YENYE KUHATARISHA NYUMBA   ( 3 )
  • Kichwa: YENYE KUHATARISHA NYUMBA ( 3 )
  • mwandishi: Ummu Nassra
  • Chanzo:
  • Tarehe ya Kutolewa: 20:4:10 1-10-1403

BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

YENYE KUHATARISHA NYUMBA ( 3 )
MUZIKI NA NYIMBO
Miongoni mwa yenye kuzoeleka katika majumba yetu ni mziki. Kwa kweli mziki umeenea kila pembe ya dunia kiasi ambacho unawaumiza Waislamu wengi kimwili na kiakili bila ya kujijua. Kila mtu amekabiliana na hali ambayo humuingiza kusikiliza muziki ama kwa hiari au kwa lazima. Kuongezeka umaarufu wa muziki kunahatarisha sana majumba ya Waislamu na hatimae kutumbukia katika balaa hilo usiku na mchana.

Ukweli ni kuwa muziki unaathiri sana mioyo ya Waislamu na kuishughulisha akili kwa mambo ya kipuuzi. Tunatumia muda na pesa nyingi katika kununulia CD za majimbo yasiyo na faida, zana za miziki, na hata kuwatumbukiza watoto wetu kwa vifaa (toys) mbali mbali vilivyojaa miziki; Tunajitia makosani na kuuporomoa itikadi sahihi ya Muislamu. Kuna dalili tosha katika Quraan na Sunnah zenye kuonyesha uharamu wa muziki. Katika Suurat Luqmaan aya ya 6 Allaah Subhaanahu wa Ta'ala anatueleza:

((وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا أُولَئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ))
Na miongoni mwa watu wapo wanaonunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipo kujua, na wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha Maulamaa pamoja na wafasiri wengi wa Quraan wameeleza kuwa neno "Lahwal-hadith" katika aya hii inakusudiwa nyimbo na zana za miziki.

Mfano Ibn Mas'uud Radhiya Allahu 'anhu amesema kuhusu Aya hii "Naapa kwa Allah hii inamaanisha ni nyimbo" Pia miongoni mwa hadithi zenye kuonyesha uharamu wa ngoma na kila aina ya muziki ni hadithi mashuhuri ya Mtume Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam:
"Watakuweko watu katika Ummah wangu watakaojaribu kuhalilisha zinaa, uvaaji wa hariri, pombe na muziki. Bukhari
Ni vyema tuelewe kuwa hakuna chochote alichokikataza Allah Subhaanahu wa Taala isipokuwa kina madhara ndani yake katika ustawi wa jamii. Jua kuwa miziki tunayoichezesha majumbani yanaweza kuchochea hisia za mja, jazba pamoja na muengezeko wa mapigo ya moyo na kushughulisha akili.

Ujumbe unaopatikana katika miziki na nyimbo nyingi hasa wakati huu tulionao huenda kinyume kabisa na maadili ya Kiislamu, huamsha hisia za mapenzi, uzinzi na uhuru wa kufanya lolote bila ya kuzingatia wajibu wa mja. Umefika wakati kwa Waislamu kutanabahi na kujaribu kwa kadiri ya uwezo wetu kuepukana na balaa hili na kurejesha mandhari nzuri ndani ya majumba yetu. Tusiziuwe nyumba zetu kwa sauti za shetani (nyimbo na miziki) na kuwawekea makaazi, Ni lazima tuziuhishe nyumba zetu kuwa ni sehemu ya kumkumbukwa Allah Subhaanahu wa Taala (dhikr) kwa kila hali; kwa sala, kusoma Quraan, na vitabu vyengine vya dini pamoja na masuala mbali mbali yanayowahusu Waislamu. Hii itatupelekea kuzungukwa na Malaika, kulindwa na kupata ridhaa ya Allah Subhaanahu wa Taala.
MWISHO