita (kuwachochea) watu (wengine) kutokomeza dini ya Muhammad (saw). Niliogopa kwamba kama singelinda na kuutetea Uislamu na Waislamu, ningeshuhudia kudhihiri katika Uislamu pengo au uharibifu ambao musiba wake ungekuwa ni mkubwa zaidi kuliko ukhalifu ambao ungedumu kwa muda wa siku chache tu."

Ni wazi kutokana na maelezo hayo kwamba, Imam Ali (as) alikuwa akipinga vikali kanuni ya 'ima yote au bila kitu', na wala hakuna haja ya kuchambua mienendo na maisha yake ili kuthibitisha jambo hilo. Kuna dalili nyingi za kihistoria zinazothibitisha ukweli huo.

Allama Amini Wakati sasa umewadia wa kuchunguza na kuona ni jinsi gani mheshimiwa Allama Ayatullah Amini, mwandishi mashuhuri wa kitabu cha al-Ghadir alivyokuwa akifikiri kuhusu suala hili na alikuwa katika kundi gani kati ya makundi mawili hayo. Je, alikuwa ikiamini kuwa umoja na udugu wa Kiislamu unaweze kuthibiti tu kupitia duara la Ushia, au dura hilo la udugu wa Kiislamu ni kubwa na pana zaidi, na ambalo linathibiti kwa kukiri na kutamka shahada mbili za Kiislamu. Tupende tusipende, ni wazi kuwa haki za Waslamu kwa Waislamu wenzao ni zile za udugu wa Kiislamu, udugu ambao umezungumziwa katika kitabu kitakatifu cha Qur'ani.

Allama Amini amezungumzia kwa kina suala hilo na kusisitiza nukta anayotaka uizingatie hapa wewe mpenzi msomaji, nayo ni hii kuwa, je, al-Ghadir ina nafasi gani katika kuleta umoja wa Kiislamu katika jamii, na kuwa je, nafasi hiyo ni chanya au hasi?

Amebainisha wazi mara kwa mara msimamo wake kuhusiana na suala la umoja wa Kiislamu ili asije akatumiwa vibaya na walalamikaji kutoka pande zote mbili za wapinzani na waungaji mkono wa msimamo wake huo. Allama Amini ni muungaji mkono mkubwa wa umoja wa Kiislamu na amekuwa na mtazamo mpana na mzuri wa uhalisia wa mambo kuhusu suala hilo.

Mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu amelijadili suala hilo kwa urefu katika kitabu chake cha al-Ghadir ambacho amekitunga katika juzuu kadhaa.

Tunazungumzia hapa baadhi ya maneneo yake kuhusiana na umoja wa Kiislamu katika kitabu hicho. Anasema hivi kuhusiana na nafasi ya kitabu hicho katika ulimwengu wa Kiislamu, katika utangulizi wa juzuu ya kwanza: "Na sisi tanayachukulia haya yote kuwa ni huduma kwa dini, kunyanyua kalima ya haki na kuhuisha umma wa Kiislamu."

Anasema katika juzuu ya tatu ukurasa wa 77, baada ya kunukuu mananeo ya Ibn Taimiyya, Aalusi na Qusweimi kuwa, Mashia wanawachukulia baadhi ya Ahlul Beit kama vile Zaid bin Ali bin al-Hussein kuwa maadui, kama ifuatavyo: "uongo na tuhuma hizo zinapanda mbegu ya ufisadi na uadui katika umma wa Kiislamu. Huzusha mifarakano, fitina na kuusambaratisha umma wa Kiislamu, pamoja na kugonganisha maslahi makuu ya Waislamu."

Vilevile anasema katika ukurasa wa 268 wa juzuu hiyohiyo akimnukuu Sayyid Muhammad Rashid Ridha aliyewatuhumu Mashia kwamba wanafurahia kushindwa kokote kwa Waislamu na kwamba hata walifurahia ushindi wa Russia dhidi ya Waislamu wa Iran na kuandika: "Hayo ni mambo yaliyozushwa na Sayyid Muhammad Rashid Ridha. Mashia wa Iran na Iraq ambao kwa kawaida hutuhumiwa kwa mambo mambo mbalimbali na vile vile wataalamu wa masuala ya Kiislamu wa nchi za Magharibi, watalii na wawakilishi wa nchi za Kiislamu na wengineo wanaoitembelea Iran hawajawahi kutoa habari wala ripoti yoyote ya aina hiyo. Mashia wote wanaheshimu roho, damu, heshima na mali ya Waislamu wote bila kujali Ushia wala Usunni wao.

Hushiriki na kuomboleza na Waislamu wenzao kila msiba unaowasibu wafuasi wa madhehebu nyingine zote za Kiislamu, kila wakati na sehemu yoyote ile unapotokea msiba huo. Washia kamwe hawajaubana udugu wa Kiislamu ambao umezungumziwa katika Qur'ani na Sunna katika jamii yao ya Kishia tu. Kuhusu jambo hilo, hawaweki tofauti kati yao na wenzao wa Kisunni."

Allama Amini pia mwishoni mwa juzuu ya tatu anakosoa baadhi ya vitabu vilivyoandikwa na waandishi wa kale kama vile al-Iqdul Farid cha Ibn Abdu Rabbu, al-Intisaar cha Abul Hussein Khayat Mu'tazili, al-Farqu baina Firaq cha Abul Mansur Baghdadi, al-Fasl cha Ibn Hazm al-Andolosi, al-Milal wa an-Nihal cha Muhammad bin Abdul Karim Shahrestani, Minhaj as-Sunna cha Ibn Taimiyya, al-Bidayatu wa an-Nihaya cha Ibn Kathir na vitabu vingine vya waandishi wa zama hizi kama vile Tarikh al-Umam al-Islamiyya cha Sheikh Muhammad Khudhari, Fajrul Islam cha Ahmad Amin, al-Jaulatu fi Rujuu' as-Sharq al-Adna cha Muhammad Thabit Misri As-Swiraa' baina al-Islam wa al-Wathaniya cha Qusweimi na al- Washia' cha Musa Jarallah na kusema:

"Lengpo letu la kukosoa vitabu hivi ni kuwatahadharisha Waislamu kuhusiana na hatari inayowakabili na kuwafahamisha kwamba, vitabu hivi vinaiweka jamii nzima katika hatari kubwa. Hii ni kwa sababu vitabu hivyo vinayumbisha umoja wa Kiislamu na kusambaratisha safu za Waislamu. Hakuna jambo jingine linalofarakanisha Waislamu, kuvuruga umoja wao na kukata kamba ya udugu wao wa Kiislamu kama vinavyofanya vitabu hivi.

Anaweka wazi mtazamo wake katika juzuu ya tano ya kitabu cha al-Ghadiri, chini ya anwani 'nadharia karimu' kuhusiana na moja ya barua zilizotumwa kwake kutoka Misri kumshukuru kuhusiana na kitabu hicho na hivyo kutowacha shaka yoyote kuhusiana na jambo hilo. Anasema: "Itikadi na mitazamo kuhusiana na madhehebu ni huru na wala haikati kamba ya umoja wa Kiislamu ambao Qur'ani imeusisitiza kwa kusema; 'Kwa hakika Waislamu wote ni ndugu.'

Udugu huo hauondolewi, hata kama mijadala na midahalo ya kielimu, kiitikadi na kimadhehebu itafikia kilele, kama tunavyoshuhudia hilo likithibiti katika maisha ya viongozi wa kidini wakiongozwa na masahaba na wafuasi wao. Licha ya kuwa sisi waandishi kutoka katika pembe mbalimbali za ulimwengu wa Kiislamu tunatofautiana katika misingi na matawi ya imani zetu, lakini ni wazi kuwa kuna jambo moja linalotuunganisha sote nalo ni kumwani Mwenyezi Mungu mmoja na Mtume Wake. Tuna moyo na hisia moja kwenye miili yetu nao ni moyo wa Uislamu na neno la ikhlasi."

Sisi sote waandishi wa Kiislamu tunaishi chini ya bendera ya Mwenyezi Mungu na kutekeleza majukumu yetu chini ya mwongozo wa Qur'ani na ujumbe wa Mtume Mtukufu. Ujumbe wetu sote ni: "Bila shaka dini (ya haki) mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu", na nara yetu sote ni: "Hakuna mungu (anayestahiki kuabudiwa) isipokuwa Allah na Muhammad ni Mtume Wake." Nam, sisi ni kundi la Mwenyezi Mungu na watetezi wa dini Yake!" Katika utangulizi wa juzuu ya nane ya kitabu chake, Allama Amini anajadili moja kwa moja nafasi ya al-Ghadir katika kuwaunganisha Waislamu chini ya anwani, 'al-Ghadir Yuwahhid Swufuf fi al-Malai al-Islami.'

Katika mjadala huo, mwanazuoni huyo anawakosoa vikali watu wanaodai kwamba kitabu cha al-Ghadir kinawatenganisha zaidi Waislamu na kuthibitisha kinyume na madai hayo kwamba, al-Ghadir kimeondoa sutafahumu na tofauti nyingi zilizokuwepo kati ya Waislamu na kuwaunganisha zaidi. Kisha anatolea ushahidi maneno ya wanazuoni na wanafikra mashuhuri wa Kiislamu wasiokuwa Mashia kuhusu jambo hilo. Mwishoni, ananukuu barua ya Sheikh Said Dahduh kuhusiana na kadhia hiyo. Tunajiepusha kuzungumzia hapa kwa undani na kwa kina maneno ya Allama Amini kuhusiana na nafasi muhimu ambayo imetekelezwa na kitabu cha al-Ghadir katika kuwaunganisha Waislamu na kuleta umoja madhubuti miongoni mwao kwa sababu kile tumekizungumzia hadi sasa kinatosha kuthibitisha jambo hilo.

Nafasi muhimu ya al-Ghadir katika kuwaunganisha Waislamu inatokana na ukweli huu kwamba; kwanza inaweka wazi mantiki ya hoja ya Ushia na kuthibitisha kwamba, ufuasi wa karibu Waislamu milioni mia moja kwa madhehebu ya Shia, ni kinyume na madai pamoja na propaganda sumu za baadhi ya watu kuwa madhehebu hii ilibuniwa kutokana na mirengo ya kisiasa na kijamii. Kitabu hicho kinathibitisha wazi kwamba, madhehebu hii ya Kiislamu inatokana na mantiki madhubuti iliyojengeka kwenye misingi ya Qur'ani na Sunna za Mtume Muhammad, jambo amablo limefanya idadi kubwa ya Waislamu kuifuata.

Pili ni kuwa kitabu hicho kinathibitisha kwamba tuhuma zisizo na msingi zinazotolewa dhidi ya Mashia zikiwemo zile zinazosema kuwa Mashi wanawafadhilisha watu wasiokuwa Waislamu juu ya Waislamu wenzao, kuwa wanafurahia kushindwa Waislamu wasiokuwa Washia, kuwa wanafanya hija katika maeneo ya maimamu wao badala ya kuhiji Makka au tuhuma nyingine nyingi zinazotolewa kuhusiana na swala pamoja na ndoa za muda, tuhuma ambazo kwa hakika zimewapelekea Waislamu wa madhehebu nyingine za Kiislamu kujitenga nao, ni uzushi na uongo mtupu usio na msingi wowote wa kimantiki wala kielimu.

Tatu ni kwamba, kitabu hicho kinamuarifisha vyema Imam Ali pamoja na kizazi chake kitoharifu, Imam ambaye ni madhulumu zaidi na ambaye ameendelea kutofahamika vyema kati ya viongozi wengine watukufu na wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Bila shaka kama kiongozi na mtukufu huyo angefahamika vyema na Waislamu, angeweza kufuatwa na Waislamu wote pamoja na kizazi chake kitoharifu.

Maoni ya wengine kuhusu al-Ghadir Maoni ya wasomi na wanafikra wengi wa Kiislamu wasiokuwa Washia kuhusiana na kitabu cha al-Ghadir ni sawa kabisa na maelezo tuliyoyatoa huko nyuma. Katika dibaji yake kwenye kitabu cha al-Ghadiri ambayo ameiandika kwenye juzuu ya kwanza ya chapa ya pili ya kitabu hicho, Muhammad Abdul Ghani Hassan Misri anasema: "Ninamwomba Mwenyezi Mungu alifanye dimbwi lako hili (al-Ghadir ina maana ya dimbwi katika lugha ya Kiarabu) liwe chanzo cha amani na mapenzi kati ya Mashia na Masunni ambao watashirikiana katika kuujenga umma wa Kiislamu."

Adil Ghudhban, mkurugenzi wa jarida linalochapishwa nchini Misri la al-Kitab anasema katika utangulizi wa juzuu ya tatu ya al-Ghadir kama ifuatavyo: "Kitabu hiki kinaweka wazi mantiki ya Ushia na Masunni wanaweza kuufahamu vyema Ushia kupitia kitabu hiki. Kuufahamu vyema Ushia kunaweza kusaidia sana katika kukurubishwa pamoja mitazamo ya Mashia na Masunni na hivyo kubuni safu moja ya Kiislamu."

Dakta Muhammad Ghulaab. Mhadhiri wa taaluma ya falsafa katika Chuo cha Misingi ya Dini cha Chuo Kikuu cha al-Azhar katika utangulizi wake wa kitabu cha al-Ghadir na ambao umechapishwa katika juzuu ya nne ya kitabu hicho anasema hivi: "Kitabu chako kimenifikia katika wakati muafaka mno. Hii ni kwa sababu hivi sasa nashughulika kuandika kitabu kuhusiana na maisha ya Waislamu katika nyanja mbalimbali.

Kwa msingi huo, nina hamu kubwa ya kupata maelezo sahihi kuhusiana na Mashia wa madhehebu ya Imamia. Kitabu chako bila shaka kitanisaidia katika hili na kunizuia kutofanya makosa kuhusiana na Mashia, kama walivyofanya wenzangu." Dakta Abdu ar-Rahman Kiali Halabi katika utangulizi wake katika juzuu ya nne ya al-Ghadir anaashiria upotovu ambao unafanywa na Waislamu katika zama hizi na kupendekeza njia kadhaa ambazo Waislamu wanaweza kuzitumia katika kujinusuru kutokana na upotovu huo.

Anasema kuwa mojawapo ya njia hizo ni kumtambua vyema mtu aliyemrithi Mtume Mtukufu kwa njia sahihi. Anasema: "Kitabu cha al-Ghadir na yaliyomo ni jambo ambalo linampasa kila Muislamu kilifahamu ili apate kujua ni jinsi gani wanahistoria walivyofanya makosa, na kuweza kuelewa ukweli uko wapi. Kwa njia hii, tunapasa kufidia makosa yaliyofanyika na kufanya juhudi za kuwaunganisha Waislamu ili tunufaike na thawabu zake."

Nam, huu ndio mtazamo wa Allama Amini (Mwenyezi Mungu Amrehemu) kuhusiana na suala hili nyeti na la kijamii katika zama zetu hizi, na haya ndiyo matokeo yake mazuri katika ulimwengu wa Kiislamu.

Marejeo: www.ghadeer.org

MWISHO