UMASKINI
  • Kichwa: UMASKINI
  • mwandishi: MWANA JAMII
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 15:34:41 1-9-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

UMASKINI NA CHANZO CHAKE

CHANZO KIKUU CHA UMASKINI WA TANZANIA

Miaka nenda miaka rudi, taifa la Tanzania limeeendelea kuhesabika miongoni mwa nchi maskini kabisa duniani. Sio tu kuhesabika uko kwa taifa hili kuko katika takwimu za wataalamu wa uchumi, bali pia kiwango cha maisha ya watanzania wengi ni cha chini sana. Watanzania tumeeendelea kuishi maisha ya dhiki sana, mulo kwa wengi kuupata imekuwa taabu, nyumba wanamoishi watu ni hohehahe, elimu ya wengi wetu ni duni, kusafiri toka sehemu moja hadi nyingine shida tupu (vijijini na mijini), huduma za afya licha ya kutopatikana kwa urahisi, zilizopo wanaomudu gharama zake ni wachache na hata hivyo hazilidhishi, vipato vya wafanyakazi, wakulima na wafanyabiashara viko hoi, ili mradi tu ni dhiki juu ya nyingine. Wakati walio wengi taabu zetu kwa kutaja chache ndio hizo, wapo wenzetu wachache nchini ambao maisha yao ni ya neema, tena neema tele. Watanzania tumeendelea kujiuliza, kulikoni bila majibu. Baadhi yetu tu, mfano wasomi na wengine,wamejaribu kutafuta majibu na ufumbuzi wa umaskini huu lakini hadi sasa bila suluhisho. Kwa kutumia nadharia kwa mfano, wapo wanaosema chanzo na kiendelezo cha umaskini wetu, ni tabia ya watanzania wengi kutojiwekea akiba, yaani baada ya kuzalisha kidogo, kidogo hicho chote kinawekwa katika matumizi, hivyo hakuna akiba na kwahiyo hakuna uwekezaji katika mradi wowote mpya wa uzalishaji au kupanua uliopo, na matokeo yake uzalishaji unaendelea kuwa kidogo kama sio kupungua, ilimradi unakuwa ni mduara tatizi usiokoma wa ufukara. Kwa kusimamia kwenye nadharia hii, wapo wanaotuhubiria watanzania kwamba tujenge tabia ya kuweka akiba jamani. Ni mahubiri mazuri sana, lakini swali la kujiuliza hapo ni je, kweli kuna mtanzania asiyetaka kuweka akiba? Kwa maoni yangu, mtanzania wa hivyo hajazaliwa, bali sisi tunaoishi roho zetu zi radhi kuweka akiba lakini hali halisi inakataa. Wengi watakubaliana nami kwamba, mfanyakazi wa Tanzania ya leo ambaye mara nyingi mshahara wake wa mwezi huisha siku kumi au kumi na tano baada ya kuupokea, kumwambia aweke akiba ni kumkejeli mchana kweupe!

Mfanyakazi wa kitanzania, maisha yake yamejaa madeni kwenye maduka ya rejareja. Laiti kama mikopo anayochukua kwenye maduka hayo ingekuwa ya bidhaa za ziada, sio, ni madeni yatokanayo na mahitaji ya sukari, chumvi, sabuni, sembe na bidhaa nyingine za namna hiyo. Kilio cha wafanyakazi hawa kimeendelea kuwa ni kile kile mwaka hadi mwaka, wakidhani tatizo ni kwamba mshahara hautoshi. Watawala wetu katika kujibu malalamiko ya mishahara kutotosha, wamekuwa wakifurahisha mikutano wanayoihutubia kwa kuimba ngonjera ile ile, ‘Mwaka huu wa bajeti tutaongeza mishahara’ mara kadhaa wanaongeza kweli.

Nyongeza hizo licha ya kuwa kiduchu zimeendelea kutotatua tatizo, bado mshahara hautoshi na hauelekei kama utatosha siku za karibuni. Kumbe shida ni nini hasa? Wengine wakasema ni kwa sababu kuna mfumko wa bei, kiasi kwamba nyongeza inapotoka tayari bidhaa madukani zimepanda mara dufu na huduma za jamii zimeenda juu vile vile. Kwa upande mwingine yapo madai kwamba umasikini wetu pengine unatokana na uvivu wa watanzania (hili linasemwa sana na wabaguzi ambo mara kadhaa wamedai eti sisi waafrika ni wavivu). Bado naendelea kujiuliza kama hilo lina chembe zozote za ukweli, ili kama hilo ndio tatizo la Tanzania, tusione aibu kulikiri na hivyo kuamua kuondokana nalo. Lakini haiingi akilini kirahisi kwamba watanzania tunaofanya kazi kutwa kucha, usiku na mchana, siku za kawaida, mwisho wa wiki na hata kwenye sikukuu hadi wengine tunaitwa walalahoi, bado tunaweza kuambiwa uvivu ndio sababu ya umaskini wetu.

MAENEO YA VIJIJINI

Maeneo ya vijijini, mkulima masikini anamka kabla ya jogoo kuwika ili awahi shambani, inamlazimu wakati mwingine kushinda njaa ili asirejee nyumbani na kuharibu kazi aliyokusudia kuimaliza siku hiyo. Msimu wote wa kilimo, mvua yake, jua kali lake na taabu nyinginezo za maporini. Maskini mkulima huyu kapinda mgongo na jembe lake la mkono ili mkono uende kinywani. Tena anapaswa alime kwa bidii hata mazao ya biashara ili apate fedha, maskini mazao yake miaka nenda miaka rudi hayapati bei inayolingana japo angalau na nguvu kazi yake aliyotumia. Bado mtu huyu aambiwe wewe ni maskini kwa sababu ya uvivu? Kadhalika kwa wafanyakazi, nitolee mfano wetu sisi walimu; mwalimu anayedamka asubuhi na mapema sambamba na wanafunzi wake, akafanya kazi zake siku nzima ya kazi, na kwa kuwa hazikuisha akabebana nazo kwenda nyumbani, ili usiku awashe kibatali na kuzimalizia (hana tofauti na Kayumba), baada ya hapo aandae anafundisha nini kesho, wakati wanafunzi wake wako likizo yeye ndio kwanza anasahihisha mitihani yao na kuandaa mpangokazi wa muhula unaofuata. Huyu naye aambiwe sababu ya umaskini wake ni uvivu, kweli? Aidha upo mtizamo kwamba, sababu ya kuendelea kwetu kuwa masikini ni kwa kuwa watanzania tunamiliki mali lakini hazina urasmi, yamkini wa kutuwezesha kupata mikopo toka taasisi za fedha na kadhalika.

Ndio maana ukaja huu makakati wa kurasmisha mali hizo kama harakati mojawapo ya kupambana na ufukara nchini. Sambamba na hilo, ipo dhana ya kwamba mikopo kwa watu binafsi na vikundi vya jamii itatuokoa ufukarani. Kwa sababu hiyo sasa tuna mamilioni ya Kikwete na mikopo mingine! Maswali bado ni mengi hapo. Ni nini kinaweza kutokea kwa mfano, iwapo watanzania watachukua hiyo mikopo midogo midogo na hatimaye kugeuka taifa la wachuuzi, tena wa bidhaa zitokazo nje, umaskini utaondoka? Uchumi utakua? La hasha, maana bado mimi naamini kutokuwepo kwa mikopo hiyo bado sio sababu ya umaskini wa wananchi.

Hata hivyo kuwepo kwake, si hatua ya kubeza. Katika harakati za kutusaidia, tumeimizwa sana kuwekeza popote fursa inapojitokeza, mfano kununua hisa katika makampuni au mashirika. Hili limefanyika sana. Watanzania tunakumbuka pia Rais mstaaafu wa awamu ya tatu alivyotuhutubia siku moja, kwamba tofauti yetu na matajiri wa nje, hususan wanaokuja nchini kuwekeza ni kwamba waliona mapema umuhimu wa hisa, na kwa kuzinunua ndiko walikopata mitaji yao wanayoihamishia sasa nchini ketu ili wachume zaidi. Hivyo akatushauri tuone haja ya kununua hisa kama kweli tunataka kuondokana na umasikini. Lakini bado tunarudi kulekule, yule mwenye mshahara usiomfikisha mwisho wa mwezi, au ambaye mazao yake hayajanunuliwa na ambaye mwenye duka anamdai, kapata wapi cha kununulia hisa. Tumeedelea kujiuliza zaidi na zaidi juu ya chanzo na suluhu ya umaskini wetu. Wapo wanaodhani kwamba sisi ni maskini kwa majaliwa ya maumbile. Sisi ni maskini kwa sababu taifa letu halikuumbwa tajiri kama yalivyo mataifa mengine. Hili ndio kwanza halina hata lepe la ukweli.

TANZANIA NI NCHI TAJIRI

Tanzania kwa asili ni nchi tajiri sana! Tena ingefaa watanzania tutambue na kujivunia ukweli huo kwamba nchi yetu imependelewa muno kuliko nchi nyingi sana duniani. Utajiri wetu wa maliasili hauna mfano. Tuna eneo kubwa sana la ardhi tena yenye rutuba, ifaayo kwa kilimo na shughuli nyinginezo za kiuchumi. Yapo mataifa ambayo watu wake si maskini kwa kiwango chetu, lakini ardhi yao waliyojaliwa ni jangwa. Hapo asomaye na afahamu ni kwa nini Namibia fedha yao ina nguvu sana ukilinganisha na ya kwetu. Tanzania tumejaliwa madini na vito vya thamani vingi sana, na vingine havipatikani popote ulimwenguni ila Tanzania tu. Kuitaja Tanzanite kumezoeleka, watanzania tufahamu pia kwamba licha ya dhahabu, almasi, bati, taja madini yoote yang’aayo na yasiyon’gaa utayakuta nchini. Ni sisi pekee vile vile tuliojaliwa madini ambayo walioyagundua waliamua kuyaita Nyerereite kwa sababu ya upekee wake duniani. Kana kwamba hilo halitoshi,wakati wenzetu wanalia kwa kukosa maji, sisi kila mahali ni mito na maziwa makubwa yanayopendeza hata kwa mpangilio na mtandao wake nchi nzima. Ziwa kubwa kuliko yote Afrika liko Tanzania, Ziwa lenye kina kirefu kuliko yote Afrika nalo liko Tanzania! Ndio maana mojawapo ya nyimbo zetu za kizalendo tunasema, tazama ramani utaona nchi nzuri, yenye mito na mabonde mengi ya nafaka! Aidha wakati mataifa mengine, yamefungiwa ndani kwa ndani kiusafiri, sisi tuna pwani ya bahari ya Hindi yenye kilometa nyingi za urefu na bandari kadhaa zinazotuhudumia wenyewe na mataifa jirani yanazitumia tena kwa kutulipa fedha nyingi tu za ushuru. Mshangao uaongezeka tunapoambiwa mataifa hayo hayo yanayotutegemea katika sekta hiyo, yanatuzidi kiuchumi. Tuseme nini kuhusu baraka ya misitu na wanyama na vivutio vingine vya utalii. Utajiri wetu katika eneo hilo umeyatia wivu mataifa mengi ambayo hayana, lakini mataifa hayo hayo watu wake si fukara kama sisi. Kulikoni? Baba wa taifa Marehemu Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kutueleza, tunahitaji watu ili kuiendeleza nchi yetu.

Ingawa hitaji la watu si tu kwamba wawe wengi bali pia wawe na maarifa na maadili, sisi Tanzania tumejaliwa hata katika hilo. Jamani, kwa sasa twapata milioni arobaini (40), lakini nchi zenye wakazi kidogo tu zinatuzidi mbali kiuchumi. Unakuta nchi kwa ujumla ina idadi ya watu sawa na wakazi wa Dar es salaam peke yake au pungufu, lakini maendeleo yao hatuwafikii hata robo. Labda nidokezee tu kwamba, idadi ya wakazi nchini Finland kwa mfano, ni milioni tano na ushee kidogo. Namibia nilikotolea mfano wa kwanza, kuna watu wasiozidi milioni mbili. Tuseme nini basi, wingi wetu ndio unaotuponza? La hasha, ingawa kwa mtazamo mwingine idadi kubwa ya watu wasio na mwelekeo ni tatizo. Litupasalo sisi ni kuutumia vizuri wingi huo, kuuondoa katika umaskini ili kila mmoja wetu azidi kuwa wa manufaa kwa taifa. Mataifa mengine, yametumia wingi wao kupiga hatua kubwa sana kimaendeleo. Kinachotakiwa ni kuwa na watu walio bora, kwa maana ya wenye elimu, afya na uwezo wa kutenda. Umasikini umekuwa chanzo cha wananchi wetu kuwa na elimu duni na afya zisizolidhisha. Bahati mbaya baadhi ya waliobahatika kupata elimu nzuri wamekimbilia nchi za nje kwa sababu ya maslahi duni yanayotolewa hapa nchini. Tuna bahati mbaya kwamba watanzania wenzetu hao wametoa mchango mkubwa sana katika kutokomeza umasikini wa nchi za wenzetu, ilihali nyumbani (kama ulivyo msemo wa mitaani) kumedoda. Hoja yangu hapo ni kwamba, wingi wetu si chanzo cha umasikini bali ni baraka ambayo laiti tungeitumia vizuri, Tanzania ingehesabika katika ulimwengu wa kwanza. Mtazamo mwingine juu ya umasikini wetu, ni ule unaoona kwamba sababu zake si za ndani bali zinatoka nje.

Mtazamo huu unauhusianisha umasikini na ukoloni tulioupitia katika historia ya nchi yetu. Kwamba kwa kutawaliwa na wakoloni wa kijerumani na baadaye waingereza, tulinyonywa na tunaendelea kunyonywa kupitia ukoloni mambo leo, utandawazi na uwekezaji wa kigeni. Hapa pana ukweli wa kiasi chake, japo hapatoshi kuwa sababu hasa inayoeleza chanzo cha ufukara nchini, na wala suluhu yake haitakuja kwa kupambana tu na mkoloni wa zamani na wa sasa. Mataifa kadhaa ulimenguni yalipitia kutawaliwa na wakoloni kama sisi, lakini leo hii wao (sio wote) si masikini kama sisi. Hapa nirudie mfano wa Finland iliyotawaliwa na Urusi na Sweden, au nchi za Asia zilizokuwa makoloni ya mwingereza.

Walijikomboa kutoka ukoloni, wakakaa chini kizalendo wakajenga nchi zao, umaskini ukatokomea. “kwani wao waliweza wana nini, na sisi tunashindwa ni kwanini?” Hata hivyo hatuwezi kupuuza hujuma za nchi zinazojifanya viranja wa ulimwengu, hususan nchi za magharibi dhidi ya nchi changa. Hawa hawa ndio wanaendelea kutuharibia kwa kutupangia nini tufanye na nini tuache. Wanaendelea pia kushirikana na wazandiki wasioitakia nchi yetu mema bali nafsi zao, japo ni watanzania wenzetu. Ndio hao aliowasema Baba wa taifa, kwamba ni miti (mipini) iliyomo kwenye mashoka ya chuma inayowakata akina miti. (shoka bila mpini halikati mti, ati) Hivyo, tunapoendelea kuulaumu/ kuusingizia ukoloni na utandawazi tusisahau kuwatazama Yuda Iskariote wetu. Wenzetu hao ni sababu mojawapo ya kudumu kwa umaskini wetu, na nadhani kwa kuwadhibiti tutaudhibiti umasikini vilevile.

MANENO YA VIONGOZI WETU

Wakati fulani nimepata kusikia baadhi ya viongozi wetu wakitaja kuwa, sisi ni masikini kwa sababu kadhaa, mojawapo ni vita tulivyopigana dhidi ya Idd Amin wa Uganda mnamo mwaka 1978/79 (miaka therathini imepita sasa) Mnh, binafsi sipuuzi athari za vita hiyo, lakini kuitaja kama sababu ya umasikini kukithiri nchini, ni kukosa kisingizio, kujisemea tu au kuogopa kujinyooshea kidole. Jamani, vita hiyo imepiganwa muda mrefu umepita sasa, tena ilidumu kwa miezi sita tu. Watasemaje majirani zetu wa Rwanda na Burundi ambao kwa sasa nchi zao (hasa Rwanda) zinatengemaa kiuchumi, na ajabu Faranga yao ina nguvu kuliko Shilingi ya Tanzania. Namibia wamepata uhuru mwaka 1990 jamani, vita vya ukombozi huko vilidumu kwa muda, ilihali sisi tulipata uhuru bila damu. Uhuru wetu wa bila kumwaga damu na utulivu wetu (wengine wanasema amani,amani umasikinini?) wa muda mrefu, zilikuwa ni sababu tosha za sisi kuwa mbali sana kimaendeleo kuliko wenzetu wengi. Mungu atupe nini ndugu zangu. Wapo vile vile wanaosema, watanzania hasa vijana, ni maskini kwa sababu ya ukosefu wa ajira. Tatizo la ajira miongoni mwa vijana kweli lipo, lakini kimantiki halikupaswa kuwepo. Katika enzi hizi za sayansi na teknolojia, ambamo matumizi ya maarifa yameongezeka, nchi yetu inatajwa kuwa mojawapo ya nchi zisizo na raslimaliwatu yenye kumudu hayo.

Hivyo tatizo si kwamba ajira hazipo, ila vijana hawana elimu. Nchi yetu vile vile inazo sekta ambazo wengi wanaoziendesha nguvu zao sasa zinaelekea machweo. Matharani sekta ya kilimo, kwa kuwa inaonekana kutokuwa na tija, vijana wanaikimbia na kuwaachia wazee vijijini. Laiti kama sekta hiyo ingebadilishwa sura yake ya sasa, wimbo wa hakuna ajira ungewekwa makumbusho. Laiti kama elimu ingetolewa kwa vijana wote hawa, tena elimu iliyo sahihi, Tanzania isingekuwa tena mahali ambapo mwekezaji kutoka nje anawakosa wenyeji wenye taaluma na ujuzi unaoendana na biashara/shughuli yake, inamlazimu kuja na wataalamu wake. Niliyoyajadili hapo juu, si mapya sana. Haja ya kuyataja inajitokeza kwa ajili ya kujenga mazingira ya hoja yangu kuu, na vile vile kulitazama suala la umasikini, chanzo chake na suluhu yake kwa mapana zaidi. Juhudi nyingi watanzania tumefanya,lakini umasikini umeendelea kusimama wima kama mlima Sayuni unaosemekana hautatikisika kamwe. Au kama Mbuyu katika mbuga za Dodoma. Tumefika mahali tumegundua kisababishi kikuu cha uamsikini wetu, na hicho ndio ninataka tukiangalie leo kwa makini ili hatimaye tuchukue hatua sahihi na mwisho umaskini nchini ugeuke historia ( tena isiyojirudia) Katika familia Fulani, wamejaaliwa mali nyingi walizorithi kutoka vizazi na vizazi. Wanafamilia waadilifu wanajitaidi kufanya kazi kwa bidii lakini wanashangaa mwisho wa siku kinachotoka jikoni, badala ya kuwashibisha ndio kwanza kinawaumisha njaa zaidi. Miaka hadi miaka wanaendelea kukondeana maskini hawa. Hatimaye wanajuliza, kulikoni huko jikoni? Mara lo, wanagundua wapishi ni wezi. Familia inakaa kikao cha dharula, agenda ni moja, WAPISHI ni WEZI. Hapo hakuna anayepindisha lugha, eti wapishi wamepungukiwa uaminifu, ooh tuna mashaka nao.

Wote wameamua kuliita sepetu ni sepetu, wala sio kijiko kikubwa. Ndugu zangu, Tanzania ndio familia yetu, kisababishi kikubwa cha umasikini wetu, njaa yetu na matatizo mengine lukuki ni kwamba; TULIOWAPA DHAMANA YA KUSIMAMIA RASLIMALI ZETU NI WEZI.

UKWELI HALISI

Siku za karibuni yametumika maneno mengi kuwasema, wangine wanasema ni MAFISADI, ni jina sahihi lakini halitoshi, pengine wanaitwa wala RUSHWA ni kweli lakini hawa ni zaidi ya wala rushwa. Msamiati mmoja rahisi ambalo hata mtanzania aliyeko darasa la kwanza hatahitaji kamusi ya Tuki kuuelewa … WEZI Wametuibia akiba zetu, wametuibia nguvu kazi zetu, wameiba jasho letu, wameiba mali asili zetu, wamewakaribisha wezi wenzao kutoka ughaibuni wakaiba na kuiba na kuiba isivyopata kutokea katika historia ya taifa letu, wakajitajirisha. Makazi yao yakawa majumba mithiri ya mahekalu, ilihali sisi wenye mali tunaishi mbavu za mbwa, usafiri wao ukawa mashangingi, VX, Lange Rover, Benz, BMW, ilihali sisi tunapougua tunasafirishwa kwa baiskeli mbovu.

Watoto wa wenzetu wakaao mijini hawana usafiri wa kwenda shule, wakati watoto wao wanawatimulia vumbi la maprado. Lo, tulidhani utajiri huo ni zao la jitihada zao kumbe wizi, tena wizi usio na haya. Ndugu watanzania, tumasikia sasa vya kutosha juu ya wizi wa mabilioni uliotokea katika Benki yetu kuu. Fedha zilizoibiwa, katika kupitia akaunti ya mabeni ya nje (shilingi bilioni 133) na hata ambazo hatujatajiwa bado, kwa mahesabu ya haraka haraka, zingeweza kutatua tatizo la shule mbovu, zisizo na vifaa vya kufundishia wala walimu. Tangia sasa mtu asituambie tena kwamba matatizo yaliyoko katika elimu yanatokana na umasikini wa nchi. Tunaujua ukweli sasa, yanatokana na WIZI. Tumesikia pia habari za kusainiwa kwa mikataba mibovu, na ununuzi wa vifaa vibovu. Nisingependa kurudia kutaja IPTL, Richmond, Buzwagi, Ununuzi wa rada, Ndege ya Rais na mengine. Hawawezi tena sasa kutudanganya kwamba waliosaini mikataba hiyo walipungukiwa maarifa, la hasha, waliisaini KIWIZIWIZI. Tumeimbiwa sana nyimbo za mrahaba kichele unaolipwa na makampuni yanayochimba madini, na jinsi usafirishaji wa madini usivyoangaliwa kiasi kwamba inabidi eti kamati iende ng’ambo kuchunguza mchanga wa madini unaosafirishwa kwenda huko. Jamani, huu wizi kumbe umeenea ndani ya taasisi zetu na katika machimbo ya maliasili zetu, kila mahali!.

Tunapoendelea kukosa huduma za afya, si kwamba nchi yetu ni masikini, bali wezi wanachota vifungu na mali ambazo zingeboresha huduma hizo. Tunapoendelea kupata ujira duni kwenye ajira zetu, si kwamba nchi yetu ni masikini, bali pato ambalo lingetumika kuboresha mishahara ya watumishi, WEZI wamelitia vinywani mwao. Tunapoendelea kuumizwa na kupanda kwa gharama za maisha, petroli juu, mchele juu, unga juu, umeme juu, sabuni juu, nauli juu; si kwamba nchi yetu ni masikini, bali kodi tunayolipa kupitia makato ya mishahara yetu, na kupitia bidhaa hizo hizo tuanzonunua, zinishia kwenye matumbo ya WEZI na washirika wao wa ndani na nje. Yamkini tunapoendelea kuwa na bejeti ya nchi inayotegemea misaada ya wahisani kwa asilimia arobaini (40%) si kwamba ni kwa sababu ya umasikini wetu, bali WEZI wanahujumu uchumi wetu. Tunapoendelea kuwa na barabara mbovu, makazi duni na kila aina za ufukara si kwamba sisi ni wavivu, hatuweki akiba au hatununui hisa. Si kwamba ni kwa kuwa tulipigana na Amin au kuna upungufu wa ajira, bali ni kwa sababu tuliowapa dhamana ya kusimamia utajiri wetu kwa manufaa ya wote wameamua kuwa WEZI waliokubuhu.

Umefika wakati sasa tuwashughulikie wezi hawa wote, mmoja baada ya mwingine, bila kumwangalia nyani usoni ili tulinusuru taifa. Umefika wakati tuseme yatosha nyimbo za ulaghai tulizoimbiwa na wanasiasa waongo, maana ukweli sasa tunaujua. Hukumu yao isiwe ya sheria mkononi (ingawa ikitokea hivyo sitashangaa). Hukumu ianze kwa msaada wa vyombo vyetu vya sheria nchini, wakamatwe wote wafikishwe mahakamani, wasio na hatia wajulikane, WEZI wote ndani ikiwa ni pamoja na kurejesha kila senti waliyoiba. Hapa nakumbuka kilichowapata wahujumu uchumi na walanguzi katika miaka ya 80 wakati Marehemu Edward Sokoine (waziri mkuu wa zamani) angali hai. Hatua ya pili ije kwa washirika wao, yaani wanasiasa waongo. Hao wanaotudanganya eti hatuibiwi, hao wanaosingizia mambo mengine eti ndio sababu kuu za umasikini wetu, kumbe sivyo. Hukumu ya hawa iliyorasmi ianzie katika chaguzi ndogo zinazojitokeza. Hatimaye kiama chao kije mwaka 2010. Tutakapoingia katika uchaguzi mkuu wa 2010, twende kwenye vituo vya kura kupiga kura dhidi ya UMASIKINI, dhidi ya WIZI, dhidi ya UONGO, dhidi ya UFISADI, dhidi ya TAKRIMA na mama yake RUSHWA, tena dhidi ya tuliowapa dhamana WAKATUSARITI. Mwaka huo tutaziba masikio yetu dhidi ya sera za ulaghai, tutapenda kusimsikiliza atakayetuambia ushiriki wake katika kutuibia au katika kupambana na wizi nchini (yaani chanzo kikuu cha ufukara wetu) Hatafurahi akituambia atatupatia mishahara minono na tutafanya ‘prakitiko’ mwezini, bali tutampenda akizungumzia uaminifu na uadilifu wake katika kutumia kodi tunazolipa kupitia mishahara na manunuzi ya bidhaa kwa ajili ya kuboresha huduma za jamii. Tutampenda kwa sababu nchi za wenzetu wanatumia kodi kwa uadilifu kabisa, kuboresha elimu, afya, miundombinu ya usafiri, mawasiliano na nisati.

Wameweza wao, na yeye hatuambie tutaweza kwa kuwa hatakuwa mshirika wa WEZI na akishirikiana nao hata kwa bahati mbaya, atajiuzulu mara moja bila kusubiri kamati Fulani imtaje, na kama pana tuhuma yuko tayari kujibu mashtaka. Juzi tu niliambiwa na rafiki yangu mmoja raia wa Finland, kwamba asilimia sitini ya mshahara wake wa mwezi (30%) inakatwa kwa ajili ya kodi. Akasema haimuumizi na wala halalamiki kwa kuwa anajua inakoenda inafanya kazi yake barabara. Mwenzenu nilipigwa na butwaa! Nikiwa bado siamini alichosema, rafiki yetu tuliyekuwa naye karibu (yeye anatoka Canada) akachangia hoja kwa kusema nchini kwao, baada ya muda fulani, serikali huwarejeshea wafanyakazi sehemu ya makato yao ya kodi, kwa kuwa inakuwa imezitumia fedha za kodi katika kuzalisha na imekwisha kupata faida tosha kwa ajili ya majukumu yake ya kuihudumia jamii katika kipindi husika. Ndugu zangu, wenzetu hawa, hata asiye na kazi ana posho ya kila mwezi! Hatutampenda mgombea atakayetuambia yeye binafsi ataleta maisha bora kwa kila mtanzania hata aliyeko jela, maana huo ni uongo. Tutamsikiliza akija na mikakati inayotekelezeka ya kuhakikisha madini yetu hayaibiwi, Benki kuu haiwi pango la wanyang’anyi na kodi zetu zinaenda kunakotakiwa, na juhudi zetu zinatunufaisha sote sio wanajinufaisha nazo waongo, wazandiki na WEZI. Kura yetu ya kuanzia mwaka huo, natamani isiangalie tena habari ‘rangi’ ya chama wala uzuri wa sura ya mtu wala kiasi cha fulana, vitenge na kofia alizogawa bure wakati wa kampeni, bali tutapiga kura tukiangalia ni wapi tunataka taifa letu lielekee kimaendeleo. Kura yetu itekuwa imelenga kukomesha rushwa mahakamani, mizaha bungeni na uzembe serikalini. Hali kadhalika italenga kutokomeza upuuzi katika taasisi zote za umma na katika jamii kwa ujumla. Hoja yangu ndugu zanguni; Taifa letu limeibiwa sana na hiyo ndio sababu kubwa ya umasikini wetu. Ni jukumu letu sote kuacha ubinafsi, tushirikiane katika kuukomesha wizi huu, na kwa njia hiyo tutaukomesha umasikini. Hatua hiyo iende sambamba na harakati nyinginezo ndogondogo na kubwa za kuupiga vita umasikini. Lengo letu liwe moja tu, kuifanya jamii ya Tanzania inufaike na ifurahie utajiri aliotujalia mwenyezi Mungu. Mungu ibariki Tanzania, utuwezeshe kushinda vita vyetu dhidi ya wezi unaoendelea kuwafunua mbele ya macho yetu, AMEN.

MWISHO